MWANANCHI
Zaidi ya watoto 600 wakimbizi kutoka
Burundi wamepotezana na wazazi wao katika harakati za kukimbia nchi yao
au kuhamishwa kutoka kambi moja kwenda nyingine mkoani Kigoma.
Baadhi ya watoto hao, walipotezana na
wazazi wao wakati wa kupanda meli za Mv Liemba na Mv Malagarasi kutokea
Burundi na wengine katika harakati za kwenda Kambi ya Nyarugusu.
Toka Mei Mosi, mwaka huu, Shirika la
Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi (UNHCR) linawasafirisha
wakimbizi hao kutoka kambi moja hadi nyingine kwa kutumia meli za Mv
Liemba na Mv Malagarasi. Hata hivyo, kutokana na idadi kubwa ya
wakimbizi katika kambi zote pamoja na utaratibu mbovu wa kuwahamisha
kutoka kambi moja kwenda nyingine.
Mfanyakazi wa Shirika la Uhamiaji la Kimataifa (IOM), Frederick Moses
alisema uhamishaji ulikuwa haufuati utaratibu maalumu kwa kuwa meli
moja kutoka Kagunga kwenda mjini Kigoma ilikuwa inabeba wanaume tu au
wanawake tu na nyingine watoto pekee hali iliyosababisha familia
kupotezana.
Takwimu kutoka Ofisi ya Ustawi wa Jamii
iliyopo katika kambi ya Uwanja wa Lake Tanganyika, zinaonyesha kuwa Mei
18, mwaka huu, watoto 53 walipotea, Mei 19 walipotea 124, Mei 20 (160),
Mei 21 (81), Mei 22 watoto 145 na Mei 24 walipotea watoto zaidi ya 20.
Hata hivyo, Mollel alisema Ustawi wa
Jamii kwa kushirikiana na Shirika la Plan International, Unicef na
Kamati ya Uokoaji ya Kimataifa (IRC), wanafanya kazi ya kuwatambua
watoto waliopotea au waliotengana na wazazi wao na kuwatafutia wazazi wa
muda wa kuwalea.
Msemaji wa Plan International, Emmanuel Kihaule alisema watoto hao huhifadhiwa hadi pale wazazi wao watakapopatikana na wale wagonjwa huwekwa katika uangalizi maalumu wa tiba.
“Wapo pia walioathirika kisaikolojia kutokana na kufanyiwa ukatili wa kijinsia, wako kwenye uangalizi maalumu,”.
Baadhi ya watoto hao walisema waliondoka
Burundi peke yao huku wengine wakisema walikuwa wanaishi mitaani mjini
Bujumbura na waliposikia mapigano wakaamua kufuata mkumbo wa kukimbia.
MWANANCHI
Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imetangaza ratiba ya Uchaguzi Mkuu kwamba Agosti 21, mwaka huu itakuwa ni siku ya uteuzi wa wagombea urais, ubunge na udiwani.
Katika taarifa yake kwa vyombo vya habari juzi, Mwenyekiti wa NEC, Jaji mstaafu, Damian Lubuva alisema tume hiyo imetoa ratiba hiyo kwa mamlaka iliyopewa na sheria.
“Tume inapenda kuviarifu vyama vya siasa
na wananchi wote kuwa ratiba hii inatolewa kwa mamlaka iliyopewa kwa
mujibu wa vifungu vya Sheria ya Taifa ya Uchaguzi.
Lubuva alisema vyama vya siasa vitafanya kampeni za uchaguzi kwa siku 64 kuanzia Agosti 22 hadi Oktoba 24, mwaka huu.
Jaji Lubuva alisema siku ya kupiga kura itakuwa Oktoba 25 kama Katiba ya Jamhuri ya Muungano inavyosema.
Katiba inasema Uchaguzi Mkuu utafanyika
Jumapili ya mwisho wa mwezi Oktoba ya mwaka wa tano tangu ulipofanyika
Uchaguzi Mkuu wa mwisho.
Wakati tume ikitangaza ratiba, vyama vya
siasa vimeanza mchakato wa kupata viongozi wa ngazi mbalimbali huku CCM
na Chadema vikitangaza siku ya kupata wagombea urais kupitia vyama
vyao. Juzi, CCM iliweka ratiba ya kupata viongozi ndani ya chama hicho
na ikatangaza kuwa kuwa Julai 12, mwaka huu mgombea urais kupitia chama
hicho atajulikana.
Chadema pia kimeshatangaza ratiba ya
uchaguzi ndani ya chama hicho kuwa mgombea urais atajulikana Agosti 4,
mwaka huu. Mgombea huyo ataingia kwenye kinyang’anyiro cha kumtafuta
mgombea wa vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA).
Chama cha Tanzania Labour (TLP), kimeshamteua, Macmillan Lyimo
kuwa mgombea wake wa urais katika Uchaguzi Mkuu utakaofanyika Oktoba
mwaka huu. Lyimo alipitishwa kuwania nafasi hiyo katika Mkutano Mkuu wa
Taifa wa chama hicho uliofanyika jijini Dar es Salaam.
Kwa upande wa chama cha NCCR – Mageuzi,
fomu za kugombea nafasi mbalimbali za uongozi zimeanza kutolewa na Mkuu
wa Idara ya Itikadi na Uenezi wa chama hicho, Dk George Kahangwa amechukua fomu za kugombea urais.
MWANANCHI
Rais Jakaya Kikwete amewataka vijana wa
CCM kutokuwa makuwadi na madalali wa wagombea urais katika Uchaguzi
Mkuu utakaofanyika Oktoba, mwaka huu.
Rais Kikwete aliyasema hayo mjini hapa
jana alipokuwa akifungua mkutano mkuu wa kwanza wa Shirikisho la
Wanafunzi wa Vyuo vya Elimu ya Juu wa CCM.
“Vijana
wasigeuke kuwa makuwadi wa kuwahonga vijana wenzao ili wamchague mtu
fulani. Kwa kufanya hivyo watakuwa wametoka kabisa nje ya mstari…“Tunataka vijana watakaosema tunatafuta viongozi wa Taifa hili, ila watu wa aina hii hapana,” Kikwete.
Alisema lengo la kuanziasha shirikisho
hilo ni kuwaandaa vijana hao ili waujue uongozi na waweze kuwa viongozi
wazuri katika siku za baadaye.
“Viongozi
wa vijana wanasafirishwa wanaletwa hapa Dodoma kwa ajili ya kumsikiliza
mzee fulani, ndiyo maana siku hizi hoja ya vijana siyo tishio kwa mtu
yeyote kwa sababu hawana mawazo ya kutoa kwa ajili ya kukijenga chama na
Taifa,” .
Pia, aliwataka vijana hao kuhakikisha CCM inaendelea kushika dola katika Uchaguzi Mkuu ujao kwa kuwa hilo ndilo jukumu lao.
MWANANCHI
Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa hana mpango wa kuhama Chama Cha Mapinduzi (CCM) na iwapo kuna mtu anamchukia ndani ya chama hicho, ni vyema akahama kwa sababu yeye hana mpango huo.
Lowassa alitoa kauli hiyo alipozungumza
na wahariri wa vyombo vya habari nyumbani kwake mjini Dodoma jana ambako
alieleza mambo mbalimbali kuhusu afya yake, suala la Richmond, elimu,
ajira, utajiri wake na hali ya kisiasa kwa ujumla.
Hata hivyo, Mbunge huyo wa Monduli
hakutaka kujibu maswali mengi kwa madai kuwa atazungumza Jumamosi mjini
Arusha atakapotangaza nia yake ya kugombea urais.
Alipoulizwa iwapo yupo tayari kuhama CCM na kwenda upinzani asipopitishwa na chama hicho kuwania urais alisema: “Sina
mpango wa kuhama chama changu, sina plan B, mimi ni plan A tu, tangu
nimemaliza Chuo Kikuu mwaka 1977 nimekuwa mwana-CCM, sijafanya kazi nje
ya CCM ukiondoa miaka ambayo nilikuwa vitani Uganda na nilipohamishiwa
Kituo cha Mikutano cha Arusha (AICC). Maisha yangu yote yapo CCM.
“Kama kuna mtu ambaye hanitaki ndani ya CCM, yeye ndiye ahame, siyo mimi,” alisema.
Lowassa aliyejiuzulu uwaziri mkuu mwaka
2008 kutokana na kashfa ya mtambo wa kufua umeme wa Richmond, alisema
kimya chake baada ya tukio hilo kilitokana na siasa nyingi za uhasama na
kutishiana.
“Nilinyamaza
ili kuipa muda Serikali ifanye kazi yake…. sikupenda kuzungumza kwa
sababu ya siasa nyingi za uhasama na kutishiana kwingi, kuna
kusingiziana kwingi, kufitiniana kwingi. Kukaa kimya ni jambo gumu sana
kwa mwanasiasa, lakini nashukuru Mungu niliweza hilo,” alisema Lowassa ambaye Jumamosi atatangaza nia ya kuwania urais mjini Arusha.
Alipoulizwa kuhusu madai kuwa afya yake inaterereka, alisema anaamini yupo fiti na akashauri wagombea urais wote wakapimwe.
“Hata nikikimbia kilomita 100 watasema
mimi mgonjwa. Hivi karibuni nilitembea kilomita tano na albino jijini
Dar es Salaam, kuna watu wakasema nimechoka sana, nimepata ‘stroke’ na
nimekimbizwa Ujerumani kutibiwa, huo ni upuuzi mtupu.Kuna chuki imeingia katika siasa zetu na kutakiana mabaya.
Afya ni
neema kutoka kwa Mungu tu. Napenda kuwahakikishia kuwa nipo fiti na
nipo fiti na kwa lolote. Nadhani ni wakati sasa kwa chama chetu waweke
utaratibu wanaogombea nafasi hii ambayo nitaitangaza Jumamosi, tukapime
wote afya na mimi nitakuwa wa kwanza kujitokeza kwenda kupima.
NIPASHE
Rais Jakaya Kikwete amemteua Anthony Peter Mavunde kuwa Mkuu wa Wilaya ya Mpwapwa, Mkoa wa Dodoma, kuanzia jana.
Aidha, Rais Kikwete amefanya uhamisho wa
wakuu 10 wa wilaya kwa nia ya kuongeza ufanisi katika uongozi wa Wilaya
mbali mbali nchini.
Taarifa ya Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais Ikulu ilieleza kuwa, katika mabadiliko hayo, Rais Kikwete amemhamisha Luteni Edward Ole Lenga kutoka Wilaya ya Mkalama, Mkoa wa Singida kwenda kuwa mkuu wa wilaya mpya ya Kyerwa, Mkoa wa Kagera.
Luteni Lenga anachukua nafasi iliyoachwa wazi na Luteni Kanali Benedict Kulikela Kitenga ambaye alifariki dunia Aprili 20, mwaka huu, 2015.
NIPASHE
Mwenyekiti Mtendaji wa IPP, Dk. Reginald Mengi,
ameeleza kusikitishwa dhidi ya majibu yaliyotolewa na Kurugenzi ya
Mawasiliano ya Rais Ikulu kuhusu taarifa za kamchafua zilizochapishwa na
gazeti la Taifa Imara Machi 20, mwaka huu.
Dk. Mengi, alisema jana kuwa majibu yaliyotolewa na Mkurugenzi wa Kurugenzi hiyo, Salva Rweyemamu, siyo ya busara kwani yanapuuza usalama wa maisha yake.
“Majibu
haya ya Salva yanaongeza hofu ya usalama wa maisha yangu jambo ambalo
siyo dogo na la kupuuzwa kama anavyoona yeye,” alisema Dk. Mengi na
kuongeza:
“Ukiangalia,
ukisoma kiundani majibu ya barua ya Rweyemamu, nina kila sababu ya
kuhofia usalama wa maisha yangu. Shughuli zake Ikulu ni za kuheshimiwa,
lakini awe na busara katika shughuli zake….kunishauri eti niende polisi
kuhusu suala hilo ni kama kunifanya nionekane sina busara kama yeye.”
Alisema uhai wa mtu siyo jambo dogo wala
siyo la kupuuzwa na kwamba busara ilihitajika katika kushughulikia
suala hilo, lakini haikuwa hivyo kwani majibu hayo yamesababisha tatizo
hilo dhidi ya usalama wa maisha yake kuwa pale pale.
Machi 23, mwaka huu, gazeti la Taifa Imara,
lilichapisha habari iliyoeleza kuwa, Kiongozi Mkuu wa ACT Wazalendo,
Zitto Kabwe, alimchongea Dk. Mengi kwa Rais Kikwete, kwamba ndiye kinara
wa kuihujumu serikali yake na alikuwa anamshawishi Zitto kujiunga na
mipango hiyo.
Habari hiyo iliendelea kudai kuwa, Dk.
Mengi aliapa kumshughulikia Rais Kikwete kwa nguvu zake zote amalizapo
muda wake wa urais huku Rais Kikwete naye akiapa kupambana na yeye (Dk.
Mengi).
Dk. Mengi alisema majibu yaliyotolewa
na kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais Ikulu, yalieleza kuwa Rais hakuwahi
kuwa na mawasiliano na Zitto Kabwe kama ilivyoelezwa na kwamba
haikufanya lolote kutokana na kubanwa na majukumu, hivyo kupuuza habari
hizo kwa kuziona ni ndogo na za upuuzi.
NIPASHE
Unyonge na umaskini uliopo nchini kwa
sasa umechangia kusababisha Watanzania wengi kuendelea kuonewa na
kunyanyasika na wengi wao wakijazana magerezani kwa kukosa fedha za
kuwahonga wenye mamlaka mbalimbali ili wasionewe.
Kauli hiyo ilitolewa na Mwanasheria Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Tundu Lissu, alipokuwa akizungumza katika mkutano wa hadhara juzi katika viwanja vya Halmashauri ya Mji wa Bariadi mkoani Simiyu.
Lissu alisema unyonge ulioambatana na
umaskini wa Watanzania, ndiyo unaowasababishia maumivu makubwa katika
maisha yao na kufanya Taifa lililokosa mwelekeo.
Alisema mbali na kukabiliwa na unyonge
huo, zaidi ya asilimia 80 ya Watanzania waliojaa magerezani ni wale
maskini walioshindwa kutoa rushwa kwa askari polisi, wakuu wa vituo na
mahakama pindi walipokamatwa kwa kutenda kosa au kusingiziwa.
Lissu alifafanua asilimia hiyo 80 ya
waliopo gerezani ni wale ambao walishindwa kutoa rushwa kutokana na hali
walizokuwa nazo za kukosa fedha ili kesi zao zifutwe na zisifikishwe
mahakamani.
Hata hivyo, alisema chanzo cha hayo yote ni nchi kuongozwa na viongozi wasiojali maslahi ya wananchi.
Aliongeza kuwa nchi imebadilika na kuwa ya unyonyaji, uonevu na yenye kupuuzia mawazo na maamuzi ya Watanzania.
“Ninapozungumzia
nchi imebadilika, namaanisha nchi inaongozwa na baadhi ya wanaoiba
fedha za wananchi katika mbolea, pembejeo, dawa, karo za watoto wa
Watanzania, barabara na maji… kwa hali hii tunataka mapinduzi ili
tuondokane na haya,” alisisitiza.
NIPASHE
Serikali imelaumiwa kuwa imeshindwa
kuweka mkazo katika kuwalinda watu wenye ulemavu wa ngozi (albino) kama
inavyofanya kwa wanyama kama tembo hali inayosababisha mauaji ya watu
hao kuendelea nchini.
Aidha, Serikali imelalamikiwa kwa
kuzitengea fedha kidogo Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto
na Wizara ya Kazi na Ajira ambazo haziwezi kusaidia kutekeleza miradi ya
maendeleo katika wizara hizo.
Mbunge wa Viti Maalum (CUF), Riziki Omari Juma,
alisema mauaji ya albino yamekuwa yakijitokeza mara kwa mara hali
inayozua maswali kwa wananchi kuhusu mahali Taifa linapopelekwa.
Juma aliitaka serikali iweke utaratibu
wa kuwalinda watu wenye ulemavu wa ngozi badala ya kuendelea kufanya
uchunguzi kusaka wahalifu kila unapotokea uhalifu.
“Kila siku matukio ya albino kukatwa
viungo na wengine kuuawa yanatokea, lakini hatuoni serikali ikichukua
hatua kuwalinda, tembo wanalindwa sana na ikitokea ameuawa mmoja tu
wahalifu wanasakwa, lakini albino akiuawa hakuna hatua zinazochukuliwa,”
alisema.
Juma aliitaka serikali kufuatia
wafanyakazi wa ndani ambao wamekuwa wakinyanyaswa na mama na baba mwenye
nyumba kwa kulipwa ujira kidogo.
HABARILEO
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe ametangaza rasmi nia yake ya kuwania Urais wa Tanzania katika Uchaguzi Mkuu ujao.
Hata hivyo, akizungumza katika kipindi
cha Nyumba ya Jirani kinachorushwa na televisheni ya taifa, TBC I juzi
usiku, Membe alisema ataanika kila kitu akiwa kijijini kwao Rondo, Lindi
Vijijini mkoani Lindi.
“Nitatangaza
nia yangu kijijini kwetu nilikozaliwa. Kule ambako nilianza kupata
mwanga wa elimu niliyonayo. “Kule nilikotokea hadi kwenda Usalama wa
Taifa, kule nilikotokea na kuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa
Kimataifa. Hata safari nyingine (ya kuwania Urais), ni vyema ikawa na
baraka za wazee kule ninakotoka, ndiyo maana nasema nakwenda kutangazia
nia kijijini kwetu.”
Membe ni mmoja wa makada mashuhuri wanaotajwa kuwania Urais kwa tiketi ya CCM.
Wengine wanaotajwatajwa ni Waziri Mkuu wa sasa, Mizengo Pinda, mawaziri wakuu wa zamani, Frederick Sumaye na Edward Lowassa, Steven Wassira, Lazaro Nyalandu, Profesa Mark Mwandosya na January Makamba waliomo katika Baraza la Mawaziri la Rais Kikwete na William Ngeleja, aliyewahi kuwa waziri katika serikali ya Kikwete na Dk Hamisi Kigwangallah, Mbunge wa Jimbo la Nzega.
MTANZANIA
Mjadala wa Kikao cha 12 cha Bunge la
Bajeti jana ulitawaliwa na vilio vya kamati za Bunge na wabunge kuhoji
sababu za Wizara ya Maendeleo ya Jamii Jinsia na Watoto kupewa fedha
kidogo ya maendeleo, huku Wizara ya Kazi na Ajira ikikosa kabisa fungu
kutoka Hazina.
Wamesema hali hiyo inasababisha wizara
hizo kutokuwa na jipya katika kuiendeleza nchi, ikiwa ni pamoja na
kumaliza tatizo la ajira nchini.
Akiwasilisha maoni ya Kamati ya Bunge ya Maendeleo ya Jamii kuhusu bajeti ya Wizara ya Kazi na Ajira, mjumbe wa kamati hiyo Maua Daftali alisema katika bajeti ya mwaka 2014/15, wizara hiyo haikupewa hata shilingi moja ya fedha za maendeleo.
“Bajeti ya wizara hii mwaka 2014/15 ni Sh17 bilioni, kati ya hizo
Sh5.8bilioni zilikuwa kwa ajili ya kulipa mishahara, Sh8.9 bilioni kwa
ajili ya matumizi mengine na Sh2.9 bilioni kwa ajili ya maendeleo,” alisema.
Alifafanua kuwa hadi Aprili mwaka huu,
fedha za mishahara zilizotoka ni Sh4.7bilioni, matumizi mengine zilitoka
ni Sh2.6 bilioni na hakukuwa na fedha yoyote ya bajeti ya maendeleo
iliyotolewa.
Kwa habari motomoto na za uhakika ni hapa hapa tangakumekuchablog
No comments:
Post a Comment