HADITHI
YAMENIKUTA SALMA MIE
ILIPOISHIA
Maneno yake yakazidi kunipandisha.
“Usiniapize mwana wa mwenzio. Binaadamu haishi kuumbwa maana yake
nini?” nikamuuliza kwa ukali.
Ibrahim hakujibu kitu. Nikaendelea kumwaambia.
“Sasa kama mimi nimeshakuwa Malaya,
nina wanaume je wewe unachukua uamuzi gani?”
“Uamuzi unao wewe mwenyewe” Ibrahim akaniambia kwa sauti
iliyonyeea.
“Basi nipe talaka yangu niondoke. Huo ndiyo uamuzi wangu. Kwanza nimeshachoka na maisha ya kuhangaika!”
Ibrahim akanyamaza kwa vile nilikuwa nimemfikisha mahali
asipopataka.
“Usijitie kunyamaza, umeyataka mwenyewe. Nipe talaka yangu!”
nikaendelea kumwaambia.
Lakini Ibrahim aliendelea kubaki kimya, nikawa ninasema peke
yangu. Mwishowe na mimi mikanyamaza.
Asubuhi kulipokucha nikajitia kufura. Sikusafisha nyumba wala
sikuchemsha chai. Nilitoka bila kumuaga mtu nikaenda kwa Rita..Nilikunywa chai huko
huko kisha nikaingia chumbani mwake nikalala mpaka saa sita. Nilipoamka
nikarudi nyumbani.
SASA ENDELEA
Sikujua kuwa walichemsha chai asubuhi au walikaa hivyohivyo,
sikutaka kujua. Nilifikia sebuleni nikawa naangalia tv.
Kumbe nilipokuwa kwa Rita mmoja wa marafiki wa Ibrahim alikuja
nyumbani akampa Ibrahim shilingi erfu kumi. Ibrahim alipogundua kuwa nimerudi,
alikuja pale sebuleni akanipa ile elfu kumi aliyopewa.
“Chukua hii elfu kumi uende sokoni. Rafiki yangu Martin alikuja
kunijulia hali akanipa” akaniambia.
“Mpe ndugu yako umtume huko sokoni” nikamwaambia kijeuri.
Ibrahim akamuita Zacharia akampa ile pesa.
“Shemeji yako atakuagiza vitu vya kununua” akamwaambia.
“Shemeji yupi!” nikamuuliza kwa kung’aka na kunyanyuka pale
nilipokuwa nimekaa.
Huku nikielekea zangu uani nilimwambia.
“Wewe muagize vitu mnavyotaka. Mimi nimuagize nini?”
Nikaenda kukaa uani. Sikujua Ibrahim alizungumza nini na mdogo
wake lakini baada ya muda kupita Zacharia alikuja uani na kuniambia amesharudi
kutoka sokoni.
“Vitu viko jikoni” akaniambia.
“Mimi sipiki, nenda ukapike mle na kaka yako”
Nilipomwaambia hivyo Zacharia aliondoka. Sikujua walivyozungumza
na kaka yake lakini baadaye acharia aliingia jikoni na kupika. Mimi nikaingia
chumbani nikalala.
Baada ya muda Ibrahim aliingia chumbani na kuniuliza.
“Unaumwa?”
Sikumjibu kitu.
Akasimama simama karibu ya kitanda kisha akatoka. Nilikaa humo
chumbani hadi saa kumi jioni nilipoingia bafuni na kuoga. Nilipotoka bafuni
nikajipara na kuvaa viwalo vya gharama kisha nikavaa baibui langu nikatoka. Sebuleni
nilimkuta Ibrahim peke yake akiwaza. Sikujua alikuwa akiwaza nini. Nikafungua
mlango na kutoka. Wakati naufunga mlango, nilimsikia akiuliza.
“Wewe nani Zacharia?”
Sikumjibu chochote, nikaondoka. Ilikuwa safari ya kuelekea kwa
Chinga.
Nilipotoka hapo nyumbani, nilikwenda kukodi pikipiki ya bodaboda
ikanipeleka Makorola nyumbani kwa shangazi yangu. Nilijifanya nilikwenda
kumsalimia, kumbe nilikuwa na langu jambo.
Vile nilivyomsingizia kuwa anaumwa nilimkuta kweli anaumwa.
Akaniambia alikuwa ameshikwa na malaria kwa karibu wiki nzima lakini baada ya
kutumia dawa ndiyo ameanza kupata nafuu.
Nilitoa shilingi elfu kumi nikampa shangazi kisha nikajidai
kumlalamikia kuhusu gubu la mume wangu na jinsi anavyonishutumu kuwa nina wanaume
wa nje.
“Yaani tangu apate ule upofu tabia yake imebadilika. Kila siku
tunagombana, akiniona ninatoka anajua ninakwenda kwa mwanaume. Akiniona
nimepigiwa simu anaitegea sikio akidhani nimepigiwa na mwanaume” nikamueleza
shangazi.
“Mvumilie. Ile hali yake ndiyo inayomfanya anaona kama umemgeuka” Shangazi akaniambia.
“Nimemvumilia sana
lakini sasa naona uvumilivu utaisha. Si hilo tu,
mume hana pesa anategemea ndugu na jamaa wamsaidie, siku nyingine tunakula mlo
mmoja tu halafu ananiletea kero kama hilo”
“Sasa utafanyaje? Kuwa naye hivyo hivyo ndiyo kilimwengu. Maisha
yana majaribu mengi”
“Mh! Mimi naona maisha yatanishinda. Usishangae shangazi ukija
kusikia nimemuacha yule mwanaume!”
“Usifanye hivyo mwanangu, si vizuri. Dunia yote itakusema wewe.
Umekuwa naye katika raha na uwe naye pia katika shida”
“Shangazi mume hana kazi hana bazi, nisitoke nikatafute kazi
mahali au biashara, nikae tu pale. Si tutakufa kwa njaa shangazi?”
“Hamtakufa. Kama ni kutafuta kazi au kufanya biashara sidhani kama atakukataza”
Nilivyoona shangazi hakuwa akiliunga mkono wazo langu la kuachana
na Ibrahim japo nilimtolea visingizio
chungu nzima vya uongo, nikanyanyuka na kumuambia.
“Vikizidi sana
nitaondoka. Utakuja sikia
nimeshaondoka”.
Hapo hapo nikamuaga na kuondoka. Nilikwenda saluni nikatengezwa
nywele na uso wangu kwa karibu saa moja. Hapo salumi palikuwa panauzwa kashata
za kungu. Nilikuwa nazifahamu ingawa sikuwa na ushabiki wa kuzila. Kabla
sijaolewa na Ibrahim ndiyo niliwahi kuzitumia sana lakini nilipoolewa nikaziacha.
Kashata hizo zinazochanganywa na unga wa mbegu inayoitwa
kungumanga unapozila hukulegeza macho na kukulainisha mwili. Wakati mwingine
ukila nyingi zinaweza kukulewesha na kukufanya usitosheke na tendo la ndoa.
Baadhi ya wanawake hupenda kuzila wanapokuwa na ahadi na wanaume
zao. Na sana sana ni wale wanawake makahaba.
Nilipoona wasichana wenzangu wanazinunua huku wakizitolea sifa na
mimi nikanunua nne na kuzila hapohapo saluni.
“Shoga ukitaka uzipatie mpaka uzinuilie, unazila kwa madhumuni
gani” msichana aliyekuwa akinishughulikia aliniambia.
“Unazinuilia vipi?” nikamuuliza
“Unazinuilia vile unavyotaka, kama
unataka zikulegeze macho, zikutie kilevi au zikufanye usitosheke na….”
hakumaliza sentensi yake akaishia kucheka.
“Usipozinuilia hazifanyi kazi?” nikamuuliza.
“Zinafanya lakini hao makonkodi wenyewe huzinuilia.Vile
unavyozinuilia ndivyo zinavyokufanya lakini kwa vle umeshazila basi”
“Nitakuja kuzinunua siku nyingine unifundishe hivyo zinavyonuiliwa”
nikamwaambia.
Baada ya kutengezwa nywele zangu sikuondoka haraka hapo saluni, Nilimpigia
simu Chinga na kumjulisha kuwa ninakwenda kwake, akaniambia ananisubiri
Ndipo nilipotoka nikakodi tena pikipiki ya bodaboda, ikanipeleka
Mtendele Hotel.
Jambo la ajabu lililojitokeza kwa upande wangu ni kuwa safari ile
niliingia mle hotelini bila kujali chochote kama
vile nilikuwa mwenyeji. Nilimjulisha tu msichana aliyekuwa mapokezi kuwa
ninakwenda kumuona Chinga chumba namba kumi na tano. Akaniruhusu.
Na hata nilipoingia chumbani kwa Chinga sikumuona haya kama ninavyomuona siku zote. Nilifikizia kujitupa
kitandani. Kichwa changu kilikuwa kizito kama
niliyekunywa kilevi. Mwili ulikuwa umenilegea na macho yalikuwa yamenilegea
kiasi kwamba nilishindwa kutazamana na Chinga. Nikajua hali hiyo ilitokana na
zile kashata nilizokula. Nikajiuliza je kama
ningezinuilia ingekuwaje?
Kama kawaida yake nilimkuta Chinga kwenye kochi akinywa bia. Kwa mara ya kwanza siku
ile Chinga alifanikiwa kunishawishi ninywe bia. Katika maisha yangu sikuwahi
kunywa bia hata siku moja. Siku ile ndiyo niliionja na kuijua ladha yake. Nilikunywa
chupa moja tu lakini kwa sababu nilishakula kashata nne za kungu nilionekana kama niliyekunywa chupa nne.
Si kwamba nilikuwa siwezi kusimama au kutembea bali nilikuwa nikiropoka
maneno mengi ambayo kwa akili yangu ya kawaida nisingeweza kuyatamka huku
nikijifanya nampenda sana
Chinga.
Ghafla Chinga alinikata kilevi chote nilichokuwa nacho
aliponiambia kuwa anatarajia kuondoka kesho yake kurudi Dar es salaam kwa vile mwenzake
anayeshirikiana naye katika biashara zao alimpigia simu na kumueleza kuwa
anahitajika Dar.
“Tutakwenda sote” nikamwaambia Chinga nikiwa nimemkumbatia.
Sikuwahi kumkumbatia Ibrahim namna ile hata siku moja tangu apate
upofu.
“Siwezi kukuchukua wakati ni mke wa mtu” Chinga akaniambia.
“Mtu gani…..yule kipofu? Yule tumeshaachana tangu jana usiku”
nikamwambia kwa sauti ya kupayuka.
“Mmeachana?” Chinga akaniuliza huku akishangaa
“Tumeachana jana, mimi si mke wake tena”
“Hebu nieleze vizuri, alikwambia anakuacha?”
“Ndiyo ameniambia”
“Ilikuwaje mpaka akakuacha?”
“Ulitokea ugomvi kati yetu. Jana asubuhi tulipokuwa tunazungumza
kwenye simu alitusikia akanyamaza hadi usiku alipoanza kunitukana kuwa mimi ni
malaya, nina wanaume wa nje.
Nikamwaambia kama mimi ni malaya anipe talaka yangu, ndipo akanipa”
“Iko wapi hiyo talaka aliyokupa?”
ITAENDELEA Kesho usikose
No comments:
Post a Comment