Sunday, May 31, 2015

SOMA MAKUBWA YALIYOANDIKWA NA MAGAZETI YA LEO, MAY 31 TZ

Uchambuzi huu wa magazeti unaletwa kwenu kwa hisani kubwa ya kituo cha Elimu Cha Candle Education Centre Tanga, kituo kinaongoza kufaulisha wanafunzi kidato cha pili hadi cha sita na wale wanaojiendeleza kielimu. Kituo kimesajiliwa na NECTA  na kiko na Hostel. Wapo Tanga mkabala na Bank ya CRDB simu, 0715 772746

J2MWANANCHI
Waziri Mkuu wa zamani, Edward Ngoyai Lowassa amesema ana ari, shauku na uwezo wa kuongoza Taifa wakati alipotangaza nia yake ya kugombea urais kwa tiketi ya CCM katika mkutano wa hadhara uliohudhuriwa na maelfu ya watu kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid.
Lowassa, ambaye ni mbunge wa Monduli akihutubia maelfu ya wakazi wa Arusha, katika Uwanja a Sheikh Amri Abeid Aluta, alisema ameamua kujitokeza tena kuwania urasi kwa kuwa anaamini yeye ndiye mtu sahihi wa kuiongoza nchi wakati huu.
Zaidi ya watu 30,000 walifurika kwenye uwanja huo wakiwa wamekaa kwenye viti na wengine ndani ya kiwanja cha mpira huku, mwanasiasa mkongwe nchini, Kingunge Ngombare Mwiru akiongoza mlolongo wa watu mashuhuri waliojitokeza kumuunga mkono mbunge huyo wa Monduli katika mbio za kuelekea Ikulu anazoziita “safari ya Matumaini”.
Akihutubia mkutano huo, Lowassa alisema pamoja na kuwa viongozi waliopita wameliongoza taifa hili vizuri, bado linahitaji kiongozi mwenye uthubutu na uongozi madhubuti unaoweza kufanya maamuzi magumu.
“Kuamini kama una uwezo na shauku, hakuna budi kwenda sambamba na uwezo wa kusimamia yale unayoyaamini. Na kwangu haya mawili ni dhahiri. Nina ari, nina shauku na nina uwezo, kama rekodi yangu inavyothibitisha,” alisema Lowassa huku akishangiliwa.
“Tunapomtafuta Rais wa Jamhuri ya Muungano ni lazima tukumbuke kwamba tunamtafuta mtu ambaye atakuwa pia ni Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama katika nchi yetu. Na kwa Chama cha Mapinduzi tunamtafuta mtu ambaye atakuwa pia mwenyekiti wa chama chetu.
“Naamini kwa vigezo vyote, nina kila sifa ya kubeba dhamana hizo nzito. Katika mambo ambayo najivunia, na sitayasahau katika historia yangu ni kushiriki kwangu kuilinda nchi yetu pale nilipohitajika. Nilishiriki kikamilifu katika Vita vya Kagera nikiwa miongoni mwa askari wa mstari wa mbele wa mapambano.”
Lowassa pia alikumbusha tukio la mwaka 1995 alipojitokeza kugombea urais kwa pamoja na Rais Jakaya Kikwete.
“Natarajia safari hii, Kikwete ataniunga mkono.”
Hata hivyo, Kikwete hakupitishwa na CCM mwaka huo na akagombea peke yake 2005, mwaka ambao Lowassa alisema aliamua kwa dhati kumuunga mkono mwenzake.
MWANANCHI
Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imesema uandikishaji wa wananchi kwenye Daftari la Wapigakura nchini utamalizika mwishoni wa mwezi ujao baada ya mashine 1,600 zaidi za kielektroniki kwa ajili ya kazi hiyo kuwasili juzi.
Ofisa ugavi mwandamizi wa NEC, Datus Matuma alisema mashine hizo zinazotumia teknolojia ya utambuzi wa alama za mpigakura (Biometric Voter’s Registration), zitaanza kupelekwa mikoa ya Mara, Arusha, Manyara na Kilimanjaro.
“Ule uvumi ambao ulikuwa ukienea nchini kwamba Tume ya Taifa haiwezi kumaliza uandikishaji, sasa umefikia mwisho kwani hizi mashine ni za kisasa na zitaanza kazi moja kwa moja kwenye mikoa hiyo niliyoitaja na mwishoni mwa mwezi Juni au mwanzoni mwa mwezi wa Julai watu wote watakuwa wameshaandikishwa,” Matuma.
Alisema wananchi wajitokeze kwa wingi kujiandikisha ili wasikose haki yao ya msingi ya kupiga kura kwani kila aliyefikisha umri wa kupiga kura anatakiwa kujiorodhesha kwenye daftari hilo.
Alisema Serikali ni sikivu ndio maana imekata kiu ya Watanzania kwa kuleta mashine hizo ambazo sasa zimefikia 8,000 na zinakidhi kabisa mahitaji ya Watanzania wote kwani zinafika kila mkoa na zitagawiwa kwenye halmashauri kwa ajili ya kuzisambaza kwenye vituo vya uandikishaji .
Hata hivyo, mwezi uliopita NEC ilitangaza kwamba hakuna mpango wowote wa kuahirisha Uchaguzi Mkuu na kusisitiza kuwa utafanyika kama ilivyopangwa.
MWANANCHI
Mjadala wa Bajeti ya Wizara ya Uchukuzi jana uligeuka shubiri kwa Waziri Samuel Sitta wakati alipobanwa na wabunge kutokana na Serikali kushindwa kuboresha usafiri wa reli na anga.
Wabunge hao, mbali na kuibua ufisadi mbalimbali unaofanywa na watendaji wa Serikali, wakiwamo wa wizara hiyo, walihoji sababu za Serikali kuwa na ndege moja tu na kushindwa na nchi ndogo ya Rwanda ambayo ina ndege saba za serikali.
Licha ya kuipitisha, walisema kuwa nchi bila kuwa na usafiri unaoeleweka wa reli, anga na barabara ni vigumu kupata maendeleo.
Akichangia mjadala huo, mbunge wa Kawe, (Chadema), Halima Mdee aliibua suala la ukiukwaji wa mauzo ya nyumba za Shirika la Reli Tanzania na Zambia (Tazara), kwamba mbali na ukiukwaji wa mauziano na ununuzi, pia mfanyabiashara aliyenunua nyumba hizo amekwepa kodi ya Serikali inayokadiriwa kufikia Sh4 bilioni
Haiwezekani, tuna taarifa hizo, nyumba zimeuzwa kwa bei ya soko na Serikali pia ilipaswa kupata kodi yake inayofikia wastani wa Sh4 bilioni… Serikali hii ni ya aina gani ambayo kila mwaka kuna kashfa za ufisadi katika wizara zake,”  Mdee.
Mbunge wa Kigoma Kusini (NCCR-Mageuzi), David Kafulila, alisema katika serikali ya Awamu ya Nne kila wizara inakabiliwa na wizi, akifafanua jinsi Mamlaka ya Manunuzi Nchini (PPRA) ilivyoshindwa kufuata vigezo ya ununuzi wa mabehewa 124 ya Kampuni ya Reli (TRL).
Alivitaja vigezo hivyo kuwa ni pamoja na utangazaji wa zabuni kutozingatiwa na pia kutofanyika kwa uchunguzi.
Alisema waziri wa uchukuzi na katibu mkuu wa wizara hiyo na waziri wa fedha ambao ndio waidhinishaji wa fedha hizo za ununuzi wa mabehewa wanatakiwa kuwajibika. Alisema suala hilo linalohusu Sh230 bilioni haliwezi kufunikwa na kupita.
Alisema Rwanda ni nchi ndogo lakini ina ndege saba wakati Tanzania ni nchi kubwa lakini ina ndege mmoja tena inahitaji matengenezo kila siku.
MWANANCHI
Mwenyekiti wa kamati ya Ulinzi na usalama Wilayani Bukombe Amani Mwenegoha amesematangu kutokea kwa mauaji ya mtoto albino Yohana Bahati Wilayani Chato, kumeibuka madai mbalimbali ya utapeli na vitisho vinavyofanywa na watu wenye ulemavu huo.
Mwenegoha alisema kuna utapeli unadaiwa kufanywa na wasichana wenye ulemavu wa ngozi wanaofanya biashara ya kujiuza miili yao Wilayani humo.
Imedaiwa kuwa wasichana hao huwageuka wanaume wanapofika kwenye nyumba za kulala wageni licha ya kukubaliana toka awali.
Kuna taarifa ambazo zimetufikia ofisini kwetu kwamba hawa wasichana wanasimama barabarani sehemu za vichochoro wakiona wanaume wakawapenda wanawaita na kuwalazimisha wawape fedha, wakikataa wanapiga kelele na kudai kuwa wanataka kuwakata viungo vyao”Mwenegoha.
Pia wanapokuwa kwenye biashara yao ya kujiuza wanapokutana na wanaume hukubaliana kiwango cha fedha, lakini wanapofika ndani hubadilika na kuwalazimisha watoe fedha zaidi ya makubaliano na wakikataa kuwa wanataka kukatwa viungo.
NIPASHE
Watu wawili wamefariki dunia mkoani Simiyu katika matukio tofauti akiwamo mtoto wa miezi mitatu aliyenyakuliwa na fisi akiwa mgogoni mwa mama  yake.
Kamanda wa Polisi  wa  mkoa wa Simiyu, Gemin Mushy  jana alisema  kuwa mtoto Ng’wanza Samwel, akiwa amebebwa na  mama  yake alinyakuliwa na fisi Mei 25, majira ya saa 1;30 jioni katika kijiji cha Ngugunu,Tarafa ya Kisesa wilayani Meatu.
Alisema katika kufuatilia tukio hilo, mabaki ya mtoto huyo yalipatikana mita 200 tu fisi kutoka eneo alilonyakuliwa huku kichwa, kifua, tumbo, mikono na miguu  ikiwa haipo.
Katika tukio jingine mpanda baiskeli aliyefahamika kwa jina la Magina Supa(20), mkazi wa Nyaumata mtaa wa Kisiwani wilayani Bariadi, aliuawa kwa kukatwa na kitu chenye ncha kali shingoni na bega la kushoto na mtu aliyekuwa amempakiza kama abiria wake.
Akifafanua, Kamanda  Mushy alisema kuwa tukio  hilo lilitokea Mei 26 majira saa 1;00 jioni katika mtaa wa Izunya, kata ya Somanda tarafa ya Ntuzu wilayani Bariadi kwa mtuhumiwa wa mauaji hayo anayedaiwa kuwa abiria wa mpanda baiskeli huyo aliyekuwa  anajishughulisha na biashara ya daladala ya baiskeli.
Kamanda huyo alisema kuwa mara  baada ya mauaji hayo, mtuhumiwa ambaye hajafahamika na anasakwa baada uhalifu huo alitoroka. Chanzo cha mauaji hayo  hakijafahamika.
NIPASHE
Walemavu wa aina mbalimbali karibu milioni nne huenda wasipige kura kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka huu kutokana na kukosekana vifaa vya kuwawezesha kushiriki  zoezi hilo.
Baadhi ya vifaa hivyo ni kama maandishi ya nukta nundu kwa wasioona,  hadi sasa  havijanunuliwa.
Kamishna wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec), Jaji Mstaafu John Mkwawa, alisema  matarajio ya kupatikana kwa vifaa hivyo yanasubiri kufunguliwa zabuni katikati ya mwezi ujao.
Alitoa maelezo hayo  baada ya kuulizwa iwapo  Nec ina vifaa vya kuwasaidia walemavu hao na kama wamepewa elimu kuhusu matumizi ya  vifaa hivyo, kwa vile mwaka 2010 walilalamikia ukosefu wa elimu na vifaa vya kuwawezesha kushirika zoezi hilo.
Jaji Mkwawa alisema jitihada zinafanywa na tangazo la kutafuta wazabuni wa kuagiza vifaa hivyo lilitolewa Mei 12, mwaka huu kwenye vyombo vya habari.
Alisema idadi ya walemavu wenye sifa za kupiga kura mwaka huu ni milioni nne hivyo Nec  haipo tayari kuwakosesha haki wananchi hao.
Kuhusu suala la utoaji wa elimu kwa watu hao ambalo mwaka 2010 walilikosa, Jaji Mkwawa aliahidi kueleza zaidi taarifa hizo kabla ya kupatikana vifaa hivyo.
Hata hivyo, alipoulizwa idadi ya vifaa wanavyokusudia kuviagiza, Jaji Mkwawa alisema  ni mapema kulielezea kabla ya zabuni kufunguliwa.
NIPASHE
Hatima ya Mpango wa Taifa wa Damu Salama (NBTS) upo kwenye hati hati  baada ya mfadhili mkuu aliyekuwa anagharamia uendeshaji wake kuondoka rasmi leo na kuiacha ikichechemea.
Serikali ya Marekani kupitia kituo cha Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa (CDC), ilikuwa akigharamia sehemu kubwa ya mishahara ya wafanyakazi, vifaa vya kuhifadhia na kusafirishia damu.
Uchunguzi wa umebaini kuwa, NBTS ina hali mbaya kwa vile mafadhili anaiacha  wakati benki hiyo  inakabiliwa na uhaba wa damu ambayo ni tegemeo kwa  wagonjwa waliopo mahospitalini hasa wanawake wajawazito, wazazi na watoto wachanga.
Msemaji wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, Nsachris Mwamwaja, alikiri kujitoa kwa mfadhili huyo na kuongeza kuwa, serikali imejipanga kukabiliana na changamoto hiyo ikiwa ni pamoja kubeba mzigo wote wa ulipaji mishahara kwa wafanyakazi na kuhakikisha  damu na vifaa vinavyohitajika vinakuwepo wakati wote.
“Tunatambua umuhimu wa damu kwa wagonjwa, hata bajeti yetu itakayowasilishwa keshokutwa bungeni tutalitilia mkazo suala hili kwa sababu mfadhili huyu alikuwa anatusaidia na sasa amejitoa hivyo hatuna jinsi,”.
Kuhusu uhaba wa damu, aliwataka Watanzania kujitokeza kuchangia damu kwa sababu mahitaji yake ni makubwa na kila mtu anaweza kuhitaji msaada huo.
“Suala la damu halihusiani na mfadhili bali watu wajitolee kwa sababu damu inasaidia kila mtu bila kujali ni nani unacheo gani, niwaombe muwe na utaratibu wa kuchangia damu ili tuokoe maisha ya watoto, wanawake, wanaume, wazee,” alihimiza.
NBTS imekuwa ikitegemewa kusambaza vitenganishi kwenye kanda zake sita ambazo ni Mwanza, Moshi, Tabora, Mbeya, Mtwara na Dar es Salaam.
HABARILEO
Maofisa watano wa Serikali, wanatarajiwa kupandishwa kizimbani hivi karibuni, kutokana na kashfa ya uagizaji wa mabehewa 274 kutoka India, huku wengine wakitarajiwa kuchukuliwa hatua za kiutawala.
Waziri wa Uchukuzi, Samuel Sitta, ameliambia Bunge jana kuwa Kamati Maalumu iliyoundwa na wizara yake, imemaliza kazi na kumkabidhi ripoti hiyo.
“Wamenikabidhi ripoti juzi na iliundwa na watu wa Ofisi ya CAG, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Takukuru  na wahandisi,” alisema Sitta.
Alikuwa akifanya majumuisho ya hoja za wabunge kuhusu makadirio ya bajeti yake kwa mwaka wa fedha 2015/16, ambayo aliyawasilisha bungeni jana asubuhi na kupitishwa na Bunge baadaye mchana.
Waziri huyo mkongwe alisema kamati hiyo ilienda hadi Calcutta, India ambako mabehewa hayo 274 yalitengenezwa na kwa mujibu wake, mabehewa hayo si chakavu, kama ilivyodaiwa awali.
Hata hivyo alisema “kuna makosa mawili hapa ambayo ni uzembe wa pande mbili, waagizaji na watengenezaji. Kuna tatizo katika specification (vipimo). “Hapa kuna majina ya watu wote waliohusika katika suala hili.
Watano tunawapeleka mahakamani, wengine tutawachukulia hatua za kiutawala.” Aidha, aliweka bayana kuwa katika maofisa hao watano watakaopelekwa mahakamani, wawili ni wanachama wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA).
Aidha, Sitta alisema si kweli kuwa hasara iliyopatikana ni Sh bilioni 200, bali ni Sh bilioni 12 na wote waliohusika watachukuliwa hatua stahili. “Pia tumemwomba Mwanasheria Mkuu ili sehemu ya hasara hii ibebwe na mtengenezaji na nyingine itabebwa na Serikali kutokana na uzembe uliofanyika,” Sitta.
Kwa habari, matukio na burudani ni hapa hapa tangakumekuchablog

No comments:

Post a Comment