Tuesday, July 26, 2016

WANAFUNZI 122 SHULE YA MSINGI MACHEMBA MUHEZA, WASOMEA CHINI YA MTI



Tangakumekuchablog
Muheza, WANAFUNZI shule ya msingi ya Machemba Wilayani hapa wamelazimika kusomea chini ya mti kufuatia upungufu wa vyumba vya madarasa na madawati na vyakati za mvua kukatisha masomo.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Mwalimu mkuu wa shule hiyo, John Ngadallah, alisema kwa muda mrefu wanafunzi wamekuwa wakilazimika kusomea chini ya miti kutokana na uhaba wa vymba vya madarasa na madwati.
Alisema shule hiyo iko na wanafunzi 354 ambapo wanafunzi 122 wanasomea chini ya mti huku shule hiyo ikiwa na vyumba vya madarasa 4.
Alisema inakuwa kero nyakati za mvua na  kulazimka kusitisha masomo kwa muda na kwa sasa jitihada zinafanywa kuhakikisha kero hiyo inamalizwa na wanafunzi kusoma darasani.
“Kama mulivyoona hapa wanafunzi wanasomea chini ya miti ni kutokana na uhaba wa vyumba vya madarsa na madawati, jambo hili linatuumiza kichwa sana kuweza kulimaliza” alisema Ngadallah na kuongeza
“Tumepeleka maombi kwa wadau wa elimu  mbalimbali lakini muitikio bado ila nina imani kupitia kwenu kilio chetu kitasikika” alisema
Aliwataka wadau wa elimu mashirika na watu binafsi wenye uwezo kuisaidia shule hiyo ili kuondokana na kero ya wananfunzi kusoma chini ya mti na kuweza kuwandaa  vijana kielimu na kuwa msaada kwa taifa.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Serikali ya kitongoji, Said Juma, alisema changamoto inazoikabili shule hiyo wamelazimika kufanya mkutano wa kijiji na kukubaliana kila kaya kuchangia matofali matatu kuanza ujenzi wa vyumba vya madarasa.
Alisema matofali hayo ni pamoja na ujenzi wa matundu ya vyoo ambapo kwa sasa shule hiyo iko na matundu mawili moja kwa wanafunzi wa kiume na jengine kwa wanafunzi wa kike.
“Changamoto ni nyingi shuleni pale lakini kwanza tumeadhimia kuanza na mambo muhimu mawili kwa matatu, kuongeza vyumba vya madarasa na madawati pamoja na matundu ya vyoo” alisema Juma
Mwenyekiti huyo aliwataka wananchi kutoa ushirikiano na kujitolea kwa moyo mmoja ili kero hiyo kuweza kumalizwa na kuwawezesha wanafunzi kusoma madarasani kwenye madawati.
                                                Mwisho




 Wanafunzi shule ya msingi Machemba halmashauri ya Wilaya ya Muheza Tanga wakisoma chini ya mti kufuatia uhaba wa madarasa na madawati.

Kwa habari, matukio na michezo ni hapahapa Tangakumekuchablog

No comments:

Post a Comment