Sunday, February 22, 2015

NAIBU MEYA TANGA AKERWA NA UCHAFU ULIOKITHIRI




Tangakumekuchablog
Tanga, NAIBU Meya halmashauri ya jiji la Tanga, Muzzamilu Shemdoe amezitaka kamati za mazingira jijini humo kuhakikisha zinafanya kazi zake na kusema kuwa kata yoyote ambayo itakuwa na mazingira machafu viongozi wake watajibishwa.
Akizungumza katika kongamano la mazingira lililowashirikisha wenyeviti wa Seikali za mitaa na kata na kuandaliwa na Asasi isiyo ya Kiserikali ya Nguvumali Community Development Emviroment (NCDE) jana, Shemdoe alisema jiji la Tanga bado ni chafu.
Alisema hali ya jiji hilo haliridhishi  na hivyo kuhitajika nguvu za ziada ikiwa na pamoja na elimu kwa wananchi na kutoa agizo kwa kamati za mazingira kila kata kuhakikisha  maeneo yao yanakuwa safi muda wote.
“Ili kuhakikisha kata zetu zinakuwa katika mazingira ya usafi ni lazima tujiwekee sheria ndogondogo ambazo zitatusukuma jiji letu kuwa safi kama yalivyo majiji mengine” alisema Shemdoe na kuongeza
“Kata yoyote ambayo haitokuwa tayari kuonyesha dhamira ya kweli katika kuyaweka maeneo yao safi tumejiwekea sheria ambazo viongozi wake tutawaita na kujieleza  sababu na wapi wamekwama” alisema
Alizitaka kamati hizo kufanya kazi zake na kuwa karibu na wananchi ikiwa na pamoja na kuhamasisha wananchi kujua wajibu wao katika kuyaweka mazingira ya usafi  sehemu zinazowazunguka.
Akizungumza katika kongamano hilo, Katibu wa Asasi ya Nguvumali Community Emveroment (NCDE), Frank Mgunda, alisema  changamoto inayowakabili wananchi ni vitendea kazi na kuwa chanzo cha jiji la Tanga kuwa katika mazingira machafu.
Alisema kutokuwa na vitendea kazi ni moja ya sababu ya mazingira hayo kuwa machafu na kusababisha kwa baadhi ya mitaa kuzuka magonjwa ya miripuko nyakati za mvua baada ya mitaro kujaa maji na kuzalisha mazalia ya mbu.
“Changamoto kubwa ni uhaba wa vifaa vya kufanyia kazi na utakuta viongozi wanahimiza usafi lakini ukiangali kwa vifaa vipi-----kuna kuzibua mitaro na uzoaji wa taka ngumu vyote ni vifaa” alisema Mgunda
Alisema ili kuweza kufikia malengo ni vyema halmashauri kugawa vifaa vya kufanyia usafi kila kata na kuweka mikakati ya eneo ambalo litaongoza kwa usafi kila mwezi kupewa zawadi ili kuleta hamasa zaidi.
Alisema kufanya hivyo kutasaidia kwa kiwango kikubwa kuwafanya wananchi kujua wajibu wao wa usafi katika mazingira inayowazunguka  na hivyo kulitaka jambo hilo kulifanya mara moja.
                                                     Mwisho

No comments:

Post a Comment