HADITHI 31
YAMENIKUTA SALMA MIE
ILIPOISHIA
Hapo ndipo tulipoelezwa na polisi hao kwamba Chinga alikuwa
jambazi na kwamba yeye na wenzake watatu walikwenda kuvunja duka moja pale
Sinza lakini tayari walikuwa wamewekewa mtego na polisi. Wakavamiwa na kuanza
kutupiana risasi na polisi. Chinga akapigwa risasi ya bega na kukimbia.Wenzake
wawili waliuawa na mmoja alikimbia na gari walilokuwa nalo.
Lo! Sikujua,kumbe Chinga ni jambazi? Nikawaza.
Ni kwa sababu tu ya tamaa yangu ya kupenda pesa sasa nimejiingiza
katika matatizo yasiyonihusu na nisiyo yajua.
Baada ya polisi kutupa maelezo yaliyoonyesha kuwa Chinga
alikuwa ni jambazi na alipigwa risasi wakati yeye na wenzazke
walipojaribu kuwashambulia polisi, Chinga alibebwa juu juu
na kupakiwa ndani ya gari ya polisi.
Vicky aliyekutwa na ille bastola mkononi aliulizwa alikuwa
akihusianaje na Chinga, akajibu kuwa alikuwa mume wake.Yeye naye akakamatwa..Mimi
nilipoulizwa nilieleza kuwa nilikuwa mtumishi wa ndani. Jibu hilo ndilo lililonisalimisha nikaachwa nibaki
na nyumba.Lakini nilitakiwa kufika kituo cha polisi cha Sinza saa mbili asubuhi
na nimuulizie Inspekta Amour.
SASA ENDELEA
Polisi hao walipoondoka na Chinga pamoja na Vicky niliingia ndani
nikaketi sebuleni na kujiwazia. Kwa kweli nilishukuru kuwa sikuwa mke wa
Chinga.
Kumbe Chinga alikuwa jambazi!. sikuwa nikijua kuwa alikuwa
akitudanganya kujidadai alikuwa mfanyabiashara anayesafiri nje ya nchi.Uongo
wake ndio ulionifanya nimuache mume wangu na nimfuate yeye hapa Dar.
Hapo ndipo nilipogundua kuwa vile vitu ambavyo amekuwa akivileta
na kuviweka humu ndani ni mali
za wizi. Na pia vile anavyotoka usiku nakurudi siku ya pili anakuwa katika
shughuli za ujambazi.
Ingawa nilisalimika kukamatwa lakini kwa upande wangu hilo halikuwa tatizo la
pekee. Tatizo ni maisha yangu kuparaganyika. Sasa hata ile chembe ya matumaini
ya kupata maisha katika Jiji hilo
sikuwa nayo tena kwani mwanaume niliyemtegemea kuwa atanihamishia Masaki ni
jambazi na ameshakamatwa.
Sikujua ni kwanini nilijiingiza katika matatizo makubwa kiasi
kile. Hivi ilikuwa ni kwa sababu ya ujinga, tamaa au nini?.
Inakuwaje anijie mtu ambaye simjui anitongoze kisha nimkubalie
kirahisi vile tena si kumkubalia kuvunja amri ya sita tu bali kumuacha mume
wangu na kuondoka naye kwa ahadi ya kwenda kunioa. Ulikuwa ujinga wa kiasi gani
niliokuwa nao! Nilikuwa nikijiambia mara kadhaa.
Nikiwa bado nimeketi hapo sebuleni nikiwaza nikasikia gari
likisimama huko nje na kisha mlango wa mbele ukagongwa. Nikanyamaza kimya.
Mlango ulipoendelea kugongwa nikauliza.
''Nani anayegonga?''
''Ni sisi polisi tumerudi tena. Fungua mlango'' Sauti ikasikika
kutoka nje.
Moyo ukanipasuka. Nikanyanyuka na kwenda kufungua mlango.
Walikuwa ni polisi walewale. Walirudi na Vicky. Wakaingia ndani.
''Tumekuja kupekua humu ndani.Tunashuku kwamba kunaweza kuwa na
vitu vya wizi na wewe utakuwa shahidi wa kila kitu tutakachokikuta'' Polisi
mmoja akaniambia.
Vicky akatakiwa kuwafungulia polisi hao kila chumba ili wakipekue.
Kila chumba kikapekuliwa. Lakini hakukuwa na kitu chochote ambacho polisi hao
walikikamata. Walipomaliza zoezi hilo
waliondoka pamoja na Vicky.
Asubuhi kulipokucha nilioga nikavaa kisha nikatoka kwenda kituo
cha polisi nilikoambiwa nifike saa mbili asubuhi.
Nilipofika katika kituo hicho nilikwenda kaunta nikajitambulisha
na kumuulizia Inspekta Amour kama
nilivyoagizwa na wale polisi usiku uliopita.
Polisi mmoja akanipeleka katika ofisi moja ambapo nilikutanishwa
na mmoja wa polisi waliokuja nyumbani usiku. Alikuwa amenisahau kidogo lakini
baada ya kujitambulisha kwake akanikumbuka.
Alichukua karatasi na kuiweka juu ya meza kisha akaniuliza jina
langu, nikamjibu.
''Una umri gani?'' Ispekta huyo akaendelea kuniuliza
''Miaka 27''
''Una mume?''
''Sina mume'' nikadanganya
''Una uhusiano gani na John?''
''Sina uhusiano naye isipokuwa aliniajiri kama
mtumishi wa ndani''
''Ni muda gani sasa tangu umekuwa mtumishi wake?''
''Nina muda wa miezi sita hivi''
''Je ulikuwa ukijua kuwa alikuwa anafanya kazi gani?''
''Kazi yake ninayoijua mimi ni ya biashara''
''Biashara gani?''
''Alikuwa akisema anasafiri nje ya nchi na kuleta bidhaa''
''Uliwahi kuziona bidhaa hizo?''
''Niliwahi kuona akileta nyumbani friji, televisheni, majiko na
vitu vingine''
''Halafu anavipeleka wapi?''
''Baadaye analeta gari na kuviondoa.Mimi nilikuwa nikijua
anavipeleka kwa wateja wake''
''Jana usiku alipotoa bastaola na kumpa mke wake wakati sisi
tumetokea, wewe uliona?''
''Ndiyo, niliona''
''Inaelekea mke wake alikuwa anajua mume wake alikuwa ni jambazi''
''Sijui. Sina hakika''
Wakati wote akiniuliza maswali ispekta huyo alikuwa anaandika
majibu yangu kwenye ile karatasi aliyoiweka juu ya meza.
''Madhumuni yetu ya kukuita hapa kwanza tulitaka kuandikisha
maelezo yako na pili kukueleza kuwa tumegundua kuwa John ni jambazi sugu
aliyekuwa anatafutwa na polisi kwa muda mrefu. John amehusika na matukio mengi
ya ujambazi hapa Jijini'' Ispekta huyo akaniambia na kuongeza
''Katika moja ya matukio ya uporaji aliyoyafanya ni uporaji wa
gari aina ya Rav 4 ambayo jana usiku baada ya kumhoji akiwa hospitali ya
Muhimbili alikiri kuhusika na uporaji wa gari hiyo na akatuambia alilipeleka
kwao Tanga kulificha.Usiku huo huo tuliwasiliana na polisi wenzetu waliopo
Tanga walifuatilie gari hilo huko
Kisosora alikolificha. Na leo asubuhi wametufahamisha kuwa wamelikamata
nyumbani kwa baba yake''
Nikakumbuka kuwa ni kweli Chinga alipokuja Tanga alikuwa na Rav 4
akadai kuwa ni mali
yake. Lakini tulipokuja Dar aliliacha gari hilo tukapanda basi. Kumbe lilikuwa gari la
wizi.
''Sasa tunasubiri tukamilishe upelelezi wetu ili afikishwe
mahakamani yeye na mke wake'' Ispekta huyo akaendelea kuniambia.
Baada ya hapo aliniruhusu niende zangu. Nikaondoka kituoni hapo
mwili ukiwa wangu umetota jasho.
Wanaume kweli ni walaghai na kama
sisi wanawake hatutakuwa waangalifu tutaingizwa katika matatizo siku zote.
Kilichoninusuru mimi kukamatwa ni kuonekana ni mtumishi wa John, vinginevyo na
mimi ningekuwa nimetiwa ndani.
Niliporudi nyumbani niliketi sebuleni na kuwaza nifanye nini.
Chinga niliyekuwa nikimtegemea hapa Dar ameshakamatwa na sikutarajia kuwa
atatoka jela leo. Huenda akafia huko huko. Sasa maisha yangu yatakuwaje?
Ghafra nikasikia mlango unabishwa. Nikainuka na kwenda kuufungua.
Nikamuona mtu mmoja aliyewasili na gari. Akanisalimia kisha akaingia ndani.
Akasimama sebuleni na kunitambulisha kuwa yeye ndiye mwenye nyumba
ile ambayo alikuwa amempangisha Chinga. Akaniambia kuwa amepata habari kuwa
Chinga ni jambazi na amekamatwa na polisi. Hivyo alikuja kufunga nyumba yake.
''Kwa vile ninamdai kodi ya miaka miwili itabidi nizuie kila
kitu kilichomo humu ndani!'' akaniambia
Kumbe ile nyumba pia Chinga haikuwa yake!
Baada ya yule mtu kunieleza hayo nilipigwa na butwaa nikawa sina
la kumjibu.Alipoona nimeduwaa akaniuliza.
“Kwani wewe ni nani wake?”
“Mimi ni mtumishi wake wa ndani” nikamjibu. Jina la utumishi
nilikuwa silitaki lakini sasa nililing’ang’ania kwa kujua ndilo litakalo
ninasua na matatizo ya Chinga.
“Sasa utalazimika uondoke. Kama
una madai yoyote itabidi uyapeleke polisi.
“Unaniambia niondoke, niende wapi?” nikamuuliza.
“Utajua mwenyewe pa kwenda. Hapo umekuja kwa hicho kibarua na
kibarua kimeshaota nyasi.Tajiri yako amekamatwa na si wa kutoka leo, sasa
utakaa hapa ungoje nini?”
Sikuwa na la kumjibu, nikabaki kimya nikiwaza.
“Fungasha kila kitu chako ninataka kufunga nyumba yangu” yule mtu
akaniambia sasa kwa kusisitizia.
“Naomba unisubirishe kidogo niende kwa jirani nikamueleza matatizo
yangu”
“Ukichelewa utakuta nimeshafunga nyumba” akaniambia.
“Sitachelewa”
Nilitoka nikaenda nyumba ya tatu kutoka ile yetu ambapo kulikuwa
na mashoga zangu wawili waliokuwa wakiishi humo. Mashoga hao Mariamu na
Sikuzani tulizoeana hapo hapo mtaani. Mara kwa mara tulikuwa nikitembeleana na
kupiga stori.
ITAENDELEA Usikose hapahapa tangakumekuchablog
No comments:
Post a Comment