HADITHI
YAMENIKUTA SALMA MIE
ILIPOISHIA
Mariam akanipeleka mpaka kwenye mlango wa chumba hicho.
“Yumo humu.Yeye amelewa na wewe umelewa. Sasa mtajuana wenyewe
lakini usisahau kupatana naye kabisa. Asije akakugeuka asubuhi”
“Sawa”
Nikaufungua mlango na kuingia humo chumbani. Nilimkuta huyo jamaa
amejilaza kitandani. Alipoona naingia akainuka na kuketi. Na mimi nikaenda
kuketi naye pale kitandani.Alikuwa amelewa sana.
Nilipoketi alinizunguushia mkono kiononi,akaniuliza. “Mrembo
hujambo?”
Nikamjibu “Sijambo, nakuhofia wewe”
“Nilikuwa nataka msichana mrembo kama
wewe” akaniambia.
“Ndiyo mimi nimeshakuja.Unataka short time au kulala kabisa?”
nikamuuliza kwa sauti ya kilevi.
“Kulala kabisa”
“Utanipa shilingi ngapi?”
“Sijui wewe unataka shilingi ngapi?”
“Elfu thelathini”
“Elfu thelathini zote za nini? wewe msichana mbona una tamaa sana ?”
“Sasa utanipa ngapi?”
“Kwa vile ni mzuri sana
nitakupa elfu ishirini”
“sawa”
Nikalala naye.
Asubuhi kulipokucha, mimi ndiye niliyeamka kwanza. Nikaenda
maliwatoni kisha nikarudi na kuvaa. Wakati ninavaa yule jamaa naye akaamka na
kuketi kitandani.
SASA ENDELEA
Nikamfuata pale kitandani ili anipe changu niondoke. Macho yetu
yakakutana. Moyo wangu ulishituka nilipomgundua kuwa ni Mashaka mdogo wake mume
wangu Ibrahim niliyemkimbia Tanga.
Na yeye aliponiona alishituka akawa amenitumbulia macho.
“Wewe si Salma mke wa kaka Ibrahim?” akaniuliza.
“Kwenda zako!” nikamwambia kwa kutaharuki.
Nikawa nageuka ili nitoke mle chumbani. Sikutaka tena pesa yake.
Mashaka akanishika mkono.
“Yaani umekuja huku Dar ku…”
“Hebu niache!”
Niliukutua mkono wake kisha nikamtandika kibao. Nikaenda kwenye
mlango nikaufungua na kutoka. Kwa kujua kuwa angeweza kunifuata na kwa aibu
niliyoipata, nilitoka mbio.
Nilipotoka hapo gesti niliendelea kwenda mbio kuvuka barabara bila
kujua kuwa kulikuwa na gari inakuja. Hafla nikashitukia nikipigwa kikumbo. Ninachokumbuka
ni kuwa gari hilo
lilinigonga likaniburuza na kunitumbukiza kwenye mfereji uliokuwa kando
ya barabara. Fahamu zikanipotea hapo hapo.
Sikujielewa tena.
Nilipokuja kuzinduka ilikuwa ni siku ya pili yake. Nilijikuta
nimelazwa kwenye chumba cha hospitali ya Muhimbili. Kitu cha kwanza kunitambulisha
kuwa nilikuwa hospitalini ni ile harufu ya dawa niliyoisikia.
Baada ya kuzinduka, mara moja niligundua hitilafu katika mwili wangu.
Jicho langu la upande wa kushoto lilifungwa bendeji wakati jicho la kulia
halikuweza kuona sawasawa na lilikuwa linakereketa na kuniuma.
Hata hivyo nilijikuta na bendeji katika kila sehemu ya mwili
wangu. Kwanza sikujua nilikuwa nimefanya
nini.Lakini wakati najiuliza ‘kulikoni?’ ndipo kumbukumbu zilipoanza kunijia.
Nikalikumbuka lile tukio la kumkimbia Mashaka mdogo wake Ibrahim
kwenye chumba cha gesti. Nilipotoka nje ya gesti kulikuwa na gari linakuja.
Gari hilo
lilinigonga wakati ninavuka barabara.
Hapo ndipo nilipojua sababu ya kuwa pale hospitali. Nikajaribu
kujiinua pale kitandani ili nikae lakini nilishindwa. Mkono wangu mmoja ulikuwa
umewekewa mpira wa damu na mwili wangu ulikuwa kama
uliokufa ganzi.
Nikapata hisia kwamba mguu wangu mmoja haukuwepo. Nikatumia mkono
wangu mmoja kujifunua shuka niliyokuwa nimefunikwa kisha nikainua kichwa na
kujiangalia. Nikaona mguu wangu wa kulia ulikuwa umekatwa!
Nikapiga yowe na kuzirai hapohapo!
Sikuweza kujua nilipotewa na fahamu kwa muda gani baada ya kuzirai
lakini nilipozinduka nilimuona daktari akinipima mapigo ya moyo.
Kadhalika nyuma ya daktari palikuwa na polisi wa usalama
barabarani ambaye alikuwa amesimama akiniangalia.Baada ya daktari kunipima
mapigo ya moyo aliniuliza.
"Unajisikiaje?"
"Sijisikii vizuri" nikamjibu kwa sauti dhaifu.
"Ni sehemu gani unasikia maumivu?"
"Kwenye miguu" nilimjibu lakini ukweli ni kwamba maumivu
zaidi niliyoyasikia ni ya uchungu wa moyo wangu.
"Mguu upi huo, ni huu mzima au uliokatwa?"
Swali hilo
lilinizidishia uchungu. Sikuweza kumjibu. Nikanyamaza kimya.
"Kama ni huo uliokatwa bado
una kidonda. Utaendelea kupata nafuu kadri kidonda kitakavyo kauka" Daktari
akaniambia.
"Kwanini nimekatwa mguu wangu?" nikamuuliza daktari huyo
kama vile aliukata kwa makusudi.
"Ulivunjika vibaya. Kwa kweli usingiweza kuungika hata
kidogo"
Nikahisi machozi yakinitiririka kwenye jicho langu moja.
"Usisikitike sana.
Shukuru kwamba uko hai. Ajali iliyokukuta ilikuwa ni moja ya ajali mbaya sana".
Nikawa nafuta machozi kwa mkono wangu.
"Nilitaka kukueleza kuhusu macho yako. Macho yako yameingia
vipande vya vioo. Jicho lako moja limeharibika kabisa, haliwezi kuona. Na hilo moja litakuwa linaona
kwa tabu kwa wiki zisizo zaidi nne” Daktari huyo akaniambia na kuongeza.
“Kuna kipande kidogo cha kioo kimeingia kwa pembeni. Sisi hatuna
uwezo wa kukitoa. Utawafahamisha ndugu zako watakapo kuja kukuangalia kwamba
unahitajika kupelekwa India
ili ukafanyiwe oparesheni ya kukutoa kabla hakijaharibu mboni ya jicho
lako"
Hapo nilishituka sana.
"Kumbe hili jicho lililofungwa limeharibika kabisa na hili
jingine mpaka lipelekwe India!"
"Ndiyo"
"Hizo pesa za kupelekwa India anatoa nani?"
nikamuuliza.
"Inabidi watoe ndugu zako"
"Ni kiasi gani?"
"Kwa pesa zetu unahitajika uwe na milioni nane. Hizo
zinahusisha usafiri wako wewe na mtu atakae kupeleka kwenda na kurudi pamoja na
gharama ya matibabu"
"Lakini mimi sina ndugu hapa Dar"
"Kwani unatokea mkoa gani?"
"Natokea Tanga"
"Utawasiliana na ndugu zako waliyoko Tanga"
Nikaguna.
"Hata huko Tanga sina ndugu mwenye pesa hizo"
"Sasa sijui tutafanyaje kwa sababu operesheni yako inahitajika
ifanyike ndani ya wiki nne. Wiki nne zikipita jicho lako litaharibika kabisa. Hutaweza
kuona tena"
Maneno hayo ya daktari yalinifanya niangue kilio. Daktari
akanibembeleza lakini nikawa simsikilizi tena. Mwisho akaniambia.
"Kuna askari hapa wa usalama barabarani,anataka kuzungumza na
wewe"
Nikamtazama yule askari. Daktari akamwaambia.
"Unaweza kuzungumza naye"
Daktari akaondoka na kutuacha.
Yule polisi alinisogelea pale kitandani akaniambia.
"Nyamaza dada yangu ili tuweze kuzungumza"
Nikajifuta machozi yangu kisha nikamtazama.
"Unaitwa nani?" akaniuliza.
Nikamtajia jina langu. Akaandika kwenye jalada alilokuwa
amelishika.
"Una umri gani?" akaniuliza tena
Nikamjibu.
"Umwenyeji wa wapi?"
"Tanga"
"Unaishi wapi hapa Dar?"
"Kwa hapa Dar nilikuwa ninaishi Sinza"
"Umfanyakazi au ni mama wa nyumbani?"
"Ni mama wa nyumbani"
"Una mume?"
"Ndiyo lakini yuko Tanga"
"Anaitwa nani?"
Nikamtajia jina la mume wangu Ibrahim.
"Tangu umeletwa hapa hospitali alishafika kukuangalia?"
"Bado"
"Lakini anayo taarifa kwamba umepata ajali?"
"Hana taarifa"
"Kwanini?"
"Hakukuwa na mtu wa kumuarifu. Hapa Dar mimi ni
mgeni,nilikuja mara moja tu ndiyo nikapata ajali. Natamani sana niwasiliane naye lakini simu yangu
iliibiwa"
"Namba yake unaikumbuka?"
"Ndiyo ninaikumbuka"
Polisi huyo alitoa simu yake na kuniambia.
ITAENDELEA hapahapa Usikose uhondo huu
No comments:
Post a Comment