YAMENIKUTA SALAMA MIE
ILIPOISHIA
Nikajilaumu kwa kuchukua maamuzi ya kumkimbia mume wangu na
kumuamini Chinga bila kutumia busara. Kwa kweli nilifanya kosa kubwa.
Lakini si hilo
tu. Kulikuwa na tatizo jingine baya zaidi la kuambukizwa virusi vya ukimwi. Kama
Chinga ameweza kumuambukiza mke wake,na mimi atakuwa ameshaniambukiza. Kilichobaki
kwangu ni kusubiri siku virusi vitakavyoanza kufanya kazi yake.
Sikuweza kujua wakati huo nitakuwa wapi na sikuweza kujua nitahudumiwa
na nani?.Lakini yote niliyataka mwenyewe.
Nilikuwa nikiishi vizuri na mume wangu,nikapata ushawishi wa
kwenda kumfanyia dawa za mapenzi kwa tamaa ya kupata pesa. Dawa zikampofua
macho mume wangu, hali ya maisha ikazorota mpaka ikabidi nimkimbie. Na huku
nilikokimbilia ninakutana na makubwa zaidi kuliko yale niliyoyakimbia.
Wakati nikiwa katika lindi hilo
la mawazo, nilisikia mlango wa chumba ukigongwa kwa kishindo. Nikajua ni yule
msichana. Nikanyanyuka na kwenda kuufungua.
“Ulikuwa umelala?” akaniuliza.
“Nimejivyoosha tu, sijalala usingizi” nikamjibu.
“Mbona hukuniuliza nitakula nini wakati mimi ni mgeni nimekuja, unaingia
ndani unalala? Kama ninataka kitu nimtume
nani?.Au huyo John hakukueleza kuwa mimi ni mke wake?”
Maneno ya yule msichana yakanitibua. Lakini nilivuta subira.
SASA ENDELEA
“Sasa maneno mengi ya nini dada? Kwani wewe ulikuwa wataka nini?”
nikamuuliza.
“Nataka chakula”
“Zungumza na huyo John, mimi sina chakula”
“Nina pesa yangu, nataka utoke ukaninunulie chipsi”
Nikaguna. Sikujua kuwa niliguna kwa nguvu mpaka akanisikia.
“Mbona unaguna? Wewe ni mtumishi wa John kweli au ulikuwa ni
mwanamke wake?”akaniuliza.
“Umenionaje?” na mimi nikamuuliza kijeuri.
“Sikuelewielewi, mtumishi gani unatumwa unaguna, au mpaka akutume
John?”
“Wewe nipe hiyo pesa yako nikakununulie hizo chipsi, hayo mengine
tumsubiri huyo John atakapo kuja”
Bila shaka majibu yangu yalimtia hofu akanyamaza. Alitoa noti ya
shilingi elfu tano akanipa.
“Kaninunulie chipsi kavu na nusu kuku” akaniambia.
Nilichukua ile elfu tano yake nikatoka huku nikiwa na
mawazo.Niliona kama nitamkatalia anaweza
kumshauri Chinga anifukuze na mimi sikuwa na pa kwenda. Nilitaka nibaki pale
nyumbani nijue Chinga atachukua uamuzi gani.
Nilikwenda katika bar moja iliyokuwa jirani ambako palikuwa na
jamaa akiuza chipsi.
Nikanunua sahani moja ya chipsi kavu na nusu kuku.Niliandaliwa na
kutiliwa kwenye mfuko mdogo wa plastiki
Wakati ninarudi nilipitia dukani nikanunua vocha kwa ajili ya simu
yangu na kuijaza hapo hapo. Njia mzima nilikuwa nikimlaani Chinga kwa ulaghai
wake na huku nikijilaumu mimi mwenyewe kwa kuchukua uamuzi bila kufikiri.
Nilimkuta Vicky ameketi sebuleni akinisubiri.Alikuwa amevua nguo zake
na kuvaa khanga. Alionesha kuwa alikuwa anatoka kuoga.
“Niwekee kwenye meza” akaniambia kisha akaniuliza.
“Kuna soda kwenye friji?”
“Zipo” nikamjibu huku nikielekea kwenye meza. Ndani ya moyo wangu
nilimwaambia “Usijifarague dada, mimi ni mke mwenzako.Tunajaribu kukuzuga tu”
Pengine nilijisemea hivyo ili kujifariji na kujipa moyo kutokana
na kule kudhalilishwa na kufanywa kama mtumwa.
Nilimuwekea ule mfuko wa chipsi kwenye meza kisha nikaenda
kumtolea soda na kumuwekea.
Wakati ninaondoka aliniuliza.
“Wewe unakula nini?”
“Kula tu” nikamwaambia.
Akainuka na kwenda kwenye meza.
“Njoo tule” akaniambia wakati anaketi.
Sikumjibu. Nikaondoka na kuingia chumbani. Kabla sijakaa nikasikia
akiniita kwa sauti kali. Jina langu alikuwa halijui, aliniita “Wee
msichana hebu njoo”
Nikatoka na kumfuata, uso nikiwa nimeukunja.
“Wasemaje?” nikamuuliza.
“Hivi ni vitu gani ulivyoniletea?” akaniuliza huku akinionyesha
ule mfuko wa chipsi.
“Si chipsi na kuku, ama ulitaka nini?”
“Kuku gani! Sijui ni nyama ya nini?.Nyama hata haikukaushwa, ina damu
damu! Wewe unaweza kula nyama kama hii?”
Aliishika na kunionyesha.
Nilitafuta neno la kumjibu nikalikosa.Nikabaki kumtazama.
“Nakuuliza wewe unaweza kula nyama hii?” akaniuliza tena.
Nilivuta subira. Sikutaka kulumbana naye, nikamwaambia .
“Bahati mbaya, sikuiona”
“Hukuiona kwani huna macho au umefanya kusudi,maana tangu nimekuja
naona umechukia?”
Sikumjibu nikaondoka. Nilipoingia chumbani sikutoka tena.
Usiku kucha sikupata usingizi kwa mawazo. Mawazo yaliponizidi
nilijaribu kumpigia Chinga lakini simu yake ikawa haipatikani. Nikaiacha simu
na kuendelea kutafuta usingizi.
Usingizi niliupata kwa tabu. Nilipolala tu nikaota ndoto niko na Rita.
Hafla ikanyesha mvua na hapakuwa na mahali pa kujisitiri. Tukawa tunatota. Mvua
ikawa kali, maji yakajaa, nito ikawa inafurika. Rita akaniambia.
“Tukimbie, maji yanakuja!”
Wakati nainua mguu nikateleza na kuanguka chini, Rita akakimbia
peke yake na kuniacha. Maji yakawa yananifuata mimi. Karibu yangu kulikuwa na
jiwe kubwa, nikapanda juu ya jiwe hilo.
Maji yakazidi kujaa mpaka yakanifikia kule juu. Nikaisikia sauti ya Rita
aliyekuwa amesimama juu ya mlima akinicheka.
Ndoto yangu ilikatishwa na kishindo cha kugongwa kwa mlango. Nikazinduka
na kufumbua macho. Kulikuwa kumeshakucha. Nikaondoka kitandani na kuvaa khanga
kisha nikafungua mlango.
Nilimkuta Vicky amesimama mbele ya mlango.
“Mtumishim gani unalala hadi saa mbili, hii nyumba haijafanyiwa
usafi?” akaniuliza kwa kufoka.
“Dada mbaona unanijia juu, kwani wewe ndiye uliyenileta hapa?. Kwanza mimi sikujui, huwezi kunipa amri zako!” na mimi
nikamjibu kwa kufoka vilevile.
Akanyea “Yaani wewe huwezi kufanyakazi za nyumbani mpaka
uamrishwe na John!” akaniuliza lakini sasa sauti yake haikuwa na nguvu.
“Siyo hivyo, amri zako zimezidi.Mimi mwenyewe ninajua majukumu
yangu, nitafanya usafi kwa wakati wangu”
“Basi dada nenda kalale. Hii nyumba itakuwa chafu mpaka John
atakapo kuja”
“Na ikae, kama usingenikuta mimi
ungemuamrisha nani?”
“Mimi nimeshajua wewe si mtumishi wa John, usingeniletea jeuri
namna hii. Na John akija unaondoka hapa nyumbani!”
“Utajiju…!” na mimi nikamwambia na kuufunga mlango kwa kubwata.
“Utajiju wewe!” Nikamsikia akinijibu huku akielekea uani.
Nilikaa kitandani nikawaza
kisha nikatoka kwenda msalani. Nilipotoka msalani nikashika fagio kwa hiari
yangu na kuanza kufagia.Vicky alikuwa chumbani. Alitoka baadaye na kunikuta
nikifagia sebuleni. Alinitupia jicho tu na kuniminyia midomo bila kunisema
chochote.
Alikuwa amevaa nguo za kutokea na mkoba wake ulikuwa kwapani. Alipofika
pale sebuleni alitoa simu yake na kuipiga. Simu ilipopokelewa nilimsikia
akisema.
“Kama nilivyokwambia, ndiyo
natoka. Hapo jioni utakaporudi utanipitia kwa dada, sawa?”
Akaisikiliza kisha akaitikia na kukata simu.Aliitia simu yake
kwenye mkoba akatoka.
Alipotoka nilikwenda kumchungulia kwa dirishani nikamuona
anaelekea kwenye kituo cha daladala. Nikaendelea kumtazama mpaka alipokata
kona.
Bila shaka walishapigiana simu na Chinga tangu akiwa chumbani. Na
alimwaambia kuwa nimemjibu jeuri ndipo akapanga safari ya kwenda kwa dada yake.
Nikawaza.
Niliacha kufagia nikaenda chumbani na kuchukua simu yangu. Na mimi
nikampigia Chinga. Nilipiga kwa muda mrefu lakini Chinga hakupokea simu yangu. Jambo
hilo lilinihuzunisha sana. Ikabidi nijiulize tena iwapo kweli
Chinga bado alikuwa na dhamiri ya kuendelea na mimi.
Kutokana na dukuduku lililonipata sikutoka tena kuendelea kufanya
usafi wa nyumba. Nikajilaza kitandani na kuendelea kuwaza.
Sikutoka mle chumbani hadi ilipotimu saa sita mchana. Nilikwenda
kuchukua soda kwenye friji nikanywa na keki nilizokuwa nimeziweka jikoni kisha
nikaenda kuoga.
Niliporudi nilimpigia simu tena Chinga lakini sasa simu yake ikawa
haipatikani.Nilizidi kuumia moyo wangu na kujuta kumkubali Chinga.
ITAENDELEA kesho hapa hapa usikose nini kitatokea
No comments:
Post a Comment