Wednesday, December 28, 2016

HADITHI, ALIYEMUUA MCHUMBA WANGU SEHEMU YA 13

HADITHI
 
ALIYEMUUA MCHUMBA WANGU 13
 
ILIPOISHIA
 
Amour akanyamaza. Alimfuata daktari na kuomba aondoke na mtuhumiwa wao kwa muda wa saa moja kisha atamrudisha tena. Aliporuhusiwa Amour aliwaagiza polisi aliokuwa nao wamtoe mtuhumiwa huyo na kumpakia kwenye gari.
 
Zoezi hilo lilipofanyika, Pascal aliwapeleka polisi hao nyumbani kwake Temeke.
 
Mke wa Pascal alishangaa kuona mume wake akipelekwa na polisi huku mguu wake mmoja ukiwa umefungwa bendeji na hauwezi kukanyaga.
 
“Wewe ndiye mke wa Pascal au Samwel?” Amour alimuuliza mwanamke huyo.
 
“Mume wangu ni Simon Puto” Mwanamke huyo alisema.
 
“Yuko wapi Simon Puto?”
 
Mwanamke huyo alimuonesha Pascal.
 
“Anaitwa Simon Puto?” Amour akamuuliza.
 
“Ndiyo”
 
“Majina ya Pascal na Samwel huyatambui?”
 
Mwanamke huyo alibetua mabega yake.
 
“Mume wangu haitwi hivyo”
 
SASA ENDELEA
 
Amour akamtazama Pascal.
 
“Kumbe wewe unaitwa Simon Puto!” akamwambia.
 
“Yote ni majina tu, mtu unaweza kuitwa au kujiita vyovyote unavyopenda” Puto alijibu.
 
“Mume wangu umefanya nini?” mwanamke huyo akaumuuliza.
 
“Nimepigwa risasi na polisi jana usiku”
 
“Kwanini?”
“Sijui”
 
“Unaitwa nani?” Amour akamuuliza yule mwanamke.
 
“Naitwa Vicky”
 
“Mume wako anafanya kazi gani?”
 
“Ananiambia kuwa anafanya biashara”
 
“Biashara gani?”
 
“Sijui”
 
“Mlioana lini?”
 
“Tuna miaka miwili”
 
“Mume wako tumemkamata kwa tuhuma za mauaji ya msichana mmoja anayeitwa Maria. Wewe unajua kuwa mume wako aliua?”
 
Vicky akatikisa kichwa. Uso wake ulishaanza kupoteza nuru.
 
“Sijui” akajibu huku akimtazama Amour kwa macho makali.
 
“Ulikuwa unamfahamu msichana anayeitwa Maria aliyekuwa akiishi Kinondoni?”
 
“Sikuwa nikimfahamu”
 
“Sawa. Tulikuwa tunahitaji kupekua nyumba yenu”
 
Mwanamke huyo akanyamaza kimya.
 
Zoezi hilo likafanyika. Polisi hao hawakupata kitu chochote ambacho wangekihitaji. Wakamchukua Vicky. Vicky alipelekwa kituo cha polisi cha Kinondoni, Simon Puto akarudishwa Muhimbili.
 
Vicky alihojiwa tena kwa karibu masaa mawili. Ikabainika kwamba tangu alipoolewa na Simon Puto, hakuwa akifahamu kuwa mume wake alikuwa jambazi. Siku zote alikuwa akimwambia kuwa yeye alikuwa mfanyabiashara lakini hakuwa akimueleza ni biashara gani aliyokuwa akifanya.
 
Mwanamke huyo aliwekwa ndani na aliachiwa siku iliyofuata.
 
Polisi walikuwa wakitafuta chanzo cha Puto kumuua Maria. Licha ya Puto mwenyewe kukanusha kumuua Maria, uchunguzi wa polisi haukufanikisha kupatikana kwa chanzo hicho.
 
Polisi pia walikuwa wakitafuta rikodi za nyuma za uhalifu za Simon Puto ambazo pia hazikupatikana.
 
Baada ya wiki moja wakampeleka Simon Puto mahakamani. Mguu wake ulikuwa umeshapona. Polisi walitumia jina hilo la Simon Puto kumfungulia mashitaka. Puto alifunguliwa shitaka moja tu la kumuua Maria kwa kukusudia.
 
Alianza kusomewa shitaka hilo katika mahakama ya hakimu mkazi ambako hakutakiwa kujibu chochote kisha kesi ilihamishiwa mahakama kuu.
 
Puto aliposomewa tena shitaka hilo na kutakiwa kukiri au kukanusha, alikana shitaka la kumuua Maria. Kesi ikahairishwa kwa mwezi mzima. Polisi wakawa wanamtafuta James ili akatoe ushahidi wake pindi kesi itakapoitishwa tena.
 
James alikuwa amepata safari ya kikazi, Aliporudi. Inspekta Amour alimfuata nyumbani.
 
“Ile kesi tumeshaifikisha mahakamani” Amour alimwambia James kwa shauku na kuongeza.
 
“Itakapoitishwa tena utahitajika kwenda kutoa ushahidi wako. Wewe utakuwa shahidi wa kwanza wa upande wa mashitaka”
 
“Sawa”
 
Amour alikubaliana na James ambaye alitajiwa tarehe ya kufika mahakamani na akaahidi kuwa atafika.
 
Kesi ilipoitishwa tena James aliomba ruhusa kazini kwake na kufika mahakamani. Alifika akiwa amechelewa na hakukutana na Inspekta Amour kabla ya kwenda kutoa ushahidi wake. Jina lake lilipoitwa aliingia ndani ya mahakama na kupanda kizimbani.
 
Kabla ya kutoa ushahidi alipewa kitabu cha Biblia na kuapishwa kisha akaulizwa kama alikuwa akimtambua Simon Puto aliyekuwa upande wa pili wa kizimba. James akatikisa kichwa.
 
“Simtambui”
 
Mwendesha mashitaka alishangaa aliposikia jibu hilo.
 
“Umekuja hapa kutoa ushahidi wa nini?” akamuuliza.
 
“Sijui”
 
“Unakumbuka kwamba mchumba wako aliuawa na wewe ulimuona mtu aliyemuua?”
 
“Lakini hayuko hapa”
 
“Mshitakiwa alipokamatwa ulikwenda kumtambua na ukathibitisha kuwa yeye ndiye muuaji”
 
James alitikisa kichwa.
 
“Sikubaliani na hilo”
 
“Ni kitu gani ambacho wewe hukubaliani nacho?’ Mwendesha mashitaka aliendelea kumuuliza.
 
“Sikubaliani kwamba mshitakiwa aliye mbele yangu ni muuaji”
 
“Ni nani?”
 
“Simtambui”
 
“Una maana kwamba yule uliyekwenda kumtambua kituo cha polisi mara tu alipokamatwa si yeye?”
 
“Si yeye”
 
“Utakuwa umemsahau?’
 
“Nina kumbukumbu timamu, si yeye!”
 
“Lakini unakubaliana kwamba aliyeuawa alikuwa mchumba wako?”
 
“Ndiyo alikuwa mchumba wangu”
 
“Sasa nikikwambia kwamba mshitakiwa aliye hapo ndiye yule uliyemthibitisha wewe mwenyewe mbele ya polisi kuwa alimuua mchumba wako, bado utakataa?’
 
James akatikisa kichwa.
 
“Nitakataa. Na ninasema kwamba mshitakiwa huyu simtambui, ni bora aachiwe tu”
 
“Unasema kweli James?”
 
“Kweli tupu. Hapa niliapishwa niseme ukweli”
 
“Sawa”
 
Mwendesha mashitaka akamtazama jaji.
 
“Mheshimiwa shahidi wangu amenikana” alimwambia.
 
ITAENDELEA

No comments:

Post a Comment