HADITHI
ALIYEMUUA MCHUMBA WANGU 8
ILIPOISHIA
“Nilionana na mwanamke mmoja
aliyenieleza kuwa alikuwa mke wa Pascal. Mwanamke huyo alinipa maelezo ya
kunishangaza. Aliniambia kuwa Pascal alikwisha kufa miezi miwili iliyopita
katika ajali ya gari iliyotokea Kimara”
“Amedanganya! Pascal yuko hai
na ndiye aliyemuua mchumba wangu” James alidakia.
“Amenithibitishia kuwa Pascal
amekufa kweli. Alinionesha picha za magazeti. Ile habari iliandikwa kwenye
magazeti na picha ya Pascal nimeiona ni kati ya watu waliokufa”
“Kwani
wewe unamjua Pascal? Ulimuona wapi?”
“Niliona picha yake kwenye
kivuli cha shahada alichosajilia simu yake”
James
akatikisa kichwa.
“Haiwezekani!”
“Ninajua
kuwa haiwezekani ndio sababu nimekufuata hapa”
James
akanyamaza na kumtazama Inspekta huyo.
“Ninataka twende nyumbani kwa
yule mwanamke ukaitazame ile picha halafu uniambie ndiye Pascal uliyemuona
wewe”
“Sawa.
Twende hata sasa hivi”
James alirudi kufunga mlango
kabla ya kuondoka na gari alilokwenda nalo Inspekta Amour.
“Mimi naamini kuwa Pascal
yuko hai. Kunaweza kuwepo na mbinu za kihalifu za kuonesha kuwa amekufa ili
polisi wasiendelee kumtafuta” James alimwambia Amour kwenye gari.
“Wewe
ndiye utakayetuthibitishia Pascal yuko hai au amekufa”
Walipofika Temeke kwenye
nyumba ambayo Inspekta Amour alifika kwa mara ya kwanza na kuzungumza na
mwanamke aliyemueleza kuwa Pascal alikuwa amekufa, walikaribishwa ndani.
“Umerudi
tena?” Mwanamke huyo alimuuliza Inspekta Amour.
“Ndio. Nilikwambia kuwa
ninaweza kurudi. Nimekuja na mtu ambaye alimuona Pascal katika siku za
karibuni, nataka aone zile picha ili aweze kututhibitishia kama ndiye
aliyemuona au la”
SASA ENDELEA
“Kwa
hiyo nikatoe zile picha niwaletee”
“Tuletee
yale magazeti ulionionesha”
Mwanamke akaingia chumbani.
Baada ya muda kidogo alitoka akiwa ameshika yale magazeti.
“Haya
hapa” alisema na kumpa Inspekta Amour.
Amour aliyachukua akayakunjua
na kumuonesha picha ya Pascal iliyokuwa imechapwa kwenye gazeti mojawapo.
“Mtu
uliyemuona ni huyu hapa?”
James
alimtazama kisha hapo hapo alitikisa kichwa.
“Huyu siye Pascal
ninayezungumza mimi, huyu ni mtu mwingine kabisa”
Amour alimuonesha James picha
ya Pascal iliyokuwa imetundikwa kwenye ukuta.
“Picha
yake nyingine ile pale, hebu itazame vizuri”
James
akaitazama picha hiyo iliyokuwa juu.
“Ile
na hii ni moja tu”
“Siye?”
“Siye
kabisa”
Amour
akakubali kwa kichwa.
“Sasa huyo ndiye Pascal aliyedaiwa
kufa katika ajali ya gari lakini picha yake ndio iko kwenye usajili wa namba ya
Pascal uliyemuona wewe”
“Imekuwaje?’
“Tunahitaji
uchunguzi. Hebu twende kule kampuni ya simu”
Amour alimuaga yule mwanamke
akatoka na James. Walifika katika ofisi ya kampuni ya simu. Amour aliomba
apatiwe kivuli cha shahada ya Pascal iliyoko kwenye usajili wa namba yake ya
simu.
Amour alipopatiwa kivuli
hicho alirudi Temeke na James na kukutana tena na yule mwanamke.
“Unaona fotokopi hii iko
kwenye usajili a namba ya Pascal…”
“Shahada iliyotolewa kopi
ilipotea miaka mingi, Pscal alishatoa ripoti polisi” Mwanamke huyo alidakia
wakati Amour akimueleza.
“Hata kama shahada yake
ilipotea lakini nani aliyesajili namba hii ya simu?”
“Siwezi kujua. Kwanza namba
ya simu iliyopo hapo haikuwa namba ya marehemu. Marehemu hakuwahi kusajili
namba kwa shahada yake”
Inspekta Amour akatazamana na
James kisha akamtazama yule mwanamke.
“Nimekuelewa. Asante sana”
alimwambia na kumtazama tena James.
“Twenzetu
James”
Walipokuwa kwenye gari
wakirudi Kinondoni Amour alimuuliza James.
“Umejua
ni nini kimefanyika?”
“Bado
sijajua”
“Muuaji wa mchumba wako
haitwi Pascal. Alitumia hila kusajili namba ya simu kwa kutumia shahada ya mtu
mwingine. Ile shahada aliiokota akaenda kujisajili nayo”
“Yule
mwanamke amesema mume wake aliipoteza shahada yake”
“Sasa huyo muuaji aliiokota
au aliiba, akaenda kujisajili nayo. Kwa hiyo jina hilo si la kwake na picha pia
si yake”
“Sasa
lengo lake lilikuwa nini?”
“Kama
atafanya uhalifu kwa kutumia ile namba asiweze kupatikana. Kama
ambavyo imetokea tumekwenda kumtafuta mtu mwingine ambaye tayari ameshakufa”
“Wahalifu ni wajanja sana na wana mbinu nyingi
za kutekeleza uhalifu wao bila kuguswa na mkono wa sheria”
“Si
wajanja, mimi nasema wajinga. Huyo jamaa nitamkamata tu”
“Natamani akamatwe hata leo.
Ameniharibia ndoto yangu ya maisha”
“Ulikuwa
na ndoto gani?”
“Nilikuwa
nimepanga kumuoa Maria mwezi ujao”
“Sikiliza
James, unaweza kupata mchumba mwingine”
“Hatakuwa
kama yule. Pengo aliloniachia halitazibika kirahisi”
“Hapo ndipo ‘kusahau’
kunapopata umuhimu. Utakapoweza kumsahau Maria na kupata mchumba mwingine,
huwezi kugundua tofauti”
Jams
akatikisa kichwa.
“Haitakuwa
rahisi sana” akasema.
“Haitakuwa
rahisi sana lakini itakuwa. Amini hivyo”
Siku iliyofuata Amour alifika
tena katika kampuni ya simu na kuulizia kama namba ya Pascal ilikuwa imefanya
mawasiliano na namba nyingine yoyote. Akajibiwa kwamba namba hiyo ilikuwa bado
haiko hewani.
“Naweza kupata namba zozote
alizowahi kufanya nazo mawasiliano nyakati za nyuma”
“Zipo”
“Nipatieni
chache tu”
Amour aliandikiwa namba nne
tofauti tofauti ambazo zilikuwa za kampuni ile ile.
Alipewa karatasi iliyoandikwa
namba hizo. Aliichukua akaaga na kuondoka.
Alipofika ofisini kwake
alizijaribu namba zote nne. Tatu zilikuwa hazipatikani lakini moja ilikuwa
hewani. Akaipiga.
Simu
iliita kwa sekunde chache kisha ikapokelewa.
“Hallo!”
Sauti iliyosikika ilikuwa ya kike.
“Habari?”
“Nzuri.
Nani mwenzangu?”
“Nilipewa
namba hii na Pascal” Amour alijaribu kumlaghai.
“Alikupa
kwa ajili gani?”
“Aliniambia
kama ninamuhitaji nikuulize wewe”
“Kwani mimi ni karani wake,
mpigie mwenyewe kwa namba yake”
Msichana
akakata simu.
Amour
akampigia tena. Alishamuona alikuwa jeuri.
Msichana
akapokea simu.
“Sasa
mbona unanikatia simu, kwani wewe ni nani wake?”
“Kwani
alipokupa namba hii alikwambia mimi ni nani wake?”
“Mbona tunaulizana maswali
dada’ngu, kwani ukinijibu itakuwaje?’
“Ulichokuwa unataka wewe ni
kujua Pascal yuko wapi au kujua uhusiano wetu?’
Amour
akajidai kutoa kicheko.
“Umekuwa mkali sana lakini
ndio tabia ya warembo wengi wa jiji hili, si kitu niambie nitampata wapi
Pascal”
“Kwa
sasa sijui yuko wapi”
“Ni
muda gani mtakutana?” Amour aliendelea kumuuliza.
Msichana
akang’aka.
“Tukutane wapi? Kwani alikwambia
ana mpango wa kukutana na mimi. Wewe kama unamtaka njoo hapa saa mbili usiku.
Kama atakuja kunywa utamkuta”
ITAENDELEA kesho Usikose
No comments:
Post a Comment