SIMULIZI ZA FAKI A FAKI
MWANAMKE 50
ILIPOISHIA
Mzee mmoja akachungulia nje.
Alimtazama Abdi kisha akanitazama mimi.
“Karibuni” akatuambia na
kurudi ndani.
Abdi akaingia na kuniambia.
“”Karibu”
Na mimi nikaingia. Tulitokea
katika ukumbi mpana kama darasa. Harufu tuliyokutana nayo humo ndani
ni ya udi na marashi.
Katikati ya ule ukumbi
palitandikwa jamvi. Katika lile jamvi niliona
sinia iliyotiwa vitu mbalimbali kama
vile ndizi mbivu, vipande vya miwa, mkate wa mchele, tende na vitu vingine.
Katika kila pembe ya lile
jamvi kuliwekwa nazi moja. Jumla zilikuwa nazi nne.
Yule mzee wa kisomali alikuwa
amesimama nyuma ya mlango.
Alimwambia Abdi maneno kwa
lugha ya kisomali. Abdi akaniambia mimi.
“Twende tukakae pale”
Alinionesha lile jamvi.
Tukaenda kukaa. Yule mzee wa
kisomali alitoka uani. Baadaye akarudi tena akiwa ameshika kitabu kikubwa cha
kiarabu na yeye akakaa kwenye lile jamvi.
Sasa niliweza kumuangalia
vizuri. Nikajiuliza mbona amefanana na yule msomali niliyemuota akinichukua
kule chumbani? Alikuwa mrefu vile vile
na pua yake pia ilikuwa ndefu.
Nikashangaa sana.
SASA ENDELEA
Mzee huyo wa kisomali
akamtazama Abdi kisha akamuuliza maneno na kwa kisomali.
Abdi akanitazama kisha
akamwambia.
“Amour”
Nikahisi labda alimuuliza
jina langu.
Mzee wa kisomali akanitazama
kisha akafungua kitabu chake. Karasa zilikuwa zimegandana akakigusisha kidole
chake kwenye ulimi kukitia mate kisha akaufungua ule ukurasa.
Akaanza kusoma maneno ya
kiarabu. Sikuwezaa kujua alikuwa anasoma nini lakini nilisikia akitaja
jina la Zena Binti Jabal Keysi. Wakati
mwingine akitaja jina langu.
Mara kwa mara nilikuwa
nikimtazama Abdi kuona kama mwenzangu alikuwa
anaelewa chochote. Abdi alikuwa amenyamaza kimya. Alikuwa ametulia kama aliyekuwa anaaguliwa.
Ghafla tukaona nazi iliyokuwa
katika pembe moja ya lile jamvi inapasuka yenyewe. Mzee alikuwa akiendelea
kusoma tu. Naizi ya pili ikapasuka. Ilipopasuka nazi ya tatu ukuta wa uliokuwa
mbele yetu ulifanya ufa
akatokea mtu.
Alikuwa mwanamke aliyevaa
vizuri. Gauni alilovaa lilikuwa limedariziwa vimemeta vya dhahabu. Alikuwa
amevaa mkufu wa dhahabu na bangili za dhahabu. Masikioni alikuwa amevaa vipuli
vya dhahabu.
Kichwani kwake nywele zake
zilibanwa kwa taji la dhahabu lililomfanya aonekane kama malikia wa visiwa vya Sheba.
Alipotokea sote tulishituka
tukamtazama. Ilinichukua sekunde mbili au tatu kutambua kuwa alikuwa Zena!
Zena alikuwa amependeza
kuliko siku zote nilizowahi kumuona. Alikuwa aking’ara kama
mwezi mpevu! Sikuweza kujua ni kitu gani kilichomleta pale na kwanini alitokea
katika hali tofauti na anavyotokea siku zote.
Siku zote nilizokutana naye
alinitokea katika hali ya kawaida, si hali kama ile ya kuibuka kutoka
kwenye ufa wa ukuta. Ilikuwa hali ambayo si tu
ilinitisha mimi, ilimtisha hata Abdi aliyekuwa ameketi karibu yangu. Nilimuona
akimtazama kwa shauku iliyochanganyika na hofu.
Mzee wa Kisomali alimtazama
kisha alimwambia maneno kwa lugha ya kiarabu.
Zena hakusema chochote. Akiwa
miguu pekupeku alikuja taratibu hadi ilipokuwa ile sinia iliyokuwa na vitu
akaipindua kwa miguu. Sinia ilipinduka, na vitu vyote vilimwagika chini.
Alipomaliza kuipindua ile
sinia alimfuata yule mzee wa kisomali akampiga kibao cha shavu. Mzee alianguka
chini. Hakuinuka tena. Sasa akamfuata Abdi. Abdi alipoona anafuatwa aliinuka
haraka akatoka mbio. Na mimi nikainuka na kutoka mbio kumfuata Abdi.
Tulitoka kwenye mlango. Abdi kama ambaye alibadili mawazo alirudi
kwenye mlango huo na kuchungulia. Na mimi nikarudi kuchungulia.
Zena hatukumuona tena.
Tulimuona yule mzee akijiinua na kukaa. Abdi akarudi. Mimi sikurudi.
Nilibaki kwenye mlango
nikichungulia.
Nikawasikia Abdi na yule mzee
wakizungumza kwa lugha ya kisomali. Mzee alikuwa akifoka na akimuashiria Abdi
aondoke.
Abdi akatoka na kuniambia.
“Twenzetu”
Wakati tunatembea kurudi
tulikoliacha gari Abdi hakunieleza chochote na mimi sikumuuliza chochote.
Nilibaki kujiuliza mwenyewe
ni kitu gani kilichokuwa kimetendeka pale hadi Zena akatokea na kumwaga vile
vitu na kisha kumpiga kibao yule mzee? Sikupata jibu.
Nilihisi kuwa jibu alikuwa
analo Abdi lakini hakuonesha dalili yoyote ya kutaka kunieleza chochote. Na
mimi nikashindwa kumuuliza.
Niliona uso wake ulikuwa
umefadhaika na alikosa raha. Hakuwa hata akinitazama.
Tulirudi kwenye gari lake tukajipakia
na kuondoka.
Wakati Abdi akiendesha gari
kurudi mjini aliniambia.
“Nina hoteli mbili. Ile
unayokaa wewe na nyingine mpya. Nataka uwe mneneja wa ile hoteli yangu mpya”
“Nitawezaje kuwa meneja wa
hoteli yako wakati nataka kuondoka?” nikamuuliza.
“Huwezi kuondoka bila
paspoti. Subiri nikutengezee paspoti”
“Utanitengezea lini?”
nikamuuliza.
“Usiwe na haraka Amour.
Ninakuhakikishia kuwa nitakutengezea isipokuwa katika kipindi hiki cha kusubiri
paspoti yako iwe tayari nataka uwe meneja wa hoteli yangu. Nitakupa nyumba na
gari na kama utahitaji mke wa kisomali
nitakutafutia msichana mrembo”
Abdi alianza kunitia tamaa ya
maisha na kunipa ushawishi wa kubaki Somalia.
Hata hivyo moyo wangu ulikuwa
mzito kukubaliana naye. Nilikuwa simuelewi japokuwa mipango aliyonieleza
ilikuwa ya maana kwa upande wangu.
“Unataka kurudi Tanga, kuna
nini? Kama utakaa hapa kwa muda mfupi tu Amour
unaweza kupata maendeleo makubwa na ukarudi kwenu ukiwa tajiri” Abdi aliendelea
kunishawishi.
Muda wote nilikuwa nimebaki
kimya nikiyatafakari maneno yake. Alipoona nipo kimya na yeye akanyamaza.
Sikuweza kujua ni kwanini aliileta ile mada ya hoteli wakati kulikuwa na tukio
jingine la kuibuka kwa Zena ambalo ndilo alilopaswa kunieleza.
Kwanza kile kisomo alichokuwa anasoma yule mzee hadi nazi
zikapasuka na Zena akatokea, nilijiuliza, kilikuwa kiosomo cha nini. Hapo pia
sikupata jibu.
Dakika chache baadaye Abdi
alilisimamisha gari mbele ya nyumba moja iliyokuwa katika mtaa mtulivu.
Aliniambia tushuke,
tukashuka.
“Nifuate” akaniambia.
Tuliingia katika geti la ile
nyumba tukakuta mafundi wakipaka rangi kwenye kuta. Alizungumza nao kwa kiomali
kisha tukaingia ndani ya ile nyumba.
Ilikuwa nyumba nzuri na ya
kupendeza. Abdi alitazama sehemu zilizokuwa zimeshapigwa rangi, akaniambia.
“Hii ni nyumba yangu.
Ninaifanyia ukarabati kwa ajili yako. Wewe utakuja kuishi hapa”
“Wewe mwenyewe unaishi wapi?”
“Nitakupeleka ukapaone
nyumbani kwangu”
“Ni lini hii nyumba itakuwa
tayari?”
“Leo watamaliza kupiga rangi.
Labda keshokutwa unaweza kuhamia. Kesho nitakuwekea fanicha mpya”
Alifungua milango ya vyumba
na kunionesha ndani.
“Patakufaa sana hapa” akaniambia.
Sikumjibu kitu. Nilikuwa bado
ninajadiliana na moyo wangu kuhusu suala la kubaki pale Somalia.
“Amour unafikiria nini.
Unataka kuiacha bahati kama hii?” Abdi
aliniambia kisha akacheka peke yake.
“Twenzetu” akaniambia.
Tukatoka tena. Tulijipakia
kwenye gari tukaondoka.
Breki ya kwanza ilikuwa mbele
ya hoteli moja iliyokuwa katika mtaa mwingine. Ilikuwa hoteli ndogo ya ghorofa
moja, Ilikuwa imeandikwa kwa herufi kubwa. AL ASAD.
“Hii ndio hoteli ambayo
nitakuachia wewe, itakuwa kama mali
yako kwani tutakuwa tunagawana faida kila mwezi na kila mwaka kama utapenda
kuendelea kubaki Somalia”
Abdi aliniambia tukiwa bado tupo kwenye gari.
Alipoona nilikuwa
nikiiangalia angalia ile hoteli, aliniambia.
“Tushuke uione vizuri”
Tukashuka.
Tuliingia ndani ya ile
hoteli. Kwa kweli ilikuwa imechangamka.
“Sasa nani anaiendesha kwa
hivi sasa?” nikamuuliza.
“Yuko mtu lakini nitamuondoa”
“Sasa ni kwanini umuondoe?”
“Lengo langu ni kukunufaisha
wewe rafiki yangu au nimefanya kosa?’
“Hapana. Ni vizuri”
Abdi alinitembeza hoteli
nzima kisha tukaingia katika ofisi ya meneja.
Meneja mwenyewe alikuwa mtu
mzima. Kichwa chake kilishaanza kutoka mvi.
JE WEWE MSOMAJI UMESHAPATA
WAZO GANI KUHUSU HUYU ABDI? MIMI BADO SIMUELEWI! LAKINI HEBU ACHA TUENDELEE
TUTAMGUNDUA TU. KWA LEO NAKOMEA HAPA. Kesho ni kama kawa kama
dawa!
No comments:
Post a Comment