Roketi kubwa ya Uchina yafanya safari ya kwanza
Uchina imerusha angani roketi kubwa zaidi kuwahi kuundwa katika taifa hilo, roketi iliyopewa jina Long March 5.
Roketi hiyo ilirushwa angani kutoka kituo cha shughuli za anga za juu cha Wenchang katika mkoa wa Hainan.Imebeba setilaiti ya kufanya majaribio ambayo imepewa jina Shijian-17.
Long March 5 inaipa Uchina uwezo wa kupeleka angani mitambo na mizigo mizito, kwa mfano mitambo ya kutumiwa kwa ajili ya mawasiliano na vifaa vya kuunda kituo cha anga za juu ambacho taifa hilo linapanga kujenga katika anga za juu.
Maelezo ya roketi hiyo yanaashiria ina uwezo wa kubeba tani 25 hadi mzingo wa chini wa dunia (LEO), kilomita kadha juu angani, na tani 14 hadi mzingo wa mbali wa dunia, ambao ni kilomita 36,000 kutoka ardhini.
Long March 5 imo kwenye kitengo sawa na cha roketi yenye nguvu zaidi ya Marekani, roketi ya Delta-IV Heavy.
Kampuni za Marekani za SpaceX na Blue Origin zinaunda vyombo vya anga za juu vyenye uwezo wa kusafirisha tani zaidi ya 50 katika mzingo wa chini wa dunia (LEO).
Shirika la anga za juu la Marekani (Nasa) pia linakaribia kufanya safari ya kwanza ya roketi kubwa ambayo wanasema ina uwezo wa kubeba tani 130 hadi LEO.
Nasa imesema itatumia roketi hiyo kutuma wana anga hadi sayari ya Mars. Safari ya kwanza ya roketi hiyo imepangiwa kufanyika 2018.
No comments:
Post a Comment