MWANANCHI
Hatimaye Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu itatoa hukumu katika kesi inayowakabili mawaziri wa zamani wa Fedha, Basil Mramba na wa Nishati na Madini, Daniel Yona pamoja na Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha, Gray Monja, Juni 30, mwaka huu.
Kesi hiyo inasilikilizwa na jopo la mahakimu watatu, John Utamwa, Sam Rumanyika na Saul Kinemela. Viongozi hao wanakabiliwa na mashtaka ya matumizi mabaya ya madaraka na kuisababishia Serikali hasara ya Sh11.7 bilioni.
Hatua hiyo imefikiwa baada ya mashahidi
saba wa upande wa mashtaka kutoa ushahidi na kuwasilisha vielelezo vyao
vilivyopitiwa na mahakama na kuwaona washtakiwa wana kesi ya kujibu
hivyo kuwataka watoe utetezi wao dhidi ya mashtaka yanayowakabili.
Katika maandalizi ya kuwasilisha hoja za
kushawishi mahakama iwaone washtakiwa hao wana hatia ama la, Jumatatu
ijayo mahakama itazipatia pande hizo mbili mwenendo wa kesi nakala ya
mwenendo wa kesi ili waweze kuandaa hoja zao za kuishawishi na
kuziwasilisha mahakamani.
Kwa mujibu wa kesi hiyo iliyofunguliwa
mwaka 2008, washtakiwa hao kwa pamoja wanadaiwa kuisababishia Serikali
hasara ya kiasi hicho cha fedha kutokana na kutoa msamaha wa kodi kwa
Kampuni ya M/S Alex Stewart ya Uingereza.
Katika utetezi wa Mgonja, alidai kuwa
yeye ndiye aliyemshauri Waziri Mramba kuisamehe kodi kampuni hiyo
iliyokuwa ikifanya kazi ya kukagua madini ya dhahabu nchini, kwa sababu
kulikuwa na mkataba uliosainiwa Juni, 2003 kati ya kampuni hiyo na Benki
Kuu ya Tanzania (BoT) uliokuwa unaonyesha malipo yafanyike bila ya
kukatwa kodi.
MWANANCHI
Mbio za urais zimezidi kupamba moto kwa upande wa upinzani baada ya Mwenyekiti wa CUF, Prof. Ibrahim Lipumba
kutangaza nia ya kugombea nafasi hiyo ya juu kisiasa nchini, akisema
ana sifa zote lakini hatakuwa na kinyongo iwapo hatapitishwa na umoja wa
vyama vya upinzani.
Profesa Lipumba, ambaye anakuwa
mwanasiasa wa tatu kutoka vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi
(Ukawa) kutangaza nia hiyo baada ya mwenyekiti wa NLD, Emmanuel Makaidi na Dk George Kahangwa wa NCCR-Mageuzi kujitokeza kutaka kuongoza Serikali ya Awamu ya Tano.
Mwanasiasa mwingine aliyejitokeza kuwania urais wa Jamhuri ya Muungano ni Maxmillan Lyimbo wa TLP, wakati Hamad Rashid wa Alliance for Democratic Change (ADC na Maalim Sharrif Hamad wa CUF wametangaza kuwania urais wa Zanzibar.
Lipumba, ambaye atakuwa akiwania urais
kwa mara ya tano, iwapo atapitishwa na Ukawa ambayo imeamua kusimamia
mgombea mmoja atakayeungwa mkono na vyama vinne, alitangaza nia yake
juzi mjini Tabora wakati wa mikutano yake ya hadhara ya kuhamasisha
wananchi kujitokeza kujiandikisha kupiga kura kwa ajili ya Uchaguzi Mkuu
uliopangwa kufanyika Oktoba 25.
“Ninachoomba
ni ushirikiano wenu katika safari yangu hii ya kuwania tena urais,”
alisema Profesa Lipumba alipokuwa akihutubia wananchi kwenye uwanja wa
mpira wa Shule ya Msingi ya Town School mjini hapa.
“Ninajua
safari hii, urais (kwa upande wa upinzani) utasimamiwa na Ukawa, lakini
naamini mimi ni mwadilifu na nina uwezo wa kuongoza nchi,” Lipumba.
Profesa Lipumba aliwaomba wapenzi na
wanachama wa CUF pamoja na Watanzania kwa ujumla, kumuunga mkono katika
safari yake hiyo ya kuelekea Ikulu.
Mwenyekiti huyo wa CUF ambaye kitaaluma
ni mchumi, alisema ana uwezo na sifa za kuwa rais na kwamba madhumuni
makuu ya kutaka kushika madaraka ni kuondoa changamoto zinazowakabili
wananchi na kupambana na ufisadi.
MWANANCHI
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe, ameliaga rasmi Bunge na kusema kuwa kama atapata nafasi anayoidhamiria basi ataingia kwa mbwembwe ndani ya ukumbi huo.
Membe ni miongoni mwa makada wa CCM
wanaotajwa kuwania nafasi ya kuchaguliwa na chama chake kugombea urais
katika uchaguzi mkuu utakaofanyika Oktoba 25.
Waziri huyo alifanya hivyo jana mara
baada ya kujibu hoja zilizotolewa na wabunge kuhusu bajeti ya wizara
yake kwa mwaka wa fedha 2015/2016.
“Sitaingia ndani sijui nitakuwa nani, labda nikipata hicho ninachodhamiria nitaingia huku kwa mbwembwe,” alisema Membe ambaye amekuwa mbunge wa Mtama kwa miaka 15.
Membe alisema Bunge linaweza kutuhumiana, kunaweza kuwa mabishano lakini inapokuwa maslahi ya Taifa, wanakuwa kitu kimoja.
“Kama nitakosa na nyie ambao mtakaokosa tutaonana huko nje…Chombo hiki ni cha hekima, heshima na elimu,”.
Baada ya kumaliza Naibu Spika, Job Ndugai, alisema Bunge ni elimu na kwamba wanajifunza mengi.
Membe ambaye alisema anasimama kwa mara ya mwisho na bajeti yake kupitishwa jana, awali alipangua hoja mbalimbali za wapinzani.
Mapema Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni
ilieleza kuutilia shaka uhusiano wa ‘ghafla’ kati ya Tanzania na
Msumbiji uliofikia hatua ya kuondoa malipo ya viza baina ya nchi hizo
mbili, kudai kuwa imebaini mbinu chafu za raia wa Msumbiji kupewa
vitambulisho vya mzanzibari mkazi ili wapige kura katika Uchaguzi Mkuu
Zanzibar.
MTANZANIA
Nyumba za kulala wageni katika Jiji la
Arusha na viunga vyake zimeanza kufurika kutokana na makundi ya watu
yanayowasili jijini hapa kushuhudia mwanzo wa ‘Safari ya Matumaini’ ya Waziri Mkuu wa zamani na Mbunge wa Monduli, Edward Lowassa, anayoianza rasmi leo.
Mwanasiasa huyo mwenye ushawishi mkubwa miongoni mwa makada wa CCM
walioonyesha nia ya kugombea nafasi ya urais kupitia chama hicho,
anatarajiwa kutangaza nia leo kuanzia saa 8 mchana katika Uwanja wa
Sheikh Amri Abeid Kaluta, jijini hapa.
Mtanzania Jumamosi limeshuhudia pilikapilika katikati ya Jiji, Mitaa ya
Kaloleni, Makao Mapya, Levolosi na maeneo ya pembezoni ambako kuna
nyumba za kulala wageni, baadhi ya watu wakiulizia vyumba ambapo katika
nyumba nyingi kuna kibao kinachosomeka ‘vyumba vimejaa’.
Baadhi ya wageni hao ambao walizungumza na gazeti hili kwa sharti la
kutotaja majina yao, walisema pamoja na kukosa vyumba, wako tayari
kulala nje hadi watakapoianza ‘Safari ya Matumaini’ pamoja na Lowassa.
“Kukosa
vyumba si tatizo kwetu, tutalala hata uwanjani, tumesubiri sana siku
hii ambayo Mzee (Lowassa) alianza kuitaja tangu mwaka 2013, tunamshukuru
Mungu imefika na tutaanza safari ya matumaini pamoja naye,” alisema mmoja wa wageni hao.
Kujaa huko kwa nyumba za kulala wageni, hoteli baadhi ya watu usiku wa kuamkia jana na leo walilazimika kulala kwenye magari.
Taarifa kutoka kambi ya Lowassa zinaeleza kuwa, watu wengi kutoka kada
mbalimbali, wanatarajia kushiriki mkutano huo ambao Waziri Mkuu huyo wa
zamani pamoja na mambo mengine, atautumia kueleza matarajio yake endapo
chama chake kitamteua kugombea urais.
Wazee maarufu, akiwemo Kingunge Ngombale Mwiru, Pancras Ndejembi, Kanali Mwisongo na Mkuu wa Majeshi Mstaafu, Mirisho Sarakikya, nao pia wanatajwa kushiriki tukio la leo.
Mbali na kufurika kwa wageni katika Jiji la Arusha wanaosubiri kwa hamu
hotuba itakayotolewa na Lowassa hii leo, pia mavazi, ikiwamo sare za CCM
zenye utambulisho maalumu kwa ajili ya siku hiyo nazo zimepanda bei
maradufu.
Maandalizi katika Uwanja wa Sheikh Amri Abeid jijini hapa yalianza tangu juzi mapema asubuhi.
Mkutano huo wa kutangaza nia wa Lowassa kama ambavyo umekuwa ukitangazwa
kwenye vyombo mbalimbali vya habari unatarajiwa kurushwa moja kwa moja
pia na vyombo vya habari kutoka ndani na nje ya nchi.
MTANZANIA
Idadi ya makada wanaotajwa kujitosa
kwenye kinyang’anyiro cha kuwania urais kupitia Chama Cha Mapinduzi
(CCM) sasa inaweza kufikia 30, baada ya wengine wengi kutarajia
kujitokeza kuanzia wiki ijayo.
Taarifa zilizolifikia gazeti hili kutoka katika vyanzo mbalimbali vya
habari ndani na nje ya CCM zinadai kuwa idadi hiyo inaweza kuongezeka na
pengine hata kufikia wagombea 35, kutokana na baadhi ya makada
waliohudhuria vikao vya juu vya chama hicho vilivyofanyika wiki
iliyopita mjini Dodoma kuonyesha nia ya kuingia katika kinyang’anyiro
hicho baada ya kipenga kupulizwa.
Mtoa taarifa mmoja ambaye pia anaongoza kitengo nyeti ndani ya CCM
(hatutamtaja jina ili kulinda kibarua chake), alilidokeza gazeti hili
kuwa hadi sasa kuna makada 25 ambao wameonyesha nia, miongoni mwao
wakiwa ni wale waliokwisha kujitangaza kuwania nafasi hiyo kubwa nchini.
“Tutegemee idadi kuongezeka zaidi baada ya kipenga kupulizwa, wapo
waliokuwa na nia muda mrefu na walibaki na siri ya kusubiri kipenga,
wapo walioshindwa kujizuia kutokana na shauku ya kutaka nafasi hiyo,
ndiyo maana wengine walionyesha nia ya wazi na wengine walijitangaza,”
alisema.
Kati ya makada hao 30 wanaotajwa kujitosa kuwania urais, 25 tayari
walionyesha nia kwa muda mrefu na wengine kujitangaza kwa nyakati
tofauti.
Hata hivyo, kati ya Juni mosi hadi Juni tano, inatarajiwa makada wengi
watajitokeza kutangaza nia zao za kuwania urais kupitia CCM.
MTANZANIA
Waziri Mkuu, Mizengo Pinda,
amesema kuna haja ya kuwa na sheria itakayowezesha uandikishaji wosia
kuwa wa lazima ili kuondokana na migogoro ya kugombania mali za marehemu
na unyanyasaji wa wajane na watoto.
Kauli hiyo aliitoa Dar es Salaam jana,
katika maadhimisho ya miaka 25 ya Chama cha Wanasheria Wanawake Tanzania
(TAWLA) na uzinduzi wa kampeni ya uandishi wa wosia.
Alisema migogoro hiyo kwa kiasi kikubwa inaathiri wanawake na watoto pindi wazazi wa kiume wanapofariki.
“Kama inawezekana nawaomba TAWLA
muanzishe mchakato wa kutengeneza sheria ya wosia ili iwe lazima kwa
kila mtu kuandika wosia na mimi nitawapa ushirikiano wa kutosha
kuhakikisha suala hilo linafanikiwa,”.
Alisema kuna dhana potofu kuwa kuandika wosia ni kujitabiria kifo, huku
wengine wakihofia kuwa wakiandika wosia watauliwa na wanufaika wa wosia
ili wamiliki mali walizoachiwa.
“Wananchi watambue kuandika wosia
kunasaidia kuondoa matatizo pale mzazi mmoja anapofariki na si uchuro
kama wengi wanavyodhani ni kujitabiria kifo,” Pinda.
Alisema wosia huwa ni siri ya anayeandika na hautakiwi kuwekwa wazi kwa wanufaika, isipokuwa kwa mwanasheria na mashahidi wawili ambao huweka bayana mgawanyo wa mali pindi mwandika wosia anapofariki.
Alisema wosia huwa ni siri ya anayeandika na hautakiwi kuwekwa wazi kwa wanufaika, isipokuwa kwa mwanasheria na mashahidi wawili ambao huweka bayana mgawanyo wa mali pindi mwandika wosia anapofariki.
NIPASHE
Mbunge wa Iringa Mjini, Mchungaji Peter
Msigwa (Chadema) , amehoji ziara za viongozi nje ya nchi zinasaidia vipi
kukuza uchumi wa nchi kulinganisha na gharama zinazotumika.
Akichangia bajeti ya Wizara ya Mambo ya
Nje na Ushirikiano wa Kimataifa kuhusu Makadirio, Mapato na Matumizi kwa
mwaka wa fedha 2015/2016, jana bungeni, Msigwa alisema, tofauti na
ziara za viongozi wa mataifa mengine ambao wanapokwenda nchi za nje
wanatangaza uchumi na kutafuta masoko, Tanzania haifanyi hivyo.
“Alipokuja Rais Oboma hapa na ujumbe
wake hakuja kushangaa shangaa, alikuwa na watu kutafuta sehemu za
kuwekeza kwenye uchumi,” alisema.
Aidha, alisema balozi za Tanzania hazina
utangazaji wa uchumi, na kutoa mfano wa ubalozi mmoja wa Tanzania nje
ya nchi ambao umeiweka khanga kama kutangaza utalii badala ya kuweka
mambo yanayoweza kutangaza fursa za biashara.
“Sisi utalii wetu ni kutangaza khanga na vitenge, hatuna utangazaji wa kiuchumi,” alisema.
Akizungumzia hali za balozi hizo nje ya
nchi alisema zinasikitisha kutokana na kuwa hoi na zingine zinakosa hata
magari, majengo yamechakaa na mengine yanatoa harufu.
Akichangia wizara hiyo, Mbunge wa Ole
(CUF), Rajab Mbarouk, alizungumzia ufisadi unaofanywa na wizara hiyo
kwenye safari za viongozi na manunuzi ya tiketi.
Aidha, alisema baadhi ya watumishi
waliomaliza muda wao kwenye balozi za Tanzania nje ya nchi wanaendelea
kulipwa posho na mishahara.
Mbunge wa Chalinze (CCM), Ridhiwani
Kikwete, alitaka wizara hiyo kuzungumia hali inayojitokeza kwenye
mataifa mengine ya nje ya unyanyasaji wa wageni.
Alisema Tanzania imekuwa ikishiriki
katka ukombozi wa nchi za Afrika na kutoa mfano nchi ya Afrika Kusini,
lakini chakushangaza Watanzania walioko huko wananyanyasika.
NIPASHE
Sakata la vitendo vya mauaji,
udhalilishaji na unyanyasaji unaofanywa na askari wa hifadhi za taifa
limewaunganisha wabunge bila kujali itikadi zao za vyama kulitaka bunge
kuunda kamati ya kufuatilia mgogoro huo na kauli ya serikali kuhusu
sakata la utoroshaji wanyama nje ya nchi.
Wabunge hao walitoa hoja hiyo juzi
wakati wa kupitisha vifungu vya bajeti ya Wizara ya Maliasili na Utalii,
ambapo walisema wafugaji wamekuwa wakiuawa, kudhalilishwa na
kunyanyasika huku mifugo yao ikikamatwa na askari wanaolinda hifadhi
hiyo kutokana na migogoro ya mipaka.
Walitaka pia serikali iseme ni lini itatoa fidia kwa wananchi walioathirika kutokana na Operesheni Tokomeza.
Akitoa hoja kuhusu suala hilo, Mbunge wa
Rombo, Mheshimiwa Joseph Selasini (Chadema), alisema alikuwa kwenye
kamati iliyoundwa kuzuia migogoro hiyo na kupata taarifa ya mwanamke
mmoja wa Kijiji cha Maweni, aliyebakwa na askari wa tokomeza na
kufariki.
“Mheshimiwa mwenyekiti suala hili
likiachwa bila kuchukuliwa hatua, litaleta aibu kwa taifa,” alisema.
Mbunge wa Vunjo (TLP), Augustine Mrema, alisema askari hao wamekuwa
wakikamata ng’ombe wa wafugaji na kuwazuia bila kuwalisha kitendo
kinachosababisha kufa na wafugaji kutolipwa fidia.
“Tunataka wizara ilaani uzuiiaji wa mifugo ambayo yanaleta mahusiano mabaya kwenye mipaka hiyo,” alisema.
Kwa upande wake, Mbunge wa Maswa
Magharibi, John Shibuda (Chadema), alilalamikia tozo kubwa na tabia
kandamizi zinazotekelezwa na askari wanyamapori.
Aliitaka wizara hiyo pia kueleza ni lini fidia zitatolewa kwa watu waliothiriwa kutokana na oporesheni tokomeza.
Mbunge wa Simanjiro, Christopher Ole
Sendeka (CCM), alipendekeza kuundwa kwa kanuni ya kukomesha ukatili na
kutoa fidia kwa waathirika. Alisema vitendo vya vya unyanyasaji wa
wanyama kupigwa risasi na askari hao ni kunyume na wanaohusika lazima
wachukuliwe hatua. Kwa upande wake , Mbunge wa Longido (CCM), Michael
Lekule Laizer, alitaka wabunge wanaotoka eneo la wafugaji na wizara
kukaa ili kumaliza jambo hilo kudumisha ujirani mwema.
Aidha, Mbunge wa Bariadi Mashariki
(UDP), John Cheyo, Livingstone Lusinde (CCM), Pauline Gekul (Chadema)
na Ridhiwani Kikwete (CCM), walitaka kujua fidia zitatolewa lini kwa
watu walioathirika na migogoro hiyo na kulaani vitendo vya askari hao
kupiga mifugo na kuiua.
UTOROSHAJI WANYAMA
Sakata hilo liliibuliwa na Mbunge wa
Mbeya Mjini (Chadema), Mchungaji Peter Msigwa, aliyetishia kutoa
shilingi kama serikali haitaeleza ilihusikaje na utoroshaji wa wanyama
nje ya nchi.
“Inawezekanaje ndege ya nje kuingia nchini, kupakia wanyama na kuondoka bila vyombo vya usalama kujua,” alihoji.
Alisema ndege hiyo ya Qatar iliingia
nchini na kuondoka na wanyama hao na hakuna taarifa ya serikali. Wanyama
hao hai zaidi ya 120 waliotoroshwa kupitia Uwanja wa Ndege wa Kimataifa
wa Kilimanjaro (KIA), kwa kutumia ndege ya kijeshi ya Qatar.
Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro
Nyalandu, akitoa ufafanuzi, alisema sakata zima la kutorosha wanyama,
watu 15 walikamatwa na mmoja wao alifungwa miaka 60.
“Katika kuzingatia utawala wa sheria
suala hilo lilimalizika mahakamani,” alisema. Hata hivyo, Sendeka
alisema hakuna namna watu wanakusanya wanyama wanaingia nao kwenye ndege
na vyombo vya usalama vinaangalia halafu anayefungwa ni mtu mmoja.
Mwanasheria Mkuu wa Serikali, George Masaju, aliingilia kati kwa
kuwataka wabunge kuiamini serikali kwa kazi inayoifanya. Alisema suala
hilo linahitaji ushirikiano wa nchi nyingine walikopelekwa wanyama.
NIPASHE
Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na
Maendeleo (Chadema), Dk. Willibroad Slaa, leo anatarajiwa kuanza ziara
ya siku sita katika mikoa mitatu kwa ajili ya kukagua mwenendo wa
uandikishaji wa wapiga kura kupitia mfumo wa kielekroniki wa Biometric
Voters Registration (BVR).
Katika taarifa iliyotolewa na Mkuu wa
Idara ya Habari na Mawasiliano, Tumaini Makene, alitaja mikoa hiyo kuwa
Mbeya, Rukwa na Katavi, ambapo pamoja na kukagua zoezi hilo, atafanya
mikutano na wananchi kwa lengo la kuwaeleza masuala yanayohusu taifa.
Kupitia mikutano hiyo Dk. Slaa,
ataendelea kuwahamasisha Watanzania wenye sifa za kupiga kura,
kujiandikisha kwa wingi katika Daftari la kudumu la wapiga kura kutumia
mfumo wa BVR.
“Katibu Mkuu atatumia fursa hiyo kukagua
shughuli mbalimbali za chama zinazofanywa na viongozi na watendaji
katika kanda ya Nyanda za Juu Kusini,” alisema. Akitoa ratiba kamili ya
ziara hiyo, Makene alisema kwamba leo Dk. Slaa atakuwa Mkoa wa Mbeya
Wilaya ya Mbozi eneo la Vwawa na kisha kufanya mkutano wa hadhara kwenye
uwanja wa Ichenjezya.
Alisema siku ya Jumapili atakuwa mji
mdogo wa Tunduma, siku inayofuatia atakwenda mkoa wa Rukwa, huo atakuwa
na mkutano kwenye kiwanja cha Stendi ya Chanji mjini Sumbawanga.
Ziara ya kiongozi huyo itahitimishwa
juni 2 atakapokuwa Mkoani Katavi, ambapo pamoja na shughuli ya kukagua
zoezi hilo atahutubia wananchi.
HABARILEO
WAZIRI wa Ushirikiano wa Afrika
Mashariki, Dk Harrison Mwakyembe, amependekeza mfumo wa kupata wabunge
wa Bunge la Afrika Mashariki kutoka Tanzania, ubadilishwe.
Alisema hayo jana mjini hapa, wakati
akiwasilisha Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara yake kwa Mwaka wa
Fedha wa 2015/2016 katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
jana.
Kwa mujibu wa Dk Mwakyembe, ipo haja ya
kubadili mfumo wa kupata wabunge hao kutoka Tanzania, hasa kwa
kuzingatia ukweli kuwa Bunge la Afrika Mashariki ndicho chombo kikuu cha
kutunga sheria za Jumuiya.
Alifafanua kwamba sheria hizo kwa mujibu
wa Mkataba wa Uanzishwaji wa Jumuiya, zinapewa nguvu juu ya sheria za
nchi wanachama katika masuala ya utekelezaji wa mkataba huo.
Alisema wajumbe wa Bunge hilo
wanaruhusiwa kimkataba kuwasilisha hoja na miswada binafsi bungeni kwa
majadiliano na uamuzi, lakini fursa hiyo imetumiwa vizuri na wawakilishi
wa baadhi ya nchi wanachama kwa maslahi mapana ya nchi zao kuliko
ilivyo kwa wawakilishi wa Tanzania.
Kutokana na hali hiyo, alisisitiza
umuhimu wa Watanzania kuacha mfumo wa sasa wa kuwapata wabunge hao na
kuangalia mfumo utakaopeleka watu watakaokuwa wazalendo na watakaotetea
maslahi ya Tanzania, katika Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Kiingereza Waziri huyo aliongeza kwamba
kwa kuwa lugha rasmi ya Jumuiya ni Kiingereza na uamuzi ndani ya Bunge
hilo unatokana na ushawishi wa hoja unaotokana na ujuzi wa kutosha wa
lugha rasmi ya majadiliano, ni vyema Bunge libadili mfumo kabla Taifa
halijaharibikiwa kabisa.
“Tubadilishe mapema iwezekanavyo
utaratibu dhaifu na mbovu tuliouendekeza kwa muda mrefu wa kupata
wawakilishi wa Taifa letu kwenye chombo hiki adhimu.
“Mfumo huu hauzingatii kabisa uzito wa
majukumu yao, uwezo mkubwa kielimu/kiuelewa wa wawakilishi wenzao, na
mvutano mkali wa kimaslahi baina ya nchi wanachama unaotaka wawakilishi
makini, imara, wazalendo wenye ujuzi, uzoefu na weledi mtambuka na
umiliki wa kuridhisha wa lugha ya majadiliano bungeni,“ alisisitiza.
Alisema bila ya uamuzi huo wa makusudi,
taifa haliwezi kukwepa sifa ya kuwa wasindikizaji katika mchakato
unaoendelea wa mtangamano, ambao umeingia ngazi za kiweledi zaidi ambazo
ni Himaya Moja ya Forodha, Soko la Pamoja, Umoja wa Fedha na hatimaye
Shirikisho la Kisiasa.
Hati za kusafiria Akizungumzia hati
kusafiria ya Afrika Mashariki ambayo ilikuwa inatumika ndani ya jumuiya
pekee, Dk Mwakyembe alisema kuanzia Novemba mwaka huu itaanza kutumika
kimataifa.
Alisema hati hiyo iliyopandishwa hadhi
itaanza kutolewa baada ya uzinduzi wake ukataofanywa na wakuu wa nchi
wanachama katika mkutano wao unaotarajiwa kufanyika Novemba, mwaka huu.
Kwa mujibu wa Dk Mwakyembe, hatua hiyo
inakamilisha juhudi zilizoanza kufanywa tangu Novemba 2013, baada ya
maelekezo ya wakuu wa nchi wanachama waliotaka nchi hizo kukamilisha
majadiliano ya kuipandisha hadhi Hati ya Kusafiria ya Afrika Mashariki
kuwa ya Kimataifa ifikapo mwezi Novemba, 2015.
Kwa habari na matukio ni hpa hapa tangakumekuchablog, usiwe mbali nami
No comments:
Post a Comment