Sunday, July 24, 2016

HADITHI, MWANAMKE SEHEMU 56

SIMULIZI ZA FAKI A FAKI 0655 340572
 
MWANAMKE 56
 
Waliyakagua yale meno ya tembo kisha nikaona krini ya meli inashushwa kutoka kwenye meli. Yale meno ya tembo yalikuwa yamepangwa kwenye turubai. Turubai hilo lilikuwa na vipete vinne vilivyowekwa kwenye pembe nne za turubai hilo. Kamba ikapitishwa kwenye vipete hivyo kisha ikapachikwa kwenye mkono wa krini.
 
Turubai likavutwa juu pamoja na pembe zake. Zilivutwa juu kuupita usawa wa meli kisha zikaingizwa ndani ya meli.
 
Abdi pamoja na wale maafisa wawili wa meli walirudi melini. Walipoteza muda wa karibu saa nzima kabla ya Abdi kurudi akiwa peke yake.
 
Aliingia kwenye kile chumba akiwa na mfuko uliotuna ambao aliuweka kwapani. Akafungua dawati mojawapo na kuuweka.
 
“Hizi ni pesa” akaniambia bila kumuuliza.
 
Sikumjibu kitu. Akarudi kuketi pale alipokuwa.
 
“Zile pembe zinakwenda Oman kwa waarabu” akaniambia lakini mimi bado nilikuwa kimya. Kitendo kile cha kunipaleka Mogadishu kwa lazima kilikuwa kimenifadhaisha sana.
 
Sikuwa nimeamini zile sababu zake kwamba alinipeleka kwa sababu za kiudugu na kiurafiki. Sikuwa na udigu naye wala urafiki naye na hatukuwa tukijuana zaidi ya kukutana siku ile.
 
Nilihisi kuna kitu ambacho alizungumza na Mapama ndio wakapanga niende Mogadishu. Sasa sikujua kama walikuwa wanakwenda kuniua au kunifanya nini.
 
Wakati niko katika lindi la mawazo nilianza kuona mataa kwa mbali. Ilikuwa ni bandari ya Mogadishu. Tulifika katika gati moja boti ikasimama.
 
Abdi akasimama alifungua dawati akauchukua ule mfuko wake wa pesa akaniambia.
 
“Tushuke”
 
Tulishukia kwenye gati. Tulikuta gari ndogo ya kifahari ya rangi nyekundu ikitusubiri.
 
Abdi alifungua mlango wa nyuma wa gari hilo akaniambia nijipakie. Nikajipakia.
 
Yeye alifungua mlango wa mbele kando ya dereva akajipakia. Gari ikaondoka.
 
ITAENDELEA KESHO
 
“Tunakwenda wapi?” Mtu aliyekuwa akiendesha alimuuliza Abdi tulipoingia kwenye mitaa.
 
“Nipeleke hotelini kwangu nikamuweke mgeni wangu halafu utaniachia gari”
 
Hapo ndipo nilipoliona na kulijua jiji la Mugadishu. Ilikuwa ni kabla  ya serikali ya Somalia ya Rais Siad Barre kupinduliwa na kuanza kwa vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyoendelea hadi leo hii na kuzua vikundi vya kigaidi.
 
Jiji lilikuwa zuri na la kisasa. Nililifananisha sana na jiji la Nairobi ambalo niliwahi kufika.
 
Baada ya kupita katika barabara kadhaa, gari hilo lilisimama mbele ya hoteli moja iliyokuwa na ghorofa tano.
 
“Zima gari unipe funguo” Abdi alimwambia dereva wa gari hilo ambaye alilizima gari na kuchomoa funguo akampa Abdi.
 
“Utatumia ile gari nyingine” Abdi alisema huku akifungua mlango wa gari na kushuka.
 
“Amour shuka twende nikakupatie chumba”
 
Abdi aliniambia huku akivuta hatua kuelekea kwenye mlango wa hoteli hiyo.
 
Nikafungua mlango wa gari hilo na kushuka, nikamfuata Abdi Msomali.
 
“Hii ni hoteli yangu” akaniambia na kuongeza.
 
“Inaitwa Handeni Hotel”
 
Alipotaja jina ‘handeni’ nilishituka kidogo kwa sababu Handeni ni moja ya walaya za mkoa wetu wa Tanga.
 
“Inaitwa Handeni au sikukusikia vizuri?” nikamuuliza.
 
“Inaitwa Handeni, pia ndio jina la eneo hili tuliopo”
 
“Handeni ni moja ya wilaya za mkoa ninaotoka mimi”
 
“Ninajua. Niliwahi kusikia kuwa Wasomali wanaoishi katika eneo hili wana asili ya kizigua. Ninajua kwamba Wazigua wako Handeni au nimekosa?”
 
“Ni kweli. Hata mimi ni mzigua”
 
“Basi hapa utakutana na ndugu zako”
 
“Lakini ndugu zangu hao ni Wasomali?”
 
“Ndio ni Wasomali kama mimi lakini babu zao walitokea Handeni miaka mingi iliyopita”
 
“Nimekuelewa”
 
NI KUDUCHU LAKINI KESHO MAMBO YATAKUWA POA.

No comments:

Post a Comment