HADITHI
YAMENIKUTA SALMA MIE
ILIPOISHIA
“Sasa mimi ningemjuaje?”
“Yukoje msichana mwenyewe?”
“Ni mfupi wa maji ya kunde. Macho yake ni makubwa”
“Amekonda au amenenepa?”
“Amenenepa. Ameniambia anatumia vidonge vya kurefusha maisha”
“Amekuja na mtoto?”
“Hana mtoto. Mtoto alikufa. Ameniambia ulimtelekeza Nzega ulipoona
ana ukimwi na wewe ulikataa kwenda kupima. Kwanini Chinga umekuwa laghai kiasi
hicho?”
“Sasa sikiliza Salma. Ni kweli huyo msichana nilioana naye lakini
nilishamrudisha kwao na nilijua ndiyo tumeshaachana”
Maneno yake yaliniongezea hasira nikamwaambia.
“Wewe fala kweli! Maneno gani unaniambia?”
“Salma usiwe mkali, utaharibu kila kitu. Hebu niambiye yuko wapi
huyo msichana?”
“Nimemuacha sebuleni, mimi nimekuja uani”
SASA ENDELEA
“Ulimwaambia kuwa wewe ni msichana wangu?” Chinga akaniuliza.
“Sijamwambia isipokuwa yeye ndiye aliyeniambia kuwa wewe ni mume
wake, akanionesha hati ya ndoa pamoja na picha zenu za harusi”.
“Sasa sikiliza ninavyokwambia, usithubutu kumwaambia wewe ni
msichana wangu”
“Unaona jinsi ulivyo laghai, kumbe unataka nimwambie nini?”
“Unajua Salma inabidi tumdanganye huyo msichana ili asituletee
matatizo. Halafu mimi nitajua la kufanya hapo baadaye”
“Chinga unataka kuniletea matatizo. Sasa tumdanganyeje?”
“Umwambie wewe ni mtumishi wangu.Usishindane naye. Mimi nitakuja
kesho nitarekebisha hilo tatizo”
Chinga aliponiambia hivyo nikaanza kumlilia.
“Yaani mimi niwe mtumishi wenu? Chinga tulikubaliana vizuri kuwa
tutaoana, nikaondoka kwa mume wangu.Sasa unanigeuka, unataka niwe mtumishi wenu?”
“Hutokuwa mtumishi kweli, ni kiasi tu cha kumdanganya huyo
msichana,vinginevyo anaweza kutushitaki kwa kukiuka kiapo cha ndoa yetu”
“Lakini kwanini ulinidanganya Chinga….kwanini ulinidanganya….sasa
hatima yangu itakuwa nini Chinga….?”
“Usijali Salma.Nina mpango wa kukuhamishia kwenye nyumba yangu ya
Masaki ambayo huyo Vicky haijui, usilie”
“Siwezi kukuamini tena Chinga. Umeniharibia maisha yangu. Kwanza umeshaniambukiza virusi vyako halafu
umenitengenisha na mume wangu….”
Hapohapo mawasiliano yakakatika.Simu ilikuwa imeisha pesa. Nikachukia
kwani bado nilikuwa na mengi ya kumueleza Chinga yalioacha dukuduku na hasira
ndani ya moyo wangu.
“Hata akiniambia nini siwezi kumuamini tena” nikajiambia.
“Maisha yangu yamekwisha. Sasa,sina mume na nitakufa kwa ukimwi
alioniambukiza Chinga. Kweli dunia hadaa ulimwengu shujaa na majuto huja
kinyume baada ya kwisha kitendo” niliendelea kujiambia kwa hasira.
Niliondoka pale uani nikarudi ndani.Niliingia chumbani nilimokuwa
ninalala na Chinga. Nikahamisha vitu vyangu na kuvitia katika chumba cha wageni
kwani chumba hicho sasa atalala mke wa Chinga. Mwenyewe Chinga ameshasema mimi
nijitambulishe kama mtumishi.
Kilikuwa kitendo cha kunishusha hadhi na kunifanya mpumbavu lakini
ningefanyaje?.Nilijua kama nitajitia kidomodomo nitafukuzwa humo ndani na
sikuwa na pa kwenda. Sikuwa na ndugu wala jamaa ninayemfahamu hapo Dar na
nisingeweza kurudi tena kwa Ibrahim.
Baada ya kuhamisha vitu vyangu pamoja na nguo zangu zilizokuwa
kwenye kabati Chinga alinipigia simu. Nikajua wakati simu yangu ilipokatika
Chinga alinyamaza akipanga uongo wa kuniambia na sasa alikwisha upata.
“Usisikitike Salma. Mimi nitakuja kesho, nitarekebisha kila kitu. Nakuomba
umpe simu huyo Vicky”
“Nimpe simu ya nini? kama unataka
kuongea naye si umpigie kwenye simu yake!”
“Sina namba yake.Tafadhali nakuomba mpe simu, kuna kitu nataka kumwambia”
Nikatoka mle chumbani nilimokuwa nimehamishia vitu vyangu,nikaenda
sebuleni na kumpa simu yule msichana.
“Zungumza na huyo mtu uliyekuwa unamuulizia” nikamwaambia.
Msichana huyo akapokea ile simu na kuuliza.
“Wewe ni John?”
akasikiliza kisha akasema.
“Mimi ni Vicky. Nimerudi leo kutoka Nzega.Wewe uko wapi?”
Alipojibiwa alivyojibiwa akauliza.
“Utakuja lini?”
Sikujua Chinga alimjibu nini lakini baada ya kujibiwa alisema.
“Asante sana kwa kunitelekeza.
Kumbe wewe John ni mbaya kiasi hicho!”
Akasikiliza alichoambiwa. Ingawa sikuweza kuyasikia maneno ya
Chinga nilijua alikuwa akipewa uongo. Hatimaye akasema.
“Hapa nyumbani nimekuta msichana uliyempigia simu, ni nani?”
Moyo wangu ulishituka kidogo.Nikasubiri kusikia yule msichana
atasema nini tena baada ya kusikiliza maelezo ya Chinga. Nikamsikia akiuliza.
“Unasema ni mtumishi wako....? Sasa umeshamueleza kwamba mimi ni
mke wako nimesharudi....? Kama umeshamueleza
sawa …nimejifungua mtoto lakini si riziki, amekufa…sawa, basi tutaongea mengi
hapo kesho utakapo rudi”
Msichana huyo akakata simu. Akaichukua ile namba ya Chinga kutoka
kwenye simu yangu na kuisajili kwenye simu yake. Akawa anaiangalia angalia simu
yangu kisha akaniuliza.
“Na hii simu ulinunuliwa na John?”
Nilijua aliniuliza hivyo kwa sababu ile simu ilimtoa roho kwani
ilikuwa ni nzuri na ni ya thamani si kama
kimeo alichokuwa nacho yeye. Bila shaka alikuwa akijiambia kama mimi ni
mtumishi wa John nisingeweza kumiliki simu kama
ile.
“Nimeinunua mwenyewe” nikamjibu kwa sauti ambayo kama angekuwa
mjuzi angedundua kuwa sikufurahishwa na swali lake kwani
lilikuwa la umbeya.
“Uliinunua kiasi gani?”
“Laki nne”
Nilipomjibu hivyo aliniangalia usoni kisha akanipa simu yangu. Nilidhani
angeniuliza nilipata wapi hizo pesa. Nilikuwa nilishamuwekea jibu lake. Lakini
kama aliyejua hakuniuliza kitu.
Aliponipa simu yangu niliondoka pale sebuleni nikaingia katika
kile chumba nilichohamishia vitu vyangu, nikafunga mlango na kujitupa
kitandani. Sikuwa na hamu ya kula chakula cha jioni wala kuoga.
Nikaanza upya kuwaza juu ya mustakabali wa maisha yangu. Nilijiambia
kuwa nilikuwa nimecheza pata potea. Nilimtumainia sana Chinga aje awe mume wangu. Nilikuwa
nimeyaweka matumaini yangu na akili yangu kwa Chinga. Sasa mambo yamegeuka. Sivyo
nilivyokuwa nimetarajia. Maisha ya mimi na Chinga hayapo tena, badala yake
nimeambiwa nibaki hapo nyumbani kama mtumishi!
Nikajilaumu kwa kuchukua maamuzi ya kumkimbia mume wangu na
kumuamini Chinga bila kutumia busara. Kwa kweli nilifanya kosa kubwa.
Lakini si hilo
tu. Kulikuwa na tatizo jingine baya zaidi la kuambukizwa virusi vya ukimwi. Kama
Chinga ameweza kumuambukiza mke wake,na mimi atakuwa ameshaniambukiza. Kilichobaki
kwangu ni kusubiri siku virusi vitakavyoanza kufanya kazi yake.
Sikuweza kujua wakati huo nitakuwa wapi na sikuweza kujua nitahudumiwa
na nani?.Lakini yote niliyataka mwenyewe.
Nilikuwa nikiishi vizuri na mume wangu,nikapata ushawishi wa
kwenda kumfanyia dawa za mapenzi kwa tamaa ya kupata pesa. Dawa zikampofua
macho mume wangu, hali ya maisha ikazorota mpaka ikabidi nimkimbie. Na huku
nilikokimbilia ninakutana na makubwa zaidi kuliko yale niliyoyakimbia.
Wakati nikiwa katika lindi hilo
la mawazo, nilisikia mlango wa chumba ukigongwa kwa kishindo. Nikajua ni yule
msichana. Nikanyanyuka na kwenda kuufungua.
“Ulikuwa umelala?” akaniuliza.
“Nimejivyoosha tu, sijalala usingizi” nikamjibu.
“Mbona hukuniuliza nitakula nini wakati mimi ni mgeni nimekuja, unaingia
ndani unalala? Kama ninataka kitu nimtume
nani?.Au huyo John hakukueleza kuwa mimi ni mke wake?”
Maneno ya yule msichana yakanitibua. Lakini nilivuta subira.
ITAENDELEA
|
Saturday, November 12, 2016
HADITHI, YAMENIKUTA SALMA MIE SEHEMU YA 30
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment