Monday, May 25, 2015

BURUNDI MACHAFUKO YAZIDI KURINDIMA

Basi moja la uchukuzi limechomwa moto mjini Bujumbura Burundi na waandamanaji waliorejea mabarabarani kupinga uamuzi wa rais Pierre Nkurunziza kuwania muhula wa tatu.
Waandamanaji wanachoma moto magurudumu  katika eneo la Kanyosha.
Kitongoji hicho kimekuwa kitovu cha maandamano haya dhidi ya awamu ya tatu ya rais Nkurunziza.
Mwandishi wa BBC mjini Bujumbura Ismael Misigaro amesema milio ya risasi inasikika mjini humo.
Maandamano haya yanarejea baada ya kuuawa kwa kiongozi wa chama cha upinzani Zedi Feruzi nje ya nyumba yake katika mji mkuu Bujumbura.
Aidha wanaharakati wa upinzani nchini humo wamesitisha mazungumzo na Serikali  ya kutaka kutanzua mzozo ulioko wa kisiasa.
Mzozo huo unafuatia hatua ya Nkurunziza kuwania urais kwa muhula wa tatu.
Uamuzi ambao wengi wanasema kuwa unaenda kinyume na sheria na ndio iliyosababisha kuwepo kwa jaribio la kumpindua, na maandamano ya wiki kadhaa.
Tayari zaidi ya raia 100,000 wa taifa hilo wametorokea mataifa jirani.

No comments:

Post a Comment