Monday, July 25, 2016

MKENYA ALIEDANDIA NDEGE ASIMULIA CHA MOTO ALICHOKIPATA

Mkenya aliyedandia helikopta asimulia.

Wanjala
Swaleh Wanjala, Mkenya mwenye umri wa miaka 41 ambaye alidandia ndege magharibi mwa Kenya ametua mjini Nairobi lakini tofauti na safari yake ya awali, amewasili kama abiria rasmi ndani ya ndege baada ya Msamaria mwema kumlipia nauli akiandamana na mamake mzazi.
Swaleh alidandia ndege iliyokuwa imebeba mwili wa mfanyabiashara Jacob Juma mjini Bungoma mwezi mei mwaka huu.
Bwana huyo alidandia licha ya maafisa wa usalama kuwazuia watu waliowasili kuona maiti.
Mwanamume huyo ambaye amebandikwa jina la mwigizaji, James Bond, aliwasili jijini Nairobi leo akiwa na furaha baada ya kutua katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Jomo Kenyatta.
‘’Nimefurahi sana, nilihisi raha tofauti na kudandia ndege ambapo niliumia kutokana na upepo mkali angani,’’ alisema.
Jamaa huyo ambaye ni baba wa watoto wanne, ameongeza kuwa anajutia kitendo chake na kuwa hatowahi kurudia tena kosa hilo.
“Bado nahisi kuwa sijapata nafuu kabisa. Niliumia kwa sababu niliruka takriban mita kumi na moja kutoka hewani baada ya kushikilia ndege kwa muda.
Tofauti na safari yake ya awali juu ya ndege, ambapo alipanda kwa hiari wakati huu, ilikuwa vigumu kumshawishi Swaleh kusafiri kwa ndege.
“Nimeingiwa na woga tangu ajali hiyo, na sipendi tena ndege, alieleleza.
Bi Evelyne Namusya, mamake Swaleh waliosafiri naye hadi Nairobi, alieleza furaha ya kusafiri kupitia ndege akiwa na mwanawe.
"Hii ni mara yetu ya kwanza kusafiri kwa ndege na ninafuraha sana. Namshukuru mdhamini Joseph kwa kutuwezesha tufanikishe ndoto hii.”

No comments:

Post a Comment