SIMULIZI ZA FAKI A FAKI 0655 340572
MWANAMKE 48
ILIPOISHIA
Nilipobaki mle chumbani
nilivua nguo nikaenda kuoga. Niliotoka bafuni nilivaa ile suti mpya
aliyoninunulia Abdi. Nikajitazama kwenye kioo na kuona nilipendeza. Angalau
ilinisahaulisha madhila niliyokuwa nayo moyoni.
Baada ya kuvaa nilishuka
chini nikaingia katika eneo la mgahawa. Yule mhudumu aliyenipokea begi
alinifuata.
Akanisemea kwa kisomali.
“Sijui hiyo lugha labda
mnifundishe” nikamwambia.
“Unajua Kiswahili peke yake?”
akaniuliza.
“Na kizigua”
“Unatoka Handeni Tanzania?”
“Umejuaje”
“Kule ndio kuna wazigua”
“Nasikia na nyinyi pia mna
asili ya huko”
“Babu zetu wametoka huko
lakini mimi unaniona mweupe mama yangu ni mbarawa”
“Mmejifundisha wapi
Kiswahili?”
“Mimi nilizaliwa Garissa nchini
Kenya,
kule watu wanazungumza Kiswahili. Wenzangu wengine wametoka Mombasa”
SASA ENDELEA
“Nashukuru kwa mazungumzo, ninahitaji chakula”
“Upatiwe menyu?”
“Kwani wewe si ndiye
unayehusika”
“Mimi pia nahusika lakini
kuna mhudumu maalum wa hapa. Ngoja nimuite”
Shamsa akamuita msichana
mmoja na kumwambia.
“Mgeni wa bosi. Bosi ameagiza
apatiwe kila atakachohitaji. Bili itakuwa juu yake”
“Sawa” Msichana alimkubalia
kisha akaniuliza.
“Nikupatie menyu?”
“Ndio nipatie”
Menyu alikuwa anayo mkononi,
akaniwekea juu ya meza.
Nikaishika na kutazama orodha
ya vyakula. Nikachagua wali kwa samaki na juisi.
Wasichana wote wawili
waliondoka na kuniacha.
Baada ya muda kidogo
nililetewa chakula nilichoagiza. Wakati nakula nilianza kujiwazia
mustakbali
wangu kule Somalia.
Nilijiuliza Abdi alikuwa na madhumuni gani kunichukua mimi Somalia,
kuniweka hoteli na kunihudumia kama rafiki yake wakati tulikuwa
hatujuani.
Pia nilijiuliza ningekaa Somalia
hadi lini. Ingawa niliingia kienyeji lakini wakati ule Somalia ilikuwa na serikali.
Nilitakiwa kuwa na paspoti. Nilijiambia kama ningekamatwa nitakuwa na kosa la
kuingia nchi ya watu bila paspoti.
Nilishindwa kumuuliza Abdi
kuwa ningekaa hapo Somali kwa siku ngapi, hasa nikikumbuka muda ule alionitolea
bastola kwa kumhoji niende Somalia
kufanya nini.
Niliogopa kuwa ningeweza
kumkasirisha na hivyo akanipiga risasi na kwenda kuutupa mwili wangu jalalani.
Mtu mwenyewe licha ya kuwa mchangafu, mkarimu na anayependa kutabasamu,
alionekana kuwa katili na asiyejali kitu.
Mtu wa aina yake kuua ni kazi
ndogo tu!
Nilipomaliza kula niliondoka
nikarudi ghorofani. Niliingia chumbani nikaenda kusimama kando ya dirisha na
kutazama mandhari ya nje.
Niliendelea kusimama hapo
nikiangalia magari na watu waliokuwa wakipita barabarani huku akili yangu
ikitafuta jibu la kwanini niko pale Somalia lakini sikupata jibu.
Nilipitisha kama nusu saa
nikiwa hapo, nikaingia chumbani na kuvua koti kisha nikajilaza kitandani.
Nilikuwa nina uchovu na
nilikuwa na usingizi. Kwa vile moyo wangu kidogo ulikuwa umetulia nikaona
naweza kulala.
Na nililala. Nilipokuja
kuzinduka niliona giza.
Ilikuwa ni usiku. Kwa vile sikuwa na saa sikuweza kujua ilikuwa ni usiku wa saa
ngapi.
Nikainuka kitandani na
kuwasha taa. Pale mchagoni mwa kitanda palikuwa na simu. Nikainua mkono wa simu
na kuzungumza na opereta.
“Abdi ameshafika?”
nikamuuliza.
“Wewe nani?”
“Mimi ni mgeni wake, niko
ghorofa ya kwanza”
“Alifika, akakupigia simu
lakini haikupokelewa akajua umelala”
“Sasa yuko wapi?”
“Ameshaondoka, ametuambia
tukuambie kuwa mtakutana asubuhi”
“Ni saa ngapi sasa?”
“Saa mbili inakwenda kwenye
na nusu”
“Nitashuka sasa hivi kuja
kupata chakula”
“Sawa, chakula kipo”
Nikauweka mkono wa simu
mahali pake na kuvua nguo. Nilikwenda kuoga tena.
Nilipomaliza nilirudia kuvaa
suti yangu kisha nikashuka chini. Niliingia katika ukumbi wa mkahawa wa hoteli
hiyo.
Mhudumu aliponiona tu
akanifuata na kunipa menyu.
“Nahtaji chai tu”
nikamwambia.
“Chai na nini?”
“kama
kuna sambusa nipatie tatu”
Mhudumu aliondoka. Baada ya
muda kidogo alirudi akiwa na chano kilichokuwa na kisahani kilichokuwa na
sambusa tatu, birika ndogo ya maziwa, kipakiti cha majani ya chai, jagi la
sukari na kikombe kitupu kikiwa na kisahani chake.
Aliniwekea juu ya meza.
Nikachukua birika na kumimina maziwa kwenye kikombe nikatia kijiko kimoja na
nusu cha sukari na kukoroga.
Baada ya sukari kukolea,
nilitumbukiza kile kipakiti cha majani ya chai ambacho kiliyafanya maziwa kuwa
na rangi ya chai.
Nilitumia nusu saa nzima
kunywa chai huku nikijiwazia. Mpaka muda ule sikuwa nimeitambua dhamira ya
Abdi.
Nikajiambia baada ya siku
tatu nitamwambia kuwa nahitaji kuondoka kurudi kwetu kwani sikuwa na sababu
yoyote ya kuendelea kukaa Somalia
huku ndugu zangu na mama yangu wakiwa hawajui niliko.
Baada ya kumaliza kunywa chai
nilikwenda kujipumzisha kwenye eneo la wazi la hoteli ambapo palikuwa na upepo
mwanana kutoka Bahari ya Hindi.
Pale nilipoteza dakika kadhaa
kabla ya kuamua kurudi chumbani kwangu.
Mawazo ya Zena yalinijia
usiku ule. Nikajiambia msichana wa kijini aliamua kunisaliti kwenye kile kisiwa
baada ya kukataa kuoana naye.
Kitendo cha kutoonana tena na
Zena kilinipa picha kwamba Zena aliamua kuachana na mimi.
Nikajiambia kama kweli
alikuwa ameamua hivyo lilikuwa jambo la kushukuru sana kwani msichana yule alikuwa
ananisababishia matatizo makubwa.
Baada ya kuwaza sana nilipitiwa na
usingizi. Sikujua nililala kwa muda gani lakini nilihisi kama
nilishituka katikati ya usiku au nilikuwa katika ndoto. Nikaona kama mlango wa
chumba nilichokuwa nimelala unafunguliwa taratibu.
Kitendo hicho kilitokea
nikiwa na kumbukumbu kamili kichwani mwangu kwamba mlango wa chumba hicho
niliufunga kwa ndani na kuhakikisha kuwa ulikuwa umefungika.
Mlango ulipokuwa wazi
nilimuona mtu akiingia. Alikuwa mzee mwembamba na mrefu. Wembamba wake
ulichanganyika na kukonda. Alikuwa na nywele ndefu, nyeupe tupu.
Alikuwa amejifunga shuka
nyeupe kiunoni na mabegani alijitanda shuka nyingine nyeupe kuziba kifua na
tumbo lake. Hata hivyo upande mmoja wa kifua chake ulikuwa ukionekana. Mbavu
zake zilikuwa zimetokeza na kuhisabika.
Akaingia mle chumbani kwa
kunyata. Wakati akiingia nilikuwa nikijiuliza nilikuwa ninaota au nilichokuwa
nakiona kilikuwa ni kweli.
Muda huo niligundua kuwa sikuwa sawa. Nilikuwa kama niliyepatwa na
jinamizi. Mwili wangu haukuwa na uwezo wa kufanya chochote hata kupiga kelele.
Kadhalika akili yangu ilikuwa
imepoteza uwezo wake na nilikuwa kama taahira
au zezeta. Sikuweza kujua ni kwanini nilijihisi kuwa vile.
Yule mzee wa kisomali alikuja
hadi karibu na kitanda nilichokuwa nimelala.
Nilimuona vizuri. Alikuwa na
pua ndefu na macho makali na madogo. Akasimama na kuniita.
“Amour!”
Nikanyamaza kimya. Nikamuona
anasema maneno fulani kwa lugha ya
kisomali kisha akanyoosha mkono wake na kupapasa kitanda nilichokuwa nimelalaa
akashika mkono wangu na kuubana.
JE NI MZEE GANI TENA HUYO NA
AMETOKEA WAPI? HAYA NI MAMBO YA KUTISHA SASA! DUH!
No comments:
Post a Comment