Sunday, November 27, 2016

YAMENIKUTA SALMA MIE SEHEMU YA 34

HADITHI
 
YAMENIKUTA SALAMA MIE
 
ILIPOISHIA
 
"Umwenyeji wa wapi?"
 
"Tanga"
 
"Unaishi wapi hapa Dar?"
 
"Kwa hapa Dar nilikuwa ninaishi Sinza"
 
"Umfanyakazi au ni mama wa nyumbani?"
 
"Ni mama wa nyumbani"
 
"Una mume?"
 
"Ndiyo lakini yuko Tanga"
 
"Anaitwa nani?"
 
Nikamtajia jina la mume wangu Ibrahim.
 
"Tangu umeletwa hapa hospitali alishafika kukuangalia?"
 
"Bado"
 
"Lakini anayo taarifa kwamba umepata ajali?"
 
"Hana taarifa"
 
"Kwanini?"
 
"Hakukuwa na mtu wa kumuarifu. Hapa Dar mimi ni mgeni,nilikuja mara moja tu ndiyo nikapata ajali. Natamani sana niwasiliane naye lakini simu yangu iliibiwa"
 
"Namba yake unaikumbuka?"
 
"Ndiyo ninaikumbuka"
 
Polisi huyo alitoa simu yake na kuniambia. 
 
SASA ENDELEA
 
"Nitakusaidia uwasiliane naye kwa sababu kuna suala la wewe kupelekwa India. Nitajie namba yake"
 
Nikamtajia.
 
Polisi huyo akaipiga namba hiyo kisha akaiweka simu sikioni. Baada ya muda kidogo akauliza. 
 
"Wewe ni Bw Ibrahim?"
 
Sikuweza kusikia alichojibiwa. Akaendelea kusema. 
 
"Sawa. Sasa bwana kuna tuikio limetokea hapa Dar. Mke wako Bi Salma alipata ajali ya gari jana asubuhi na amelazwa hapa katika hospitali ya Muhimbili. Sijui kama unataarifa hizo?"
 
Wakati polisi huyo akizungumza hivyo moyo wangu ulikuwa ukinienda mbio. Sijui Ibrahim alimjibu nini lakini nilimsikia yule polisi akimtajia wodi niliyokuwepo kisha akasikiliza kidogo kabla ya kukata simu.
 
"Amesemaje?" nikamuuliza yule polisi kwa haraka.
 
"Kumbe na yeye yuko hapa hapa Muhimbili.Amesema alikuja wiki moja iliyopita kufanyiwa operesheni ya macho yake.Leo ndiyo amepewa ruhusa. Atakuja hapa hapa kukuona"
 
"Kumbe yuko hapa hapa Muhimbili?" nikamuuliza yule polisi.
 
"Inaelekea huna mawasiliano na mume wako. Kwani hujui kuwa mume wako yuko hapa?"
 
Nikatunga uongo hapohapo. 
 
"Tatizo ni simu yangu iliibiwa"
 
"Basi sasa mtakutana hapa hapa"
 
"Amekwambia hivi sasa anaona?"
 
"Kwani alikuwa haoni?"
 
"Alikuwa haoni kabisa"
 
“Natumaini hivi sasa atakuwa anaona kwa sababu amesema anakuja kukuona"
 
"Na aje, nataka nionane naye"
 
Baada ya kupita nusu saa hivi, mlango wa chumba nilichokuwamo ulifunguliwa..Kwanza aliingia yule daktari aliyekuwa ametoka kisha akaingia mtu mwingine. Nikamkazia jicho langu moja lililokuwa halioni sawasawa na nikagundua alikuwa Ibrahim mume wangu.
 
Safari hii alikuwa amevaa miwani ya macho yenye vioo vyeupe
badala ya ile ya jua. Macho yake niliweza kuyaona. Sasa yalikuwa yanaona. Nikasadiki kuwa Ibrahim alikuwa amepona.
 
"Msichana uliyemuulizia ni huyu hapa, je unamfahamu?" daktari huyo aliyeingia akamuuliza Ibrahim.
 
Ibrahim alisogea karibu na kitanda na kuniangalia vizuri. Nikamuona akitikisa kichwa.
 
"Simfahamu" akamwaambia yule daktari.
 
Jibu lake hilo lilinishitua.
 
"Mume wangu Ibrahim, mimi ni Salma mke wako nimepata ajali ya gari. Nimekatwa mguu wangu na jicho langu moja limeharibika." nikamwaambia kwa mkazo ili aweze kunitambua.
 
"Unasema ulipata ajali?" akaniuliza.
 
"Ndiyo mume wangu nilipata ajali" nilimjibu kwa unyonge na kwa nidhamu"
 
"Jicho limeharibika na mguu mmoja umekatwa" Ibrahim aliendelea kusema huku akiniangalia kwenye kile kigutu changu kilichokuwa kimefungwa bendeji.
 
"Mguu wake ulivunjika vibaya. Kwa kweli mfupa ulisagika kabisa.Tukaona tuuondoe"daktari akamwaambia.
 
Hata hivyo Ibrahim hakuonyesha kushituka wala kutaharuki tangu aliponiona. Alikuwa kama anamuangalia mtu asiyemjua kabisa.
 
"Pole sana" akaniambia na kuongeza. 
 
"Nashindwa kukukumbuka. Ni kweli nilikuwa na mke anaitwa Salma lakini alinitoroka miezi mingi iliyopita.Hivisasa sina mke."Ibrahim akasema.
 
Maneno yake yakaniacha njia panda.
 
"Una maana si yeye?" yule polisi akamuuliza.
 
"Si mke wangu.Kwanza ninashangaa akiniita mume wake"
 
"Hebu tueleze vizuri. Umesema mke wako alikutoroka miezi mingi iliyopita?"daktari akamuuliza.
 
“Nilipopata upofu mke wangu alinitoroka na mwanaume baada ya kunifanyia visa vingi. Nimetoa taarifa polisi na kwa wazazi wake. Wote wanafahamu kuwa sina mke. Sasa nashangaa akijitokea mwanamke akisema ni mke wangu. Si kweli. Mimi simjui."
 
Ibrahim alivyomaliza kusema nikamuona anageuka ili aondoke, nikamshika mkono.
 
"Mume wangu najua umesema hivyo kwa sababu ya chuki. Naomba unisamehe niliyokukosea, niko chini ya miguu yako Ibrahim" nikamwaambia huku machozi yakinitoka.
 
"Sitakusamehe na jina hilo 'mume wangu' ulikome kabisa.Mimi si mume wako.Kama unakumbuka nilikwambia usimcheke kilema, binadamu haishi kuumbwa. Yaliyonipata mimi na wewe yanaweza kukupata. Sasa umeyaona?"
 
"Ni kweli mume wangu uliniambia" nilisema huku nikilia kwa sauti. 
 
"Naomba unisamehe. Ni ibilisi tu aliyenipitia"
 
"Kama ni ibilisi amekupitia, sasa mwambie asikuwache hapa hospitali, akuhudumiye na utakapo toka akupeleke nyumbani kwake" Ibrahim akaniambaia kijeuri.
 
"Lakini jamani pamoja na makosa mliyofanyiana, kiubinaadamu bwana Ibrahim ulipaswa umsikilize huyu bibi kutokana na matatizo yaliyomtokea. Ukimuacha hapa hospitali, kwa kweli atateseka” Yule daktari akamwambia Ibrahim.
 
Ibrahim akawa anamtazama.
 
Daktari huyo akaendelea kumueleza.
 
 Istoshe jicho lake moja limeshaharibika, lile jingine limeingia kipande cha kioo. Oparesheni yake inahitaji zaidi ya shilingi milioni kumi nchini India. Anahitaji msaada. Kama jicho hili litaachwa kwa wiki nne nalo litaharibika. Atakuwa haoni kabisa"
 
"Umezungumza suala la msingi dokta" polisi aliyekuwepo hapo akamuunga mkono na kuendelea kueleza. 
 
"Bwana Ibrahim pamoja na matatizo unayoyazungumza bado una dhima na mke wako. Ulipaswa kwanza kusahau yaliyopita. Msaada wako ni muhimu sana. Baada ya hapo mtakuja kuyazungumza matatizo yenu".
 
Nilidhani kwamba Ibrahim angelegea na kuyasikiliza yale maneno aliyokuwa anaambiwa lakini alitikisa kichwa chake kwa hasira.
 
"Kutokana na vitendo alivyonitendea huyu bibi, sina dhima naye. Huyo aliyemtorosha huko Tanga akamleta hapa Dar ndiye atakayebeba dhima yake. Amhudumie mpaka apone lakini si mimi Ibrahim. Kwaherini"
 
Ibrahim akageuka ili atoke.
 
"Ibrahim usiniache!" nikampigia kelele.
 
Ibrahim hakusita wala kunisikiliza. Aliendelea kwenda zake
 
"Ibrahim....Ibrahim....nisemehe mume wangu!" nikamwambia kwa kelele.
 
Ibrahim alifungua mlango akatoka.
 
Daktari alitikisa kichwa kusikitika kisha akaniangalia
 
"Salma unakabiliwa na wakati mgumu sana. Mume wako ameshakukataa, kumbe mlikuwa na matatizo yenu. Sasa sijui itakuwaje!" daktari alisema kisha na yeye akatoka.
 
Mimi nilikuwa ninalia. Nililia kwa sababu nilijua kuwa nimeshakuwa mlemavu wa miguu na macho na nisingepata msaada wowote kwingine.
 
Yule polisi aliniangalia, mwisho wake nilimuona na yeye akifungua mlango na kutoka. Nikabaki peke yangu.
 
Kwa kweli majuto huja kinyume baada ya kwisha kitendo. Sasa nilikuwa ninajuta. Nilijuta kwa kudanganyika. Kwanza nilidanganywa na Rita mpaka nikakubali kwenda kwa mganga aliyenipa dawa zilizoharibu macho ya mume wangu jambo ambalo lilisababisha maisha yetu kuharibika.
 
ITAENDELEA






No comments:

Post a Comment