HADITHI
YAMENIKUTA SALMA MIE
ILIPOISHIA
Nilikaa pale hospitali kwa wiki mbili. Sikumuona Sikuzani wala
Mariam aliyekuja kunitazama hata siku moja, wakati nilikuwa na hakika kuwa
walipata habari kuwa niligongwa na gari na niko Muhimbili.
Baada ya wiki hizo mbili, kidonda kilichokuwa mguuni kwangu
kilikuwa kimepona ingawa hakikuwa kimekauka kabisa. Kadhalika sehemu za mwili
wangu nilizoumia nazo zilikuwa zimepona. Hapo hospitali nilipewa magongo mawili
ya msaada ili niweze kuendea msalani.
Daktari aliyekuwa katika wodi yangu alinipa ruhusa lakini
aliniambia niende nikatafute msaada wa pesa sehemu yeyote ile ili niweze
kupelekwa India
kufanyiwa operesheni ya jicho kabla ya wiki nne kumalizika.
Nilitoka hapo hospitali nikiwa sijui pa kwenda.Vile
nilivyofikishwa pale hospitali ndivyo nilivyotoka, sikuwa na kitu chochote
zaidi ya mfuko wa plastiki na shilingi elfu tano nilizosaidiwa na daktari kwa
ajili ya usafiri.
SASA ENDELEA
Sikuwa na pakwenda zaidi ya kupanda daladala na kurudi kule Sinza
kwa kina Mariam.
Nilipofika Sinza, wakazi wa nyumba niliyokuwa ninaishi waliponiona
walipatwa na mshangao. Kwanza hawakunitambua
mpaka nilipojitambulisha.
Nikaambiwa kuwa Mariam na Sikuzan hawakuwepo.
"Wamekwenda wapi?" nikawauliza
"Wamefungwa" dada mmoja aliyekuwa shoga mkubwa wa kina
Mariam akaniambia. Nikashituka.
"Wamefungwa kwa kosa gani"?nikamuuliza.
"Walikamatwa usiku.Wakashitakiwa kwa kosa la kuendesha
biashara ya umalaya"
"Ilikuwa lini?"
"Siku ya pili baada ya siku ile uliyopata ajali"
"Wamefungwa kwa miaka mingapi?"
"Si miaka, ni miezi sita tu kila mmoja"
Hapo nikajua sababu ya kutomuona Mariam wala Sikuzan kuja
kunitembelea hospitali nilikokuwa nimelazwa.
"Siku waliyohukumiwa nilikwenda mahakamani.Mariam alinipa
funguo ya chumba chao akaniambia kama utatokea
nikupe"
"Shida yangu ilikuwa ni kutoa vitu vyangu ili niviuze nipate
nauli ya kunirudisha Tanga. Siwezi tena kuishi Dar" nikamwaambia
"Sasa ngoja nikupe huo ufunguo"
Dada huyo aliyekuwa akiitwa Agnes aliingia chumbani mwake
akanitolea ufunguo na kunipa.Nikafungua ule mlango na kuingia mle chumbani. Nikafungua
dirisha ili niweze kuona vizuri. Agnes naye akaingia.
Nikaanza kukusanya vitu vyangu. Kulikuwa na mabegi yangu mawili ya
nguo.Nikayafungua na kutoa nguo zote zilizokuwemo.Nilichagua nguo chache tu,
nikazirudisha kwenye begi moja. Nguo zingine nikamwaambia Agnes ninaziuza.
"Nitafutie wateja, nataka nipate nauli"
"Nauli ya shilingi ngapi?"
"Nataka nipate kama shilingi
laki moja hivi kwani huko niendako sijui kukoje. Hivi vyombo vingine pia
ninaviuza,sitavichukua"
Agnes akachukua baadhi ya vyombo na kuchagua nguo alizozipenda,
akaniuliza anipe kiasi gani.
"Nipe utakazo nipa dadaangu"
"Elfu themanini, sijui kama
utaridhika nazo kwa hivyo vitu nilivyochukua"
"Nipe tu dadaangu"
Agnes aliponipa pesa hizo, nilimuambia akanitafutie wateja wengine
wa kununua vile vitu vilivyobaki.
"Labda nichukue hizi nguo niende nazo hukohuko.Sasa niambie
bei yako"
"Bei yoyote dadaangu,elfu kumi, kumi na tano, wewe uza
tu"
Agnes akachukua zile nguo na kutoka nazo. Nikabaki mle chumbani
kwa karibu masaa mawili. Aliporudi alikuwa hana nguo hata moja. Akanipa
shilingi laki moja.
"Nimekwenda kuziuza kwa majirani" akaniambia.
"Nakushukuru dadaangu. Hivi vyombo vyangu vilivyobaki nitawaachia
mashoga zangu kina Mariam.Wakitoka jela watakuja kuvikuta. Utawaambia nimetoka hospitali
na nimerudi Tanga”
"Sawa mdogo wangu. Nitakuja kuwaambia"
"Tatizo langu kubwa ni huu mguu wangu uliokatwa na haya macho
yangu. Hili jicho langu moja limeharibika kabisa. Hili jingine nimeambiwa
limeingia kipande cha kioo huku pembeni, nalo linaweza kuharibika kama sitapelekwa India.Na siku nilizoambiwa zimebaki wiki
mbili tu.Sijui nitafanya nini?"
"Ukifika Tanga utawaeleza ndugu zako. Natumaini
watakuchangia"
Sikumjibu kitu. Niliguna tu kisha nikanyanyuka.
"Dadaangu ndiyo natoka naenda Ubungo. Gari lolote nitakalo
lipata ndilo nitakaloondoka nalo"
Agnes alinishindikiza hadi kwenye kituo cha daladala.Tukaagana
hapo, nikapanda daladala na yeye akarudi.
Nilipofika Ubungo moyo wangu ulikuwa mzito sana kurudi Tanga. Kwa muda nikawa nimesimama
nikitafakari.Nilihisi kurudi Tanga ilikuwa sawa na kujimaliza kabisa.Tatizo
langu sasa lilikuwa kupata msaada wa kuokoa jicho langu. Nilikuwa na uhakika
kwamba huko Tanga nisingepata ndugu yeyote wa kunisaidia pesa hizo hasa
kutokana na visa nilivyovifanya.
Kama kuna mahali pa kupata
msaada, nilijiambia, ni hapa hapa Dar
es salaam.
Nikajiuliza sasa niende wapi
kutafuta msaada huo? Niende Ikulu…niende wizara ya afya…au niende kwa mbunge?
Wakati naendelea kutafakari nikamuona
Mzee mmoja mwenye asili ya Kiasia amesimama karibu yangu akizungumza na simu.
Alipomaliza kuzungumza nikamfuata.
“Shikamoo Baba” nilimwamkia.
“Marahaba” akanijibu.
Nilimuhisi alikuwa
akinidhania kuwa nilikuwa ombaomba
niliyetaka kumuomba msaada.
Nikamuona akijipekua
mifukoni.
“Sihitaji pesa baba, kuna
maneno nataka kukwambia. Naomba unisikilize.” nikamwambia.
Mzee huyo akanishangaa kidogo.
“Unasemaje?” akaniuliza.
“Baba kama
unavyoniona nina matatizo lakini tatizo kubwa ninalotaka kukueleza ni kuhusu
jicho langu hili” nikamwambia na kumuonyesha lile jicho langu linaloona.
“Mimi nilipata ajali ya gari
hivi karibuni iliyosababisha mguu wangu mmoja ukatwe na jicho langu moja
kuharibika.
“Sasa hili jicho langu ambalo
linaona lilingia kipande cha kioo kwa pembeni. Madaktari wa Muhimbili wameniambia
ni chembe ndogo sana
ya kioo. Sasa tatizo liliopo ni kwamba natakiwa kupelekwa India kufanyiwa upasuaji kabla ya
wiki mbili. Madakdari wameniambia baada ya wiki mbili kumalizika jicho hili
nalo litaharibika kabisa na nitakuwa kipofu”
Yule mzeebaada ya
kunisikiliza kwa makini aliniuliza.
“Sasa ulikuwa unahitaji
nini?”
“Nilikuwa nahitaji msaada wa
kupelekwa India
kutibiwa” nikamjibu haraka .
“Kwani wewe huna ndugu?”
“Ninao lakini ndugu zangu ni
maskini, hawawezi kupata pesa zinazohitajika.”
“Zinahitajika kiasi gani.”
“Nimeambiwa zinahitajika
shilingi milioni nane”
“Bado si tatizo kwa sababu
zipo taasisi zinazosaidia watu kama nyinyi.
Kuna taasisi moja ya misheni ilianzishwa mwaka jana. Ishapeleka watu wengi
nchini India
kutibiwa maradhi yaliyoshindikana hapa kwetu.”
ITAENDELEA
No comments:
Post a Comment