MWANANCHI
Kamati Kuu ya CCM, ambayo ndiyo
inaanzisha mambo yote muhimu ya chama hicho, leo inakutana kuandaa
ajenda za mkutano wa Halmashauri Kuu, huku suala linalosubiriwa kwa hamu
likiwa ni hatima ya makada sita wanaotajwa kuwania urais ambao
wanatumikia adhabu ya kuzuiwa kujihusisha na uchaguzi.
Kwa mara ya kwanza, CCM inakabiliwa na
kazi ngumu ya kuamua hatima ya makada iliowafungiwa katika kipindi
muhimu cha kuteua mgombea mpya wa urais kutokana na mwenyekiti wa sasa
wa chama hicho, Jakaya Kikwete kutoweza kugombea nafasi hiyo kwa kipindi cha tatu kutokana na matakwa ya kikatiba.
Mmoja wa watu walio karibu na uongozi wa
chama hicho aliiambia Mwananchi jana kuwa CCM imejikita zaidi katika
kutafuta mwanachama atakayekipa ushindi kwenye Uchaguzi Mkuu, lakini
suala la makada waliofungiwa ambao baadhi yao wanapewa nafasi kubwa ya
kupitishwa, halitachukua muda mrefu kulijadili.
Kikao hicho kitafanyika kwenye ukumbi wa
Halmashauri Kuu uliopo jengo la makao makuu ya CCM mjini hapa, maarufu
kama White House mjini Dodoma.
Ukumbi huo una historia ya muda mrefu
ndani ya CCM ya kutolewa kwa uamuzi mgumu katika matukio kadhaa ya
kisiasa, ukiwamo ule ulioweka historia ya Aboud Jumbe kuingia akiwa Rais
wa Zanzibar na mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, lakini akatoka bila
cheo chochote mwaka 1984.
Pia kwenye ukumbi huo kulifanyika uamuzi
wa mambo mengine makubwa, hasa nyakati za kuchuja wagombea urais au
uongozi wa chama, mambo ambayo pia yanaweza kutokea katika vikao
vinavyoanza leo au vya baadaye.
Alipoulizwa kuhusu kikao hicho jana, katibu wa itikadi na uenezi wa CCM, Nape Nnauye
alisema Rais Kikwete ataongoza kikao cha leo kilichopangwa kuanzia saa
4:00 asubuhi na kwamba maandalizi yamekamilika, huku baadhi ya wajumbe
wakiwa wameshawasili.
Alipoulizwa kuhusu nini wategemee
wanachama na wananchi, Nape alijibu kwa kifupi kuwa watarajie kuwa “CCM
watatoka wakiwa kitu kimoja” kuliko inavyotarajiwa na wengi.
Hata hivyo, mbali na hofu kuhusu hatua
za kinidhamu kwa wajumbe walioadhibiwa kwa kuanza kampeni mapema na
kukiuka maadili, taarifa nyingine kutoka kwa baadhi ya wajumbe wa vikao
hivyo zilidai kuwa mkutano huo utajikita zaidi kuangalia utaratibu mzima
wa kuchukua fomu za wagombea wote wa urais, ubunge na udiwani.
“Vikao hivi vinaangalia utaratibu tu wa
jinsi ya kuchukua fomu na wala havitagusia suala la mchujo wa wagombea
urais wala ubunge,” alisema mtoa taarifa huyo.
Kamati Kuu imetanguliwa na vikao vya mfululizo vya Sekretarieti na Kamati ndogo ya Kanuni.
Kamati ya Kanuni na Maadili ilitarajiwa kukutana jana usiku au leo asubuhi kabla ya Kamati Kuu.
MWANANCHI
Kitendo cha Chama cha Wananchi (CUF)
kufanya uchaguzi wa Kura za Maoni katika majimbo ya Kawe na Ubungo
yanayoshikiliwa na wabunge wa Chadema, kimeibua hisia tofauti miongoni
mwa vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa).
Mvutano huo unatokana na kinachoelezwa
ni makubaliano ya vyama hivyo kuwa kila kimoja kiandae wagombea wake
katika majimbo yote ambao watashindanishwa katika Ukawa, bila kuhusisha
majimbo ambayo tayari yana shikiliwa na vyama vinavyounda umoja huo.
Mbali na kigezo hicho, mgawanyo wa
majimbo unazingatia matokeo ya uchaguzi wa mwaka 2010, idadi ya madiwani
kwa kila chama, matokeo ya uchaguzi wa Serikali za Mitaa 2014, mtandao
wa chama nchini na nguvu ya mgombea iwapo Chadema kitamsimamisha katibu
mkuu wake, Dk Willibrod Slaa kwa mara ya pili.
Juzi, CUF ilifanya uchaguzi wake wa kura
za maoni katika Mkoa wa ya Dar es Salaam ambapo pamoja na majimbo
mengine, iliwapitisha Leila Hussen kukiwakilisha chama hicho katika
Jimbo la Kawe na Mashaka Ngole katika Jimbo la Ubungo.
Kutokana na hatua hiyo, vyama vya
NCCR-Mageuzi na NLD vimesema CUF imeanza kwenda kinyume na makubaliano
ya Ukawa, ingawa CUF na Chadema wameeleza kuwa haikuwa kosa kufanya kura
ya maoni kwenye majimbo hayo.
Ingawa viongozi hao wametofautiana
kimtazamo kuhusu hatua hiyo ya CUF, wamesisitiza kuwa kuweka mgombea
mmoja wa upinzani kupitia Ukawa bado ni njia sahihi na pekee
itakayowezesha kuiondoa CCM.
Mwenyekiti wa NLD, Dk Emmanuel Makaidi
alisema Ukawa haijafikia uamuzi wa kuiachia Chadema majimbo ya Ubungo na
Kawe, lakini CUF imekosea kuwasimamisha wagombea katika majimbo hayo
kwa kuwa vikao vya kuwapata wagombea wa upinzani bado vinaendelea.
“Ukweli
ni kwamba hakuna kikao cha Ukawa kilichopitisha kuyaacha majimbo hayo
kwa Chadema, ila CUF wamefanya kosa moja tu, kutangaza wagombea wake
hadharani. Kama ni mchakato wa maandalizi, walipaswa kuwaanda wagombea
hao ndani ya chama chao ili kusubiri uamuzi wa vikao vya Ukawa,” Dk Makaidi
“Hata sisi NLD tuna wagombea wetu Dar es Salaam, lakini hatuwezi kuwatangaza kwa sababu tunasubiri vikao vya Ukawa.”
Alipoulizwa kuna tatizo gani kumtangaza
mgombea sasa huku wakiendelea kusubiri vikao vya Ukawa alijibu, “Huku ni
kuwachanganya wananchi. Kama kila chama kitatangaza mgombea wake sasa
halafu Ukawa ikaja na mgombea mmoja, huku ni kuchanganya watu.”
NIPASHE
Spika wa Bunge, Anne Makinda, amemzuia Waziri Mkuu Mizengo Pinda, kujibu swali la Mbunge Kigoma Kaskazini, David Kafulila (NCCR-Mageuzi), aliyehoji kwa nini mmiliki wa kampuni ya kufua umeme ya Independent Power Tanzania Limited (IPTL), Habinder Seth Singh, anaendelea kulipwa na Tanesco Sh. bilioni tano kila mwezi licha ya azimio la bunge.
Kafulila alisema: “Bado Seth anaendelea kulipwa Sh. bilioni tano (capacity charge) kila mwezi.”
Alisema moja ya maamizio ya bunge ilitaka mmiliki huyo asilipwe fedha hizo.
Kabla ya Waziri Mkuu Pinda kuanza kujibu, Spika Anne alisema: “Hili swali ni jipya kabisa, naomba Waziri Mkuu usilijibu.” Baadaye alimwita mbunge mwingine kuuliza swali.
Pia alieleza kwamba katika hukumu ya Mahakama ya Kimataifa ya Usuluhishi wa Migogoro ya Uwezeshaji (ICSID), ilitaka Tanesco kutolipa kiasi hicho cha fedha, lakini mpaka sasa bado Seth anaendelea kulipwa Sh. bilioni tano kila mwezi.
Kafulila aliuliza swali hilo ikiwa ni
swali la nyongeza kufuatia lile alilouliza awali kuhusu taasisi ya
Serikali ya Marekani inayotoa misaada kwa nchi zinazoendelea (MCC)
kusitisha kutoa msaada wa fedha baada ya mwaka jana kufanya hivyo kwa
kutangaza kutotoa Dola za Marekani milioni 700 kwa Tanzania kutokana na
sakata la akaunti ya Tegeta Escrow.
Alisema Waziri wa Fedha alilidanganya
Bunge kwa kusema taasisi hiyo haijasitisha kutoa fedha kwa Tanzania
kutokana na sakata hilo.
Lakini alisema Katibu Mkuu wa wizara
hiyo hiyo, alitoa taarifa baadaye akisema taasisi hiyo imesitisha kutoa
fedha ilizokusudia sababu kubwa ikiwa ni sakata la escrow.
Kafulila alitaka kujua msimamo wa serikali kuhusu uwongo uliotolewa na Waziri wa Fedha.
Akijibu Waziri Mkuu Pinda alisema; “Mbunge anataka nitoe msimamo kuhusu uwongo aliotoa waziri wangu…hili si la kwangu ni la Bunge.”
Kuhusu tatizo la bajeti ya maendeleo
toka kwa wahisani, alisema limekuwa likitokea kwa kipindi cha miaka
minne sasa na sio kwa sababu ya sakata la akaunti ya escrow.
NIPASHE
Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni
imeshangilia kukwama kwa Katiba mpya ikisema unabii wao umetimia kwa
kasi ambayo haikutegemewa.
Kambi hiyo imesema licha ya kuiandaa
katiba hiyo kwa kutumia mafisadi, kuipitisha kwa kuipigia kura za wafu,
kuipokea japo ilisusiwa na wadau wengi kilichojiri ni kwamba Rais Jakaya
Kikwete, ataondoka madarakani bila kuacha Katiba mpya.
“Uhakika
pekee tulio nao ni kuwa Rais Profesa Dokta Jakaya Kikwete, ataondoka
madarakani bila Katiba mpya aliyowaahidi Watanzania,” Tundu Lissu.
Akiwasilisha taarifa ya kambi hiyo jana
bungeni kuhusu hotuba ya makadirio ya Bajeti ya Wizara ya Katiba na
Sheria kwa mwaka 2015/16 iliyosomwa bungeni jana na Waziri wake, Dk. Asha-Rose Migiro,
Lissu alimnukuu Rais akiwahakikishia wananchi siku ya maadhimisho ya
miaka 50 ya Muungano mwaka jana, kuwa Katiba ingepatikana mwaka huu.
Aliiponda kuwa iliandaliwa na wajumbe wa
Bunge Maalum lililojaa mafisadi watuhumiwa wa kashfa za Escrow,
Richmond/Dowans, Operesheni za Tokomeza na Kimbunga dhidi ya Watanzania
waishio mipakani.
“Ilipitishwa
na kura zilizopigwa na wafu, mahujaji waliokuwa wanafanya Hijja
wakimpiga shetani mawe katika Mlima Arafa, Saudi Arabia, wagonjwa
waliolazwa hospitalini,” Lissu.
Alisisitiza kuwa hii ni serikali
iliyoshindwa japo CCM inadai kuwa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa)
uliweka mpira kwapani na kuondoka uwanjani, lakini CCM licha ya kubaki
na washirika wao wameshindwa.
Lissu alihoji ni lini kura ya maoni itafanyika na kwa kutumia sheria ipi?
“Kwa
maoni ya Kambi Rasmi ya Upinzani, kama Tume ya Uchaguzi itasajili
wapiga kura nchi nzima, hakuna na hakutakuwa na uhakika wa kufanyika
kwa kura ya maoni kuhalalisha katiba inayopendekezwa,” .
Anasema kitakachokwamisha ni matakwa ya
Sheria ya Kura ya Maoni ambayo imeweka utaratibu mgumu wa uendeshaji wa
kura ya maoni, ambapo kila hatua inayotakiwa kuchukuliwa haiwezekani
kuahirishwa wala kuongezewa muda.
“NEC
ilishaeleza kuwa Sheria ya Kura ya Maoni ina maeneo ambayo hayawezi
kutekelezeka na baadhi yake kuwa na tafsiri zaidi ya moja yakiwamo
uhesabuji wa kura ya maoni na utangazaji wa matokeo,” alisema na kuongeza:
“Suluhisho
la changamoto hii ni sheria ya Kura ya Maoni ifanyiwe marekebisho
kwenye maeneo ambayo hayatekelezeki au kuwa na tafsiri zaidi ya moja.”
Alisema na kuongeza kuwa hadi sasa serikali haijaleta muswada wa
marekebisho ya sheria hiyo ili kuwezesha kufanyika kwa kura ya maoni
siku za usoni.
“Kama
ilivyokuwa ahadi hewa ya kura ya maoni mwezi uliopita serikali
inadanganya Watanzania kuwa kutakuwa na kura ya maoni katika mazingira
ya sasa ya kisheria. Kwa sababu hiyo, huyu ni Waziri aliyeshindwa.”
Akizungumzia bajeti finyu ya mahakama,
alisema tishio kubwa kwa uhuru wa mahakama za Tanzania, sio kuingiliwa
na wanasiasa na watendaji wakuu wa serikali bali ni serikali kuinyima
fedha.
“Tishio
ni serikali kutumia udhibiti wake wa hazina ya taifa kuinyima mahakama
rasilimali za kuiwezesha kutimiza wajibu wake kikatiba,”.
NIPASHE
Migomo ya wanafunzi wa vyuo vikuu
iliyoanza juzi kuishinikiza Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu
(HESLB) kuwalipa fedha za kujikimu, sasa imesambaa nchi nzima.
Jeshi la Polisi Wilaya ya Temeke jana
lilitumia mabomu ya machozi kuwatawanya wanafunzi wa Chuo Kikuu
Kishiriki cha Elimu (Duce) cha Chuo Kikuu cha Dar es Salaam waliokuwa
wamekusanyika katika eneo la chuo hicho kwa nia ya kufanya mgomo na
maandamano.
Tukio hilo lilitokea jana saa 2.00
asubuhi, baada ya polisi kufika katika eneo hilo wakiwa na silaha za
moto na mabomu ya machozi.
Waziri Mkuu wa Serikali ya Wanafunzi wa chuo hicho, Bugemwe Melkizedeki, alithibitisha wanafunzi hao kutaka kufanya mgomo.
Hata hivyo, alisema yeye pamoja na viongozi wengine wa serikali ya wanafunzi wakati mgomo huo ukiandaliwa kufanyika.
Alisema wakati huo yeye na viongozi wenzake walikuwa benki wakifuatilia malipo hayo.
Melkizedeki alisema hadi kufikia saa
4.00 asubuhi jana, wanafunzi wote 3,500 walikuwa wameingiziwa fedha
hizo, ambazo ni Sh. bilioni 1.3.
Alisema katika tukio hilo, wanafunzi
nane walikamatwa na polisi, ambao walipelekwa katika kituo cha polisi
Chang’ombe kabla ya kuachiwa kwa dhamana.
Miongoni mwa wanafunzi waliokamatwa, ni
pamoja na Esau Meshack, anayesoma Kitivo cha Ualimu, ambaye alisema
mgomo huo umeathiri ratiba nzima ya mtihani.
Alisema wakati mgomo huo unafanyika, alikuwa anaingia kwenye mtihani ndipo yeye na wenzake walipokamatwa na polisi.
Meshack alisema walifikishwa katika
kituo hicho cha polisi, ambako walipekuliwa, huku wakipigwa virungu,
makofi kwenye masikio na kudhalilishwa kwa kuvuliwa nguo.
Wakati hayo yakijiri, wanafunzi wa Chuo
Kikuu cha Sayansi na Teknolojia cha Mtakatifu Joseph jijini Dar es
Salaam, Kitivo cha Ualimu wa mwaka wa kwanza wa masomo, wamepanga
kufanya maandamano leo. Tofauti na wenzao wa Duce, maandamano hayo
yanalenga kushinikiza kufunguliwa kitivo hicho chenye wanafunzi zaidi ya
400 baada ya kufungwa kutokana na kudai fedha za kujikimu.
Mwanafunzi wa Sayansi ya Ualimu wa
Hesabu katika chuo hicho, Mayagi Mustaph, alisema zaidi ya wanafunzi 400
wanashindwa kuingia darasani kutokana na chuo kufungwa.
Waziri wa Fedha wa Serikali ya Wanafunzi
hao, Joseph Jingu, alipoulizwa kuhusiana na hilo, alisema wao kama
serikali ya wanafunzi waliuomba uongozi wa chuo kukifungua kitivo ili
kuruhusu wanafunzi kuendelea na masomo ifikapo Jumatatu ijayo.
Wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Iringa (UoI)
jana waliandamana kuishinikiza HESLB kuwapa fedha hizo, ambazo wanadai
zimecheleweshwa muda mrefu na hivyo kuwafanya waishi katika mazingira
magumu.
Wanafunzi hao wakitaka kuandamana chuoni
hapo, huku wakitamka kuwa kama wasingeingiziwa fedha jana, lazima
waandamane kuelekea kwenye ofisi ya mkuu wa mkoa.
Askari wa Jeshi la Polisi walionekana
wakirandaranda maeneo ya chuo, kuanzia saa 2.00 asubuhi hadi saa 6.30
mchana wakiwa na silaha mbalimbali, yakiwamo maji ya kuwasha, mabomu ya
machozi na risasi za moto.
Mkuu wa Wilaya ya Iringa, Anjelina
Mabula, aliwataka wanafunzi hao kutoandamana, kwani suala lao
linafuatiliwa kwa karibu na HESLB.
Kuhusu wanafunzi 89 wa Chuo Kikuu cha
Ruaha (Rucu) waliokamatwa na polisi juzi na kushikiliwa katika kituo cha
polisi cha wilaya mkoani humo, Kamanda Mungi alisema wameachiwa kwa
dhamana.
Wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) wamegoma kushinikiza serikali kupatiwa fedha hizo pamoja na kulalamika kukatwa fedha nyingi kwa ajili ya Bima ya Afya.
Mgomo huo ulianza juzi usiku na
kuendelea hadi jana kwa wanafunzi wa Kitivo cha Elimu, Kozi Maalumu kwa
ajili ya walimu wa masomo ya sayansi na hisabati pamoja na Kitivo cha
Sanaa ya Lugha na Sayansi ya Jamii.
HABARILEO
Katika hali isiyokuwa ya kawaida, mamia
ya wanafunzi wa Kitanzania wanaosoma katika shule za msingi nchini
Kenya, wameripotiwa kufukuzwa nchini humo.
Tayari 50 kati yao, wamerejeshwa nchini
huku wengine kadhaa wakiwa bado wamekwama katika eneo la Narok
Magharibi. Baadhi ya walioathirika ni wale ambao wako katika hatua za
mwisho za kuhitimisha elimu yao ya msingi katika darasa la nane.
Vijana hao wanatarajiwa kufanya mitihani
yao ya kumaliza shule Oktoba mwaka huu ; na kufukuzwa kwao kunawaweka
katika wakati mgumu zaidi kimasomo.
Mkuu wa Wilaya ya Ngorongoro, Hashim Mgandilwa alikiri kuwepo na tatizo hilo na alilieleza gazeti hili jana kuwa: “Ni
kweli wanafunzi wetu waliokuwa wanasoma Kenya wamefukuzwa nchini humo
na 44 kati yao wamesharudi nchini, ila tuna wasiwasi kwamba mamia
wengine watakuwa bado wamekwama huko na tuko mbioni kuwafuatilia zaidi.”
Meneja wa Baraza la Wafugaji katika Tarafa ya Ngorongoro, Peter Metele
naye alikiri kuwepo kwa tatizo hilo na kuongeza kuwa yeye ndiye
anayefanya kazi ya kwenda kuwachukua wanafunzi waliotimuliwa Kenya.
Imeelezwa kuwa chanzo cha kutimuliwa kwa
watoto hao ni msuguano, ulioibuka baada ya kufanyika kwa operesheni
maalumu ya kuwaondoa wahamiaji haramu kutoka nchi jirani ya Kenya,
wanaodaiwa kuvamia maeneo ya Loliondo na Sale.
Hadi sasa watoto 27 wamehifadhiwa kwenye
nyumba ya kulala wageni ya Cobra katika eneo la Wasso, Loliondo.
Wengine takribani 10 wamepelekwa kwenye kata ya Arash na waliobakia wako
majumbani mwao.
“Tumewahifadhi
kwenye nyumba za kulala wageni kwa sababu kuna wale wanaotoka vijiji
vya mbali sana na tunataka tujitahidi kufanya mazungumzo na viongozi wa
upande wa Kenya ili waruhusiwe kurejea mashuleni, iwapo tutafanikiwa
basi iwe rahisi kuwarudisha Kenya,” Metili.
Imedaiwa kuwa wanafunzi waliofanikiwa
kurejeshwa ni wale wanaodhaminiwa na Baraza la Wafugaji na wale
waliopelekwa na taasisi mbalimbali, ambao ilikuwa rahisi kutumiwa
usafiri, ila kwa waliopelekwa na wazazi wao, bado wamekwama Kenya.
“Tulishafanya
mazungumzo ya awali na viongozi wa upande wa Kenya siku ya tarehe 12
Mei mwaka huu, lakini ingawa tulikubaliana mengi, ikiwemo
wafanyabiashara wetu kuruhusiwa kupeleka bidhaa Kenya inaonekana kuwa
wananchi wa Narok wao wana maamuzi yao tofauti na serikali yao hivyo
wanasisitiza kuendeleza mzozo, na sasa wameamua kuongeza tatizo kwa
kuwatimua watoto,” alisema Mkuu huyo wa Wilaya.
HABARILEO
Madai ya wanawake wa wilaya ya Rombo,
Kilimanjaro, kukodi wanaume kutoka nchini Kenya, baada ya kukosa huduma
za ndoa kutoka kwa waume zao kwa muda mrefu, kutokana na ulevi wa gongo
uliopindukia, zimemfadhaisha Mbunge wao, Joseph Selasini (Chadema).
Mbunge huyo amefikia hatua ya kusema
kuwa familia yake na wananchi wa huko, wamefadhaika na kuingiwa na
wasiwasi kuwa huenda wenzi wao katika ndoa zao ikiwemo ya mbunge, si
waaminifu.
Selasini alisema hayo jana, alipokuwa
akiuliza swali kwa Waziri Mkuu, Mizengo Pinda ambapo alisema ingawa hali
hiyo imewafadhaisha, lakini alitetea utengenezaji wa pombe za kienyeji,
ikiwemo pombe haramu ya gongo.
Katika utetezi huo, Selasini alitaka
Serikali iangalie namna ya kusaidia uboreshwaji wa pombe za kienyeji,
kwa kuwa kipato chake kimekuwa kikisaidia ada za watoto, kujikimu na
kuongeza kipato cha familia.
Akijibu swali hilo, Pinda alisema kwa
namna Selasini anavyozungumza, huenda anatetea suala la kuhalalisha
pombe haramu aina ya gongo, na kama ndio hiyo Serikali itaendelea kupiga
vita utengenezaji na matumizi ya pombe hiyo kwa sababu viwango vyake
havipimiki.
“Mheshimiwa
Selasini, kwa maelezo yako utakuwa unazungumzia gongo, sasa hii ni
pombe haramu na Serikali inaendelea kuipiga vita kwa kuwa viwango vyake
havipimiki.
“Lakini
huenda kwa siku zijazo, jambo hili linaweza kuangaliwa na kiwanda cha
Konyagi kuhusu namna ya kuiboresha kwa sababu hata Konyagi ni jamii ya
gongo, lakini inapimika na haina madhara makubwa kwa watumiaji,” alisema Pinda.
Hata hivyo, katika swali la nyongeza la
mbunge huyo, alimtaka Waziri Mkuu kukanusha tuhuma za Mkuu wa Wilaya ya
Rombo, Lembrice Kipuyo alizotoa wiki iliyopita akidai kuwa wanawake wa
wilaya hiyo, wanakodisha wanaume kutoka nchi jirani ya Kenya kwa ajili
ya kuwahudumia mahitaji ya kimwili, kwa kuwa waume zao wameshindwa
kutokana na ulevi uliopindukia.
“Mheshimiwa
Waziri Mkuu, tunaomba kauli ya serikali kuhusu jambo hili, na mkanushe
taarifa hizo kwani zimeleta mfadhaiko kwenye familia na hata familia
yangu, wanandoa wana wasiwasi kwamba wenza wao wanatoka nje ya ndoa,
lakini pia kauli hiyo ni ya kudhalilisha wananchi wa Rombo”, Selasini.
Akijibu swali hilo, Pinda alisema
hajasikia tuhuma hizo ;na kwamba kama zimetolewa na Mkuu huyo wa Wilaya
ni vyema aliyetoa, azikanushe mwenyewe kwa kuwa ndiye anayejua alizitoa
katika mazingira gani na wapi.
Aidha, alisema ni vyema apewe muda wa kulifahamu jambo hilo ;na kusema ataiagiza Ofisi ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), kuangalia jambo hilo kama Mkuu huyo wa Wilaya alichokisema, sio sahihi ili hatua nyingine zifuate.
MTANZANIA
Watu wenye ulemavu jana wamelazimika
kufunga makutano ya barabara za Kawawa na Uhuru kwa kulala katikati ya
taa za kuongoza magari kwa zaidi ya saa sita kama njia ya kupinga hatua
ya Manispaa ya Ilala kuwavunjia meza zao za biashara katika Soko la
Mchikichini.
Wafanyabiashara hao walikusanyika katika
eneo hilo, hali iliyowafanya madereva wa magari wanaotumia barabara
hizo kusota kwenye foleni kwa muda mrefu.
Mwenyekiti wa Umoja wa Wafanyabiashara Walemavu, Kidumke Mohamed,
alisema juzi walipofika katika maeneo yao ya biashara walishangaa
kukuta zaidi ya meza 200 wanazofanyika biashara zikiwa zimevunjwa na
mizigo yao ikichukuliwa na mgambo wa Manispaa ya Ilala.
Alisema hawajui kuwa ni nani aliyeharibu
vitu vyao, wakati Serikali iliwaruhusu kwa barua ya maandishi kufanya
biashara katika soko hilo huku wakisubiri kutafutiwa eneo lingine.
“Tumeamua
kufunga barabara hii ili tuweze kupata suluhu kwa viongozi wa Serikali.
Hasara tumepata na haujui la kufanya mpaka sasa zaidi ya kuwa masikini,”Mohamed.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Chama cha
Walemavu Wilaya ya Ilala, John Mleba, alisema Serikali imeamua kuvunja
sheria ya makubaliano ya maandishi kwa kuwavunjia maeneo yao ya
biashara.
“Tatuwezi
kuondoka hapa wala kuruhusu barabara kupita hadi pale litakapopatiwa
ufumbuzi wa suala letu hili la eneo la biashara na mali zetu ambazo
zimeharibiwa.
“…hapa
hatutoki hadi Mkuu wa Mkoa, Said Meck Sadiki atakapokuja ili kutatua
suala hili, yeye ndiye aliyeturuhusu kufanya biashara katika soko hili
kwa makubaliano ya maandishi, sasa tunashangaa wametufanyia hivi bila
kutupa taarifa.
“Wangetupatia taarifa mapema sisi tungeondoa vitu vyetu, lakini wameviharibu na vingine wamevibeba wakati sisi tunapata fedha za kujikimu kimaisha kupitia biashara hizi,”Mleba.
“Wangetupatia taarifa mapema sisi tungeondoa vitu vyetu, lakini wameviharibu na vingine wamevibeba wakati sisi tunapata fedha za kujikimu kimaisha kupitia biashara hizi,”Mleba.
Kutokana na hali hiyo, Mkuu wa Wilaya ya
Ilala, Raymond Mushi, alifika katika eneo hilo kwa lengo la kutafuta
suluhu ikiwemo kuwataka wafanyabiashara hao kufungua barabara lakini
alijikuta akifukuzwa.
Baada ya dakika chache, Mkuu wa Polisi wa Wilaya ya Ilala, naye alijikuta akifukuzwa na wafanyabiashara hao.
Wakati wa barabara hiyo ikiwa imefungwa, wafanyabiashara hao waliruhusu kupita magari ya jeshi pamoja na yale ya wagonjwa.
Ilipotimu sasa tisa alasiri uongozi wa Manispaa ulikwenda tena kuwahisi viongozi hao ili waende kukaa kikao cha pamoja ili kutafuta suluhu la mgogoro huo.
Ilipotimu sasa tisa alasiri uongozi wa Manispaa ulikwenda tena kuwahisi viongozi hao ili waende kukaa kikao cha pamoja ili kutafuta suluhu la mgogoro huo.
Katika kikao hicho, DC Raymond Mushi
alikiri kutokea kwa tukio hilo na kusema kuwa lengo la kubomoa vibanda
hivyo ni kupisha utanuzi wa barabara ya watembea kwa miguu katika eneo
hilo.
Alisema kutokana na hali hiyo,
waliafikiana kwa njia ya maandishi kwa mara ya pili kuwa wenye uwezo
warudi na watengeneze meza zao na kuendelea kufanya biashara na wale
wasiokuwa na uwezo wasubiri uchunguzi wa kutathmini athari zilizotokea
ili walipwe fidia ya vitu vyao vilivyoharibika.
Kwa habari na matukio motomoto ni hapa hapa tangakumekuchablog
No comments:
Post a Comment