RIWAYA
MPYA
ALIYEMUUA
MCHUMBA WANGU
KIDOKEZO
James Matei alimshuhudia
waziwazi mchumba wake Maria Temba akipigwa risasi na kuuawa, kitendo ambacho
kiliyakatisha matumaini yake ya kufunga ndoa na kuoana na msichana huyo
aliyempenda kuliko kitu kingine chochote.
Muuaji alipokamatwa na
polisi, James alithibitisha kwa uchungu mwingi mbele ya polisi kuwa mtu huyo
ndiye aliyempiga risasi mchumba wake. Akawataka polisi wahakikishe kuwa sheria
inafuata mkondo wake.
Muuaji alifikishwa mahakamani
na Matei alitakiwa kwenda mahakamani kutoa ushahidi, ushahidi ambao polisi
waliamini ungetosha kumtia hatiani muuaji huyo.
Lakini Matei aliposimama
kizimbani aliushangaza upande wa mashitaka alipobadilika ghafla na kumtetea
muuaji huyo aliyemshuhudia akimuua mchumba wake. Akaitaka mhakama imuachie
huru.
Hata baada ya kukumbushwa
kuwa yeye ndiye aliyemthibitisha kituo cha polisi kuwa alimpiga risasi Maria na
kusababisha kifo chake, James alikana maelezo yake na kusisitiza kuwa hakuwa
akimtambua.
Mahakama ilipomuachia huru, James
alimkumbatia muuaji huyo na kuishukuru mahakama kuwa imetenda haki.
Je
imekuwaje Matei akabadilika ghafla?
SASA ANZA RIWAYA HII.
HADITHI
ALIYEMUUA MCHUMBA WANGU
Kujuana kwao kulitokea kama bahati nasibu. Siku hiyo James Matei alikuwa katika
matembezi yake ya kawaida akiwa kwenye gari lake aina
ya Rav 4. Alikuwa akipita katika katika mitaa ya Kinondoni akitokea kwenye
saluni moja alikokwenda kupunguzwa nywele.
Ilikuwa majira ya saa kumi na
moja jioni. Hali ya hewa ilikuwa imebadilika tangu saa tisa. Wingu zito
lilikuwa limetanda hewani na kusababisha mwanga wa jua kutoweka na kuwa
na kila dalili ya kunyesha mvua.
Akiwa kwenye barabara ya
Mwanamboka James alimuona msichana aliyekuwa amesimama peke yake kwenye kituo
cha daladala. Wakati anakikaribia kituo hicho mvua ikaanguka ghafla. Yule
msichana alianza kutota.
Kwa sababu tu za kibinaadamu
James alipunguza mwendo akalisimamamisha gari karibu na kituo hicho. Alishusha
kioo akamtazama yule msichana.
“Twende”
alimwambia.
Msichana aliyekuwa amejikunja
alikimbilia kwenye gari hilo
akafungua mlango wa nyuma na kujipakia.
“Pole sana” James alimwambia msichana huyo
mwembamba na mrefu wa wastani.
“Asante kaka” Msichana alimjibu huku
akijifuta maji kwenye uso wake.
“Najua
ulikuwa unasubiri daladala, unakwenda wapi?”
“Siendi
tena, naomba msaada wako unirudishe nyumbani”
“Nyumbani
ni wapi?”
“Twende
mbele kidogo”
James
alitia gea ya kwanza na kuiondoa gari.
“Mimi naitwa James, mwenzangu
unaitwa nani?” James akamuuliza msichana huyo.
“Naitwa
Maria”
“Bila
shaka ni mwenyeji wa Arusha”
“Umejuaje?”
“Lafidhi
yako ndiyo iliyonitambulisha”
“Mimi
ni muarusha, wewe je?’
“Mimi
ni mngoni lakini nilizaliwa Tanga”
“Nimefurahi
kukufahamu”
“Na
mimi nimefurahi kukufahamu. Unaishi hapa kinondoni?”
“Mtaa
wa tatu tu utakuwa umenifikisha nyumbani”
Baada ya James kumfikisha
katika mtaa huo, Maria alimuonesha nyumba aliyokuwa anaishi. Ilikuwa nyumba ya kota ya shirika la nyumba
la taifa.
“Asante kaka yangu” Maria
akamshukuru James wakati James alipolisimamisha gari mbele ya nyumba hiyo.
“Asante na wewe. Itabidi utote tena
kidogo. Mlango wako uko mbali”
“Si
kitu, umenisaidia sana”
Msichana alikuwa bado amesita
kwenye siti kama vile kulikuwa na kitu
akikisubiri kutoka kwa James. Pengine alidhani angeombwa namba ya simu au
alihisi James angetaka wakutane siku nyingine ili ampe ahadi ya uongo.
Kama vile James alitambua mawazo yake, alimtazama na
kutabasamu.
“Haya, jioni njema”
akamwambia.
“Asante kaka”
Msichana akawa kama ameruhusiwa kutoka kwenye gari, akafungua mlango na
kushuka. Aliufunga tena kisha akakimbia kuelekea kwenye mlango wa nyumba hiyo.
James akaliondoa gari na
kuendelea na safari zake. Alivyoachana na msichana huyo alikuwa kama amemuondoa akilini mwake. Hakutarajia kama
angekutana naye tena na hivyo mawazo yake yalikuwa kwenye mambo yake mengine.
Mvua ilikuwa ikiendelea
kunyesha kwa nguvu na ndiyo iliyomfanya aamue kurudi nyumbani kwake mapema.
Wakati anakaribia kufika nyumbani kwake Msasani akasikia simu ikiita katika
siti ya nyuma.
Aligundua mapema kuwa haikuwa
simu yake kutokana na kuwa na mlio tofauti. Kadhalika simu yake ilikuwa kwenye
mfuko wake wa shati, haikuwa kwenye siti ya nyuma. Akashituka na kugeuza uso
wake nyuma. Akaona simu iliyosahauliwa kwenye siti inaita. Akajiuliza ni simu ya
nani?
Mara moja akapata jibu kuwa
huenda msichana aliyempa lifti alikuwa amesahau simu yake. Aliegesha gari kando
ya barabara kisha akaishika ile simu na kuitazama. Alijiuliza aipokee au
aiache?
Kwa sababu ya kutaka
kuwasiliana na mwenyewe aliona aipokee, akaipokea.
“Hallo!”
“Hallo…samahani kaka,
nimesahau simu yangu” Sauti ya msichana iliyokuwa imejaa tashiwishi ilisikika
kwenye simu.
“Wewe
ni nani?” James akamuuliza.
“Mimi
ni yule msichana uliyenipa lifti dakika chache zilizopita”
“Maria”
“Ndiyo
Maria. Nashukuru kwa kunikumbuka”
No comments:
Post a Comment