SIMULIZI ZA FAKI A FAKI 0655 340572
MWANAMKE 56
ILIPOISHIA
Abdi alifungua mlango wa
nyuma wa gari hilo
akaniambia nijipakie. Nikajipakia.
Yeye alifungua mlango wa
mbele kando ya dereva akajipakia. Gari ikaondoka.
“Tunakwenda wapi?” Mtu
aliyekuwa akiendesha alimuuliza Abdi tulipoingia kwenye mitaa.
“Nipeleke hotelini kwangu nikamuweke
mgeni wangu halafu utaniachia gari”
Hapo ndipo nilipoliona na
kulijua jiji la Mugadishu. Ilikuwa ni kabla
ya serikali ya Somalia
ya Rais Siad Barre kupinduliwa na kuanza kwa vita vya wenyewe kwa wenyewe
vilivyoendelea hadi leo hii na kuzua vikundi vya kigaidi.
Jiji lilikuwa zuri na la
kisasa. Nililifananisha sana na jiji la Nairobi ambalo niliwahi
kufika.
Baada ya kupita katika
barabara kadhaa, gari hilo
lilisimama mbele ya hoteli moja iliyokuwa na ghorofa tano.
“Zima gari unipe funguo” Abdi
alimwambia dereva wa gari hilo
ambaye alilizima gari na kuchomoa funguo akampa Abdi.
“Utatumia ile gari nyingine”
Abdi alisema huku akifungua mlango wa gari na kushuka.
“Amour shuka twende
nikakupatie chumba”
Abdi aliniambia huku akivuta
hatua kuelekea kwenye mlango wa hoteli hiyo.
Nikafungua mlango wa gari hilo na kushuka,
nikamfuata Abdi Msomali.
“Hii ni hoteli yangu”
akaniambia na kuongeza.
“Inaitwa Handeni Hotel”
Alipotaja jina ‘handeni’
nilishituka kidogo kwa sababu Handeni ni moja ya walaya za mkoa wetu wa Tanga.
“Inaitwa Handeni au
sikukusikia vizuri?” nikamuuliza.
“Inaitwa Handeni, pia ndio
jina la eneo hili tuliopo”
“Handeni ni moja ya wilaya za
mkoa ninaotoka mimi”
“Ninajua. Niliwahi kusikia
kuwa Wasomali wanaoishi katika eneo hili wana asili ya kizigua. Ninajua kwamba
Wazigua wako Handeni au nimekosa?”
“Ni kweli. Hata mimi ni
mzigua”
“Basi hapa utakutana na ndugu
zako”
“Lakini ndugu zangu hao ni
Wasomali?”
“Ndio ni Wasomali kama mimi
lakini babu zao walitokea Handeni miaka mingi iliyopita”
“Nimekuelewa”
SASA ENDELEA
“Kama
usingefika hapa ungeijuaje historia?”
“Kwa kweli nisingeijua”
Tulikuwa tumeshaingia ndani
ya jingo hilo
la hoteli. Tulikwenda mapokezi ambapo niligundua msomali huyo alikuwa
akiheshimiwa sana
na wafanyakazi wa hapo.
“Nipatieni chumba kimoja”
alimwambia mmoja wa wahudumu wa mapokezi huku akiegemea kaunta hiyo.
Mhudumu huyo ambaye alikuwa
msichana wa kisomali aliyekuwa amevaa sare ya koti jeusi na sketi alichukua
kitabu cha wageni na kukifungua.
“Niandike jina gain bosi?”
akamuuliza Abdi kwa nidhamu huku akishika kalamu.
“Niandike mimi mwenyewe”
akamwambia.
“Nitumie jina gani?”
“Una maana hujui ninaitwa
nani?”
“Samahani bosi, ninalijua
jina lako”
Msichana aliandika kwenye
kitabu hicho kisha akainua uso wake na kumtazama Abdi.
“Niandike chumba cha daraja
gani?”
Abdi akanitazama. Bila shaka
alikuwa akinipima kama ninastahili chumba cha
daraja gani.
“Mpatie chumba cha daraja la
kwanza”
Mhudumu aliandika kisha
akanitazama mimi.
“Ungependa ukae ghorofa ya
ngapi?”
“Ghorofa ya kwanza au ya
pili”
“Nitakupatia ghorofa ya
kwanza”
Msichana alijaza kwenye
kitabu kisha akamtazama Abdi.
“Mgeni atakaa kwa siku ngapi”
Abdi akanitazama tena kisha
akamjibu.
“Hapo paache tu…”
Msichana akageuka na kuchukua
funguo.
“Nimekupatia chumba namba 85
ghorofa ya pili” akaniambia.
Sikumjibu kitu kwa sababu
hicho chumba sikukitaka mimi.
“Mpeleke” Abdi akamwambia.
“Twende nikakuoneshe chumba
chako” Msichana akaniambia.
Alitoka nyuma ya kaunta
akaelekea kwenye ngazi.
“Mfuate akakuoneshe chumba
utakachokaa” Abdi akaniambia.
Nilimfuata yule msichna.
Wakati anapanda ngazi nilikuwa nyuma yake. Niliuona mwili wake. Ulikuwa wa
kuvutia. Alikuwa na umbo lililofinyangwa kisomali hasa..
Nilifuatana naye hadi ghorofa
ya kwanza. Akanionesha chumba namba 84. Akakifungua na kuingia ndani pamoja na mimi.
Baada ya kukiona chumba hicho
msichana alitoka na kuniacha. Kwa vile sikuwa nimepata maelezo yoyote kutoka
kwa Abdi na mimi nikatoka. Nilifunga mlango nikashuka ngazi.
Nilimkuta Abdi akinisubiri
mapokezi.
“Umekiona chumba?”
akaniuliza.
“Nimekiona”
Akamgeukia mhudumu wa
mapokezi.
“Mtakuwa mnamuhudumia kwa
kila kitu muda wote atakaokuwa hapa. Mtampatia chai ya asubuhi, chakula cha
mchana na cha jioni, vinywaji na kila kitu atakachohitaji ikiwa ni pamoja na
kufua nguo zake na kuzipiga pasi. Bili itakuwa juu yangu” akamwambia.
“Sawa bosi, tumekuelewa”
Abdi akanitazama.
“Twenzetu” akaniambia.
Sikujua aliniambia twenzetu
wapi lakini kwa vile nilishakuwa kama mateka
wake sikumuuliza kitu nikamfuata.
Tulitoka nje ya hoteli
tukajipakia kwenye gari lake
na kuondoka.
Tukiwa ndani ya gari
nilitarajia angeweza kuniambia tunakwenda wapi lakini hakuniambia kitu.
Nilimuona alikuwa katika lindi la
mawazo. Sikujua alichokuwa akiwaza.
Baadaya kukata mitaa miwili mitatu alilisimamisha
gari mbele ya jingo moja la ghorofa
lililokuwa na maduka makubwa. Akaniambia tushuke.
Tukashuka na kuingia katika
duka mojawapo. Wakati tunaingia aliniambia.
“Hili pia ni duka langu”
“Ahaa…kumbe pia una maduka?”
nikamuuliza.
Licha ya kwamba nilikuwa na
fadhaa kwa kutojua hatima yangu, nilijaribu kujichangamsha na kuzungumza naye
kwa vile alionesha kama ananijali.
“Sina maduka, nina duka moja
tu” akaniambia.
Tulipoingia ndani ya duka hilo nililiona lilikuwa
duka kubwa la nguo za wanaume. Kulikuwa na suti, mashati, fulana, suruali na
aina kadha wa kadha ya nguo za kiume.
“Angalia nguo unazopenda,
upate nguo za kubadili” akaniambia.
Ilikuwa kweli nilihitaji
kubadili nguo. Licha ya kuwa sikuwa na nguo za kubadili, zile nilizovaa
zilikuwa zimechafuka na zilikuwa zinanitia aibu.
Nikachagua nguo. Nilichukua
shati moja na suruali moja pamoja na
viatu na soksi.
“Ongeza” Abdi akaniambia.
Nikaongeza shati moja.
Abdi akanichagulia mashati
mengine matatu.
“Ongeza suruali tatu”
akaniambia.
Nikachagua suruali zingine
tatu, nikawa na suruali nne.
Abdi akaniita upande uliokuwa
na suti.
Nilipokwenda alinaiambia.
“Mimi napenda sana kuvaa suti na wewe
chagua suti moja ya kuvaa”
Nikatabasamu. Ilikuwa ni mara
ya kwanza kukunjua uso wangu tangu ile boti tuliyokuwa tukisafiria kutoka Pemba ilipozama.
Abdi alipoona natabasamu
akacheka.
“Chagua suti moja au
nikuchagulie mimi?” akaniuliza.
Kabla sijamjibu alishachomoa
suti moja ya rangi ya kijivu.
“Chukua hii” akaniambia.
MAMBO YANAZIDI
KUSONGA. Hebu endelea kufuatilia ujue pana siri gani hapa. KWA LEO NASAINI OFF!
MAMBO NI KESHO.
No comments:
Post a Comment