HADITHI
ALIYEMUUA MCHUMBA WANGU 12
ILIPOISHIA
Walipotoka nje ya hospitali
kila mmoja alipanda gari lake wakaondoka na wakaja kukutana tena kwenye kituo
cha polisi cha Kinondoni.
Wakiwa ndani ya ofisi ya
idara ya upelelezi Amour alimuonesha James pama la mtuhumiwa ambalo lilikuwa limehifadhiwa.
“Pama
lake ndio hilo hilo” James akasema.
“Hili
linamsaidia kuficha uso wake ndio maana analitumia”
Amour pia alimtolea simu ya
mtuhumiwa. Aliingia sehemu ya picha na kumtaka amuoneshe picha za marehemu
Maria ambazo mtu huyo alikuwa amejitumia.
James baada ya kuangalia
picha zilizokuwemo aligundua picha tatu zilizokuwa kwenye simu ya Maria. Picha
mbili Maria alikuwa amejipiga akiwa na James na picha moja alijipiga akiwa peke
yake.
“Picha alizojitumia
hajazifuta, ni hizi hapa” James alimwambia Amour huku akimuonesha picha hizo.
Amour
akazitazama.
“Alihitaji
picha hizi kwa ajili gani?”
“Anajua
mwenyewe”
“Inaonekana
alilenga kukuua na wewe”
“Pengine
lakini amewahiwa yeye”
SASA ENDELEA
“Pia tulimkuta na
vitambulisho viwili vya kazi. Kimoja kina jina la Pascal na kingine kina jina
la Samwel. Bila shaka jina lake halisi ni Samwel lakini bado tunaendelea na
uchunguzi”
“Nakushukuru sana Inspekta
kwa uchunguzi wako. Hivi sasa ninasubiri afikishwe mahakamani”
“Tutamfikisha mahakamani
baada ya uchunguzi wetu kukamilika na haitakuwa muda mrefu.
“Kwa
hiyo mimi naenda kazini”
“Wewe
nenda kazini, tutakapokuhitaji nitakupigia simu”
“Asante
sana”
James alimpa mkono wa kumuaga
Inspekata Amour akanyanyuka na kuondoka.
Mchana kutwa siku ile Amour
alikuwa katika pilika pilika ya kutafuta ushahidi zaidi wa kumuhusisha
mtuhumiwa aliyemkamata na mauaji ya Maria.
Alikwenda katika maktaba ya
polisi ambapo alama za vidole za Pascal zilikuwa zikifanyiwa uchunguzi.
Alibaini kwamba Pascal hakuwahi kukamatwa siku za nyuma na hakukuwa na
kumbukumbu yoyote kwamba aliwahi kuhusika na matukio ya uhalifu.
Isipokuwa ilibainika kwamba
moja ya alama za vidole iliyokutwa kwenye simu ya Maria siku alipouawa ilikuwa
ni ya mtuhumiwa aliyekamatwa.
Mchana wa siku ile Amour
alikwenda tena hospitali ya Muhimbili akiwa na polisi kadhaa.
Dhamira yake ilikuwa kumhoji
mtuhumiwa huyo hapo hapo hospitali.
“Jina
lako nani?’ Amour alimuuliza.
“Naitwa
Pascal Lazza” Mtuhumiwa huyo alimjibu.
“Hapana,
unadanganya. Tuambie jina lako halisi”
“Jina
langu halisi ndilo hilo”
“Jana tulikukuta na
vitambulisho viwili, kimoja kina jina la Samwel lakini vyote vina picha yako”
“Pia
unaweza kuniita Samwel”
“Wewe
ni jambazi uliyekubuhu, unatumia majina mawili”
“Ndiyo
mkuu”
“Jina
la Pascal Lazza ulilipata wapi?”
“Alinipa
baba yangu”
“Wewe
muongo mkubwa…”
Amour alimueleza kuwa jina
hilo lilikuwa la mtu mwingine aliyekwisha kufa. Lakini yeye aliokota au aliiba
shahada yake ya kupigia kura na kwenda kujisajili kwenye namba yake ya simu na
hivyo kuendelea kulitumia jina hilo katika shughuli zake za uhalifu.
Mtuhumiwa huyo akanyamaza
kimya kuonesha kuwa alichoambiwa kilikuwa kweli.
“Kwa
hiyo wewe unaitwa Samweli?”
“Ndiyo
mkuu”
“Unaishi
wapi?”
“Ninaishi
Temeke”
“Una
mke”
“Ndiyo
mkuu”
“Ulipata
wapi bastola?”
“Niliinunua na nilikuwa
katika mipango ya kuomba kibali cha kuimiliki kihalali”
Akionesha kuyapuuza maelezo
yake, Amour alimuuliza swali jingine.
“Ni
kwanini ulimuua Maria?”
Pascal
alikunja uso na kumtazama Inspekta Amour.
“Maria!
Maria ni nani?” akamuuliza huku akionesha mshangao.
“Ni msichana ambaye wewe
ulimuua kwa kumpiga risasi nyumbani kwake Kinondoni hivi karibuni”
Pascal
akatikisa kichwa.
“Tangu
nizaliwe sijaua mtu. Huyo msichana simfahamu”
“Eti
nini…?”
“Nakwambia
ukweli Inspekta”
“Kwanini
ulinikimbia pale ABC Club, Kimara?”
“Sikukukimbia,
niliondoka na hamsini zangu”
“Na
kwanini nilipokusimamisha hukutaka kusimama?”
“Nisimame
wakati sikufahamu!”
“Kwanini
ulitaka kunigonga na gari?”
“Ni bahati mbaya. Ni kwa
sababu ulikaa mbele ya gari na mimi nilikuwa na haraka”
“Unadhani
majibu yako yatakusaidia?”
Pascal
akakenua mdomo kama aliyekuwa anataka
kutabasamu.
“Kwanini
afande?”
“Tutakutoa hapa twende
ukatuoneshe nyumbani kwako kisha tutakurudisha hapa hapa”
“Nitashukuru
sana”
Amour
akakunja uso.
“Kitu
gani kinachokufanya ushukuru?” akamuuliza.
“Kunikutanisha na mke wangu.
Ninaamini mpaka sasa hajui niko wapi”
Amour akanyamaza. Alimfuata
daktari na kuomba aondoke na mtuhumiwa wao kwa muda wa saa moja kisha
atamrudisha tena. Aliporuhusiwa Amour aliwaagiza polisi aliokuwa nao wamtoe
mtuhumiwa huyo na kumpakia kwenye gari.
Zoezi hilo lilipofanyika, Pascal aliwapeleka polisi
hao nyumbani kwake Temeke.
Mke wa Pascal alishangaa
kuona mume wake akipelekwa na polisi huku mguu wake mmoja ukiwa umefungwa
bendeji na hauwezi kukanyaga.
“Wewe ndiye mke wa Pascal au
Samwel?” Amour alimuuliza mwanamke huyo.
“Mume
wangu ni Simon Puto” Mwanamke huyo alisema.
“Yuko
wapi Simon Puto?”
Mwanamke
huyo alimuonesha Pascal.
“Anaitwa
Simon Puto?” Amour akamuuliza.
“Ndiyo”
“Majina
ya Pascal na Samwel huyatambui?”
Mwanamke
huyo alibetua mabega yake.
“Mume
wangu haitwi hivyo”
ITAENDELEA
No comments:
Post a Comment