MWANANCHI
Waziri Mkuu wa zamani, Edward Ngoyai Lowassa
amesema ana ari, shauku na uwezo wa kuongoza Taifa wakati alipotangaza
nia yake ya kugombea urais kwa tiketi ya CCM katika mkutano wa hadhara
uliohudhuriwa na maelfu ya watu kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid.
Lowassa, ambaye ni mbunge wa Monduli akihutubia maelfu ya wakazi wa Arusha, katika Uwanja a Sheikh Amri Abeid Aluta, alisema ameamua kujitokeza tena kuwania urasi kwa kuwa anaamini yeye ndiye mtu sahihi wa kuiongoza nchi wakati huu.
Zaidi ya watu 30,000 walifurika kwenye
uwanja huo wakiwa wamekaa kwenye viti na wengine ndani ya kiwanja cha
mpira huku, mwanasiasa mkongwe nchini, Kingunge Ngombare Mwiru
akiongoza mlolongo wa watu mashuhuri waliojitokeza kumuunga mkono
mbunge huyo wa Monduli katika mbio za kuelekea Ikulu anazoziita “safari ya Matumaini”.
Akihutubia mkutano huo, Lowassa alisema
pamoja na kuwa viongozi waliopita wameliongoza taifa hili vizuri, bado
linahitaji kiongozi mwenye uthubutu na uongozi madhubuti unaoweza
kufanya maamuzi magumu.
“Kuamini
kama una uwezo na shauku, hakuna budi kwenda sambamba na uwezo wa
kusimamia yale unayoyaamini. Na kwangu haya mawili ni dhahiri. Nina ari,
nina shauku na nina uwezo, kama rekodi yangu inavyothibitisha,” alisema Lowassa huku akishangiliwa.
“Tunapomtafuta
Rais wa Jamhuri ya Muungano ni lazima tukumbuke kwamba tunamtafuta mtu
ambaye atakuwa pia ni Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama
katika nchi yetu. Na kwa Chama cha Mapinduzi tunamtafuta mtu ambaye
atakuwa pia mwenyekiti wa chama chetu.
“Naamini
kwa vigezo vyote, nina kila sifa ya kubeba dhamana hizo nzito. Katika
mambo ambayo najivunia, na sitayasahau katika historia yangu ni
kushiriki kwangu kuilinda nchi yetu pale nilipohitajika. Nilishiriki
kikamilifu katika Vita vya Kagera nikiwa miongoni mwa askari wa mstari
wa mbele wa mapambano.”
Lowassa pia alikumbusha tukio la mwaka 1995 alipojitokeza kugombea urais kwa pamoja na Rais Jakaya Kikwete.
“Natarajia safari hii, Kikwete ataniunga mkono.”
Hata hivyo, Kikwete hakupitishwa na CCM
mwaka huo na akagombea peke yake 2005, mwaka ambao Lowassa alisema
aliamua kwa dhati kumuunga mkono mwenzake.
MWANANCHI
Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imesema
uandikishaji wa wananchi kwenye Daftari la Wapigakura nchini
utamalizika mwishoni wa mwezi ujao baada ya mashine 1,600 zaidi za
kielektroniki kwa ajili ya kazi hiyo kuwasili juzi.
Ofisa ugavi mwandamizi wa NEC, Datus Matuma alisema mashine hizo zinazotumia teknolojia ya utambuzi wa alama za mpigakura (Biometric Voter’s Registration), zitaanza kupelekwa mikoa ya Mara, Arusha, Manyara na Kilimanjaro.
“Ule
uvumi ambao ulikuwa ukienea nchini kwamba Tume ya Taifa haiwezi kumaliza
uandikishaji, sasa umefikia mwisho kwani hizi mashine ni za kisasa na
zitaanza kazi moja kwa moja kwenye mikoa hiyo niliyoitaja na mwishoni
mwa mwezi Juni au mwanzoni mwa mwezi wa Julai watu wote watakuwa
wameshaandikishwa,” Matuma.
Alisema wananchi wajitokeze kwa wingi
kujiandikisha ili wasikose haki yao ya msingi ya kupiga kura kwani kila
aliyefikisha umri wa kupiga kura anatakiwa kujiorodhesha kwenye daftari
hilo.
Alisema Serikali ni sikivu ndio maana
imekata kiu ya Watanzania kwa kuleta mashine hizo ambazo sasa zimefikia
8,000 na zinakidhi kabisa mahitaji ya Watanzania wote kwani zinafika
kila mkoa na zitagawiwa kwenye halmashauri kwa ajili ya kuzisambaza
kwenye vituo vya uandikishaji .
Hata hivyo, mwezi uliopita NEC
ilitangaza kwamba hakuna mpango wowote wa kuahirisha Uchaguzi Mkuu na
kusisitiza kuwa utafanyika kama ilivyopangwa.
MWANANCHI
Mjadala wa Bajeti ya Wizara ya Uchukuzi jana uligeuka shubiri kwa Waziri Samuel Sitta wakati alipobanwa na wabunge kutokana na Serikali kushindwa kuboresha usafiri wa reli na anga.
Wabunge hao, mbali na kuibua ufisadi
mbalimbali unaofanywa na watendaji wa Serikali, wakiwamo wa wizara hiyo,
walihoji sababu za Serikali kuwa na ndege moja tu na kushindwa na nchi
ndogo ya Rwanda ambayo ina ndege saba za serikali.
Licha ya kuipitisha, walisema kuwa nchi bila kuwa na usafiri unaoeleweka wa reli, anga na barabara ni vigumu kupata maendeleo.
Akichangia mjadala huo, mbunge wa Kawe,
(Chadema), Halima Mdee aliibua suala la ukiukwaji wa mauzo ya nyumba za
Shirika la Reli Tanzania na Zambia (Tazara), kwamba mbali na ukiukwaji
wa mauziano na ununuzi, pia mfanyabiashara aliyenunua nyumba hizo
amekwepa kodi ya Serikali inayokadiriwa kufikia Sh4 bilioni
“Haiwezekani,
tuna taarifa hizo, nyumba zimeuzwa kwa bei ya soko na Serikali pia
ilipaswa kupata kodi yake inayofikia wastani wa Sh4 bilioni… Serikali
hii ni ya aina gani ambayo kila mwaka kuna kashfa za ufisadi katika
wizara zake,” Mdee.
Mbunge wa Kigoma Kusini (NCCR-Mageuzi), David Kafulila,
alisema katika serikali ya Awamu ya Nne kila wizara inakabiliwa na
wizi, akifafanua jinsi Mamlaka ya Manunuzi Nchini (PPRA) ilivyoshindwa
kufuata vigezo ya ununuzi wa mabehewa 124 ya Kampuni ya Reli (TRL).
Alivitaja vigezo hivyo kuwa ni pamoja na utangazaji wa zabuni kutozingatiwa na pia kutofanyika kwa uchunguzi.
Alisema waziri wa uchukuzi na katibu
mkuu wa wizara hiyo na waziri wa fedha ambao ndio waidhinishaji wa fedha
hizo za ununuzi wa mabehewa wanatakiwa kuwajibika. Alisema suala hilo
linalohusu Sh230 bilioni haliwezi kufunikwa na kupita.
Alisema Rwanda ni nchi ndogo lakini ina
ndege saba wakati Tanzania ni nchi kubwa lakini ina ndege mmoja tena
inahitaji matengenezo kila siku.
MWANANCHI
Mwenyekiti wa kamati ya Ulinzi na usalama Wilayani Bukombe Amani Mwenegoha
amesematangu kutokea kwa mauaji ya mtoto albino Yohana Bahati Wilayani
Chato, kumeibuka madai mbalimbali ya utapeli na vitisho vinavyofanywa na
watu wenye ulemavu huo.
Mwenegoha alisema kuna utapeli unadaiwa
kufanywa na wasichana wenye ulemavu wa ngozi wanaofanya biashara ya
kujiuza miili yao Wilayani humo.
Imedaiwa kuwa wasichana hao huwageuka wanaume wanapofika kwenye nyumba za kulala wageni licha ya kukubaliana toka awali.
“Kuna
taarifa ambazo zimetufikia ofisini kwetu kwamba hawa wasichana
wanasimama barabarani sehemu za vichochoro wakiona wanaume wakawapenda
wanawaita na kuwalazimisha wawape fedha, wakikataa wanapiga kelele na
kudai kuwa wanataka kuwakata viungo vyao”Mwenegoha.
Pia wanapokuwa kwenye biashara yao ya
kujiuza wanapokutana na wanaume hukubaliana kiwango cha fedha, lakini
wanapofika ndani hubadilika na kuwalazimisha watoe fedha zaidi ya
makubaliano na wakikataa kuwa wanataka kukatwa viungo.
NIPASHE
Watu wawili wamefariki dunia mkoani
Simiyu katika matukio tofauti akiwamo mtoto wa miezi mitatu
aliyenyakuliwa na fisi akiwa mgogoni mwa mama yake.
Kamanda wa Polisi wa mkoa wa Simiyu, Gemin Mushy jana alisema kuwa mtoto Ng’wanza Samwel,
akiwa amebebwa na mama yake alinyakuliwa na fisi Mei 25, majira ya
saa 1;30 jioni katika kijiji cha Ngugunu,Tarafa ya Kisesa wilayani
Meatu.
Alisema katika kufuatilia tukio hilo,
mabaki ya mtoto huyo yalipatikana mita 200 tu fisi kutoka eneo
alilonyakuliwa huku kichwa, kifua, tumbo, mikono na miguu ikiwa haipo.
Katika tukio jingine mpanda baiskeli
aliyefahamika kwa jina la Magina Supa(20), mkazi wa Nyaumata mtaa wa
Kisiwani wilayani Bariadi, aliuawa kwa kukatwa na kitu chenye ncha kali
shingoni na bega la kushoto na mtu aliyekuwa amempakiza kama abiria
wake.
Akifafanua, Kamanda Mushy alisema kuwa
tukio hilo lilitokea Mei 26 majira saa 1;00 jioni katika mtaa wa
Izunya, kata ya Somanda tarafa ya Ntuzu wilayani Bariadi kwa mtuhumiwa
wa mauaji hayo anayedaiwa kuwa abiria wa mpanda baiskeli huyo aliyekuwa
anajishughulisha na biashara ya daladala ya baiskeli.
Kamanda huyo alisema kuwa mara baada ya
mauaji hayo, mtuhumiwa ambaye hajafahamika na anasakwa baada uhalifu
huo alitoroka. Chanzo cha mauaji hayo hakijafahamika.
NIPASHE
Walemavu wa aina mbalimbali karibu
milioni nne huenda wasipige kura kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka huu
kutokana na kukosekana vifaa vya kuwawezesha kushiriki zoezi hilo.
Baadhi ya vifaa hivyo ni kama maandishi ya nukta nundu kwa wasioona, hadi sasa havijanunuliwa.
Kamishna wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec), Jaji Mstaafu John Mkwawa, alisema matarajio ya kupatikana kwa vifaa hivyo yanasubiri kufunguliwa zabuni katikati ya mwezi ujao.
Alitoa maelezo hayo baada ya kuulizwa
iwapo Nec ina vifaa vya kuwasaidia walemavu hao na kama wamepewa elimu
kuhusu matumizi ya vifaa hivyo, kwa vile mwaka 2010 walilalamikia
ukosefu wa elimu na vifaa vya kuwawezesha kushirika zoezi hilo.
Jaji Mkwawa alisema jitihada zinafanywa
na tangazo la kutafuta wazabuni wa kuagiza vifaa hivyo lilitolewa Mei
12, mwaka huu kwenye vyombo vya habari.
Alisema idadi ya walemavu wenye sifa za
kupiga kura mwaka huu ni milioni nne hivyo Nec haipo tayari kuwakosesha
haki wananchi hao.
Kuhusu suala la utoaji wa elimu kwa watu
hao ambalo mwaka 2010 walilikosa, Jaji Mkwawa aliahidi kueleza zaidi
taarifa hizo kabla ya kupatikana vifaa hivyo.
Hata hivyo, alipoulizwa idadi ya vifaa
wanavyokusudia kuviagiza, Jaji Mkwawa alisema ni mapema kulielezea
kabla ya zabuni kufunguliwa.
NIPASHE
Hatima ya Mpango wa Taifa wa Damu Salama (NBTS) upo kwenye hati hati baada ya mfadhili mkuu aliyekuwa anagharamia uendeshaji wake kuondoka rasmi leo na kuiacha ikichechemea.
Serikali ya Marekani kupitia kituo cha
Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa (CDC), ilikuwa akigharamia sehemu kubwa ya
mishahara ya wafanyakazi, vifaa vya kuhifadhia na kusafirishia damu.
Uchunguzi wa umebaini kuwa, NBTS ina
hali mbaya kwa vile mafadhili anaiacha wakati benki hiyo inakabiliwa
na uhaba wa damu ambayo ni tegemeo kwa wagonjwa waliopo mahospitalini
hasa wanawake wajawazito, wazazi na watoto wachanga.
Msemaji wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, Nsachris Mwamwaja,
alikiri kujitoa kwa mfadhili huyo na kuongeza kuwa, serikali imejipanga
kukabiliana na changamoto hiyo ikiwa ni pamoja kubeba mzigo wote wa
ulipaji mishahara kwa wafanyakazi na kuhakikisha damu na vifaa
vinavyohitajika vinakuwepo wakati wote.
“Tunatambua
umuhimu wa damu kwa wagonjwa, hata bajeti yetu itakayowasilishwa
keshokutwa bungeni tutalitilia mkazo suala hili kwa sababu mfadhili huyu
alikuwa anatusaidia na sasa amejitoa hivyo hatuna jinsi,”.
Kuhusu uhaba wa damu, aliwataka
Watanzania kujitokeza kuchangia damu kwa sababu mahitaji yake ni makubwa
na kila mtu anaweza kuhitaji msaada huo.
“Suala
la damu halihusiani na mfadhili bali watu wajitolee kwa sababu damu
inasaidia kila mtu bila kujali ni nani unacheo gani, niwaombe muwe na
utaratibu wa kuchangia damu ili tuokoe maisha ya watoto, wanawake,
wanaume, wazee,” alihimiza.
NBTS imekuwa ikitegemewa kusambaza
vitenganishi kwenye kanda zake sita ambazo ni Mwanza, Moshi, Tabora,
Mbeya, Mtwara na Dar es Salaam.
HABARILEO
Maofisa watano wa Serikali, wanatarajiwa
kupandishwa kizimbani hivi karibuni, kutokana na kashfa ya uagizaji wa
mabehewa 274 kutoka India, huku wengine wakitarajiwa kuchukuliwa hatua
za kiutawala.
Waziri wa Uchukuzi, Samuel Sitta, ameliambia Bunge jana kuwa Kamati Maalumu iliyoundwa na wizara yake, imemaliza kazi na kumkabidhi ripoti hiyo.
“Wamenikabidhi ripoti juzi na iliundwa na watu wa Ofisi ya CAG, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Takukuru na wahandisi,” alisema Sitta.
Alikuwa akifanya majumuisho ya hoja za
wabunge kuhusu makadirio ya bajeti yake kwa mwaka wa fedha 2015/16,
ambayo aliyawasilisha bungeni jana asubuhi na kupitishwa na Bunge
baadaye mchana.
Waziri huyo mkongwe alisema kamati hiyo ilienda hadi Calcutta, India ambako mabehewa hayo 274 yalitengenezwa na kwa mujibu wake, mabehewa hayo si chakavu, kama ilivyodaiwa awali.
Hata hivyo alisema
“kuna makosa mawili hapa ambayo ni uzembe wa pande mbili, waagizaji na
watengenezaji. Kuna tatizo katika specification (vipimo). “Hapa kuna
majina ya watu wote waliohusika katika suala hili.
Watano tunawapeleka mahakamani, wengine tutawachukulia hatua za kiutawala.” Aidha,
aliweka bayana kuwa katika maofisa hao watano watakaopelekwa
mahakamani, wawili ni wanachama wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo
(CHADEMA).
Aidha, Sitta alisema si kweli kuwa
hasara iliyopatikana ni Sh bilioni 200, bali ni Sh bilioni 12 na wote
waliohusika watachukuliwa hatua stahili.
“Pia tumemwomba Mwanasheria Mkuu ili sehemu ya hasara hii ibebwe na
mtengenezaji na nyingine itabebwa na Serikali kutokana na uzembe
uliofanyika,” Sitta.
Kwa habari, matukio na burudani ni hapa hapa tangakumekuchablog