Thursday, November 10, 2016

HADITHI, YAMENIKUTA SALMA MIE SEHEMU YA 29

HADITHI hii inaletwa kwenu kwa hisani ya Freys Coach Tanga hadi Singida kila siku saa 12 asubuhi na 12 na 30. Freys wako na mabasi mawili yaendayo Singida kila siku Luxury Coach na Ordinary. Ofisi zake zipo barabara ya 12 Ngamini, simu 0622 292990
 
YAMENIKUTA SALMA MIE
 
ILIPOISHIA
 
Kila ninapomuuliza hutoa sababu mpya. Kuna siku anazoniambia amelala nje ya Jiji kuitokana na kazi zake za biashara na kuna siku ambazo huniambia amechelewa kurudi nyumbani kwa sababu alikuwa na mikutano na wafanyabiashara wenzake.
 
Pale ninapoonesha kukasirika kwa kumshuku kuwa ana wasichana wengine, Chinga alikuwa hodari wa kunibembeleza na kujitakasa kwamba hakuwa na msichana yeyote wa nje. Nikawa sina budi nikubaliane naye.
 
Ilipita miezi minne. Kuna siku Chinga aliniaga kuwa anakwenda Tanga kumsalimia baba yake na kuchukua gari lake. Aliniachia pesa za kutosha na ndani ya nyumba kulikuwa na kila kitu. Nakumbuka aliondoka asubuhi. Ilipofika jioni wakati nimeketi sebuleni nikiangalia tv nikasikia gari likasimama huko nje.
 
Nilipochungulia kwenye dirisha niliona teksi imesimama mbele ya mlango. Nikaona msichana anashuka. Alionekana kama anatoka safari kwani dereva alimteremshia masanduku mawili.
 
Teksi ikaondoka.Yule msichana akaja kubisha mlango. Nikanyanyuka na kwenda kumfungulia.
 
“Hujambo?” akaniuliza.
 
“Sijambo, karibu”
 
SASA ENDELEA
 
Nilifikiri angeniuliza kitu, badala yake nilimuona mwenzangu akiingiza masanduku yake na kuyaweka sebuleni kisha akaketi kwenye sofa. Alikuwa ameshika kitambaa akijipangusa pangusa usoni. Wakati naenda kuketi ili nimuulize yeye ni nani, akaniuliza.
 
“John yuko wapi?”
 
“John? John ni nani?” nikamuuliza. Sikwenda tena kuketi.
 
“Huyu mwanaume anayeishi kwenye nyumba hii” akanijibu kwa sauti tulivu.
 
“Humu ndani hakuna mwanaume anayeitwa John, labda umekosea nyumba”
 
Msichana akafungua sanduku lake moja akatoa picha moja na kunionyesha.
 
“Mtu niliyemuulizia ni huyu, au pia humfahamu?” akaniuliza.
 
Nilipoitazama ile picha ilikuwa ni ya Chinga. Moyo wangu ukashituka.
 
“Huyu si Chinga?” nikamuuliza yule msichana.
 
“Chinga?” yule msichana akaniuliza akiwa amekunja uso wake.
 
“Chinga ni nani?”
 
“Si ndiye aliye katika picha hii”
 
“Mimi najua anaitwa John, jina la Chinga silijui”
 
“Basi hayupo.Kwani wewe nani?”
 
“Mimi ni mke wake, natoka Nzega. Ndiyo nimefika sasa hivi”
 
Moyo wangu ukashituka tena.
 
“Kwani Chinga ana mke? Chinga hana mke. Siku zote ulikuwa wapi wewe?” nikamuuliza kwa kutaharuki.
 
Yule msichana hakutaka kubishana na mimi.Alitia mkono wake kwenye lile sanduku akatoa hati ya ndoa pamoja na picha kadhaa za harusi. Akanionesha.
 
Ile hati ya ndoa ilikuwa na jina la John Boniface ikionyesha kuwa alifunga ndoa na Vicky Leonard wilayani Nzega miaka mitatu iliyopita. Zile picha zilimuonyesha Chinga akifunga ndoa na yule msichana mbele ya Padri.
 
Kwa kweli nilishituka, nilishangaa na nilichanganyikiwa si tu kujua Chinga alishaoa wakati alinidanganya kuwa hajaoa, bali pia kuona ndoa aliyofunga ni ya kikristo wakati najua ni muislamu, tena akitumia jina la John badala ya Chinga.
 
“Umeamini kuwa mimi ni mke wake?” yule msichana akanieleza huku akizirudisha zile picha ndani ya sanduku.
 
Nguvu zilikuwa zimeniishia na nilihisi mwili wangu ukitetemeka kwa ghadhabu, nikajikaza na kumuuliza msichana huyo.
 
“Kwani siku zote hizo ulikuwa wapi?”
 
“Nimekuambia ninatoka Nzega, mimi na John tulikutana Nzega na tulioana huko huko akanileta hapa Dar. Baada ya miezi michache nikapata ujauzito.Wakati wa ujauzito wangu nilikuwa nikiumwa mara kwa mara na nilidhoofika. Nilipochukuliwa vipimo nikaonekana nimeambukizwa ukimwi….”
 
Alipofika hapo moyo ulinishituka kwa mara nyingine tena, sasa kujua kuwa Chinga alikuwa ana ukimwi na alikuwa ameshaniambukiza mimi.
 
Msichana alikuwa akiendelea kunieleza. 
 
“Baada ya kugundulika hospitalini kuwa nina ukimwi nilishauriwa nimpeleke mume wangu naye akapimwe. John akakataa kwenda kupimwa. Akaniambia yeye haumwi kwa hiyo hana sababu ya kupimwa. Akanirudisha Nzega niende nikaugulie kwetu. John alipoondoka Nzega ndiyo hakurudi tena. Huu ni mwaka wa pili”
 
Msichana aliendelea kunieleza.
 
“Bila shaka alijua nitakufa. Mpaka namba ya simu akaibadilisha ili tusiwasiliane. Lakini nimetumia tiba ya kurefusha maisha, hali yangu ikarudi kuwa ya kawaida ingawa mtoto niliyezaa alikufa. Sasa nimerudi kwa mume wangu”.
 
Msichana huyo alimaliza maelezo yake nikajikuta nimeduwaa nikimtazama. Hapo utagundua wazi kuwa nilikuwa  nimechanganganyikiwa. Kwanza ni kwa kujua kuwa nilikuwa nimeshabambikiwa virusi vya ukimwi. Na pili kujua kuwa Chinga alikuwa na mke wake na kwa mujibu wa ndoa za kikristo asingeweza kuongeza mke wa pili.
 
Jambo la tatu  lililonichanganya ni kugundua kuwa Chinga hakuwa mwanaume muaminifu. Alikuwa ni laghai na tapeli kwa wanawake. Amedanganya na kufunga ndoa ya kikristo akijifanya ni mkristo wakati ni muislamu. Mbali ya hayo ameonyesha tabia ya ukatili kwa kumtelekeza mke wake mjamzito bila ya kujali mtoto wake aliyomo tumboni.
 
Nilikuwa nimejitumbukiza mahali pabaya sana.Nikajifananisha na mtu aliyeruka jivu na kujikuta anakanyaga  moto!
Nilijiuliza kutokana na hali hiyo hatima yangu ingekuwa nini? Nilishatoroka kwa mume wangu kwa tamaa ya kuolewa na Chinga na kumbe Chinga mwenyewe ana mke wake na amesharudi. Sasa itakuwaje?.
 
Sikutaka kuendelea kusema na akili yangu. Nilitaka nipate majibu ya haraka kutoka kwa Chinga mwenyewe. Ingawa Chinga hakuwepo Dar lakini simu zilikuwepo, ningeweza kuzungumza naye kwa simu.
 
Nikamuacha yule msichana pale sebuleni nikaelekea uani.
 
“Wewe dada unakwenda wapi?” yule msichana akaniuliza wakati ninaelekea uani. Sikugeuka wala sikumjibu. Nilikuwa kama nimepagawa.
 
“Mbona hujaniambia John yuko wapi, unaenda zako?” akaendelea kuniuliza lakini pia sikumjibu.
 
Nilipofika uani, kwa vile simu nilikuwa nayo mkononi, nikampigia Chinga. Madhumuni yangu ya kutoka uani ni kutaka yule msichana asisikie nitazungumza nini na Chinga.
 
“Hellow  Dear!” Chinga akasema baada ya kupokea simu yangu.
 
“Nani Dear wako?” nikamjibu kwa kufoka na kuongeza. 
 
 “Wewe Chinga kumbe ni mwanaume laghai kiasi hicho! Kama ningekujua nisingemuacha mume wangu na kuja kuishi na wewe hapa Dar”
 
“Kwanini Dear unaniambia hivi?”
 
“Hilo neno Dear sitaki kulisikia. Wewe ni laghai nimeshakugundua! Uliniambia kuwa huna mke kumbe ulishaoa, tena umefunga ndoa ya kanisani.Ulijifanya mkristo na jina ulibadili ukajiita John!”
 
“Et! Nini?” Chinga akajifanya anang’aka. Akaongeza. 
 
“Mimi nilishakuambia usisikilize maneno ya watu.Wanawake wa Dar si wazuri ni wa mbeya na wanafiki. Sasa wameshakudanganya unaanza kufoka. Hao wanataka kututenganisha tu”
 
“Una maana wewe hujaoa?” nikamuuliza.
 
“Sijaoa. Mke wangu mtarajiwa ni wewe”
 
“Hujafunga ndoa kanisani Nzega na msichana anayeitwa Vicky kisha ukamtelekeza kwao na uja uzito ulipoona umemuambukiza ukimwi?”
 
Nilikuwa na hakika kwamba Chinga aligwaya baada ya kumwambia hivyo kwani sauti yake ilitoweka kwenye simu kwa sekunde kadhaa kabla ya kusikika tena ikiwa imenywea..
 
“Nani amekuambia maneno hayo?” akauliza kwa ukali kidogo.
 
“Si suala la kuambiwa, huyo msichana amekuja kutoka Nzega na yupo hapa nyumbani anakusubiri!” nikamwambia kwa mkazo.
 
Chinga akabadilika hapo hapo na kuniuliza.
 
“Unasema kweli?”
 
“Sasa mimi ningemjuaje?”
 
“Yukoje msichana mwenyewe?”
 
“Ni mfupi wa maji ya kunde. Macho yake ni makubwa”
 
“Amekonda au amenenepa?”
 
“Amenenepa. Ameniambia anatumia vidonge vya kurefusha maisha”
 
“Amekuja na mtoto?”
 
“Hana mtoto. Mtoto alikufa. Ameniambia ulimtelekeza Nzega ulipoona ana ukimwi na wewe ulikataa kwenda kupima. Kwanini Chinga umekuwa laghai kiasi hicho?”
 
“Sasa sikiliza Salma. Ni kweli huyo msichana nilioana naye lakini nilishamrudisha kwao na nilijua ndiyo tumeshaachana”
 
Maneno yake yaliniongezea hasira nikamwaambia.
 
“Wewe fala kweli! Maneno gani unaniambia?”
 
“Salma usiwe mkali, utaharibu kila kitu. Hebu niambiye yuko wapi huyo msichana?”
 
“Nimemuacha sebuleni, mimi nimekuja uani”
 
ITAENDELEA

No comments:

Post a Comment