HADITHI
YAMENIKUTA SALMA MIE
ILIPOISHIA
Si kwamba nilikuwa siwezi kusimama au kutembea bali nilikuwa
nikiropoka maneno mengi ambayo kwa akili yangu ya kawaida nisingeweza kuyatamka
huku nikijifanya nampenda sana Chinga.
Ghafla Chinga alinikata kilevi chote nilichokuwa nacho
aliponiambia kuwa anatarajia kuondoka kesho yake kurudi Dar es salaam kwa vile mwenzake anayeshirikiana
naye katika biashara zao alimpigia simu na kumueleza kuwa anahitajika Dar.
“Tutakwenda sote” nikamwaambia Chinga nikiwa nimemkumbatia.
Sikuwahi kumkumbatia Ibrahim namna ile hata siku moja tangu apate
upofu.
“Siwezi kukuchukua wakati ni mke wa mtu” Chinga akaniambia.
“Mtu gani…..yule kipofu? Yule tumeshaachana tangu jana usiku”
nikamwambia kwa sauti ya kupayuka.
“Mmeachana?” Chinga akaniuliza huku akishangaa
“Tumeachana jana, mimi si mke wake tena”
“Hebu nieleze vizuri, alikwambia anakuacha?”
“Ndiyo ameniambia”
“Ilikuwaje mpaka akakuacha?”
“Ulitokea ugomvi kati yetu. Jana asubuhi tulipokuwa tunazungumza
kwenye simu alitusikia akanyamaza hadi usiku alipoanza kunitukana kuwa mimi ni
malaya, nina wanaume wa nje.
Nikamwaambia kama mimi ni malaya anipe talaka yangu, ndipo akanipa”
“Iko wapi hiyo talaka aliyokupa?”
SASA ENDELEA
“Ni talaka ya mdomo tu, inatosha. Yeye hawezi kuandika kwa sababu
haoni. Niliondoka kwake tangu jana, nililala kwa shangazi Makolora”
“ Kama ni hivyo basi tutaondoka
pamoja”
“Safari itakuwa saa ngapi?”
“Nategemea kuondoka na basi la saa mbili asubuhi”
“Si una gari yako?”
“Gari nimeiacha kwa mzee. Kule Dar nina gari nyingine”
“Umeshakata tikiti?”
“Tutakata hapo hapo kesho”
“Sasa tukutane wapi?”
“Tukutane stendi ya mabasi saa moja asubuhi”
Kwa vile nilitaka kuondoka na Chinga nililazimika kutunga uongo
ambao Chinga aliukubali kwamba mume wangu ameniacha wakati haikuwa kweli.
Burudani yangu na Chinga siku ile iliisha saa sita usiku. Kwa vile
hakuwa na gari alinikodia teksi inipeleke Makolora kwa shangazi kwa vile
nilimdanganya kuwa nimehamia kwa shangazi baada ya Ibrahim kuniacha.
Wakati teksi inanipeleka Makolora nilimwambia dereva.
“Siendi Makolora, ninaenda Usagara”
“Usagara sehemu gani?” akaniuliza
Nikamuelekeza. Dereva akanipeleka hadi mlangoni. Nikashuka kwenye
teksi na kwenda kuujaribu mlango, nikakuta umefungwa. Sikuona haja ya kumgongea
mtu, nilivua viatu vyangu nikaenda kwenye ukuta wa nyuma ya nyumba. Nikarusha
viatu vyangu kwa ndani kisha nikaurusha mkoba wangu.
Baada ya hapo nikauparamia ukuta huo hadi nikaweza kuupanda na
kujirusha kwa ndani.
Nilipoanguka nilijiumiza mguu wangu wa kushoto. Nikainuka na kuokota
viatu vyangu pamoja na mkoba wangu kisha nikachechemea kuelekea kwenye dirisha
la chumba cha Zacharia, nikamgongea.
Niligonga mara ya kwanza, mara ya pili na mara ya tatu. Zacharia
akaamka na kuuliza.
“Wewe nani?”
Sikumwambia mimi nani isipokuwa nilimwambia.
“Nifungulie mlango” nikijua ataitambua sauti yangu.
“Wewe ni shemeji?”
akaniuliza.
“Ndiyo, nifungulie”
Baada ya kimya kifupi Zacharia akafungua dirisha na kunichungulia.
“Nikufungulie mlango gani?” akaniuliza huku akionesha kushangaa
kunikuta niko uani nikitaka kufunguliwa mlango.
Bila shaka alikuwa akijiuliza nimetokea wapi.
“Fungua mlango wa uani” nikamjibu na kuondoka pale kwenye dirisha
na kuelekea mlango wa uani.
Nilipofika nilisimama kwa muda kidogo kabla ya Zacharia
kunifungulia mlango, nikaingia.
Zacharia hakuniuliza chochote na mimi sikumwambia chochote.
Nikaenda kwenye mlango wa chumba chetu huku nikijiambia kama
utakuwa umefungwa kwa ndani nitakwenda kulala katika chumba cha wageni.
Wakati ninaujaribu huo mlango niliukuta haukuwa umefungwa kwa
ndani. Mlango ulifunguka nikaingia ndani. Niliwasha taa. Ibrahim alikuwa
amelala usingizi. Nikachukua sanduku langu nikalifungua na kuliweka chini kisha
nikafungua kabati na kutoa nguo zangu zile za maana, nikazipanga ndani ya lile
sanduku kisha nikachukua vitu vyangu vyote muhimu navyo nikavipanga juu ya zile
nguo. Nikalifunga sanduku na kuliweka juu ya kabati.
Nikavua nguo zangu na kuingia msalani. Nilipotoka nilivaa vazi
langu la kulalia nikalala. Nilipojitupa kitandani tu usingizi ukanipitia.
Niliamka dakika chache kabla ya saa kumi na mbili asubuhi.
Nilipoamka Ibrahim alikuwa bado amelala. Nikaenda kupiga mswaki na kuoga haraka
haraka. Nilipotoka nilivaa nguo ambayo nilishaitayarisha tangu ule usiku.
Nilikaa kando ya kioo na kujikwatua kidogo kisha nikavaa baibui
langu. Nikachukua sanduku langu na kutoka. Zacharia alikuwa bado hajaamka.
Nikaenda kwenye mlango wa mbele nikaufungua na kutoka.
Nikatembea haraka haraka hadi kwenye kituo cha daladala, nikakodi
teksi iliyonipeleka kwenye stendi ya mabasi.
Nilikuwa nataka kumpigia simu Chinga ili nimjulishe kuwa nilikuwa
nimeshafika stendi nilipogundua kuwa simu yangu niliisahau nyumbani.
Kidogo nilipata mshituko ulionifanya nichanganyikiwe kwa sababu
ningekosa mawasiliano na Chinga ambaye nilikuwa sijui kuwa alishafika hapo
stendi au la, na kama alikuwa ameshafika yuko
mahali gani. Pili nilichanganyikiwa kwa
sababu endapo Chinga angenipigia au atanipigia simu itakuwa haipokelewi jambo
ambalo litamchanganya na yeye.
Baya zaidi ni kuwa Ibrahim akisikia simu yangu inaita na mimi
mwenyewe nimeondoka anaweza kuipokea yeye.
Nikalaani. Kwa vyovyote vile nisingeweza kurudi nyumbani kuchukua
simu yangu kwa sababu Ibrahim atakuwa ameshaamka na lengo langu lilikuwa ni
kumkimbia asijue nimekwenda wapi.
Lakini mbali na hilo kama nitarudi nyumbani nitazidi kupoteza wakati na Chinga
anaweza kuondoka peke yake na kuniacha jambo ambalo sikuitaka litokee.
Nikaamua kusamehe simu na kubaki hapo hapo stendi nikitumaini kuwa
nitaweza kumuona Chinga kama amefika. Nilikwenda
kwenye mabasi yanayokwenda Dar er salaam. Nikawa nazunguuka huku na huko
kumtafuta.
Ghafla nikahisi mtu ananigusa bega kwa nyuma, nikageuka na
kumtazama. Nilishituka nilipoona ni Chinga na yeye alikuwa ameshika sanduku.
“Mbona hupokei simu? Ninakupigia lakini simu inaita tu”
akaniambia.
“Simu nimeisahau nyumbani” nikamjibu.
“Sasa itakuwaje na basi litaondoka sasa hivi?”
“Kwani umeshakata tikiti?”
“Nimekata baada ya kukuona unashuka kwenye teksi”
“Kumbe uliniona?”
“Nilikuona,nilikuwa kwenye ofisi ya kukatia tikiti ya kampuni ya
mabasi ya Rahaleo”
“ Kama umeshakata tikiti sawa.
Hiyo simu si muhimu nitaiacha”
“Nilipoona hupokei simu nilikutumia ujumbe kukueleza kuwa ninakata
tikiti ya basi la Rahaleo linaloondoka saa mbili na kukutaka uharakishe kufika
stendi”
Aliponiambia hivyo nilishituka kidogo kwa sababu nilihisi Ibrahim
akisikia kumeingia ujumbe kwenye simu yangu anaweza kumpa Zacharia amsomee na
hivyo kugundua mipango yangu.Lakini nikasema potelea mbali liwalo na liwe.
Kuondoka ni lazima niondoke na Chinga.
“Siwezi kujilazimisha kuendelea kuishi na mwanaume ambaye simtaki”
nikajiambia kimoyomoyo.
Chinga akaniambia tuingie kwenye basi ambalo lilikuwa karibu na
mahali tulipokuwa tumesimama. Tukajipakia kwenye basi hilo la kampuni ya Rahaleo.Tulitafuta siti
zetu, tulipoziona tuliweka masanduku yetu kwenye kifaa cha kuwekea mizigo.
Tukaketi.
Vile tunaketi tu niliona mtu ambaye sikumtarajia akiingia ndani ya
basi hilo,
mkono mmoja akiwa ameshika bakora yake na mkono mwingine ameshikwa na kijana
ambaye bila shaka ndiye aliyemleta hapo stendi.
Alikuwa Ibrahim!
Moyo wangu ulishituka. Furaha niliyokuwa nayo yote ikanipotea. Nikabaki
kumtazama kuona alikuwa anataka kufanya nini.
Nilishajua kuwa alinifuata mimi baada ya kuugundua ule ujumbe
niliotumiwa na Chinga ambao ulimtambulisha kuwa nilikuwa nimetoroka kwake na
nilikuwa ninasafiri na mwanaume kwenda Dar er salaam kwa basi la Rahaleo.
Mabasi ya Rahaleo yalikuwa yakifanya safari zake Da er salaam na
Tanga.
Hata kama Chinga hakuandika kuwa tunakwenda Dar lakini kwa vile
alitaja basi la Rahaleo, Ibrahim alishajua kuwa tunakwenda Dar. Bila shaka
baada ya Zacharia kumsomea ujumbe huo wa Chinga kwenye simu yangu, Ibrahim
alimwaambia aangalie kwenye kabati ambako waliona nilikuwa nimechukua nguo zangu
zote muhimu na vitu vyangu vyote.
ITAENDELEA kesho hapa hapa tangakumekuchablog
No comments:
Post a Comment