HADITHI
YAMENIKUTA SALMA MIE
ILIPOISHIA
“Sasa hili jicho langu ambalo
linaona lilingia kipande cha kioo kwa pembeni. Madaktari wa Muhimbili wameniambia
ni chembe ndogo sana
ya kioo. Sasa tatizo liliopo ni kwamba natakiwa kupelekwa India kufanyiwa upasuaji kabla ya
wiki mbili. Madakdari wameniambia baada
ya wiki mbili kumalizika jicho hili nalo litaharibika kabisa na nitakuwa
kipofu”
Yule mzee baada ya
kunisikiliza kwa makini aliniuliza.
“Sasa ulikuwa unahitaji
nini?”
“Nilikuwa nahitaji msaada wa
kupelekwa India
kutibiwa” nikamjibu haraka .
“Kwani wewe huna ndugu?”
“Ninao lakini ndugu zangu ni
maskini, hawawezi kupata pesa zinazohitajika.”
“Zinahitajika kiasi gani.”
“Nimeambiwa zinahitajika
shilingi milioni nane”
“Bado si tatizo kwa sababu
zipo taasisi zinazosaidia watu kama nyinyi.
Kuna taasisi moja ya misheni ilianzishwa mwaka jana. Ishapeleka watu wengi
nchini India
kutibiwa maradhi yaliyoshindikana hapa kwetu.”
SASA ENDELEA
“Ofisi zao ziko wapi?”
nikamuuliza.
“Kwani wewe unazo karatasi
zako za hospitali zinazoonyesha matatizo ulionayo?”
“Ninazo, ngoja nikuoneshe”
“Hapana, usinioneshe mimi. Kama unazo ni vizuri kwani zitarahisisha wewe kupata
msaada. Hao watu ofisi zao ziko hapa hapa Ubungo. Subiri nitakupeleka kwa gari
langu”
***************************
Sitamsahau mzee yule
aliyenipeleka katika taasisi ile ya misheni ambayo iliniwezesha mimi kupelekwa India
kuokoa jicho langu.
Huko huko India nilipata rafiki
aliyeninunulia mguu wa bandia ambao ulipachikwa kwenye mguu wangu uliokatwa. Kadhalika akaninunulia jicho
la kutengenezwa ambalo lilikuwa halioni
lakini liliwekwa katika tundu la jicho langu lililoharibika na kuonekana kama jicho zima. Lakini lilikuwa halipepesi wala
kuchezacheza.
Operesheni yangu ya kuondoa
kipande cha kioo kwenye jicho langu ilichukuwa saa tatu. Nikakaa Hosptali kwa
siku saba. Siku ya nane nilipewa miwani nikaruhusiwa kuondoka.
Siku niliporudi nchini
nilipokelewa na maafisa wa taasisi
iliyonipeleka huko. Wakanipangishia chumba cha kulala katika hoteli kwa siku moja kabla ya kurudi Tanga.
Kwa kweli niliwashukuru sana. Ingawa sikuwa na
mguu mmoja wala jicho moja lakini nilikuwa na afadhali sana. Hivi sasa usichana ulikuwa umenirudia
kidogo kwani sikuwa nikitembea kwa magongo na haikuwa rahisi kwa mtu kujua kuwa
nilikuwa na mguu wa bandia.
Kadhalika jicho la bandia
nililowekewa lilifanya nisionekane kuwa na upofu.na kwa vile nilitakiwa kuvaa
miwani, haikuwa rahisi kwa mtu kunitambua.
Baada ya kulala hoteli kwa
siku moja, siku iliyofuata nilipanda basi kurudi Tanga. Kwa vile baba yangu
mzazi alikwishakufa nilifikizia kwa kwa shangazi yangu Makorora.
Shangazi aliponiona badala ya
kufurahi aliangua kilio.
Nikambembeleza na kumsihi anyamaze.
Aliponyamaza akaniambia kuwa aliambiwa na Ibrahimu kuwa nilikuwa nimepofuka
jicho na mguu wangu mmoja ulikatwa kutokana na ajali ya gari.
Nikamwambia shangazi ni kweli
mguu wangu mmoja umekatwa na ule niliokuwa nao ni wa bandia.
Pia nikamwambia jicho
langu moja limepofuka na nimewekewa
jicho la bandia.
Nikamueleza kila kitu
kilichotokea mpaka Ibrahimu alivyokuja kunikataa hospitali.
“Mimi simlaumu Ibrahimu.
Umeyataka mwenyewe mwanangu. Ulikuwa mzima, sasa umeshapata ulemavu wa kudumu kwa
balaa lako”
“Shoga ndiye aliyeniponza
shangazi”.
“Shoga yako nani?”
“Yule jirani yangu, anaitwa
Rita”
“Rita alikuja hapa kwangu
akasema wewe ulikwenda kwa mganga akakupa dawa zikamuaribu macho ibrahimu”
shangazi akaniambia.
“Rita ni mnafiki tena ni
mnafiki mkubwa. Huko kwa mganga si alinipeleka yeye, mbona hakukwambia?”
“Aniambie ili iweje, wakati
alikuja kukusema wewe”
“Akwambie ule ukweli
ulivyokuwa kwamba yeye ndiye aliyenishawishi niende kwa mganga”
“Sasa ndio ukome kusikiliza
maneno ya mashoga “
“Nimeshakoma”
“Sasa huyo Ibrahim
ameshakuacha?”
“Hakunipa talaka lakini ni kama ameshaniacha. Siwezi tena kurudi kwake”
“Haya, sasa kaa hapa utulie.
Ulilolitaka umeshalipata”
“Nitakaa, nitafanyaje
shangazi. Hata nikimfuata kumbembeleza, kwa hivi nilivyo sasa hawezi kunitaka
tena”
Lakini baada ya kuwaza sana siku ile ile
niliamua kumtumia ujumbe Ibrahim kumjulisha kuwa nimesharudi Tanga na niko kwa
shnangazi.
Nilidhani labda angerudisha
moyo na angekuja kunichukua au kunitazama. Badala yake nilitumiwa jibu lililouliza.
“Nani wewe uliyemtumia sms
mume wangu?”
Moyo ukanipasuka.
Nikamuonesha shangazi ile meseji niliyotumiwa.
“Nilisikia kuwa Ibrahimu
ameshaoa mke mwingine. Inawezekana aliyekujibu ni mke wake” Shangazi akaniambia.
Nikashituka.
“Hah! Ibrahim ameshaoa mke mwingine?”
“Kila jambo linakwenda kwa
riziki. Riziki inapokwisha hutokea sababu yoyote watu wakaachana. Kama yeye ameshaoa na wewe utakuja kupata mume atakuoa”
“Mume gani atakayenitaka mimi
shangazi?”
“Hilo
si tatizo. Tatizo ni vipi utaendesha
maisha yako. Fikiria utafanya nini, utairudishaje heshama yako katika
jamii. Kama unahisi si rahisi kupata mume kwa sasa, achana na
mawazo ya mume. Angalia mustakabali mwingine. Tafuta kazi ya
kukushughulisha uweze
kujiingizia kipato”
“Nitafanya kazi gani shangazi
wakati nimeshakuwa mlemavu?”
“Kazi zipo nyingi za
kujiajilri mwenyewe. Hata ukiuza chapati au maandazi ni kazi. Mbona nimeshaona
wasichana wengi tu wanaouza chapati, maandazi, vitumbua na wana maisha mazuri
tu. Jambo la msingi kwako ni kuamua tu”.
Nikatikisa kichwa changu
kusikitika.
“Yaani hivi sasa ninajuta
shangazi. Nilichezea shilingi chooni”
“Sasa imeshatumbukia kwenye
shimo. Acha kuifikiria kwa maana hutaipta tena. Cha msingi ni kufikiria jnsi
utakavyoipata nyingine”
Ushauri wa shangazi yangu
ulikuwa wa maana sana.
Hivi sasa ni mwaka mmoja tangu tukio hilo
litokee. Nimeanzisha biashara ya kahawa na kashata barazani mwa nyumba ya
shangazi. Nimeweka meza na mabechi manne. Ninauza kahawa kuanzia saa moja
asubuhi hadi saa nane kisha ninatoa tena meza saa kumi jioni hadi saa nne
usiku.
Nilianza na wateja wachache
wa kahawa lakini baada ya muda mfupi nikawa napata wateja wengi. Kwa siku nilikuwa
nikiuza birika saba mpaka nane za kahawa. Kipato chngu cha kila siku
nilimshinda hata yule anayefanta kazi ofisini.
Wateja wangu walinishauri
niwawekee bao la kete. Nikanunua bao hilo
na kuwawekea. Hivi sasa baraza ya nyumba ya shangazi yangu imekuwa haitoshi.
Kuanzia asubuhi watu wanacheza bao. Kadhalika wakati wa jioni na usiku.
Lakini mbali na wacheza bao
kulikuwa na wateja ambao walikuwa ni mashabiki wa timu za mpira wa miguu na
vyama vya siasa. Kuna siku watu hujadili mambo ya kisiasa na kuna siku mjadala
unakuwa kwenye mpira.
Jina langu likabadilika, sasa
nikaitwa mama kahawa. Ukifika eneo la Makorora ukimwambia mtu yoyote nioneshe
kwa mama kahawa atakuleta hadi barazani kwangu. Nimekuwa maarufu.
Kwa vile nilikuwa nimesha
jiunga na kitengo cha matibabu ya HIV au VVU, huko nilikutana na muathirika mwenzangu
mwanaume aliyenipenda nakutaka kunioa. Alikuwa ni mtu wa umri mkubwa nikimlinganisha
na mimi. Nikaenda kumueleza shangazi yangu. Shangazi akaniuliza.
“Anafanya kazi gani?”
Nikamjibu ni mvuvi wa samaki.
“Kama
amekupenda muache akuoe. Utaishi peke yako hadi lini wakati bado umsichana”
Sikutosheka na jibu la
shangazi yangu nilikwenda kumueleza daktari wetu wa kitengo. Akaniambia.
“Mnaweza kuoana lakini kabla
ya ndoa yenu mje kwangu niwafundishe jinsi mtakavyoweza kuishi kwa pamoja.”
Siku ya pili yake nikaenda na
yule mwanaume kwa daktari. Tukapewa mafundisho mengi ya manufaa katika ndoa
yetu. Haukupita hata mwezi mmoja nikaoana na yule mwanaume. Alikuwa anaitwa
Kasim.
Kasim akaniruhusu niendelee
na kazi yangu ya kahawa na tukawa tunaishi palepale nyumbani kwa shangazi.
Mpaka ninakisimulia kisa hiki tumeshapata mtoto mmoja wa kiume asiye na VVU. Na
tumenunua banda la uani palepale Makorora.
Ingawa miezi mingi imeshapita
tangu nilipoachana na Ibrahim, ningali ninaendelea kumkumbuka mara kwa mara na
sifikirii kama nitamsahau kabisa kabisa kwa
sababu nilikuwa nampenda.
Mimi salma yamenikuta hayo na
mpaka leo ninajutia makosa yangu, je wewe ninayekusimulia kisa hiki umepata
fundisho gani kutoka kwangu?
Mwisho nawahadharisha akina
dada wenzangu walio katika ndoa, waache tamaa na kuwasumbua waume zao ambao
vipato vyao ni vya chini. Ukijilinganisha na aliye juu utakufuru kama miimi nilivyojilinganisha na Rita aliyenunuliwa gari
na mume wake.
Laiti ningejilinganisha na
msichana aliye chini yangu anayechapa lapa asubuhi kwenda kutafuta kibarua cha
kubeta buni kwa malipo ya shilingi elfu tano kwa siku, ningeshukuru. Na yaliyonitokea
yasingenitokea.
Pia muangalie mashoga wa
kushauriana nao. Mashoga wengine si wazuri kama
alivyokuwa shoga yangu Rita aliyenipa ushauri uliotaka kuniangamiza.
Akina dada zangu mridhike na
yale maisha mnayoishi na waume zenu, wasije wakatokea akina Chinga
wakawalaghai.
Kisa changu kinaishia hapa.
Ningefarijika kupata sms zenu lakini msithubutu kunitumia kwani mume wangu ana
wivu ni kiama. Nisije nikalikoroga tena!
No comments:
Post a Comment