Uchambuzi huu wa magazeti unaletwa kwenu kwa hisani kubwa ya kituo cha Elimu Cha Candle Education Centre Tanga. Kituo kinaongoza kufaulisha wanafunzi kidato cha pili hadi cha sita na wanaojiendeleza kielimu. Wapo Tanga mkabala na Bank ya CRDB simu 0715 772746
MWANANCHI
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi amesema atakuwa bega kwa bega na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe katika mbio zake za kuwania urais.
Membe, ambaye amekuwa akizungumzia kutangaza nia kuwania urais kama “kusubiri kuoteshwa”,
ameshasema siku ikifika atachukua fomu lakini anatarajia kutangaza
rasmi mpango wake jimboni kwake Mtama, sasa anaungwa mkono na mmoja kati
ya viongozi wa juu wa Serikali na CCM kutoka Zanzibar ambayo ina nafasi
ya pekee katika kuamua mgombea urais wa chama hicho.
Balozi Iddi ambaye amewahi kuwa Naibu
Waziri wa Mambo ya Nje tangu mwaka 2006, alitoa msimamo huo wa kwanza
kwa kiongozi wa juu wa Serikali jana jijini Dar es Salaam wakati
akifunga mkutano wa siku tatu wa mabalozi wa Tanzania katika nchi
mbalimbali, akimwakilisha Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein aliyeshindwa kuhudhuria kutokana na msiba wa dada yake.
“Namtakia Membe safari njema na ninamuahidi kuwa tutakuwa naye bega kwa bega katika safari hii ngumu kwake,” alisema Balozi Idi bila ya kutaja neno urais.
Kauli ya makamu huyo wa Rais ilikuja
baada ya Membe, ambaye amesema wakati ukifika atachukua fomu za kugombea
urais, kuwaaga mabaozi hao kabla ya kumkaribisha mgeni huyo rasmi.
Katika hotuba yake ya mwisho kwa
mabalozi hao, Membe aliweka wazi kuwa hatarudi tena bungeni akiwa waziri
baada ya kuongoza wizara hiyo kwa takriban miaka minane.
Alirejea kauli yake ambayo amekuwa
akiitoa mara kwa mara kuwa ameamua kuondoka wizarani hapo ili kujaribu
nafasi kubwa zaidi katika siasa na kuwakaribisha bungeni mjini Dodoma
ili wasikilize hotuba ya bajeti yake ya mwisho.
MWANANCHI
Bunge la Bajeti lililokuwa livunjwe Juni
27, mwaka huu litaongezwa siku 10 ili kutoa nafasi ya kujadiliwa kwa
miswada takriban 10 kinyume na historia yake.
Mkutano huo wa 20 wa Bunge la 10 ni wa
mwisho katika uhai wa chombo hicho cha kutunga sheria kabla ya kuvunjwa,
kupisha Uchaguzi Mkuu wa Oktoba.
Taarifa zilizolifikia gazeti hili na kuthibitishwa na Ofisi ya Bunge na Rais Jakaya Kikwete,
zilieleza kuwa tayari makubaliano yamefikiwa baina ya Bunge na Serikali
ili kuwezeshwa kufikishwa miswada hiyo katika kipindi hiki cha Bunge la
Bajeti.
Akifungua Mkutano Mkuu wa Tano wa Chama
cha Walimu Tanzania (CWT), juzi usiku, Rais Kikwete alisema makubaliano
hayo yamekwishafanyika na miswada itakayojadiliwa mmojawapo ni wa
kuanzishwa tume ya utumishi ya walimu, ambayo inawezesha walimu nchini
kuwa na chombo kimoja cha kuwasimamia.
“Tayari
tumezungumza na Spika wa Bunge na tumekubaliana katika kikao
kinachoendelea kitaongezwa siku 10 ili kuwezesha kumaliza shughuli za
serikali ikiwamo miswada,”.
Chanzo kingine cha habari ndani ya
Serikali kilieleza kuwa moja kati ya miswada itakayowasilishwa na
Serikali ni pamoja na marekebisho ya sheria ya uchaguzi pamoja na
muswada wa sheria ya vyombo vya habari.
Sababu nyingine inayotajwa kuhusu
kuongezwa muda kwa Bunge hilo ni Mkutano Mkuu wa Taifa wa CCM ambao
ndiyo wenye jukumu la kuchagua mgombea urais wa chama hicho, ambao
utafanyika kwa siku mbili kuanzia Julai 11 hadi 12.
Wabunge wote wa CCM ni wajumbe wa
mkutano huo, hivyo kama Bunge litavunjwa Juni 27, 2015 watapoteza sifa
za kuwa wajumbe wa mkutano huo.
Hata hivyo, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye alipoulizwa kuhusu chama hicho tawala kuhusishwa na nyongeza ya siku za Bunge hilo alisema, “Huo
ni upuuzi mwingine sasa. Vikao vya CCM vimepanga ratiba kabla hata ya
huo uamuzi wa Bunge unaousema. Hakuna ukweli katika hilo.”
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Jenista Mhagama alipoulizwa kuhusu suala hilo alishindwa kukubali wala kukataa na kutaka atafutwe Katibu wa Bunge.
Tayari Chama cha Wamiliki wa vyombo vya
Habari Tanzania (Moat), kimeunda timu maalumu itakayokwenda bungeni
kuwashawishi wabunge wasiupitishe muswada wa sheria wa vyombo vya habari
baada ya kubaini umejaa kasoro.
Muswada huo ulioandaliwa na Serikali
ulitakiwa kuwasilishwa katika mkutano wa 19 wa Bunge kwa hati ya dharura
bila mafanikio na tayari Rais Kikwete amesema atausaini kabla
hajaondoka madarakani.
Naibu Spika, Job Ndugai alipoulizwa alisema: “Hilo
jambo bado hatujakaa katika kamati ya uongozi kulijadili vizuri. Bado
hatujajua Serikali inaleta miswada gani. Ila pamoja na hayo, hicho kitu
(kuongeza muda) kitakuwapo.”
NIPASHE
Wabunge wameishukia serikali kwa
kushindwa kutatua tatizo la foleni katika Jiji la Dar es Salaam ambalo
sasa linaigharimu serikali hasara ya Sh. bilioni nne kila siku.
Aidha, wameitupia lawama Wizara ya
Ujenzi kwa kusababisha vifo vya makandarasi wanne ambao walifikwa na
umauti huo kutokana na serikali kushindwa kuwalipa madeni wanayodai.
Mbunge wa Kuteuliwa na Rais, James Mbatia,
akichangia bajeti ya Wizara ya Ujenzi kwa mwaka 2015/2016, alisema
tatizo la msongamano wa magari katika Jiji la Dar es Salaam limekuwa
sugu bila kuwapo mipango yoyote ya serikali katika kulipatia ufumbuzi.
Alisema Januari 13, mwaka 2009, alimwandikia barua Waziri Mkuu, Mizengo Pinda,
kuhusu tatizo la msongamano wa magari na kutoa mapendekezo 10 ambayo
yangesaidia kukabiliana na tatizo hilo, lakini bahati mbaya hakuna
kilichofanyika hadi sasa hali inayoonyesha serikali kutokuwa makini
katika kushughulikia mambo ya msingi.
Mbatia alisema moja ya mapendekezo hayo
ni kuitaka serikali isimamishe au kutoendelea kutoa vibali vya kujenga
ofisi, maduka makubwa na madogo katikati ya Jiji.
Alisema pendekezo lingine lilikuwa ni
kutaka Ofisi za Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Wizara
ya Mambo ya Ndani, Wizara ya Ulinzi, Wizara ya Maliasili na Utalii,
Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Wizara ya Ujenzi, Mahakama Kuu ya
Tanzania, Makao Mkuu ya Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) na uwanja
ndege vihamishwe katikati ya Jiji.
“Hali
ni mbaya Dar es Salaam, watu wanakaa kwenye foleni kwa zaidi ya saa
nane, foleni hii inaigharimu serikali zaidi ya Sh. bilioni nne kwa siku
ambazo zingetumika kujenga zahanati na kununua madawati ambayo
yangesaidia watoto shuleni,” alisema.
Alisema Sh. bilioni nne ambazo serikali
inapata hasara kila siku kutokana na foleni zingetumika kununua madawati
80,000 kwa bei ya Sh. 50,000 kwa dawati moja.
Mbatia alisema pia fedha hizo
zingetumika kujenga vituo viwili vya afya vya kisasa, ambavyo gharama
zake kila kimoja ni Sh. bilioni mbili.
NIPASHE
Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni imeitaka
Wizara ya Ujenzi kutoa majibu ya deni la zaidi ya Sh. bilioni 800
inayodaiwa wizara hiyo na makandarasi katika bajeti ya mwaka 2014/2015.
Akiwasilisa hotuba ya Kambi hiyo kuhusu
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara kwa mwaka wa fedha 2015/2016,
Msemaji Mkuu wa Kambi hiyo, Felix Mkosamali, alisema
katika mwaka wa fedha wa 2013/2014, wizara hiyo ilitengewa Sh.
662,234,027,000 kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maendeleo, lakini hadi
kufikia Januari 2014, madeni ya makandarasi na washauri yalikuwa Sh.
663,870,636.26.
Alisema mfano mzuri ni bajeti 2014/2015
wizara ilikuwa na madeni yaliyofikia Sh. bilioni 760 huku bajeti ya
maendeleo kwa wizara na taasisi zake ikiwa ni Sh. bilioni 762.
“Kambi
rasmi ya upinzani bungeni inamtaka waziri kueleza ukweli Bunge lako
tukufu kwamba kwenye bajeti ya 2014/2015 ni fedha kiasi gani zimelipa
madeni na fedha kiasi gani zimekwenda kwenye miradi ya maendeleo,” alisema.
Mkosamali alisema hata kwa mwaka huu wa
fedha, Bajeti ya Maendeleo ni Sh. 890,572,000.00 kwa wizara na taasisi
zilizo chini ya wizara huku madeni yakiwa zaidi ya Sh. bilioni 800.
“Hakuna uhalisia kati ya fedha za maendeleo zinazoombwa na madeni
husika.”
Alisema wizara hiyo imekuwa kiandika
hotuba ndefu kuwachanganya wabunge kwa kuonyesha barabara zilizojengwa
miaka ya 80 na miaka 90 kama vile zimejengwa hivi karibuni.
Alisema wizara haijatoa ufafanuzi
unaoridhisha juu ya fedha zinazotengwa na kilomita zinazojengwa, mfano
wa Barabara ya Dar es Salaam – Chalinze – Morogoro (kilomita 200),
sehemu ya Dar es Salaam Chalinze imetengewa Sh. bilioni 2.45. “Hakuna
ufafanuzi kwani kilomita 100 haziwezi kujengwa kwa Sh. bilioni mbili
tu.”
Kambi hiyo ilisema licha ya mbwembwe
nyingi za waziri, madaraja yaliyoahidiwa kujengwa mwaka 2014/15 likiwamo
la mto Sibiti lililotengewa Sh. bilioni tatu, lakini fedha hizo
hazijatolewa na Hazina na mkandarasi ameondoka eneo la ujenzi na Daraja
la Kigamboni ambalo liliahidiwa kukamilika mwezi Juni, mwaka huu, ambalo
linaonyesha ahadi haitatekelezeka.
Kambi hiyo ilisema licha ya wizara na
hata Waziri Mkuu kujigamba kujenga kilomita 13,000 za lami katika awamu
ya nne, zimejengwa chini ya kiwango na zinabomoka na kuharibika miezi
sita au pungufu au mwaka mmoja baada ya matengenezo.
Alitoa mifano hiyo kuwa ni Dar es Salaam
– Dodoma ambayo imebonyea upande wa kushoto na inatengenezwa kila
wakati, lakini inaharibika, Bagamoyo – Msata, ambayo imeanza kuharibika
kabla haijamalizika, Dodoma – Iringa, imejaa mashimo maeneo kadhaa na
Dodoma – Mwanza hasa maeneo ya m lima wa Sekenke iliyobomoka muda mfupi
mara tu ya kukabidhiwa serikalini.
Kambi hiyo ilikiponda kivuko hicho
chenye kubeba abiria 300 kwa karibu Sh. bilioni nane, lakini kinatumia
saa tatu kutoka Dar es Salaam hadi Bagamoyo.
“Ni
jambo la ajabu kununua kivuko cha kizamani chenye spidi ndogo. Azam
Bakhresa ana meli inayotoka Dar kwenda Zanzibar kwa muda wa dakika 90 tu
na kinabeba abiria 500, ambacho kwa taarifa tulizonazo kimenunuliwa kwa
kati ya Sh. bilioni nne hadi tano tu,” alisema.
Kambi hiyo ilisema inaamini juu ya
ujenzi wa barabara zipitazo juu ili kuepusha kero kwenye maeneo ya
Tazara, Moroco, Ubungo, Magomeni, Selander bridge na maeneo mengine
yenye msongamano.
Hata hivyo, ilisema serikali haina nia ya dhati ya kuonyesha msongamano huo kwa kujenga angalau barabara moja inayopita juu.
Mkosamali alisema licha ya mbwembwe za
uwasilishaji wa waziri wa bajeti hiyo, kila inapofikia mwaka wa
uchaguzi, serikali imekuwa ikiahidi kujenga barabara kwa lengo la kupata
kura, lakini haitimizi ujenzi wa barabara hizo.
Alitaja barabara hizo kuwa ni ya
Nyakanazi, Kibondo, Kasulu, Kidahwe zenye urefu wa kilomita 310 ambayo
ilikuwa ahadi ya Serikaliya awamu ya tatu na awamu ya nne.
MTANZANIA
Hali ya njaa imeikumba Burundi hasa
katika mji mkuu wa Bujumbura baada ya wasafirishaji wa mazao kusimamisha
huduma yao kuhofia usalama wao.
Kutokana na hali hiyo Serikali imekuwa
ikihaha kuwaomba wananchi hasa waliokimbia wa mikoa ya milimani ya
Makamba na Ngozi kurejea nchini humo waendelee na kilimo.
Mkazi wa Bujumbura ambaye jina lake
linahitafadhiwa kwa sababu za usalama, alisema kwa wiki moja sasa huduma
muhimu za vyakula zimekuwa adimu nchini humo.
“Hali
imekuwa ni mbaya na sasa nchi inakabiliwa na njaa na hatujui la kufanya,
fedha zipo lakini bidhaa hakuna hasa chakula, yakiwamo mahindi na
mchele.
“Awali
tulikuwa tukipata chakula bila tatizo nchi ilipokuwa imetulia lakini
tangu yalipoingia machafuko ya kupinga hatua ya Nkurunziza (Pierre,
Rais) kuwania urais kwa muhula wa tatu, tunaoana nchi ilipofika sasa,” alisema mkazi huyo wa Bujumbura.
Juzi, Rais Nkurunziza alifanya ziara ya kushtukiza katika mpaka wa
Kagunga nchini Tanzania na Burundi na kuwataka warundi wasiikimbie nchi
yao akisema kwa sasa ina amani.
Pia aliwataka wananchi kuchangia gharama
za kuendesha uchaguzi wa nchi hiyo baada ya wahisani kusimamisha
misaada yao kwa Burundi.
Nchi hiyo imekumbwa na machafuko kwa
wiki kadhaa sasa ambako waandamanaji wakiwa wakipambana na polisi
wakipinga hatua ya Nkurunziza kutaka kugombea urais kwa muhula wa tatu.
Wanasema kitendo hicho ni kukiuka katika ya nchi hiyo inayotamka mtu atagombea urais kwa vipindi viwili tu.
Lakini Nkurunziza na chama chake cha
CNDD-FDD amekuwa akidai kwamba hicho kitakuwa kipindi chake cha pili
kuchaguliwa na wananchi kwa sababu katika muhula wa kwanza alichanguliwa
na Bunge.
HABARILEO
Rais Jakaya Kikwete amesema atahakikisha
anamaliza matatizo yote yanayowakabili walimu kote nchini katika
kipindi kilichobaki cha utawala wake.
Alitoa ahadi hiyo wakati akizungumza na
walimu wapatao 1,500 kutoka wilaya 153 na mikoa yote ya Tanzania Bara,
pamoja na wawakilishi kutoka Visiwani.
Akizungumza kwa hisia kali katika eneo
la Ngurdoto wilayani Arumeru mkoani hapa katika Mkutano Mkuu wa Tano wa
Chama cha Walimu (CWT), Rais Kikwete alisisitiza kuwa serikali na Chama
Cha Mapinduzi (CCM) anachokiongoza, kinaendelea kujali maslahi ya walimu
kama watumishi muhimu zaidi katika Taifa.
Alisema kwamba kilio chao ni cha umma na
ni wajibu wa viongozi wote kutilia maanani. “Nimeyasikia matatizo yenu
kupitia risala maalumu, na mengi tulikwishaanza kuyafanyia kazi.
Nawaahidi kutatua matatizo yenu kabla
sijaondoka rasmi mwishoni mwa mwaka huu, na hata kama nitastaafu hapo
baadaye, mengine yaliyosalia yataendelea kutatuliwa na viongozi wa
serikali ijayo nami binafsi nitaacha maagizo hayo,” alisema Kikwete.
Rais Kikwete aliyeingia madarakani mwaka
2005, anatarajiwa kumaliza muda wake wa uongozi Oktoba mwaka huu, baada
ya kuitumikia nchi katika awamu mbili za miaka mitano mitano.
Kikwete pia aliwashauri walimu kuunda
chombo kimoja, kitakachowasajili na kuwawakilisha kama Bodi, badala ya
hali iliyopo sasa, ambapo kuna utitiri wa vyombo vinavyowawakilisha
kiasi cha kusababisha usumbufu wakati mwingine.
Awali, Katibu Mkuu wa Chama cha Walimu
Taifa (CWT), Yahaya Msulwa alisoma risala ya walimu iliyomuomba Rais
Kikwete awatatulie matatizo yao kadhaa kabla hajaondoka rasmi
madarakani, kwani mengi ni yale yaliyodumu muda mrefu.
Miongoni mwa madai ya walimu ni pamoja
na malimbikizo ya mishahara, posho, malipo ya uhamisho, ucheleweshwaji
wa barua za ajira na likizo, na pia maombi yao ya kulipwa posho za muda
wa ziada wanaolazimika kuwa kazini.
Wawakilishi kutoka nchi sita pia wako
hapa kuhudhuria mkutano huo ambazo ni Uganda, Kenya, Denmark, Rwanda na
Ghana, ambapo pia viongozi wastaafu wa CWT taifa na wale wa kutoka
visiwa vya Zanzibar.
Naibu Katibu Mkuu wa CWT, Ezekiah Oluoch
alisema chama hicho kimekuwa kikipata ushirikiano mzuri kutoka Serikali
ya Awamu ya Nne, na kwamba wanatarajia uhusiano huo mzuri kuendelea
hata katika serikali ijayo ya Awamu ya Tano.
Malengo ya mkutano mkuu wa taifa wa CWT
ni pamoja na kujadili taarifa za kazi ya chama na taarifa za mapato na
matumizi na kupitia mpango mkakati wa miaka mitano 2015-2020.
Uchaguzi mkuu CWT Mkutano mkuu wa CWT
leo unatarajiwa kukamilishwa kwa uchaguzi mkuu, ambao umevutia wagombea
28 wa nafasi ya urais wa chama hicho chenye nguvu, kutokana na kuundwa
na idadi kubwa ya watumishi wa umma.
Miongoni mwa wagombea hao ni Rais wa
sasa wa chama hicho, Gratian Mukoba ambaye pia Rais wa Shirikisho la
Vyama vya Wafanyakazi Nchini (TUCTA).
Uchaguzi huo unatarajiwa kufanyika
katika ukumbi wa hoteli hiyo ya Ngurdoto, huku wajumbe wa mkutano huo na
jamii ya walimu kote nchini ikisubiri kwa hamu matokeo.
HABARILEO
Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC)
imeachiwa jukumu la kuamua siku ya kufanyika Uchaguzi Mkuu baada ya
wabunge kutaka uchaguzi usiwe unafanyika katika siku za kuabudu ambazo
ni Ijumaa, Jumamosi na Jumapili.
Mbali ya Mbunge wa Nkenge, Assumpter Mshama
(CCM), kuhoji katika swali lake la msingi, lakini wabunge wengi
walisimama kutaka kuuliza maswali ya nyongeza kuhusu siku hiyo ya
kufanyika Uchaguzi Mkuu.
Katika swali lake, Mshama alihoji ni
lini Serikali itaacha kutumia siku ya Jumapili kwa ajili ya uchaguzi
(kupiga kura) ili watu wa madhehebu ya Kikristo wapate muda wa kushiriki
ibada kikamilifu.
Pia alihoji Serikali inapoteza kitu
gani, kama itapanga upigaji kura katika Uchaguzi Mkuu kufanyika siku za
kawaida za kazi. Kwa kawaida, Tanzania hupiga kura siku ya Jumapili
katika chaguzi zake mbalimbali na mwaka huu, Uchaguzi Mkuu umepangwa
kuwa Jumapili ya Oktoba 25.
Katika maswali yao ya nyongeza, Mshama
na Mbunge wa Ludewa, Deo Filikunjombe (CCM), walitoa mifano ya nchi
zilizofanya uchaguzi wao katika siku za kawaida, wakizitaja Malawi,
Kenya, Uganda na India.
Hata hivyo, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), Jenista Mhagama alisema suala hilo ni la Kikatiba na kuwa NEC ndiyo yenye jukumu la kuamua kama inaweza kubadili tarehe hizo.
“Kwa
madhumuni ya utekelezaji bora wa majukumu yake yaliyoainishwa katika
Ibara hii, Tume ya Uchaguzi itakuwa ni Taasisi huru inayojitegemea,
itafanya maamuzi yake rasmi kuhusu utekelezaji wa majukumu yake kwa
vikao na Mtendaji Mkuu wake atakuwa ni Mkurugenzi wa Uchaguzi ambaye
atateuliwa na kufanya kazi kwa Mujibu wa Masharti ya Sheria iliyotungwa
na Bunge.”
“Hivyo,
Tume ya Uchaguzi kwa mamlaka haya iliyopewa Kikatiba inaweza kufanyia
kazi ushauri huo kwa kuzingatia wakati, hali halisi na mazingira
yaliyopo kwa wakati husika,” Mhagama.
Hili litawezesha kufanyika uchaguzi kwa amani kwa mujibu wa Katiba na sheria za nchi.”
No comments:
Post a Comment