HADITHI
ALIYEMUUA MCHUMBA WANGU 6
ILIPOISHIA
James akaeleza kwa kirefu
sababu za kumshuku mtu huyo. Alieleza alivyokutana naye kwa mara ya kwanza
kwenye hoteli. Na pia alivyofika nyumbani kwa Maria na kujirushia picha za
Maria kwenye simu yake na kisha kuondoka.
Akaendelea kueleza jinsi
Maria alivyomtumia meseji usiku ule akimueleza kuwa mtu huyo alikuwa amefika
nyumbani kwake ambapo James aliwasha gari na kuwafuata. Lakini njiani Maria
akampigia simu. Kabla ya kuongea lolote, simu ikakatwa. Na yeye alipojaribu
kumpigia simu ikawa haipatikani.
“Nilipofika nyumbani kwa
Maria nilikuta gari la yule mtu, wakati nashuka kwenye gari nikamuona yule mtu
anajipakia kwenye gari lake, nikamfuata lakini kabla ya kumfikia aliondoa gari
kwa kasi.
“Taa ya nje ya nyumbani kwa
Maria ilikuwa imezimwa. Nilipoingia ndani ndipo nilipomkuta Maria amelala chini
chumbani kwake. Akaniambia kwa kauli yake kuwa amepigwa risasi na Pascal”
“Uliwahi kumuuliza ni kwanini
Pascal alimpiga risasi?” Inspekta Amour alimuuliza James.
“Nilimuuliza lakini hakuwahi
kunijibu, wakati wake ulikuwa umeshafika”
SASA ENDELEA
“Gari
la Pascal ni aina gani?’
“Ni
hizi Toyota Corolla ya rangi ya kijani”
“Nipatie
namba yake ya usajili”
“Sikuwahi
kuzikariri”
“Ulisema uliwahi kuchukua
namba yake ya simu kutoka kwenye simu ya Maria, nipatie ile namba”
“Nimeshaipiga mara nyingi
lakini haipatikani” James alimwambia Inspekta baada ya kumsomea namba hiyo
kutoka kwenye simu yake.
“Hii
ni kazi yetu sisi, sisi tunaamini kuwa tutampata”
“Nitashukuru sana
kama atapatikana, na mimi mwenyewe pia
ninamtafuta”
“Sawa.
Wewe ndio umemuona, unaweza kututajia yukoje”
“Ni
mrefu, mweusi na anavaa pama jeusi”
“Wakati ulipomuona akijipakia
kwenye gari leo alikuwa amevaa nini?”
“Alivaa suti nyeusi na hata
siku ya kwanza nilipomuona alikuwa amevaa suti nyeusi”
“Sawa. Sisi tutamtafuta
lakini tunaomba ushirikiano wako. Ukisikia tetesi yoyote kuhusu yeye usisite
kuja kutufahamisha. Au ukimuona mahali haraka tupigie simu”
“Sawa” James alimkubalia
lakini ndani ya moyo wake alijiambia vingine.
Alijiambia kama atamuona mtu
huyo mahali popote atamalizana naye hapo hapo na hatahitaji kuwaarifu polisi.
Alikuwa na uhakika kuwa uwezo wa kummaliza alikuwa nao.
“Sasa unaweza kwenda lakini
kesho asubuhi ufike tena hapa kituoni”
“Nitafika”
James akaondoka na kurudi
Kinondoni nyumbani kwa marehemu. Nyumba ilikuwa imefurika ndugu na jamaaa.
Wazazi pamoja na kaka wa marehemu ambao walipata taarifa hizo mapema walikuwa
miongoni mwa waombolezaji waliokuwa wakibubujikwa na machozi.
Mara tu baada ya James
kuondoka kituo cha polisi, Inaspekta Amour alipokea taarifa ya uchunguzi wa
alama za vidole zilizopatikana kwenye vitasa vya milango nyumbani kwa Maria na
pia kwenye simu yake.
Uchunguzi huo wa alama za
vile ulionesha kuwa kulikuwa na aina tatu za alama hizo zilizopatikana kwenye
vitasa vya milango na kwenye simu ya Maria.
Kazi ya kwanza ya Inspekta
Amour ilikuwa ni kutafuta alama hizo zilikuwa ni za akina nani. Usiku huo huo
alikwenda hospitali ya Muhimbili ambako mwili wa marehemu Maria ulihifadhiwa.
Alifuatana na kachero Stambuli ambaye alikuwa mtaalamu wa uchunguzi wa alama za
vidole.
Walipofika Muhimbili
walichukua alama za vidole vya Maria. Alama hizo zilikujalinganishwa na alama
zilizopatikana nyumbani kwa Maria ambapo ilifahamika kwamba aina moja ya alama
hizo ilikuwa ni ya marehemu mwenyewe.
Asubuhi yake James alipofika
kituo cha polisi, alama zake za vidole zikachukuliwa na kupelekwa kufanyiwa
uchunguzi. Ikagundulika kuwa aina ya pili ya alama zilizokutwa nyumbani kwa
marehwmu, ilikuwa alama ya vidole vya James.
Polisi walishuku kwamba aina
ya tatu ya alama hizo ilikuwa ni ya Pascal aliyekuwa akituhumiwa kwa mauaji.
Kazi ya pili ya polisi
ilikuwa ni kulinganisha alama hizo zilizoshukiwa kuwa za Pascal na alama za
wahalifu mbali mbali waliowahi kukamatwa na polisi. Dhamiri ya polisi ilikuwa
ni kuona kama alama hizo zitalingana na alama
za mhalifu mmojawapo.
Zoezi hilo lilifanyika makao ya polisi ambako ndiko
kulikokuwa na maktaba ya alama zote za wahalifu waliowahi kukamatwa hapa nchini.
Inspekta Amour aliamini kuwa endapo alama hizo
zitagundulika kuwa ni za mmoja wa wahalifu waliowahi kukamatwa, wataweza
kumgundua Pascal mara moja kwani kwa kawaida alama hizo uhifadhiwa pamoja na
picha ya muhusika, jina lake na rekodi yake
Kwa hiyo polisi wataweza
kuiona picha ya Pascal pamoja na rikodi yake. Kama
picha hiyo itathibitishwa na James kuwa ndiye Pascal mwenyewe, itakuwa ni kazi
rahisi kumkamata kwani polisi watajua atapatikana wapi kwa mijubu wa kumbukumbu
zake walizonazo.
Kutokana na uwingi wa alama
za vidole za wahalifu zilizokuwa maktaba ya polisi, zoezi ya kutafuta alama
hizo ni za nani lilitarajiwa kuchukua zaidi ya siku moja.
Baada ya maziko ya Maria
kufanyika Kinondoni, James alijiambia alikuwa na kazi moja tu ya kumtafuta mtu
aliyemuua mchumba wake na kumkatisha ndoto yake njema ya kuoana na msichana
huyo.
Mara kwa mara James alikuwa
akiijaribu ile namba ya Pascal lakini mara zote alizoipiga ilikuwa haipatikani.
Sambamba na kumsaka Pascal kwenye simu alikuwa akilitafuta lile gari mitaani
akiamni kuwa kama litakuwa bado liko Dar kuna
siku atanasa.
Wakati wakisubiri uchunguzi
wa alama za vidole uliokuwa ukifanywa na polisi wa makao makuu ya polisi,
Inspekta Amour alikuwa akiifuatilia ile namba ya Pascal. Alifika katika kampuni
ya simu iliyomiliki namba ile na kutaka kupata rikodi yake.
Inspekta Amour alifahamishwa
kuwa ilisajiliwa kwa jina la Pascal Lazza wilaya ya Temeke mwaka mmoja
uliopita. Kwa mujibu wa kivuli cha shahada ya Pascal ambacho kilionesha alikuwa
mfanyakazi wa Kampuni ya mabati ya jijini, Pascal alikuwa mkazi wa Temeke.
Baada ya kupata maelezo yote
aliyohitaji, Inspekta Amour aliona kazi ya kumtafuta Pascal itakuwa fupi. Ni
kiasi tu cha kwenda katika kampuni ya mabati kumuulizia na kumtia mikononi.
Inspekta Amour alitoka katika
ofisi ya kampuni ya simu akiwa na furaha. Alikuwa na uhakika kwamba angeweza
kumkamata Pascal siku ileile.
Alipotoka kwenye ofisi ya
kampuni ya simu, alikwenda Temeke ambako ndiko kilipokuwa kiwanda hicho cha
mabati. Kwanza alifika kituo cha polsi cha
Temeke akaomba polisi watatu wa kituo hicho ili kwenda kumkamata Pascal.
Alipowapata polisi hao
alikwenda nao kwenye kiwanda hicho na kuonana na meneja wa kiwanda aliyekuwa
mtu mwenye asili ya kiasia.
“Kuna mfanyakazi wako mmoja
anaitwa Pascal Lazza” Inspekta Amour alimwambia meneja huyo aliyeonekana
kushituka.
“Pascal Lazza alikuwa
mfanyakazi wetu lakini kwa sasa hafanyi kazi hapa” Meneja huyo alijibu huku
akitikisa kichwa.
“Anafanya
wapi?”
“Sijui,
lakini hapa kwetu alishaacha kazi”
Amour akiwa amepatwa na
mshangao kutokana na jibu hilo
aliwatazama polisi wenzake kabla ya kuuliza.
“Aliacha
kazi lini?”
“Kama miezi sita iliyopita”
“Aliacha
kazi au alifukuzwa kazi?’
“Aliacha
kazi mwenyewe”
“Tulikuwa
tunamtafuta, unadhani tutampata wapi?”
“Sijui”
Jibu hilo la mkato liliwavunja nguvu polisi hao
ambao walilazimika kuondoka ofisini hapo. Dodosa dodosa ya Inspekta Amour
kwenye mitaa ya Temeke ilimfikisha katika nyumba ambayo ilielezwa alikuwa
akiishi Pascal.
Inspekta Amour alipolitaja
jina la Pascal, mwanamke aliyekuwa amemkaribisha kwenye nyumba hiyo alitoa
tabasamu la huzuni.
“Mbona Pascal sasa hivi ni
marehemu, Pascal alishakufa” Mwanamke huyo alimwambia Amour aliyeonekana
kushangaa.
“Alikufa
lini?”
“Sasa
ni karibu miezi mitatu”
“Unamzungumzia Pascal Lazza
aliyekuwa akifanya kazi kiwanda cha mabati?”
“Ndiye yeye ninayekwambia,
alishakufa. Mimi hapa ninayekueleza ni mjane wake”
“Ninapata taabu kuamini kwa
sababu Pascal amekuwa akionekana na anawasiliana na watu”
Mwanamke
huyo akashituka.
“Pascal
ameonekana wapi?”
ITAENDELEA
No comments:
Post a Comment