HADITHI
ALIYEMUUA MCHUMBA WANGU 4
ILIPOISHIA
Lakini kusudio lake halikutimia.
Aliweza kuwa nyuma yake katika mitaa miwili tu, kufika mtaa wa tatu gari hilo lilimchenga.
Hakuliona tena. Ikambidi James arudi kazini kwake.
Wakati wote akiwa ofisini
alijiuliza mtu yule ni nani na kwanini alitaka kujua kuhusu uchumba wake na
Maria. Alipoona hapati jibu akaamua kuachana na mawazo hayo. Aliendelea na kazi
zake hadi jioni alipotoka ofisini.
Alikwenda moja kwa moja
nyumbani kwa Maria Kinondoni. Wakati anaikaribi nyumba ya Maria alishituka
alipoliona gari la yule mtu aliyemuandama likiondoka nyumbani kwa Maria.
“Huyu mtu anafahamiana na
Maria?” James akajiuliza bila kupata jibu. Alilisimamisha gari akashuka na
kuelekea kwenye mlango wa nyumba ya Maria.
Aliusukuma mlango na kuingia
ndani. Alimkuta Maria akitoka kuoga.
“Ndio
unafika?” Maria akamuuliza.
Badala
ya kumjibu James naye alimuuliza.
“Ulikuwa
na mgeni yeyote humu ndani?”
“Mgeni
gani?’
“Yule
mtu nilimuona akiondoka na gari hapo nje”
“Mtu
yupi?”
“Yule
niliyekueleza kwenye simu”
SASA ENDELEA
“Sijamuona,
mimi nilikuwa naoga’
“Wakati
nafika nilimuona anaondoka na gari”
“Mh! Mtu mwenyewe simjui na
kwakweli hakuna mtu aliyeingia humu. Labda alibisha mlango, alipoona kimya
akaondoka”
“Kama aliingia utajuaje wakati ulikuwa unaoga?”
Macho ya Maria yalikwenda
kwenye simu yake aliyokuwa ameiweka kwenye kochi. Simu ilikuwepo.
“Sidhani
kama aliingia…”
Maria
aliichukua simu yake.
“Hii
simu sikuiweka hivi…”
Maria
alianza kuikagua simu yake kwa wasiwasi.
“Oh simu imetumika! Kuna
picha zangu zimetumwa kwenye namba hii…!”
“Picha
gani?”
“Picha nilizojipiga mwenyewe
na picha tulizopiga tukiwa sote…hebu tazama”
James
aliishika ile simu na kuangalia mfumo wa utumaji picha.
“Hii
namba huifahamu?”
“Siijui”
Maria alimjibu kwa wasiwasi na kuongeza.
“Huyo
mtu aliingia kweli na kujitumia picha zangu sasa hivi”
“Lazima
tumjue yule mtu ni nani na kwanini anatufuatafuta”
“Tutamjuaje
na ameshakwenda zake”
“Muda
ule nilimfuata na gari lakini alinichenga”
“Muda
upi?”
“Pale hoteli. Nilipotoka
nilimuona ameegemea gari akizungumza na simu. Aliponiona akaingia kwenye gari
na kuondoka na mimi nikamfuata”
“Ukamuona
anakwenda wapi?”
“Alinichenga tukapoteana.
Sasa wakati naja kwako nikaona gari lake
linaondoka”
Maria
akatikisa kichwa.
“Sijui
huyo mtu ni nani jamani!”
“Nitamchunguza
na nitamjua”
James alibonyeza namba ya
kutuma pesa. Akaingiza ile namba ya Pascal na kiasi cha pesa. Likaja jina la
mmiliki wa namba ile. Lilikuwa Pascal Lazza.
“Anaitwa
Pascal Lazza. Ndiye yeye. Aliniambia anaitwa Pascal”
“Hebu
mpigie umuulize”
James
akaipiga ile namba.
Sauti
ya mtandaoni ikamwambia kuwa namba haipatikani.
“Ameshazima
simu. Namba yake haipatikani”
“Mimi
sipendi kuandamwa andamwa namna hii!”
“Nitaijaribu
wakati mwingine. Ngoja niichukue”
James aliiweka ile namba kwenye
simu yake akairudisha simu ya Maria.
Maria
aliingia chumbani kwake na kuvaa kisha akarudi sebuleni.
“Mimi
nafikiri kuna kitu, si bure” James alimwambia Maria.
“Kama kitu gani?” Maria alimuuliza kwa wasiwasi.
“Nafikiri
tatizo liko kwenye uchumba wetu”
“Una
maana kuna watu hawataki tuoane?”
“Kitu
kama hicho”
“Wanajidanganya James, sisi
tutaoana tu. Hakuna wa kutuzuia. Watakuuliza maswali, wataiba picha lakini
haitasaidia”.
Siku chache zilizopita, Mahakama
ilikuwa imemuachia huru Maria baada ya kutomkuta na hatia katika kesi iliyokuwa
ikimkabili ya kupoteza kwa makusudi faili la kesi ya mshitakiwa kwa lengo la
kupoteza ushidi.
Ingawa hakuwa amerudishwa
kazini, alishukuru kesi hiyo kuisha kwa vile ilikuwa imemuweka roho juu. Alijua
kuwa alikuwa ametenda kosa lakini alitoswa na mtu ambaye alimshawishi kutenda
kosa hilo bila
kujua kuwa lingemletea balaa.
Licha ya kutorudishwa kazini,
kule kusalimika na kifungo kulimuweka katika nafasi iliyomuwezesha kufunga
uchumba na James, kijana ambaye alimpenda kidhati moyoni mwake.
Alijiambia kama atakosa kazi
lakini atapata mume aliyempenda hakutakuwa na tatizo.
Alijitahidi sana kumficha James habari ya kesi yake, ingawa
James alifahamu kuwa Maria alikuwa na kesi lakini hakuweza kuijua kwa undani
kwa vile kesi hiyo iliisha siku chache tu kabla ya uchumba wao.
Siku iliyofuata baada ya siku
ile ambayo walitokewa na Pascal, walianza kupanga harusi yao. Waliazimia kuoana siku chache zijazo
wakati Jemes akiwa kwenye likizo. Na walianza maandalizi mapema.
Ilikuwa ni mwishoni mwa wiki
ileile wakiwa kwenye maandalizi ya harusi yao,
James akapokea meseji ya kushitusha kutoka kwa Maria. Ilikuwa saa mbili usiku.
James alikuwa amemaliza kuvaa baada ya kutoka kuoga. Simu yake ilipotoa mlio wa
kupokea meseji aliichukua na kuitazama. Akaona meseji iliyotoka kwa Maria.
Alipoifungua
meseji hiyo iliandikwa.
“James
njoo haraka yule mtu amekuja”
ITA ENDELEA kesho hapa hapa usikose
No comments:
Post a Comment