Wednesday, November 16, 2016

TANZANIA NI KISIWA CHA AMANI, BALOZI - RAMADHANI MWINYI

 Tangakumechablog

Tanga, NAIBU Katibu Mkuu Wizara ya Ushirikiano Afrika Mashariki, Balozi Ramadhani Mwinyi, ameiondoa hofu Serikali ya Uganda juu ya suala zima la ulinzi na usalama wa Mradi wa Bomba la Mafuta Tanga.
Akizungumza na ujumbe kutoka Serikali ya Uganda ikiongozwa na Katibu Mkuu Wizara inayoshughulikia masuala ya  Jumuiya ya Afrika Mashariki, Editha Mwanje, alisema Serikali ya Tanzania imejipanga katika Nyanja mbalimbali za ulinzi.
Alisema ulinzi umeimarishwa katika njia nyingi zikiwemo za baharini na nchi kavu kuhakikisha bomba hilo linalindwa kwa maslahi ya Watanzania na Wauganda ambao watafaidika kupitia ajira mbalimbali.
“Kwanza niseme Tanzania haina kitisho chochote cha usalama iwe baharini wala nchi kavu, lakini kwa ujio huu tutazidisha ulinzi maradufu iwe ni angani baharini na nchi kavu” alisema Mwinyi na kuongeza
Niseme kuwa bomba hili liko na faida kwa makundi mbalimbali hata wajasiriamali wadogowadogo na hii inamaana kuwa kila mmoja aone fursa ambayo itamkomboa katika maisha kwa kuwekeza miradi tofauti tofauti” alisema
Kwa upande wake, Katibu Mkuu Wizara kutoka Uganda anaeshughulikia masuala ya  Jumuiya Afrika Mashariki, Editha Mwanje, amefurahishwa na maandalizi ya ujio wa bomba hilo na kusema kuwa Tanzania imejipanga.
Alisema kulikuwa na kila sababu ya Tanzania kupata mradi huo kutokana na ukubwa wa bandari yake  na kina kirefu cha maji ambacho kiko na uwezo wa kuegesha meli nyingi.
“Tunaridhishwa na maandalizi ya mradi wa bomba la mafuta na Serikali ya Uganda iko pamoja nanyi na ndio maana kila wakati tunawatembelea’ alisema Mwanje
Alisema mbali ya kujionea kasi ya maandalizi ya bomba la mafuta pia Waganda wako na shauku ya kuja kuwekeza Tanga jambo ambalo litaongeza kasi ya ukuaji wa uchumi kwa nchi mbili hizo.
                                        Mwisho


  Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Ushirikiano Jumuiya Afrika Mashariki, Balozi Ramadhani Mwinyi, akizungumza na Kaimu Meneja wa Bandari Tanga, Henry Arika wakati wakielekeza Chongoleani kwa kutumia usafiri boti eneo ambalo bomba la mafuta litajengwa.


Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Ushirikiano Jumuiya Afrika Mashariki, Balozi, Ramadhani Mwinyi, akizungumza na waandishi wa habari Tanga mara baada ya kuongoza ujumbe wa Serikali ya Uganda walipotembelea eneo litakapojengwa bomba la mafuta Tanga hadi Uganda.

No comments:

Post a Comment