HADITHI
ALIYEMUUA MCHUMBA WANGU 11
ILIPOISHIA
Licha ya kwamba mtu huyo
alikuwa amepigwa risasi, polisi mmoja alimpiga teke kisha akamtia pingu.
“Hayaaminiki haya, yanafanya
ujambazi kwa kutumia uchawi. Lazima tulitie pingu”
“Inuka”
Polisi mmoja alimwambia.
“Acha tulipekue kwanza,
linaweza kuwa na bastola” Mwenzake akamwambia.
“Bastola
yake hii hapa, nimeshaichukua”
Polisi aliyemtia pingu
alipoiona bastola ya mtu huyo alihamaki akampiga kibao.
“Hili
liuaji kweli, lina bastola!”
“Mpakieni kwenye gari
apelekwe kituoni kisha apelekwe hospitali” Amour aliwambia polisi hao.
“Inuka
mwenyewe!” Polisi mmoja akamuamuru.
Mtu
huyo alijaribu kuinuka lakini hakuweza.
“Pumbavu!”
Polisi mmoja alimwambia na kumpiga kibao.
Walimshika mikono wakamburuza
na kwenda kumrusha kwenye gari lao.
“Mpelekeni kituoni, mimi
nakuja. Ninakwenda kuchukua gari langu” Amour aliwambia.
Wakati anakwenda kulichukua
gari lake ABC Club, Amour alimpigia mkuu wa kituo cha polisi cha Kinondoni na
kumueleza kuwa alikuwa amemkamata mtu waliyekuwa wanamtafuta aliyehusika na
mauaji ya Maria.
“Umemkamata
wapi?” Mkuu huyo aliuliza kwenye simu.
Amour
alimueleza tukio zima lilivyotokea.
SASA ENDELEA
“Kwa
sasa hivi yuko wapi?”
“Yuko kituo cha polisi cha
Kimara. Tunaandikisha maelezo yake kabla ya kumpeleka hospitali”
“Sawa.
Mimi nakuja huko huko kumuona”
“Sawa
afande”
Amour
akakata simu.
Dakika chache baadaye akawa
amefika kituo cha polisi cha Kinondoni. Mtuhumiwa aliyekamatwa alikuwa
ameshapekuliwa, alikutwa na simu moja, pesa taslim shilingi laki moja na
vitambuliso viwili vilivyokuwa na majina tofauti, kimojawapo kikiwa na jina la
Pascal Lazza.
“Tulikuwa tunakusubiri
uandike maelezo” Mmoja wa polisi wa kituo hicho alimwambia Amour.
Baada ya Amour kukamilisha
zoezi hilo, mkuu wa kituo cha polisi cha Kinondoni akawasili na kumuona
mtuhumiwa aliyekuwa amekamatwa.
“Sasa moja kwa moja apelekwe
hospitali ya Muhimbili. Atakuwa chini ya ulinzi wa polisi” akaagiza.
Kulipokucha asubuhi James
alikuwa ameshajiandaa kwenda kazini. Wakati anatoka ndipo simu yake ilipoita.
Alipoona
namba ya Inspekta Amour akaipokea haraka.
“Hello
Inpekta!”
“Habari ya asubuhi?” Sauti ya
Inpekta Amour ikasikika kwenye simu.
“Nzuri,
za huko”
“Huku
tuna habari mpya, yule mtu tumemkamata jana usiku!”
“Nani,
Pascal?”
“Ndiyo
Pascal”
James
alishituka sana.
“Unaniambia
kweli Inspekta?”
“Kweli
kabisa. Nimemkamata mimi mwenyewe”
“Umemkamatia
wapi?”
“Nilimkamata
kwenye klabu moja ya usiku pale Kimara”
“Ninahitaji
kumuona”
“Ndiyo sababu nimekupigia
simu. Ninataka twende Muhimbili Hospital, ukamtambue”
“Yuko
Muhimbili?”
“Nilimpiga
risasi ya mguu. Amelazwa Muhimbili”
“Sasa
nije hapo kituoni au…?”
“Itakuwa
vyema kama utakuja hapa”
“Basi
nakuja sasa hivi”
“Sawa”
James badala ya kutoka kwenda
kazini, aliwasha gari lake akaenda kituo cha polisi. Alikutana na Inspekta
Amour nje ya kituo. Alisalimiana naye na kupeana naye mkono.
“Umekuja na gari yako, sasa
tangulia Muhimbili. Mimi nakuja” Amour akamwambia James.
“Nikusubiri
nje?’
“Ndiyo
nisubiri. Hutaweza kuingia peke yako”
“Sawa”
James akarudi kwenye gari
lake akaliwasha na kuelekea Muhimbili.
Wakati anafika Muhimbili
aliliona gari la Inspekta Amour likiwa nyuma yake. Alishuka kwenye gari na
Amour akashuka. Wakafuatana hadi ndani ya jengo hilo la hospitali. Kwanza
walikwenda katika ofisi ya madaktari wakakutana na daktari aliyekuwa
akimshughulikia mtuhumiwa wao.
“Umekuja
Inspekta?” Daktari huyo akamuuliza Inspekta Amour.
“Ndiyo nimekuja na mtu ambaye
ninataka amtambue ili tujue kama ndiye mtu tuliyekuwa tunamtafuta”
“Sawa.
Nitawapeleka akamuone”
Walitoka
pamoja.
“Vipi, hali yake inaendelea
vizuri?” Amour akamuuuliza daktari huyo.
“Anaendelea vizuri. Kwa
bahati njema ile risasi haikuvunja mfupa. Iliingia kwenye nyama. Baada ya
kuitoa tumemuweka dawa na kumfunga bendeji”
“Ni
vizuri ili apone haraka tumfikishe mahakamani”
Katika chumba alichokuwa
amelazwa mtu huyo kulikuwa na askari mwenye bunduki aliyekuwa akimlinda.
Walipoingia kwenye chumba
hicho, Amour na James walimkuta mtu huyo akiwa amefungwa bendeji mguuni.
Alikuwa ametulia kimya akiwaza.
James
alipomuona tu hakungoja kuulizwa.
“Ndiye
yeye” alisema akionesha uhakika wa asilimia mia moja.
Amour
akamtazama James.
“Una
uhakika kwamba ndiye yeye?” akamuuliza.
“Inspekta
umemaliza kazi, sijui nikupe zawadi gani”
“Wewe utakuwa shahidi wetu
muhimu kwa sababu kwa mujibu wa maelezo yako umemuona mtuhumiwa mara mbili”
“Nina
hakika naye na nilisema sitamsahau…”
Aliposema hivyo James alikuwa
amekunja ngumi mkono mmoja akakipiga ngumi kadhaa kiganja chake cha mkono
mwingine kusisitiza maneno yake.
“Basi
imetosha, sasa turudi kituoni”
Walimuaga
daktari na kuondoka.
“Inspekta umefanya kazi
nzuri, ninakusifu” James alimwambi Amour.
“Hizi ni kazi zetu” Amour
akamjibu huku akitabasamu kupewa sifa.
“Mimi
nilidhani asingepatikana tena”
“Ulikosea kudhani hivyo. Sisi
polisi tunajua kwamba mbio za sakafuni huishia ukingoni. Wewe fanya uhalifu
wako na kuwa mjanja wa kuwakwepa polisi lakini ujue mbio zako zitaishia
ukingoni. Iko siku utakamatwa tu”
“Ni kweli mbio za sakafuni
huishia ukingoni” James aliikariri methali ya Inspekta Amour.
Walipotoka nje ya hospitali
kila mmoja alipanda gari lake wakaondoka na wakaja kukutana tena kwenye kituo
cha polisi cha Kinondoni.
Wakiwa ndani ya ofisi ya
idara ya upelelezi Amour alimuonesha James pama la mtuhumiwa ambalo lilikuwa
limehifadhiwa.
“Pama
lake ndio hilo hilo” James akasema.
“Hili
linamsaidia kuficha uso wake ndio maana analitumia”
Amour pia alimtolea simu ya
mtuhumiwa. Aliingia sehemu ya picha na kumtaka amuoneshe picha za marehemu
Maria ambazo mtu huyo alikuwa amejitumia.
James baada ya kuangalia
picha zilizokuwemo aligundua picha tatu zilizokuwa kwenye simu ya Maria. Picha
mbili Maria alikuwa amejipiga akiwa na James na picha moja alijipiga akiwa peke
yake.
“Picha alizojitumia
hajazifuta, ni hizi hapa” James alimwambia Amour huku akimuonesha picha hizo.
Amour
akazitazama.
“Alihitaji
picha hizi kwa ajili gani?”
“Anajua
mwenyewe”
“Inaonekana
alilenga kukuua na wewe”
“Pengine
lakini amewahiwa yeye”
ITAENDELEA
No comments:
Post a Comment