Uchambuzi huu wa magazeti unaletwa kwenu kwa hisani kubwa ya kituo cha Elimu Cha Candle Education Centre Tanga. Kituo kinaongozakufaulisha wanafunzi kidato cha pili hadi cha sita na wanaojiendeleza kielimu. Wapo Tanga mkabala na Bank ya CRDB simu 0715 772746
NIPASHE
Wakati wananchi wakilalamikia uandikishaji katika Daftari la Kudumu la Wapigakura kwa mfumo mpya wa kielektroniki wa Biometric Voters Registration (BVR), maofisa 10 wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC)
wameshambuliwa na kujeruhiwa na watu wanaodhaniwa kuwa ni majambazi
wakati wakienda kuandikisha wapigakura wilayani Momba, mkoani Mbeya.
Walikumbwa na mkasa huo katika msitu wa
Nyimbili, wakiwa njiani kutokea katika kata ya Chitete walikokuwa
wanaandikisha wapigakura.
Mbali ya maofisa hao, dereva wa gari la halmashauri ya wilaya hiyo, Pius Kajula ambaye ni mkazi wa Kamsamba, alijeruhiwa vibaya katika tukio hilo.
Akizungumza wodini katika Hospitali ya
Serikali Mbozi, Kajula alisema tukio hilo lilitokea juzi usiku wakiwa
njiani kutoka katika kijiji cha Chilulumo kuelekea kijiji cha Chitete
baada ya kumaliza kuandikisha kata za Chilulumo, Ivuna na Mkomba.
Alisema saa 2:30 usiku akiwa anaendesha
gari katika msitu huo ambao ni mkubwa na wenye kona nyingi, ghafla
alikuta barabara imefungwa kwa magogo.
Alisema baada ya kuona hali hiyo
alitambua kuwa kuna jambo la hatari na alipoanza kurudi nyuma ili
kutafuta mwanya wa kugeuza gari kurudi walikotoka ili kuokoa maisha yake
na aliowabeba walijikuta wameshazungukwa na watu hao.
Alisema akiwa kwenye harakati hizo,
lilitokea kundi la watu kutoka ndani ya msitu huo wakiwa na mapanga na
marungu na kuwaamuru waliokuwa ndani ya gari hilo kushuka.
Kajula alisema alijitahidi kupambana nao
ili kuokoa maisha yao lakini ilishindikana na watu hao walianza kupiga
gari hilo kwa mawe na kuvunja vioo vyote.
Alisema kutokana na mashambulizi hayo alilazimika kusimamisha gari na kuwaeleza maofisa hao washuke ili kujinusuru.
Alisema wakiwa wanashuka, watu hao
walianza kuwashambulia kwa silaha hizo na katika harakati za kujiokoa
alijeruhiwa kwa kukatwa mkono wa kulia na kichwani.
Alisema watu hao waliwaamuru kulala chini na kuwapekua na kuwapora vitu mbalimbali, ikiwamo simu na Sh. 175,000 taslimu.
Kajula alisema baada ya uporaji huo,
watu hao walitoa magogo barabarani na kumlazimisha kuondoa gari ambalo
aliendesha kwa mkono mmoja hadi Kituo cha Polisi Itaka kabla ya kwenda
hospitali kwa matibabu.
Muuguzi Msaidizi wa Hospitali ya Mbozi, Tulakela Kilatu,
alisema majeruhi wote walipokelewa katika hospitali hiyo juzi majira ya
saa 9:00 usiku na kutibiwa kabla ya kuruhusiwa isipokuwa dereva huyo.
NIPASHE
Taasisi tano za serikali zimeisababishia serikali hasara ya Sh. bilioni 10 kwa kipindi cha miaka miwili.
Kwa mujibu wa taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali (CAG) Prof. Mussa Juma Assad,
ya mwaka 2013/14 inaonyesha uwapo wa mashaka makubwa juu ya uwezo wa
taasisi hizo kuendelea kujiendesha endapo hatua za makusudi
hazitachukuliwa na serikali katika kuzinusuru.
Taasisi hizo ni Taaisi ya teknolojia Dar es Salaam (DIT), Bodi ya Maziwa Tanzania (TDB), Chama cha hakimiliki na Hakishirikishi Tanzania (COSOTA), Chuo Kikuu Huria (OUT) na TFC.
Aidha, CAG amebaini mapungufu katika mradi wa ujenzi wa jengo la ‘Linear Accelerator Treatment’ katika Taasisi ya Saratani ya Ocean Road wa Sh. Bil 3.333.
Taarifa hiyo imebainisha kuwa kwa mujibu
wa mkataba huu, ujenzi ulitakiwa kumalizika ndani ya wiki 32, lakini
hadi kufikia Disemba mwaka jana kazi pekee iliyokamilika ni maandalizi
ya eneo la ujenzi.
“Kiasi
cha fedha kilichokuwa kimelipwa kwa mujibu wa hati ya malipo kilikuwa
Sh. milioni 349 ikijumuisha bima na malipo ya awali,” ilifafanua.
CAG alibainisha kuwa kwa mujibu wa
Menejimenti ya Taasisi ya ORCI mkataba huo ulitekelezwa kwa kuzingatia
bajeti iliyotengwa ya Sh. bilioni nane kutoka serikalini na hakuna kiasi
chochote kilichokuwa kimepokelewa kwa kipindi cha mwaka wa fedha.
NIPASHE
Matukio ya kuvamia askari wakiwa
lindoni, vituo na vizuizi vya polisi nchini yameendelea kulitafuna Jeshi
la Polisi na safari hii, Askari wa Kikosi cha Tazara, Jijini Dar es
Salaam, ameporwa SMG na kujeruhiwa vibaya.
Tukio hilo lilitokea juzi usiku saa sita
kwa watu wanaosadikiwa ni majambazi wakiwa na silaha za jadi kumvamia
askari huyo akiwa kwenye lindo la Tazara na kupora silaha hiyo.
Kwa mujibu wa taarifa kutoka eneo la
tukio, watu wawili wakiwa na silaha za jadi, nyakati za saa sita usiku
walivamia eneo hilo na kupora silaha hiyo na kutokomea nayo.
Taarifa hizo zinafafanua kuwa askari
huyo alijeruhiwa vibaya sehemu mbalimbali za mwili na amelazwa hospitali
kwa matibabu zaidi, ingawa jina lake halikutajwa wala hospitali
aliyolazwa.
Kamanda wa Kikosi hicho, Kamanda Bieteo, alithibitisha kuwepo kwa tukio hilo na kusema kuwa hawezi kutoa ufafanuzi kwa simu bali kwa taarifa ya maandishi.
“Tukio
lipo ni kweli wamemvamia askari akiwa lindoni kumjeruhi na kumpora
silaha…siwezi kutoa ufafanuzi zaidi kwa simu, leo nitatoa taarifa kwa
maandishi,”.
Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Suleiman Kova, alipoulizwa, alithibitisha, lakini akamuelekeza mwandishi kuwasiliana na Kamanda Bieteo.
Hivi karibuni, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mathias Chikawe, alisema idadi ya matukio ya uvamizi wa vituo vya polisi imeongezeka kutoka sita kwa mwaka 2014 hadi nane kwa mwaka 2015.
Alisema katika matukio hayo jumla ya
askari saba waliuawa kwa mchanganuo kwenye mabano Chamazi (2), Mkuranga
(2) na Ushirombo (3)
MTANZANIA
Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu,
jana alijikuta katika wakati mgumu baada ya wabunge wengi kushutumu
utendaji wake wakisema umekuwa chanzo cha wizara hiyo kuzorota katika
maendeleo.
Kwa mujibu wa wabunge hao, kitendo cha
waziri huyo kushindwa kutekeleza agizo la mahakama kuhusu tozo mpya
katika hoteli za utalii kimefanya Serikali kupoteza zaidi ya Sh bilioni
20 kila mwaka.
Wabunge hao pia walishangazwa na kitendo
cha wizara hiyo kulazimisha mfumo wa ‘Double Entry’ unaosababisha
hasara badala ya mfumo wa ‘Single Entry’ unaotaka mtalii kulipa ada ya
kiingilio kila anapoingia hifadhini.
Waliyasema hayo walipojadili makadirio ya mapato na matumizi ya bajeti ya wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2015/2016.
Akisoma maoni ya wabunge, Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Mazingira, James Lembeli alisema licha ya kamati yake kutoa ushauri na Bunge kutoa maagizo, waziri huyo amegoma kuyatekeleza.
“Takwimu
zinaonyesha kwa miezi 10 yaani Julai, 2014 hadi Machi, 2015 Hifadhi ya
Serengeti na Hifadhi ya Ziwa Manyara zilipoteza zaidi ya Sh bilioni 1.4
kutokana na wizara kulazimisha mfumo wa ‘Double Entry’. Kamati inahoji
kuna maslahi gani waziri kutetea mfumo ambao unaipotezea Serikali
mapato?” alihoji Lembeli.
Lembeli alisema katika mkutano wa 18 wa
Bunge, kamati ilishauri na Bunge likaazimia kwamba waziri huyo atekeleze
hukumu ya Mahakama Kuu Kanda ya Arusha, iliyomtaka Nyalandu kutangaza
katika gazeti la Serikali tozo mpya zitakazotumika katika hoteli za
utalii nchini.
Akiwasilisha hotuba ya Kambi Rasmi ya Upinzani Mbunge wa Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa (Chadema) alisema kinachoonekana ni wizara hiyo kukosa dira kufikia malengo yake.
Msigwa alisema changamoto ambazo zipo ni
sawa na zile za kamati ya bunge, hivyo ni wajibu wa waziri kuweka wazi
kuwa ana maslahi gani na migogoro mingine ambayo imefikiwa mwafaka hata
ile ya uamuzi wa mahakama.
“Nashindwa
kujua hivi hata hili la kuwa tumepoteza Sh bilioni 1.4 na Sh biloni 3
linakuwa gumu kufanyiwa uamuzi ni kwa maslahi ya nani au ndiyo mnajenga
mazingira mazuri ya Ukawa kuchukua nchi,” alisema.
Awali, akiwasilisha bajeti yake, Waziri
Nyalandu alisema wizara yake imejipanga kuhakikisha inatatua migogoro
yote baina ya wananchi na maeneo yaliyohifadhiwa na kuhakikisha uhifadhi
na matumizi endelevu ya maliasili kwa maendeleo ya utalii yanalindwa
kwa ukamilifu kwa mujibu wa sheria.
Alisema katika kuhakikisha migogoro ya
mipaka na uvamizi na maeneo yaliyohifadhiwa inakomeshwa, wizara
itaendelea kurekebisha na kuweka alama za kudumu za mipaka na kufanya
doria za mara kwa mara na kuelimisha umma.
Nyalandu alisema tayari ameipatia
ufumbuzi wa kudumu migogoro mbalimbali ya ardhi ukiwamo ule wa Mbarali,
ambao umedumu kwa miaka saba bila kupatiwa suluhisho.
Kwa mujibu wa Nyalandu, Tanzania inafuatiwa na Botswana, Kenya, Zambia, Afrika Kusini, Namibia, Uganda, na Zimbambwe.
MTANZANIA
Waziri wa Ujenzi, Dk. John Magufuli, ametangaza rasmi kugombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Amesema kwa kuwa Chama Cha Mapinduzi
(CCM) kimetangaza rasmi kwa wanachama wake wenye sifa kujitokeza kuwania
nafasi hiyo kubwa ya uongozi nchini, ameona hana budi kutangaza rasmi
azma yake.
Dk. Magufuli, mmoja wa mawaziri ambao
kwa muda mrefu wamehusishwa kwenye kinyang’anyiro cha nafasi hiyo,
alisema anaingia kwenye mchuano huo akiwa na sifa zote stahiki za kupiga
na kupigiwa kura.
Alitangaza azma yake nje ya ukumbi wa
Bunge mjini Dodoma, muda mfupi baada ya kumalizika kipindi cha maswali
na majibu bungeni, jana asubuhi.
Baada ya kuulizwa kama ana mpango huo,
mara moja alisema: “Swali hili nimeulizwa mara nyingi. Mara zote
nimekataa kulijibu kwa sababu chama chetu (CCM) kuna utaratibu wake wa
namna ya kuomba nafasi ya uongozi. Muda ulikuwa haujawadia.
“Lakini
utakumbuka wiki hii hapa hapa Dodoma, vikao vya juu vya chama chetu
vimetoa ratiba kwa wanaotaka kuwania nafasi mbalimbali kujitokeza.
“Kwa
maana hiyo sasa niko huru kujibu swali lako kwa kusema rasmi ‘nitagombea
urais’. Nafanya hivyo kwa sababu naamini ninazo sifa za kuchagua na
kuchaguliwa kama mwanachama wa CCM kwa nafasi yoyote inayojitokeza
kulingana na Katiba ya chama chetu na pia Katiba ya nchi,” Dk. Magufuli.
Alisema siku ya kuchukua fomu
ataitangaza baadaye pindi akishakamilisha taratibu za namna ya kuanika
hadharani mambo anayokusudia kuyatekeleza endapo wana CCM watampa ridhaa
ya kupeperusha bendera ya chama hicho.
Dk. Magufuli, amekuwa mbunge tangu mwaka
1995. Baada ya kushinda ubunge mwaka huo, alichaguliwa kuwa Naibu
Waziri wa Ujenzi; Wizara iliyokuwa ikiongozwa na Anna Abdallah.
MWANANCHI
Wakati Serikali na wadau wa usafiri
wakiendelea kutafuta mwarobaini wa ajali nchini, imeelezwa kuwa malori
ya Tanzania yamesababisha ajali 227 nchini Zambia kati ya Januari na
Mei.
Kwa mujibu wa taarifa zilizotolewa kwenye Gazeti la Lusaka Times la
Zambia, imeelezwa kuwa Tanzania inatakiwa kutafuta suluhisho la kudumu
la kudhibiti ajali zinazosababishwa na malori ya Tanzania wanayokwenda
nchini humo.
Likikariri ripoti iliyotolewa na Kikosi
cha Usalama Barabarani cha Zambia mwezi huu, gazeti hilo limesema katika
ajali hizo 227, ajali 37 zilipoteza maisha ya watu 42.
“Kati
ya ajali hizo waliopata majeraha makubwa walikuwa 51, wenye majeraha
madogo walikuwa 59 huku ajali 133 zilisababisha uharibifu wa magari na
mali,” inasema ripoti hiyo.
Ripoti hiyo ilitaja sababu kubwa ya
ajali hizo kuwa ni mwendo kasi, vizuizi barabarani, uchovu wa safari
ambao umekuwa ukisababisha baadhi ya madereva kuegesha malori yao vibaya
na kusababisha madhara kwa watumiaji wengine wa barabara.
Mkurugenzi Mtendaji wa Wakala wa Usafirishaji na Usalama Barabarani (RTSA) Zambia, Zindaba Soko
akizungumza katika mkutano uliomkutanisha na Mkurugenzi wa Usafirishaji
kutoka Mamlaka ya Usafiri wa Nchi Kavu na Majini Tanzania (SUMATRA), Leo Ngowi mjini Ndola Zambia, alisema Serikali ya nchi hiyo itaondoa vikwazo barabarani ambavyo vimekuwa vikisababisha ajali.
Mkurugenzi huyo alisema iwapo nchi za
Kusini mwa Afrika zitatekeleza utaratibu wa kuondoa urasimu utasaidia
kupunguza muda wa kukaa mipakani, kupunguza gharama za kufanya biashara
na kufanya safari nyingi kuliko ilivyo sasa kama pia watazingatia sheria
za usalama barabarani.
Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP), Johansen Kahatano
kutoka Kikosi cha Usalama Barabarani akizungumzia suala hilo alisema
Polisi ilituma mwakilishi katika mkutano huo nchini Zambia ambapo
walipata taarifa za ajali hizo.
MWANANCHI
Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), Maalim Seif Sharif Hamad
jana alichukua fomu ya kuomba kuteuliwa na chama hicho kugombea urais
wa Zanzibar kwa mara ya tano huku akisema ushindi wake hautachezewa na
mtu.
Mara ya kwanza Maalim Seif aliwania
urais wa Zanzibar mwaka 1995 na amekuwa akifanya hivyo katika chaguzi
zilizofuatia na sasa anawania tena kuingia Ikulu Oktoba.
Baada ya kuchukua fomu katika ofisi za
chama hicho zilizopo Bububu jana, Maalim Seif alisema ataheshimu matokeo
ya urais endapo uchaguzi utakuwa huru na wa haki.
Maalim Seif ambaye pia ni Makamu wa
Kwanza wa Rais wa Zanzibar, alisema matarajio yake makubwa katika
uchaguzi ujao ni kwamba utafanyika katika mazingira ya amani na utulivu.
Alisema ni matumaini yake kwamba mara hii ataongoza na kuibuka kuwa rais endapo uchaguzi utakuwa huru na haki.
“Kama wananchi wa Zanzibar watanipigia kura kwa wingi nawahakikishia hakuna mtu yeyote atakayechezea ushindi wangu,” Maalim Seif.
Akizungumzia afya yake kuelekea Uchaguzi
Mkuu, Maalim Seif alisema anagombea nafasi hiyo akiwa mzima wa afya na
hana shaka, hivyo wananchi waondoe hofu katika hilo.
“Nachukua fomu ya urais na matarajio yangu makubwa ni kushinda katika uchaguzi mkuu ambao utafanyika katika mazingira ya amani,” alisema.
Hafla ya Maalim Seif kuchukua fomu
ilihudhuriwa na viongozi mbalimbali wakiwamo mawaziri katika Serikali ya
Umoja wa Kitaifa kutoka CUF. Maalim Seif aliwataka wanachama wengine
kujitokeza kugombea nafasi hiyo kwa kuwa ni haki yao kikatiba.
Kwa habari na matukio usiache kutembelea blog hii kila wakati, habari, matukio na mengi mengineo yanayojiri utayapata hapa hapa tangakumekuchablog
No comments:
Post a Comment