HADITHI
ALIYEMUUA MCHUMBA WANGU 5
ILIPOISHIA
Ingawa hakuwa amerudishwa
kazini, alishukuru kesi hiyo kuisha kwa vile ilikuwa imemuweka roho juu. Alijua
kuwa alikuwa ametenda kosa lakini alitoswa na mtu ambaye alimshawishi kutenda
kosa hilo bila
kujua kuwa lingemletea balaa.
Licha ya kutorudishwa kazini,
kule kusalimika na kifungo kulimuweka katika nafasi iliyomuwezesha kufunga
uchumba na James, kijana ambaye alimpenda kidhati moyoni mwake.
Alijiambia kama atakosa kazi
lakini atapata mume aliyempenda hakutakuwa na tatizo.
Alijitahidi sana kumficha James habari ya kesi yake,
ingawa James alifahamu kuwa Maria alikuwa na kesi lakini hakuweza kuijua kwa
undani kwa vile kesi hiyo iliisha siku chache tu kabla ya uchumba wao.
Siku iliyofuata baada ya siku
ile ambayo walitokewa na Pascal, walianza kupanga harusi yao. Waliazimia kuoana siku chache zijazo
wakati Jemes akiwa kwenye likizo. Na walianza maandalizi mapema.
Ilikuwa ni mwishoni mwa wiki
ileile wakiwa kwenye maandalizi ya harusi yao,
James akapokea meseji ya kushitusha kutoka kwa Maria. Ilikuwa saa mbili usiku.
James alikuwa amemaliza kuvaa baada ya kutoka kuoga. Simu yake ilipotoa mlio wa
kupokea meseji aliichukua na kuitazama. Akaona meseji iliyotoka kwa Maria.
Alipoifungua
meseji hiyo iliandikwa.
“James
njoo haraka yule mtu amekuja”
SASA ENDELEA
Kwa vile alikuwa ameshamaliza
kuvaa alitoka haraka akajipakia kwenye gari lake na kuondoka. Wakati akiendesha
kwa mwendo kasi James alikuwa ameazimia atakapofika ampige yule mtu kisha
amfikishe polisi ili akajieleze yeye ni nani na kwanini anawafuatilia.
Alikuwa anakaribia kufika,
simu yake ilipoita. Alipoitazama aliona alikuwa Maria. Akaipokea haraka.
“Hallo
Maria!”
“Haaa….!”
Sauti ya Maria ilisikika kisha ikakata.
James akaitazama simu na
kuona ilikatwa ghafla. Akampigia Maria lakini simu ya Maria ikawa haipatikani.
Akaiweka simu na kuendelea kulikimbiza gari hadi katika mtaa aliokuwa akiishi
Maria.
Mbele ya nyumba ya Maria
aliliona gari la Pascal lakini taa ya nje ya nyumba ya Maria ilikuwa imezimwa.
Kulikuwa kiza. Alilisimamisha gari lake
nyuma ya gari hilo. Wakati anafungua mlango ili ashuke
alimuona Pascal akijipakia kwenye gari.
James alishuka na kumfuata.
Pascal akawahi kuliondoa gari na kuondoka kwa kasi. James akakimbilia kwenye
mlango wa nyumba ya Maria ambao aliukuta uko wazi. Akaingia ndani.
Kwenye
sebule hakukuwa na mtu. James akasimama na kuita.
“Maria!
Hakukuwa na jibu, nyumba
ilikuwa kimya. James alikwenda kwenye mlango wa chumba cha Maria akausukuma na
kuingia ndani.
Alichokutana nacho kilimfanya
atoe macho na kuacha mdomo wazi. Maria alikuwa amelala chini, damu nyembamba
ilikuwa ikimtoka kifuani na kuchirizika hadi sakafuni. James alichutama na
kumuinua upande wa kichwani.
Maria
alikuwa akipumua kwa taabu.
“Maria umepatwa na nini?”
James akamuuliza kwa sauti iliyotaharuki.
Maria
alijitahidi kuinua mdomo akatamka kwa taabu.
“Pascal…Pascal…amenipiga
risasi…ameniambia alikuwa akinitafuta sana
na amethibitisha kuwa ni mimi…”
“Amekupiga
risasi kwa kosa gani lakini…?”
Nguvu zilikuwa zimemuishia
Maria. Hakuweza kutamka tena. Akaguna na kufumba macho.
“Maria…Maria…!”
James akamuita huku machozi yakimtoka.
Maria
alikuwa kimya.
“Maria!”
James alimuita kwa sauti ya juu huku akimtikisa.
Maria alikuwa kama hakuwepo tena. Uliokuwepo pale ulikuwa ni mwili
mtupu usio na uhai.
“Maria unanitoka hivi hivi
wakati tulibakisha siku chache tu tuoane na ulinisisitizia kuwa
tutaoana…Maria…” James alisema kwa hasira na uchungu huku matone ya machozi
yake yakiangukia kwenye uso wa Maria.
“Ni nani huyu Pascal?
Umemkosea nini Maria?” James aliendelea kujisemea peke yake.
“Siamini kama umekufa Maria”
James aliendelea kusema peke yake.
Aliulaza
chini mwili wa Maria kisha akalipapasa shavu lake.
“Buriani Maria” akamwambia na
kuongeza. “Nakuhakikishia kuwa nitamsaka Pascal na nitamkomoa”
Akanyanyuka na kugeuka kwenye
mlango ili atoke lakini akautazama tena mwili wa aliyekuwa mchumba wake.
“Tangulia
Maria. Mbele yako nyuma yangu. Nitamsaka Pascal!”
Aliposema hivyo aliinua hatua
na kutoka mbio mle chumbani. Aliufungua mlango wa nje akalikimbilia gari lake.
Alitumia sekunde tatu tu kufungua mlango, kujipakia na kuliwasha gari hilo na kuondoka kwa kasi.
Alilikimbiza gari hilo katika mitaa kadhaa
ya Kinondoni akilitafuta gari la Pascal. Alikuwa ameapa kama
atamuona zitakuwa za Pascal au zake. Lakini aligundua kuwa gari hilo lilikuwa limeshafika
mbali na asingeweza kuliona tena.
Akageuza njia na kuelekea
kituo cha polisi cha Kinondoni. Dakika chache tu baadaye akawa anazungumza na
Inspekta Amour aliyekuwa msaidizi wa mkuu wa kituo hicho.
Baada ya kumueleza jinsi
mauaji ya mchumba wake yalivyotokea, timu ya polisi ikiongozwa na inspekta huyo
ilitinga nyumbani kwa Maria.
James aliwaongoza hadi kwenye
chumba cha Maria na kuwaonesha maiti ya Maria iliyokuwa imelala kimya. Kama si ile damu iliyokuwa imevuja kwenye kifua chake,
mtu yeyote angemdhania kuwa alikuwa mzima bali alikuwa amelala.
Polisi wakaanza kushughulika
na kuchukua vipimo ikiwa ni pamoja na kumpiga picha marehemu, kuchukua alama za
vidole kwenye milango na kumpekua marehemu.
Baada ya zoezi hilo lililochukua takriban
dakika sitini, Mwili wa Maria ulipakiwa kwenye gari la polisi kupelekwa
hospitali. James akatakiwa kufika kituo cha polsi kwa ajili ya kutoa maelezo
zaidi.
Aliyemhoji
James alikuwa inspekta Amour.
“Unaitwa
nani?”
“Naitwa
James Matei”
“Umri
wako?”
“Miaka
thelathini na miwili”
“Marehemu
alikuwa anaitwa nani?”
“Anaitwa
Maria Faustus Wimbi”
“Ulijuana
lini na Maria?”
“Miezi
michache tu iliyopita”
“Hebu
nieleze mlivyokutana kwa mara ya kwanza”
James akaeleza alivyokutana
na Maria kwa mara ya kwanza hadi walipofikia kufunga uchumba.
“Nani unamshuku kumuua
mchumba wako?” Inaspekta Amour akaendelea kumuuliza.
“Ninamshuku
mtu mmoja anayejiita Pascal”
“Kwa
nini unamshuku mtu huyo?’
James akaeleza kwa kirefu
sababu za kumshuku mtu huyo. Alieleza alivyokutana naye kwa mara ya kwanza
kwenye hoteli. Na pia alivyofika nyumbani kwa Maria na kujirushia picha za
Maria kwenye simu yake na kisha kuondoka.
Akaendelea kueleza jinsi
Maria alivyomtumia meseji usiku ule akimueleza kuwa mtu huyo alikuwa amefika
nyumbani kwake ambapo James aliwasha gari na kuwafuata. Lakini njiani Maria
akampigia simu. Kabla ya kuongea lolote, simu ikakatwa. Na yeye alipojaribu
kumpigia simu ikawa haipatikani.
“Nilipofika nyumbani kwa
Maria nilikuta gari la yule mtu, wakati nashuka kwenye gari nikamuona yule mtu
anajipakia kwenye gari lake, nikamfuata lakini kabla ya kumfikia aliondoa gari
kwa kasi.
“Taa ya nje ya nyumbani kwa
Maria ilikuwa imezimwa. Nilipoingia ndani ndipo nilipomkuta Maria amelala chini
chumbani kwake. Akaniambia kwa kauli yake kuwa amepigwa risasi na Pascal”
“Uliwahi kumuuliza ni kwanini
Pascal alimpiga risasi?” Inspekta Amour alimuuliza James.
“Nilimuuliza lakini hakuwahi
kunijibu, wakati wake ulikuwa umeshafika”
ITAENDELEA kesho hapahapa usikose
No comments:
Post a Comment