Friday, July 29, 2016

HADITHI, MWANAMKE SEHEMU YA 49

SIMULIZI ZA FAKI A FAKI 0713 340572
 
MWANAMKE 49
 
ILIPOISHIA
 
Baada ya kuwaza sana nilipitiwa na usingizi. Sikujua nililala kwa muda gani lakini nilihisi kama nilishituka katikati ya usiku au nilikuwa katika ndoto. Nikaona kama mlango wa chumba nilichokuwa nimelala unafunguliwa taratibu.
 
Kitendo hicho kilitokea nikiwa na kumbukumbu kamili kichwani mwangu kwamba mlango wa chumba hicho niliufunga kwa ndani na kuhakikisha kuwa ulikuwa umefungika.
 
Mlango ulipokuwa wazi nilimuona mtu akiingia. Alikuwa mzee mwembamba na mrefu. Wembamba wake ulichanganyika na kukonda. Alikuwa na nywele ndefu, nyeupe tupu.
 
Alikuwa amejifunga shuka nyeupe kiunoni na mabegani alijitanda shuka nyingine nyeupe kuziba kifua na tumbo lake. Hata hivyo upande mmoja wa kifua chake ulikuwa ukionekana. Mbavu zake zilikuwa zimetokeza na kuhisabika.
 
Akaingia mle chumbani kwa kunyata. Wakati akiingia nilikuwa nikijiuliza nilikuwa ninaota au nilichokuwa kitendo  nakiona kilikuwa ni kweli.
 
Muda huo niligundua kuwa  sikuwa sawa. Nilikuwa kama niliyepatwa na jinamizi. Mwili wangu haukuwa na uwezo wa kufanya chochote hata kupiga kelele.
 
Kadhalika akili yangu ilikuwa imepoteza uwezo wake na nilikuwa kama taahira au zezeta. Sikuweza kujua ni kwanini nilijihisi kuwa vile.
 
Yule mzee wa kisomali alikuja hadi karibu na kitanda nilichokuwa nimelala.
 
Nilimuona vizuri. Alikuwa na pua ndefu na macho makali na madogo. Akasimama na kuniita.
 
“Amour!”
 
Nikanyamaza kimya. Nikamuona anasema maneno fulani kwa lugha  ya kisomali kisha akanyoosha mkono wake na kupapasa kitanda nilichokuwa nimelalaa akashika mkono wangu na kuubana.
 
SASA ENDELEA
.
Aliubana kwa nguvu nikaona kama nilishikwa kwa koleo.
 
“Inuka” akaniambia.
 
Kwa sababu nilikuwa kama taahira nisiyejielewa nikainuka kweli.
 
“Shuka kwenye kitanda” akaendelea kuniambia.
 
Nikashuka kwenye kitanda. Nilikuwa nimevaa chupi tu. Akaichukua ile shuka aliyoitanda mabegani mwake akanifunga nayo kiunoni kisha akanishika tena mkono na kuniambia.
 
“Twende”
 
Nikatoka naye mle chumbani.
 
Tulishuka ngazi, akatumia mlango wa nyuma wa hoteli kunitoa. Nilikuta gari limewekwa sambamba na mlango. Nikafunguliwa mlango wa nyuma wa gari, nikajipakia bilakuambiwa.
 
Mzee naye aliingia katika siti ya nyuma. Kulikuwa na mtu aliyekuwa kwenye siti ya dereva ambaye sikuweza kumuona vizuri. Sikujua alikuwa nani.
 
Kama ningemchunguza ningeweza kumjua lakini akili yangu haikuona umuhimu wa kutaka kumjua wala kujua nilikuwa napelekwa wapi.
 
Gari likapigwa moto na kuondoka. Safari ikaanza. Mji ulikuwa kimya na hakukuwa na watu wowote walioonekana barabarani zaidi ya walinzi wa maduka waliokuwa wakisinzia.
 
Baada ya mwendo wa karibu kilometa tano nilihisi kuwa tulikuwa tumeuacha mji kwani sikuona  tena majumba ya ghorofa isipokuwa nyumba ndogo ndogo.
 
Tulikuwa tumeingia  katika maeneo ya ambayo kwa lugha ya kwetu tungeyaita ‘uswahilini’
 
Mwanga wa gari tulilokuwemo ulimulika mapaka yaliyokuwa yakirandaranda kutafuta vyakula vilivyotupwa kwenye mapipa ya takataka. Ingawa ilikuwa usiku maji taka yalikuwa yakitiririka kutoka kwenye majumba ya watu na kuunda vidimbwi vya  maji taka kandokando ya barabara.
 
Wakati wote nilikuwa nashindana na akili yangu. Nilikuwa naona kichwa kizito kama niliyelemewa na usingizi, wakati huo huo sikutaka usingizi unichukue.
 
 Kila muda nilikuwa najigutuka na kukaza macho yangu ili nisilale. Lakini mwisho wake nilizidiwa nguvu, usingizi wa moja kwa moja ukanichukua ghafla.
 
Hata sikuweza kujua tena lile gari lilielekea wapi.
 
Lakini nilipokuja  kuzinduka nilijiona mimi na yule mzee tumekaa kando ya shimo lililokuwa mbele yetu. Shimo hilo lilichimbwa usawa wa kaburi kando ya mti mkubwa. Mahali tulipokuwa palikuwa ni porini.
 
Kulikuwa na taa ya chemli iliyokuwa inawaka pembeni mwa kaburi hilo na kufanya sehemu ile tuliyokuwa iwe na mwanga kwani eneo lote lilikuwa na kiza totoro.
 
Yule mzee wa kisomali aliingia kwenye lile kaburi akasimama na kuniambia.
 
“Ingia”
 
Na mimi nikaingia.
 
“Kaa hapo chini”
 
Akanionesha mahali pa kukaa, nikakaa. Nikaona analishika sikio langu la upande wa kulia na kusema maneno kwa lugha ya kisomali kama mtu aliyekuwa anasoma dua kisha akaniinamia na kukigandamiza kichwa chake kwenye komo langu.
 
Alinishika na kunigandamiza kwa nguvu sana mpaka nikasikia maumivu ya kichwa. Nilitaka  kupiga kelele nilipomuona amerushwa na kuanguka chini. Alikuwa kama aliyerushwa na umeme.
 
Akainuka taratibu na kutoka kwenye lile kaburi. Kilichofuatia baada  ya hapo sikukifahamu, nilishitukia tu nikiamka kitandani pale hoteli nilipokodiwa chumba na Abdi.
 
Nikahisi kwamba labda nilikuwa katika ndoto. Moyo ulikuwa ukinienda mbio. Nikainuka na kwenda kuutazama  mlango wa mle chumbani. Niliukuta umefungwa kwa ndani. Kitu ambacho kiliashiria kuwa hakukuwa na mtu aliyeingia humo chumbani.
 
Lakini ni ndoto gani ile? Nikajiuliza. Kila kitu nilikiona waziwazi kama vile kinatokea kweli.
 
Kama ilikuwa ndoto ilikuwa ya ajabu sana, nikajiambia.
 
Wakati ule nilipoamka kulikuwa kumekucha. Nikaingia maliwatoni. Nilipotoka nikavaa nguo. Nilivaa  suti ile ile niliyonunuliwa na Abdi.
 
Nikashuka chini na kuingia mkahawani. Nilipatiwa kifungua kinywa. Wakati nakunywa chai nikamuona Abdi akiingia.
 
“Amour salaam alaykum” akanisalimia kwa bashasha huku akinipa mkono.
 
“Alayka salaam. Habari ya  tangu jana?”
 
“Nzuri bwana, umeamkaje?”
 
“Nashukuru, nimeamka salama. Sijui wewe”
 
Na yeye akaagiza kifungua kinywa.
 
“Kuna sehemu nataka twende” akaniambia.
 
“Wapi?”
 
“Mogadishu ni kubwa sana. Kuna sehemu nyingi nataka kukuonesha”
 
“Sawa”
 
Tulipomaliza kunywa chai tukatoka.
 
“Jana nilikufuata usiku nikakuta umelala” Abdi aliniambia wakati tunatoka.
 
“Nililala mapema kwa sababu ya uchovu”
 
“Niliwambia wale wasichana wasikuamshe. Nilijua ulikuwa na uchovu mwingi”
 
Tulitoka nje ya hoteli tukajipakia kwenye gari. Lilikuwa ni gari la aina nyingine sio lile la jana yake.
 
Baada ya kujipakia tukaondoka.
 
“Nataka uuone mji wetu vizuri” Abdi alikuwa akinizungumzisha huku gari likiwa katika mwendo  wa taratibu au wa kinyonga . Nilikuwa sijui tunakwenda wapi.
 
“Mji wenu ni mzuri sana. Una majumba makubwa na umejengeka sana” nikamwambia.
 
“Bado. Kuna maeneo mengi hujayaona”
 
“Inavyoonekana mmepiga hatua kubwa ya maendeleo”
 
“Sana”
 
Baada ya mwendo wa karibu nusu saa tuliingia katika maeneo ya mashamba. Nilikuwa nikijiuliza alikuwa akinipeleka shambani kwake au alitaka kunionesha kitu gani?
 
Tulitokea katika mtaa mmoja uliokuwa umezagaa uchafu. Tulipishana na mbuzi, kondoo na kuku wa kienyeji. Abdi alikuwa akikata kona ovyo kukwepa mashimo na vidimbwi vya maji machafu.
 
“Tuache gari hapa” Abdi akaniambia huku akifunga breki pembeni mwa njia. Bila shaka alishindwa kuendesha kutokana na barabara yenyewe kujaa mazagazaga.
 
Tulishuka tukatembea kwa miguu. Tulizipita nyumba mbili za ghorofa. Zilikuwa nyumba zilizoonekana zimeshapitwa na muda wake wa kuishi watu kwani zilichakaa sana. Huenda zilijengwa miaka mia moja iliyopita. Enzi za utawala wa kikoloni.
 
Tuliingia mtaa mwingine uliokuwa na tifutifu jingi. Tukapita msikiti. Tulikwenda mbele kidogo, Abdi akasimama mbele ya mlango wa nyumba moja iliyokuwa imepakwa rangi nyeupe.
 
Mlango wake ulikuwa umechorwa picha ya nyota na mwezi.
 
Abdi alibisha mlango huo. Baada ya muda kidogo mlango ukafunguliwa.
 
Mzee mmoja akachungulia nje. Alimtazama Abdi kisha akanitazama mimi.
 
“Karibuni” akatuambia na kurudi ndani.
 
Abdi akaingia na kuniambia.
 
“”Karibu”
 
Na mimi nikaingia. Tulitokea katika ukumbi mpana kama  darasa. Harufu tuliyokutana nayo humo ndani ni ya udi na marashi.
 
Katikati ya ule ukumbi palitandikwa jamvi. Katika lile jamvi niliona  sinia iliyotiwa vitu mbalimbali kama vile ndizi mbivu, vipande vya miwa, mkate wa mchele, tende na vitu vingine ikiwemo chupa kubwa lenye  asali.
 
Katika kila pembe ya lile jamvi kuliwekwa nazi moja. Jumla zilikuwa nazi nne.
 
Yule mzee wa kisomali alikuwa amesimama nyuma ya mlango.
 
Alimwambia Abdi maneno kwa lugha  ya kisomali. Abdi akaniambia mimi.
 
“Twende tukakae pale”
 
Alinionesha lile jamvi.
 
Tukaenda kukaa. Yule mzee wa kisomali alitoka uani. Baadaye akarudi tena akiwa ameshika kitabu kikubwa cha kiarabu na yeye akakaa kwenye lile jamvi.
 
Sasa niliweza kumuangalia vizuri. Nikajiuliza mbona amefanana na yule msomali niliyemuota akinichukua kule chumbani? Alikuwa  mrefu vile vile na pua yake pia ilikuwa ndefu.
 
Nikashangaa sana.
 
KUNA NINI HAPA? HUYU MZEE NI NANI? ANA MIPANGO GANI NA ABDI? MAJIBU Y MASWALI  HAYO UTAYAPATA KESHO

No comments:

Post a Comment