SIMULIZI ZA FAKI A FAKI
MWANAMKE 47
ILIPOISHIA
Ilikuwa kweli nilihitaji
kubadili nguo. Licha ya kuwa sikuwa na nguo za kubadili, zile nilizovaa
zilikuwa zimechafuka na zilikuwa zinanitia aibu.
Nikachagua nguo. Nilichukua
shati moja na suruali moja pamoja na
viatu na soksi.
“Ongeza” Abdi akaniambia.
Nikaongeza shati moja.
Abdi akanichagulia mashati
mengine matatu.
“Ongeza suruali tatu”
akaniambia.
Nikachagua suruali zingine
tatu, nikawa na suruali nne.
Abdi akaniita upande uliokuwa
na suti.
Nilipokwenda alinaiambia.
“Mimi napenda sana kuvaa suti na wewe
chagua suti moja ya kuvaa”
Nikatabasamu. Ilikuwa ni mara
ya kwanza kukunjua uso wangu tangu ile boti tuliyokuwa tukisafiria kutoka Pemba ilipozama.
Abdi alipoona natabasamu
akacheka.
“Chagua suti moja au
nikuchagulie mimi?” akaniuliza.
Kabla sijamjibu alishachomoa
suti moja ya rangi ya kijivu.
“Chukua hii” akaniambia.
SASA ENDELEA
Nikaichukua ile suti.
“Nenda kajaribu hizo nguo
kwenye kile chumba pale” akaniambia huku akinionesha mlango wa chumba hicho.
Nikaingia kwenye hicho
chumba. Unapoingia katika chumba hicho unajiona mwenyewe kwani kilikuwa na vioo
vitupu. Nilizijaribu nguo zote na kuona zilikuwa sawa.
Nilipotoka katika chumba hicho
nilimwambia Abdi.
“Bado viatu na soksi”
“Kachague jozi mbili za viatu
na soksi” akaniambia.
Nikaenda kuchukua jozi mbili
za viatu na jozi mbili za soksi.
Abdi alinifuata na
kuninong’oneza.
“Chukua na chupi kumi”
Aliponiambia hivyo sote
tukacheka.
Baada ya kufanya manunuzi
hayo ambayo Abdi aliyalipia kwa dola za Kimarekani tuliondoka kwa gari.
Tulirudi kule hoteli ambako Abdi aliniacha.
“Nitakupitia baadaye”
aliniambia wakati nikishuka kwenye gari. Alinyamaza kidogo kisha akaongeza.
“Najua utahitaji kujiweka
vizuri kidogo na pia kupata chakula kizuri”
“Ndio. Nahitaji vyote hivyo”
“Kwa upande wa chakula
nimeshaagiza utakula unachopenda”
“Sawa”
“Mimi naondoka kidogo,
nitakupitia baadaye”
Abdi akatia gea gari lake na kuondoka.
Niliingia hotelini nikiwa na
begi langu lililokuwa na nguo. Mhudumu mmoja alioniona aliniekea lile begi
akapanda ngazi na kwenda kunisubiri kwenye mlango wa chumba changu.
Nilipofika nilifungua mlango
nikamwambia.
“Karibu ndani”
Alikuwa msichana mweupe wa
kisomali mwenye mwili wa kutamanisha.
Msichana alitabasamu
akaliingiza lile begi chumbani kwangu kisha akaniaga na kutoka.
Sikujua kama wasomali
walikuwa wanazungumza Kiswahili. Pale hotelini niligundua baadhi ya wasomali
walikuwa wanajua kuzungumza Kiswahili tena Kiswahili cha kipwani kilichonyooka.
Nilipobaki mle chumbani
nilivua nguo nikaenda kuoga. Niliotoka bafuni nilivaa ile suti mpya
aliyoninunulia Abdi. Nikajitazama kwenye kioo na kuona nilipendeza. Angalau
ilinisahaulisha madhila niliyokuwa nayo moyoni.
Baada ya kuvaa nilishuka
chini nikaingia katika eneo la mkahawa. Yule mhudumu aliyeniokea begi
alinifuata.
Akanisemea kwa kisomali.
“Sijui hiyo lugha labda
mnifundishe” nikamwambia.
“Unajua Kiswahili peke yake?”
akaniuliza.
“Na kizigua”
“Unatoka Handeni Tanzania?”
“Umejuaje”
“Kule ndio kuna wazigua”
“Nasikia na nyinyi pia mna
asili ya huko”
“Babu zetu wametoka huko
lakini mimi unaniona mweupe mama yangu ni mbarawa”
“Mmejifundisha
Kiswahili?”
“Mimi nilizaliwa Garisa
nchini Kenya,
kule watu wanazungumza Kiswahili. Wenzangu wengine wametoka Mombasa”
JE NINI KITATOKEA? Usikose hapo kesho hapahapa tangakumekuchablog
No comments:
Post a Comment