Sunday, July 31, 2016

MBINU 7 ZA KUZUNGUMZA MBELE YA UMATI WA WATU

Mbinu Saba(7) Za Kuondokana Na Hofu Ya Kuongea Mbele Ya Kundi Kubwa La Watu

Katika maisha zipo hofu za aina nyingi zinazomtesa binadamu. Lakini mojawapo ya hofu kubwa ambayo inasumbua sana wengi ni hofu ya kuongea mbele za watu. Hii ni hofu ambayo  huwatesa wengi sana, hasa pale wanaposikia kwamba wanakwenda kuzungumza mbele ya umati wa watu.
Wengi wanaposikia suala la kuongea mbele ya watu hali ya hofu kubwa huwaingia ndani mwao. Kutokana na hofu hiyo husababisha kwa wengine kushindwa kula vizuri, kijasho huwatoka na wakati mwingine kuhisi hata kukimbia kama uwezekano huo upo.

Mara nyingi  hofu hii huwatokea wengi sana. Na ni hali ambayo karibu kila mmoja wetu ameshawahi kukutana nayo katika maisha yake au anayo mpaka sasa. Je, inapotokea unashindwa kuongea mbele za watu huwa unachukua mikakati gani? Je, huwa unaacha kama ilivyo au ni hatua gani ambazo unachukua?

Ni muhimu kujiuliza maswali hayo na kupata majibu kwa sababu suala la kuongea mbele za watu ni la muhimu kwa kila mtu na huwezi kulikwepa. Zipo shughuli nyingi ambazo huwa zinatutaka kuwa wasemaji wakuu, hapo unafanyaje kama huwezi kumudu kuzungumza mbele ya umati? Kama kweli nia yako ni kumudu kuongea mbele za watu makala hii itakupa majibu, kivipi?

Hivi Ndivyo Unavyoweza Kumudu Kuongea Mbele Ya Kundi Kubwa La Watu.

 1. Jiandae.
Ili uweze kufanikiwa vizuri kuongea mbele za watu, kwanza tambua kwa kina kile unachokwenda kukizungumza. Ikiwezekana ukiweke kwenye maandishi, kisha kifanyie mazoezi mara kwa mara. Unaweza ukafanya mazoezi hayo siku tatu kabla au hata moja.

Kwa kadri utakavyozidi kufanyia mazoezi utajikuta unakimdu vizuri na hiyo haitakupa shida sana wakati wa kuzungumza. Kwa kufanya hivyo akili yako itatulia kuliko ambavyo ungekurupuka na kwenda kuzungumza. Maandalizi ni muhimu sana ili kufanikiwa katika hili.

2. Ondoa mawazo ya kukosolewa.
Wengi wanashindwa kongea mbele za watu wengi kwa sababu ya kuogopa kukataliwa au  kuogopa kukosolewa. Wanakuwa wanaamini kwa vyovyote vile ni lazima watakosolewa. Haya ni mawazo hasi yanayowatesa sana na kuwasumbua wengi.
Lakini kwa vyovyote vile, Ukitaka kumudu kuongea mbele za watu wengi, jiamini kwanza wewe. Amini kuwa unaweza na hakuna mtu mwingine mwenye uwezo wa kuzungumza mada hiyo kuliko wewe. Acha kuamini sana katika kukoselewa, hilo litakusaidia kusimama imara.

3. Acha kufikiria watu unaongea nao.
Inaweza ikakupa shida sana kuongea mbele za watu hasa kila unapofikiria kundi kubwa la watu unaloongea nalo. Kundi hilo linaweza kuwa ni la wasomi au watu ambao wamekuzidi umri. Sasa kila ukifikiria kundi hilo unaanza kujiona kama hutaweza kuzungumza kitu.

Badala ya kufikiria kundi hilo, jitahidi kuweka mawazo yako yote kile unachokizungumza. Kiamini unachokizungumza kuwa utakizungumza kwa usahihi. Hapo ndipo mawazo yako unatakiwa uweke hapo na siyo sehemu nyingine. Hiyo itakusaidia kukuondolea hofu kwa sehemu kubwa.

4. Epuka kuongea kwa haraka.
Siri kubwa ya mafanikio ya kuongea mbele za watu ni kujifunza kongea polepole na kwa vituo. Wengi wanashindwa kumudu kuongea mbele za watu kwa sababu ya kutaka kuongea haraka haraka ili wamalize. Hii ni sumu kubwa inawafanya watu wengi washindwe kumudu kuongea mbele za watu kwa ufasaha.

Unapoongea kwa haraka kitu kinachokutokea kwanza, unakuwa unashindwa kupangilia maneno vizuri lakini pia inakuwa inakufanya ushindwe kupumua vizuri na kukufanya uongee kwa tabu. Kwa hali hiyo ni lazima kuepuka kuongea kwa haraka ili kufanikiwa kuongea mbele za watu vizuri.

5. Fikiria unaongea na mtu mmoja tu.
Sumu kubwa ya wengi kushindwa kuzungumza mbele za watu ni kuchukulia unazungumza na kundi kubwa la watu sana. Huu unaweza ukawa ndiyo ukweli halisi, lakini ili uweze kufanikiwa katika hili ni lazima kwako kujidanganya na kuchukulia kuwa unaongea na mtu mmoja.

Hapa ndipo siri ya mafanikio ilipo. Jifanye unaongea na mtu mmoja binafsi ingawa mbele yako lipo kundi kubwa. Wakati wa mazungumzo unaweza ukasisitiza jambo kwa kusema ‘unanielewa ninachosema’ badala ya kusema ‘mnanielewa ninachosema’ Hiyo itakupa nguvu ya kuondoa hofu ndani mwako.
.
6. Tuliza akili na mawazo yako.
Kwa kuwa utakuwa umeshajua kwamba unaonenda kuongea na watu wengi ni vizuri ukajua kuituliza akili yako. Kabla ya kile unachokwenda kuongea kunywa maji mengi, hiyo haitoshi unaweza ukalala zaidi usiku wke kabla ili kuiweka akili yako sawa.

Hayo yanaweza yakawa ni sehemu ya maandalizi ya kile unachokwwenda kukiongea. Ukumbuke pia akili yako inahitaji utulivu huu, ili usiwe na papara za hapa na pale. Hiyo itakusaidia kumudu zoezi zima la kuongea mbele za watu, ikiwa utakuwa makini kwa hilo.

7. Jifunze.
Tafuta namna ya kujifunza na kuweza kuongeza ujuzi wako wa kuongea mbele za watu. Unaweza ukajifunza kupitia vitabu mbalimbali au unaweza ukatafua ‘mentor’ au mshauri ambaye ameboboa katika hilo eneo na akakuongeza na kukusaidia kufikia hatua yaw ewe kuweza kumdu kuongea mbele za watu bila wasiwasi.

Haijalishi wewe ni mbovu kiasi gani wa kuongea mbele za watu. Lakini, kwa makala hii itakuwa chachu au hamasa kwako ya kuweza kukusaidia kuweza kumudu kuongea mbele za watu bila woga. Kitu kikubwa endelea kujifunza, fanyia mazoezi na mwisho wa siku utamudu hili pia na kuwa mshindi.
MG

No comments:

Post a Comment