Tanga.Chuo Kikuu cha
Kumbukumbu ya Sebastian Kolowa (Sekomu),kimesema hakitakumbwa na wimbi
linaloendelea linalotokana na mchakato wa Serikali wa kuwafichua wasio na sifa
kwa sababu tangu kilipoanzishwa kinajiendesha kwa umakini.
Mkuu wa Chuo hicho,Dr
Stephen Munga alitoa maelezo hayo LEO alipokuwa akizungumza na Tangakumekuchablog mara baada
ya kuzindua maonesho ya shughuli zinazoendeshwa na Sekomu yanayofanyika katika
tawi lake lililopo jijini Tanga.
Alisema msimamo wa Sekomu
wa tangu kilipoanzishwa kutosajili wanafunzi wanapojiunga wasio na sifa ndiyo
unaokiweka huru kipindi hiki ambacho Serikali inataka kila jambo liendeshwe kwa
utaratibu unaohitajika kwa chuo kikuu.
“Upepo unaovikumba vyuo
vikuu nchini hautatukumba Sekomu kwa sababu tumekuwa tukishirikiana na Serikali
tangu tulipoanza na msimamo wetu wa kuzingatia kanuni na sheria ndiyo
unaotuacha huru hivi sasa”alisema Dr Munga.
Akizungumzia kuhusu
maonesho hayo,Mkuu huyo wa Sekomu alisema yana lengo la kukiweka karibu na
jamii hasa katika kipindi hiki ambacho kinakaribia kufikisha miaka 10 tangu
kuanzishwa kwake lakini pia ni kuonyesha upekee wake nchini na Afrika mashariki
kwa ujumla hasa katika utoaji wa elimu maalumu.
“Sekomu ni chuo cha kwanza
kwa nchi za Afrika Mashariki kutoa shahada ya kwanza ya elimu maalumu,wakati
tukianza tulionekana kama chuo cha ajabu
lakini tunashukuru sasa hivi vyuo vingi vimeiga kutokana na umuhimu wake katika
makundi maalumu”alisema Dr Munga.
Kaimu Makamu Mkuu wa
Sekomu,mipango na biashara,Geofrey Kingazi alisema miongoni mwa yanayooneshwa
katika maonesho hayo ni machapisho ya kazi za utafiti na kazi zinazofanyika
chuoni ukiwamo mbinu zinazotumika
kuwajengea uwezo wanafunzi wa makundi maalumu.
Khalid Mohamed anayechukua masomo shahada ya elimu
katika chuo kikuu cha Sekomu aliupongeza uongozi wa chuo hicho kikuu kwa
kuzingatia sheria na kanuni ambapo wakati hivi sasa
wenzao wa vyuo vingine wanapohangaika wao hawana wasiwasi kutokana na kutimiza
masharti yote yanayohitajika.
MWISHO
No comments:
Post a Comment