Thursday, November 10, 2016

WAANDAMANA KUPINGA USHINDI WA TRUMP

Maelfu waandamana dhidi ya ushindi wa Trump Marekani

Wanafunzi wa shule ya upili ya Berkeley wakiandamana kupinga ushindi wa Trump
Rais wa Marekani Barack Obama amemwalika Rais mteule wa Marekani Donald Trump katika White House, huku maandamano ya kupinga ushindi wa Trump yakifanyika miji mingi Marekani.
Rais Obama amesema lengo la mkutano wao litakuwa kujadiliana kuhusu shughuli ya mpito na kupokezana madaraka.
Amesma anataka shughuli hiyo iwe laini na bila matatizo
Bw Trump wa Republican atakuwa rais wa 45 wa Marekani baada ya kupata ushindi wa kushangaza dhidi ya Hillary Clinton wa chama cha Democratic, chake Rais Obama.
Bw Obama alifanya kampeni kali kumzuia Bw Trump kushinda, na alisema hafai kuongoza. Wakati mmoja alisema hata hafai kuwa mwuzaji dukani.
Lakini rais huyo sasa amewahimiza Wamarekani wote kukubali matokeo ya uchaguzi wa Jumanne.
"Sasa tunatafuta ufanisi wake katika kuunganisha na kuongoza nchi hii," Bw Obama alisema kuhusu Trump.
Licha ya Rais Obama kuhimiza umoja na Bi Clinton kuwaambia wafuasi wake kwamba Bw Trump anafaa kupewa "nafasi ya kuongoza", ushindi wake umezua maandamano katika miji na majimbo kadha Marekani.
Mamia ya waandamanaji wanaompinga Trump walikusanyika nje ya jumba kuu la Bw Trump, Trump Tower eneo la Manhattan jijini New York Jumatano jioni, wakibeba mabango yaliyokuwa na ujumbe "Not my president" (Si Rais wangu), pamoja na mabango mengine.
Polisi hapo awali waliweka vizuizi vya saruji pamoja na kuchukua hatua nyingine za kiusalama nje ya jumba hilo refu linalopatikana barabara ya 5th Avenue, jumba ambalo huenda likawa makao makuu ya Bw Trump wakati wa kipindi cha mpito kabla yake kuingia White House.

Kuliripotiwa pia taarifa za waandamanaji kuziba lango la kuingia jumba la Trump Tower mjini Chicago Jumatano jioni, wakiimba: "No Trump, No KKK, No Fascists USA" (Hatumtaki Trump, Hatutaki KKK, Hatutaki Wafashi Marekani) na "Not my president!" (Si Rais wangu).
Mjini Oakland, California, na Portland, Oregon, waandamanaji waliteketeza bendera za Marekani
Wakati wa hotuba yake baada ya kutangazwa mshindi mapema Jumatano, Bw Trump aliahidi kuponya vidonda vya migawanyiko, baada ya uchaguzi huo uliokuwa na ushindani mkali, na kuahidi kwamba atakuwa "rais wa Wamarekani wote".
Msemaji wa White House Josh Earnest amesisitiza kwamba Bw Obama atakuwa na uwazi kuhusu kuhakikisha shughuli laini ya mpito atakapokutana na Bw Trump, ingawa aliongeza kwamba: "Sijasema kwamba utakuwa mkutano rahisi."
Rais huyo mteule atasindikizwa kwenda White House Alhamisi na mkewe, Melania, ambaye atakutana na Mke wa Obama, Michelle.

No comments:

Post a Comment