HADITHI
YAMENIKUTA SAMLA MIE
ILIPOISHIA
Baada ya yule mtu kunieleza hayo nilipigwa na butwaa nikawa sina
la kumjibu.Alipoona nimeduwaa akaniuliza.
“Kwani wewe ni nani wake?”
“Mimi ni mtumishi wake wa ndani” nikamjibu. Jina la utumishi
nilikuwa silitaki lakini sasa nililing’ang’ania kwa kujua ndilo litakalo
ninasua na matatizo ya Chinga.
“Sasa utalazimika uondoke. Kama
una madai yoyote itabidi uyapeleke polisi.
“Unaniambia niondoke, niende wapi?” nikamuuliza.
“Utajua mwenyewe pa kwenda. Hapo umekuja kwa hicho kibarua na
kibarua kimeshaota nyasi.Tajiri yako amekamatwa na si wa kutoka leo, sasa
utakaa hapa ungoje nini?”
Sikuwa na la kumjibu, nikabaki kimya nikiwaza.
“Fungasha kila kitu chako ninataka kufunga nyumba yangu” yule mtu
akaniambia sasa kwa kusisitizia.
“Naomba unisubirishe kidogo niende kwa jirani nikamueleza matatizo
yangu”
“Ukichelewa utakuta nimeshafunga nyumba” akaniambia.
“Sitachelewa”
Nilitoka nikaenda nyumba ya tatu kutoka ile yetu ambapo kulikuwa
na mashoga zangu wawili waliokuwa wakiishi humo. Mashoga hao Mariamu na
Sikuzani tulizoeana hapo hapo mtaani. Mara kwa mara tulikuwa nikitembeleana na
kupiga stori.
SASA ENDELEA
Nilipofika niliwakuta wamekaa barazani wakizungumza. Nikawaeleza
matatizo yaliotokea pale nyumbani kwetu. Nikawambia kwamba licha ya Chinga
kukamatwa, mwenye nyumba amenifuata kunitoa akitaka kufunga nyumba yake kwa
sababu anamdai Chinga kodi ya miaka miwili na pia hataki mpangaji ambae ni
jambazi.
“Sasa umechukua uamuzi gani?” Mariamu akaniuliza.
“Nichukue uamuzi gani shoga na mwenye nyumba anataka nyumba yake. Itabidi
nitoke na pakwenda sipajui. Sasa nilikuwa naomba nijihifadhi hapa kwenu kwa
siku mbili tatu ili nijue nitaenda wapi”
“Na vile vitu vilivyomo mle ndani utavipeleka wapi?” akaniuliza
Sikuzani.
“Mimi nitachukua vitu vyangu vidogovidogo tu.Vile nilivyovikuta
nitaviacha. Mwenye nyumba amesema atavizuia kwa sababu anadai kodi ya miaka
miwili”
Baada ya kunisikiliza kwa makini Mariamu akaniambia.
“Sasa shoga kama unavyotuona tuko wawili na chumba chetu ni
kimoja, kama utaweza kujibana humo humo chumbani kwa siku hizo tatu, karibu”
“Nitawashukuru mashoga zangu kwa msaada huo kwani mwenzenu
nimechanganyikiwa” nikawambia.
“Wala usichanganyikiwe shoga. Hali hiyo ni ya kawaida Jijini hapa.
Kila siku watu wanatimuliwa kwenye nyumba za watu.Wengine hutolewa nyumbo na
kuwekewa nje, hawajui pa kuvipeleka. Ni afadhali wewe umesitirika”
“Basi mashoga zangu ngojeni nikafungashe vyombo vyangu nivilete”
Nikarudi nyumbani na kuanza kukusanya nguo na vitu vyangu vingine,
nikavitia kwenye mabegi mawili. Begi moja lilikuwa langu mwenyewe na jingine
nililichukua mle ndani. Nikachukua ndoo tatu za plastiki. Mbili nilizijaza
vyombo vya kutumia kama vile sufuria, sahani, mabakuli,
vikombe na kadhalika. Ndoo moja nikaitia vitu vilivyokuwemo ndani ya friji.
Kwanza nikapeleka begi moja kisha nikarudia
jingine. Nilipomaliza mabegi, nilibeba zile ndoo. Nilitangulia kubeba ndoo mbili
kisha nikairudia ile moja.
Nilipomaliza nilimwaambia yule mtu aliyekuwa akinisubiria kuwa
nimeshaondosha vitu vyangu ingawa vingine nilivyochukua havikuwa vyangu bali
nilivichukua nikaanzie maisha huko mbele ya safari.
Yule mtu akafunga milango ya vyumba vyote.Nikatoka naye, akamalizia
kufunga mlango wa mbele kisha akaniaga na kuingia kwenye gari yake. Na mimi
nikaondoka kwenda kwa mashoga zangu.
Mambo ya Dar ni makubwa!.Wale mashoga zangu ni wasichana warembo
kweli kweli lakini nilipoingia chumbani mwao kuweka vyombo vyangu niliona
hawakuwa na kitanda. Walikuwa wanalala kwenye godoro lililowekwa chini na
kufungiwa chandarua. Humo chumbani mwao hamkuwa na chochote zaidi ya kimeza
kilichokuwa na vipodozi pamoja na kipande cha kioo kilichovunjika.
Zaidi ya hapo walikuwa na ndoo karibu nne zilizokuwa na maji na
madishi matatu, mawili yakiwa yamejaa vyombo. Nguo zao walikuwa wakiweka kwenye
mabegi, kila mmoja alikuwa na begi lake. Kwa kweli kile chumba kilikuwa kama geto.lakini nilishukuru kupata sitara kwani sikuwa
na pa kwenda.
Ingawa niliwaambia mashoga hao kuwa ningekaa hapo kwa siku mbili
tatu, ukweli ni kuwa sikujua nitaenda wapi baada ya siku hizo. Hapo ndipo
nilipoanza maisha kwa mashoga zangu hao. Habari ya Chinga nikaisahau kabisa. Kama
nikudanganywa nimeshadanganywa na kama ni
balaa limeshanikuta.Sikuwa na haja ya kufikiria tena yaliyopita.
Zile siku tatu nilizowaahidi wale mashoga zangu zikapita lakini
hakukuwa na aliyeniuliza.
Maisha yalikuwa tofauti sana.
Pale tulikuwa tunaishi kihuni. Wale wasichana tunakuwa pamoja mchana, tunapika
kwa kuchangia hela na tunakula pamoja. Ikifika usiku wenzangu wananiachia
chumba na tunakutana tena asubuhi.
Baada ya wiki mbili nikaanza kuishiwa hela ya kuchangia
chakula.Wenzangu walinisaidia kwa siku tatu. Siku ya nne wakaniambia watakapo
toka usiku nitoke nao.
Ilipofika usiku wakati wenzangu wakijipara na mimi
nikajipara.Tukatoka pamoja. Hawakuwa wakienda mbali.Tulizunguuka mtaa wa pili
ambako kulikuwa na baa na gesti humo humo.Tukaingia katika ile baa tukakaa
kwenye viti.
Jinsi wenzangu walivyokuwa wakisalimiana na wahudumu wa baa ile
walionekana kuwa ni wenyeji. Mara kwa mara wahudumu hao walikuwa wakiwauliza
Mariamu na Sikuzani.
“Mmetuletea mgeni?” na wao walijibu “Nishoga yetu
tunamtembeza tembeza”
Wakati tumeketi mashoga zangu wakaanza kunisomesha.Wakaniambia
hapo baa ndiyo mahali wanapopatia riziki zao kutoka kwa wanaume wanaotaka
huduma zao.
Nilivyowaelewa ni kwamba walikuwa wanajiuza. Hakukuwa na
aliyeniambia wamenileta hapa kwa ajili ya gani, ilikuwa ni akili kichwani
mwangu kwamba na mimi nijiunge nao.
Sikutaka kujivunga wala kushangaa kwa sababu kwa upande wangu maji
yalikuwa shingoni. Sikuwa na namna ya kuishi katika jiji hilo.Ilibidi niwaige
wenzangu ili nipate namna ya kuishi kwani sikutaka kurudi Tanga.
“Sasa wenzangu mnieleweshe inakuwaje?” nikawauliza huku nikilazimisha
kicheko cha uongo ili wasizielewe hisia zangu kwamba jambo hilo sikulipendelea hata kidogo lakini sikuwa
na budi.
Mariamu ndiye aliyechukua jukumu la ualimu akaniambia.
“Akitokea mteja akitaka kutoka na wewe, mwaambie kwanza akununulie
bia unywe kiasi kidogo tu cha kukuondoa aibu na kukufanya uchangamke. Usinywe sana kiasi cha
kutojitambua kwani atakwenda kukufanya vitendo visivyo na maana. Umenielewa
shoga?
“Nimekuelewa”
“Ukifika huko mtakako kwenda patana naye bei kwanza. Sisi
tunamuangalia mtu uwezo wake na pupa yake. Kama
tumemgundua ana pesa na anakupapatikia unamtoza shilingi elfu hamsini kwenda
mbele kwa kulala naye. Kama unamuona ni wa
kawaida tu akikupa hata ishirini unakubali”
“Sasa ninamuambia anipe kabisa au….?”
“Anaweza kukupa kabisa au asubuhi mkitoka. Kuna wakati wa ambao, wateja
hana hata elfu kumi unachukua. Na kuna wateja wengine wanatumia gesti hii hii.
Unalala naye hapa hapa”
Nikawa natingisha tingisha kichwa kuonesha kumkubalia.
“Kuna wanaume wengine ni wa ‘short time’.Hao kwa usiku mmoja
unaweza kuwapata wengi siku za mwisho wa mwezi”
“Na hao mnawatoza kiasi gani?”
“Unapatana naye. Akiingia sawasawa unamla hata elfu kumi na tano
lakini isiwe chini ya elfu kumi”
Wakati tunazungumza walitokea wanaume wawili,wakajiunga na sisi. Waliagiza
bia na sisi walitununulia bia moja moja. Tukawa tunakunywa huku tunazungumza. Mmoja
wa watu hao alionekana kunipenda mimi na mwengine akaelemea kwa Mariamu.
Sikuwa na shaka kwamba walikuwa wanajua kuwa kukaa kwetu pale baa
ilikuwa ni kwa ajili ya kusubiri wanaume. Kwa kweli nilikuwa nikiona aibu kwa
sababu licha ya kwamba kazi yenyewe ni ya aibu nilikuwa sina uzoefu nayo.
Baada ya mazungumzo marefu jamaa hao wakataka tukachukue vyumba
pale gesti.Wakati huo tulikuwa tumeshakunywa bia mbili mbili.
Niliondoka na mwenzangu Mariam kwenda upande wa gesti.Wakati tunakwenda
Mariam aliniambia.
“Mkiingia
chumbani patana naye kabisa. Wanaume wengine
hawaaminiki. Kama atataka mlale wote utamwambia
akupe shilingi elfu ishirini lakini usimpunguzie chini ya kumi na tano.
Na kama ni ‘short time’ ni elfu kumi na tano na isiwe chini
ya elfu kumi.Umenielewa?”
“Nimekuelewa”
Mtoa vyumba alikuwa mwanaume. Mariam ndiye aliyezungumza naye.
“Ni vyumba vya ‘short time’ au vya kulala?” jamaa huyo akatuuliza.
“Hatujajua” Mariam akamjibu
“Atalipa nani?”
“Watalipa wao.Tupe hivyo vyumba, mwenzangu atamsubiri mtu
wake chumbani. Mimi nitakwenda kuwaita wakija utawauliza. Kama
ni ‘short time’ au vya kulala utawatoza kabisa”
“Sawa”
ITAENDELEA kesho hapahapa usikose uhondo huu nini kitamtokea Salma baada ya kurubiniwa na mashoga zake.
No comments:
Post a Comment