Ligi ya wanawake kuanza kurindima leo katika viwanja 6
LIGI
ya Taifa ya Wanawake inatarajiwa kuanza leo kwa viwanja sita kuchezwa
mechi za ufunguzi ingawa hafla ya uzinduzi wa ligi hiyo utafanyika
Uwanja wa Jamhuri mkoani Dodoma katika mchezo ambao Baobao ya hapo
itakapocheza na Victoria Queens ya Kagera.
Ligi hiyo ya kwanza kufanyika nchini Tanzania, lakini pia kwa nchi za
Afrika Mashariki na Kati imetokea kuvutia wadau kadhaa wakiwamo Azam Tv
ambao wamedhamini kwa kuonyesha mubashara (live), michezo hiyo 30
itakayofanyika viwanja mbalimbali hapa nchini.
Viongozi mbalimbali wa Serikali wakiwamo mawaziri na wabunge ambao kwa
sasa wako kwenye vikao mjini Dodoma kwa pamoja wanatarajiwa kuwa katika
hafla hiyo ambayo pilikapilika zake zinatarajiwa kuanza saa 8.00 mchana
kabla ya mchezo kuanza saa 10.00 jioni kwa saa za Afrika Mashariki.
TFF imepeleka uzinduzi huo Dodoma ikiwa na lengo la kuhamasisha soka
mikoani tofauti na Dar es Salaam ambako ilizoeleka zaidi miaka ya nyuma
kabla ya kuwa na mpango wa mashindano ya aina hiyo yanayoshirikisha timu
12 kutoka kona mbalimbali za nchi.
Kadhalika, kwa siku ya Novemba mosi ya uzinduzi huo vingozi wengi wa
Serikali wakiwamo wabunge wanatajiwa kuwa Dodoma ambako watapata fursa
pekee ya kushuhudia burudani ya mpira wa miguu wa ushindani
itakayosukuma hamasa ya kutoa michango yao mbalimbali kwa ajili ya soka
la wanawake.
Mbali ya mchezo huo wa kundi B kati ya Baobao na Victoria, michezo
mingine itakuwa ni kati ya Sisterz na Panama utakaofanyika Uwanja wa
Tanganyika huko Kigoma wakati Marsh Academy ya Mwanza itacheza na
Majengo Women ya Singida kwenye Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza.
Kundi A kutakuwa na michezo mitatu ambako Viva Queens ya Mtwara itacheza
na Mburahati Queens ya Dar es Salaam kwenye Uwanja wa Nangwanda Sijaona
wakati Fair Play ya Tanga itapambana na Evergreen ya Dar Salaam katika
mchezo utakaofanyika Uwanja wa Mkwakwani mjini Tanga huku JKT Queens
ikiwa ni wenyeji wa Mlandizi Queens ya Pwani kwenye Uwanja wa Karume,
Dar es Salaam.
No comments:
Post a Comment