SIMULIZI ZA FAKI A FAKI
MWANAMKE 55
ILIPOISHIA
Chumba hicho kilikuwa kikubwa
kuliko cha boti ya Mapama na kilikuwa kizuri kilichozungukwa na kuta za vioo.
Ndani kilikuwa na sehemu ya kulala na makochi ya kukalia.
“Karibu, kaa hapo” Msomali
akaniambia akinionesha moja ya makochi yaliyokuwa katika kile chumba.
Nikakaa.
“Asalaam alaykum” Msomali
akaniambia huku akiketi upande wa pili wa chumba hicho.
“Waalaika Salaam” nikamjibu
kwa sauti iliyonywea huku nikimtazama usoni kwake.
“Nimeelezwa na Nahodha kuhusu
wewe na mkasa uliowatokea mlipokuwa mnakuja. Ameniambia kulitokea joka kama nondo na kuwaangamiza wenzake, ni kweli?”
“Ni kweli”
“Kwani walitaka kukufanya nini?”
“Walitaka kuniua”
“Wapumbavu wale, mtu unaomba
msaada wanataka kukuua. Sasa hilo
joka lilitoka wapi?”
Nikabetua mabega yangu.
“Sijui”
“Bila shaka hilo ndilo lililokuokoa usiuawe, ungekuwa
umeshatoswa na kuliwa na papa”
Hapo sikumjibu kitu.
“Wewe unaitwa Umar?” Msomali
akaniuliza.
“Hapana”
“Unaitwa Amiri?”
“Hapana”
“Basi utakuwa unaitwa Amour”
Nikamkubalia.
“Ndio naitwa Amour,
umejuaje?”
Msomali huyo akacheka. Badala
ya kunijibu akaniambia.
“Nataka twende Somali mara
moja”
Nikashituka na kumuuliza.
“Kwani hapa tuko wapi?’
SASA ENDELEA
“Hapa ni Somalia, nina maana nataka twende
Mugadishu”
“Kufanya nini?”
“Nitakuwa na kazi na wewe”
“Mimi nataka kurudi.
Nilishamwambia Nahodha akishafaulisha mzigo wake turudi”
“Sasa amri ni yangu mimi si ya
Nahodha. Mimi nataka twende Mugadishu”
“Mimi sitakwenda huko”
Msomali huyo hakunisikiliza
akainuka na kutoka katika kile chumba.
Na mimi nikainuka na kumfuata.
Alipoona nimetoka alihamaki
akaniuliza.
“Unataka kuleta ubishi?”
“Hapana”
“Nani amekuamrisha utoke?”
“Nilikwambia sitakwenda
Mugadishu, nahitaji kurudi”
Msomali huyo hakusema kitu
tena, alitia mkono ndani ya shati lake
akatoa bastola na
kunielekezea.
“Sasa chagua moja, nikutoe
roho au baki kwenye hii boti!” akaniambia kwa hasira.
Nikanywea hapo hapo.
“Nenda kakae”
Ikabidi nirudi kwenye kile
chumba. Nilijua kama nitaendelea kubishana naye anaweza kuniramba risasi.
Wasomali hawa hawana huruma, kuna wengine hawana utu kabisa.
Nikakaa kinyonge kwenye kohi
huku macho yangu yakimtazama yule Msomali kwa macho ya kulaani. Nikamuona mapama
akiingia kwenye ile boti.
Akasimama na yule Msomali na
kuzungumza naye kwa kirefu. Sikuweza kusikia walichokuwa wanazungumza. Mara
moja moja Mapama alikuwa akinitazama. Nilikuwa nikimuonesha ishara ya kumuita
ili nimuulize mbona ananigeuka.
Lakini Mapama licha ya kuona
kuwa nilikuwa ninaashiria kumuita hakunijali hata chembe.
Pembe za ndovu zilikuwa
zikiendelea kingizwa kwenye boti hiyo. Kazi ilipokwisha, Msomali aliingia katika
kile chumba akafungua dawati mojawapo na kutoa mfuko ambao alitoka nao.
Ule mfuko ulikuwa na pesa.
Sikujua zilikuwa pesa za wapi isipokuwa niliona Msomali akitoa vitita vya noti
na kumhesabia Mapama. Mapama naye alizitia pesa hizo kwenye mfuko wa ngozi
aliokuwa ameushika kisha nikaona wanaagana kwa furaha.
Hapo ndipo nilipotoa sauti
nikamuita.
“Nahodha!”
Nilimuita zaidi ya mara tatu
lakini hakunipatiliza akatoka kwenye ile boti na kuingia kwenye boti yake. Yule
Msomali akaingia kwenye kile chumba. Bastola yake ilikuwa bado mkononi ingawa
aliishika kwenye mtutu.
Boti ya Mapama ikawashwa
moto. Nikajua kuwa Mapama alikuwa ameshaniuza kwa wasomali hao. Kwa lugha
nyingine ilikuwa sawa na kusema kuwa Nilikuwa nimetekwa nyara na kupelekwa
mahali bila hiyari yangu.
Boti ya Mapama ikaondoka,
ilikata kona ndefu na kugeuka ilikotoka. Nikaachwa mikononi mwa wasomali.
Nilikuwa nimetaharuki na
akili yangu iliniruka. Boti ya wasomali ikawashwa, nayo ikaondoka kuelekea Somalia.
Sikujua Mapama alikuwa
amezungumza nini na yule msomali na pia sikujua walikuwa wananipeleka Somalia
kwa ajili gani.
Pia nilikuwa nimeshangazwa na
jinsi msomali huyo alivyolitambua jina langu ambalo sikuwahi kumtajia hata
Mapama.
Kijana huyo wa kiosamali
alikuja kukaa kando yangu na kuendelea kutafuna mirungi yake. Bastola yake
aliipachika kiunoni. Bila shaka alifanya hivyo mbele yangu ili kunionya
nisimletee ukaidi.
Lakini ukiacha muda ule
aliponichomolea bastola hiyo ambapo alionesha kukasirika, uso wake ulikuwa wa kirafiki wakati wote.
“Mimi naitwa Abdi” akaniambia
wakati akiendelea kutafuna mirungi kisha akaniuliza.
“Unakula mirungi?”
Nikatikisa kichwa. Mdomo
ulikuwa mzito kumjibu.
“Najua wewe ni mzaliwa wa
Tanga lakini sijui unaishi sehemu gani?” akaniuliza.
Swali lake hilo
nalo lilinishangaza. Alijuaje kuwa mimi ni mzaliwa wa Tanga?
“Ninaishi sehemu inayoitwa
Msambweni” nikamjibu.
“Wazazi wakao wako wapi?”
“Baba yangu alikwishakufa,
mama yangu ndio yupo”
Msomali huyo alinikubalia kwa
kichwa.
“Unafanya shughuli gani?”
“Nimeajiriwa katika shirika
moja linaloitwa CTC”
“Najisikia ni mwenye furaha sana kukutana na mtu kama
wewe”
“Umelitambuaje jina langu
pamoja na mahali nilipozaliwa?” nikamuuliza.
Badala ya kunijibu aliangua
kicheko.
“Nilikuwa nakisia tu kumbe nilipatia”
“Haiwezekani ukisie halafu
iwe sawa”
“Amour sina jibu jingine la
kukupa kwa sasa”
“Uliwahi kufika Tanga?”
Abdi akatikisa kichwa.
“Sijawahi”
“Kwanini unalazimisha twende Somalia?”
“Ni kwa sababu za kiudugu na
kiurafiki tu. Utakuwa huko kwa muda tu halafu utarudi kwenu na kama utapenda kuendelea kuishi huko huko nitakupatia
nyumba, kazi na gari”
“Kwa vyovyote vile itabidi
nirudi, mama yangu na ndugu zangu hawajui niko wapi”
“Basi utarudi”
Boti iliendelea kusonga
mbele. Baada ya mwendo wa kilometa tano hivi tukakutana na meli iliyokuwa
imetia nanga. Boti ilikwenda kusimama ubavuni mwa meli.
Abdi aliniacha akatoka kwenye
kile chumba. Kuna ngazi iliyoshushwa kutoka kwenye meli. Abdi alipanda ngazi
hiyo akaingia ndani ya meli. Baada ya muda kidogo alishuka akiwa na maafisa
wawili wa meli hiyo ambao niliwatambua kutokana na mavazi yao.
Waliyakagua yale meno ya
tembo kisha nikaona krini ya meli inashushwa kutoka kwenye meli. Yale meno ya
tembo yalikuwa yamepangwa kwenye turubai. Turubai hilo
lilikuwa na vipete vinne vilivyowekwa kwenye pembe nne za turubai hilo. Kamba ikapitishwa
kwenye vipete hivyo kisha ikapachikwa kwenye mkono wa krini.
Turubai likavutwa juu pamoja
na pembe zake. Zilivutwa juu kuupita usawa wa meli kisha zikaingizwa ndani ya
meli.
Abdi pamoja na wale maafisa
wawili wa meli walirudi melini. Walipoteza muda wa karibu saa nzima kabla ya
Abdi kurudi akiwa peke yake.
Aliingia kwenye kile chumba
akiwa na mfuko uliotuna ambao aliuweka kwapani. Akafungua dawati mojawapo na
kuuweka.
“Hizi ni pesa” akaniambia
bila kumuuliza.
Sikumjibu kitu. Akarudi
kuketi pale alipokuwa.
“Zile pembe zinakwenda Oman
kwa waarabu” akaniambia lakini mimi bado nilikuwa kimya. Kitendo kile cha
kunipaleka Mogadishu kwa lazima kilikuwa
kimenifadhaisha sana.
Sikuwa nimeamini zile sababu
zake kwamba alinipeleka kwa sababu za kiudugu na kiurafiki. Sikuwa na udugu
naye wala urafiki naye na hatukuwa tukijuana zaidi ya kukutana siku ile.
Nilihisi kuna kitu ambacho
alizungumza na Mapama ndio wakapanga niende Mogadishu. Sasa sikujua kama
walikuwa wanakwenda kuniua au kunifanya nini.
Wakati niko katika lindi la
mawazo nilianza kuona mataa kwa mbali. Ilikuwa ni bandari ya Mogadishu. Tulifika katika gati moja boti
ikasimama.
Abdi akasimama alifungua
dawati akauchukua ule mfuko wake wa pesa akaniambia.
“Tushuke”
Tulishukia kwenye gati.
Tulikuta gari ndogo ya kifahari ya rangi nyekundu ikitusubiri.
Abdi alifungua mlango wa
nyuma wa gari hilo
akaniambia nijipakie. Nikajipakia.
Yeye alifungua mlango wa
mbele kando ya dereva akajipakia. Gari ikaondoka.
ITAENDELEA KESHO
No comments:
Post a Comment