Thursday, December 8, 2016

HADITHI, , ALIYEMUUA MCHUMBA WANGU, SEHEMU YA 2

HADITHI
 
ALIYEMUUA MCHUMBA WANGU 2
 
ILIPOISHIA
 
Aligundua mapema kuwa haikuwa simu yake kutokana na kuwa na mlio tofauti. Kadhalika simu yake ilikuwa kwenye mfuko wake wa shati, haikuwa kwenye siti ya nyuma. Akashituka na kugeuza uso wake nyuma. Akaona simu iliyosahauliwa kwenye siti inaita. Akajiuliza ni simu ya nani?
 
Mara moja akapata jibu kuwa huenda msichana aliyempa lifti alikuwa amesahau simu yake. Aliegesha gari kando ya barabara kisha akaishika ile simu na kuitazama. Alijiuliza aipokee au aiache?
 
Kwa sababu ya kutaka kuwasiliana na mwenyewe aliona aipokee, akaipokea.
 
“Hallo!”
 
“Hallo…samahani kaka, nimesahau simu yangu” Sauti ya msichana iliyokuwa imejaa tashiwishi ilisikika kwenye simu.
 
“Wewe ni nani?” James akamuuliza.
 
“Mimi ni yule msichana uliyenipa lifti dakika chache zilizopita”
 
“Maria”
 
“Ndiyo Maria. Nashukuru kwa kunikumbuka”
 
SASA ENDELEA
 
“Sasa tufanyeje? Niko karibu kufika nyumbani kwangu”
 
“Nyumbani kwako ni wapi?”
 
“Msasani”
 
“Tafadhali kaka nakuomba unisaidie”
 
James alisita kidogo. Kurudi tena Kinondoni kulimpa uzito. Lakini baada ya kuwaza kidogo alimjibu.
 
“Nitakuletea”
 
“Utaniletea muda huu?”
 
“Ndio nageuza gari nirudi”
 
“Nashukuru sana kaka yangu”
 
Msichana akakata simu.
 
James akaweka gea ya nyuma kugeuza gari na kurudi. Alimkuta msichana amesimama barazani  mwa nyumba yake akisubiri. Alipolisimamisha gari alishuka na kamfuata. Mvua ilikuwa ikimtosa. Msichana naye akaamua kumfuata. Wakakutana katikati. Wote wakawa wanatota.
 
James akamshika mkono msichana na kwenda naye barazani kwake.
 
“Ungenisubiri tu huku huku, unaona umetota bure” James akamwambia.
 
“Hapana. Wewe ndio ungenisubiri kwenye gari”
 
“Wakati nakuletea hii simu ungenisubiri tu. Kwanini utote?”
 
Msichana akatabasamu. James aliyaona meno yake meupe yaliyokuwa yamepangika vyema. Yalikuwa na mwanya mwembamba wa juu.
 
“Yaani utote wewe?” akamuuliza James.
 
“Atote mmoja, si sote” James akamjibu huku naye akitabasamu.
 
Msichana hakuwa na la kusema. Aliendelea kutabasamu.
 
James alitoa simu yake na kumpa.
 
“Simu yako hii hapa”
 
“Asante sana kaka yangu. Katika dakika chache tu za kukufahamu wewe nimegundua kuwa wewe ni mtu mwema sana”
 
“Hata na wewe”
 
“Mungu akupe moyo huo huo”
 
“Asante sana”
 
“Hebu nisubiri”
 
Msichana aliingia ndani. Punde tu alitoka akiwa ameshika kitambaa kipya. Akampa James.
 
“Jifute maji usoni kwako”
 
“Asante”
 
James alikichukua kitambaa hicho akajifuta uso wake uliokuwa ukichirizika maji ya mvua.
 
Alipomaliza msichana alimwambia.
 
“Chukua namba yangu”
 
James akatoa simu yake.
 
“Ni ngapi?”
 
Msichana akamtajia.
 
James aliihifadhi kwenye simu yake kisha akampigia msichana. Simu ya msichana ikaita.
 
“Hii ndio namba yako” Msichana alimuuliza.
 
“Ndiyo hiyo”
 
“Asante. Sasa utasubiri mvua au utaenda zako?”
 
“Acha niende, mvua si tatizo kwa sababu nina gari. Kwa heri”
 
“Karibu sana kaka yangu”
 
James alitoka mbio kuelekea alikoliacha gari. Akafungua mlango na kujipakia. Wakati anaondoka msichana alimpungia mkono wa kumuaga na yeye akampungia.
 
Huo ulikuwa mwanzo wa James na Maria kujuana. Mawasiliano ya simu yakaanza taratibu. Siku James alimpigia Maria kumsalimia, siku nyingine Maria akampigia James.
 
Muda si mrefu wakawa marafiki. Hapo ndipo James alipoanza kumpenda Maria na alimueleza wazi kuwa alitaka awe mchumba wake.
 
“Mbona ninaye mchumba!” Maria akamwambia James.
 
“Unasema kweli?”
 
“Yesu Kristo…kwanini nikudanganye”
 
“Unajua nimekupenda sana”
 
“Ni sawa. Lakini hatukuandikiwa kuoana. Umechelewa”
 
“Una maana huyo mchumba ulikuwa naye tangu tunaanza kujuana?”
 
“Nilikuwa naye. Sema hukuwahi kuniuliza na mimi sikuwhi kukueleza”
 
“Ni vizuri. Mnatarajia kuoana lini”
 
“Karibuni tu”
 
“Maria sikuamini. Naona kama unanitania tu”
 
“Amini, siwezi kukutania”
 
James alikuja kugundua kuwa licha ya Maria kuwa na uhusiano na mtu mmoja ambaye hakumuelewa pia alikuwa na kesi ya jinai iliyokuwa inamkabili.
 
Alikuwa karani wa mhakama aliyekuwa amesimamishwa kazi kutokana na tuhuma ya kupoteza kwa makusudi faili la kesi muhimu akiwa na lengo la kupoteza ushahidi.
 
Alikuwa nje kwa dhamana na kesi yake ilikuwa ikiendelea mahakamani.
 
Pamoja na kudai kuwa alikuwa na mchumba, Maria alianza kubadilika kidogo dogo na kuendeleza uhusiano wake na James. Ilifikia wakati ambapo James alimuuliza kuhusu mchumba aliyekuwa naye.
 
“Sina mchumba” Maria akamjibu.
 
“Si uliniambia una mchumba wako?’
 
“Nilikudanganya tu. Nilitaka kukupima nione kama utabadilika na pia nilitaka kukujua vizuri”
 
“Tangu mwanzo nilihisi kuwa unanidanganya”
 
“Unajua nini…nilitaka kukujua vizuri”
 
“Sasa umeshanijua vizuri”
 
“Sana”
 
“Ninafaa kuwa mchumba wako”
 
“Unafaa sana. Kawaone wazazi wangu. Kwa bahati njema wapo hapa Dar”
 
ITAENDELEA

No comments:

Post a Comment