Saturday, February 21, 2015

SOMA HABARI KUU ZILIZOPEWA UZITO MAGAZETI YA LEO,TZ

Zimekupita Habari MAGAZETINI leo FEB21? Hapa ziko stori kubwa tano..

mhGuPOc
MTANZANIA
Kiongozi wa vijana waliopata mafunzo ya Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), waliokuwa wakiishinikiza Serikali kuwapatia ajira, George Mgoba amelazwa katika Hospitali ya Amana Dar es Salaam baada ya kutekwa na kuteswa na watu wasiojulikana tukio ambalo linafanana na kile alichofanyiwa Mwenyekiti wa Chama cha Madaktari, Dk. Steven Ulimboka au Mhariri Mtendaji wa Kampuni ya New Habari (2006) Ltd, Absalom Kibanda.
Mgoba ni miongoni mwa vijana waliowawakilisha wenzao zaidi ya 300 kukutana na viongozi wa juu wa Serikali hivi karibuni, akiwemo Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue kuzungumzia kilio chao na kupinga upendeleo wa ajira ndani ya Jeshi.
Gazeti la MTANZANIA lilifika Hospitalini ambako lilifanikiwa kuzungumza na Msemaji wa vijana hao, Omary Bakari, ambaye alisema alipokea simu saa nne siku ya Jumatatu hiyo hiyo ikimtaarifu kuwa Mwenyekiti wao, Mgoba, amelazwa katika Hospitali ya Tumbi, Kibaha ikimtaarifu kuwa mwenzao huyo alikuwa mahututi hospitali hapo.
Alipozungumza na mgonjwa ili kufahamu kilichompata alieleza kuwa alipigiwa simu na watu waliojitambulisha kuwa ni vijana wenzake wa JKT
wakimtaka waonane eneo la Mabibo Mwisho ili wazungumze mipango ya maandamano.
“Nusu saa baada ya kupigiwa simu alifika eneo walilopanga na kukutana na watu hao ambao walikuwa ni wanawake wawili na mwanaume mmoja, waliokuwa na gari aina ya Noah,” alisema.
Akinukuu maelezo ya mgonjwa, Bakari alisema baada ya kusalimiana kwa kupeana mikono na wanawake hao, mmoja wao alimwambia ajitoe kitu katika sikio na mara baada ya kufanya kitendo hicho alihisi mwili kupata ganzi na hivyo kupoteza fahamu papo hapo.
Alisema baada ya kuhakikisha amezimia inavyoonekana watu hao walimfunga kamba mikononi na miguuni na kisha kitambaa usoni na kwenda naye kusikojulikana.
“Baada ya muda mchache kupita Mgoba alipata fahamu na kujikuta akiwa amefungwa kamba pamoja na kitambaa usoni na hakujua anakopelekwa, ila alisema wakati huo alihisi wanaingia kwenye bonde ambako walimshusha,” alisema.
Alisema walipomshusha walianza kwa kumpiga, huku wakimtaka ataje ni nani aliyemtuma kuandamana kati ya Ukawa au Lowassa?
“Aliposhindwa kusema aliyemtuma ndipo walipombana sehemu za siri, vidole na mbavu na kisha kumpiga mateke na baada ya kumuona ameishiwa nguvu wakamvua nguo na kumlazimisha afanye tendo la ndoa na mmoja wa wanawake hao,” alisema.
Alisema walipoona ameshindwa kufanya tendo hilo wakamnyoa nywele na kisha kuanza kutafuta mshipa uliopo pembeni ya paji la uso, lakini walishindwa kuupata na hivyo kuamua kumchoma sindano mkononi.
“Walihakikisha hana nguvu, ndipo walisikika wakisema wamemaliza kazi, hivyo wakamchukua na kumtupa msitu wa Mailimoja wilaya ya Kibaha Mkoa wa Pwani.
“Akiwa msituni alijisikia kupata fahamu, ambapo alianza kutambaa kuelekea barabarani ambako msamaria mwema mmoja alimuona na kisha kumpeleka Kituo cha Polisi cha Mailimoja, Kibaha,” alisema.
Alisema Polisi wa Kibaha ndio waliochukua jukumu la kumpeleka katika Hospitali ya Tumbi saa nne usiku, kabla ya kufanya uamuzi mwingine wa kuwasiliana na ndugu pamoja na jamaa zake.
Kwa mujibu wa Bakari, polisi hao baada ya kufanya mazungumzo na ndugu wa Mgoba kwa minajili ya kumhamisha hospitali ili apatiwe matibabu zaidi, badala yake walimpeleka katika Kituo Kikuu cha Polisi (Central) kilichopo jijini Dar es Salaam.
“Cha kushangaza huko Central walimuweka rumande na baadaye walimtaka atoe maelezo pasipo kujali hali aliyokuwa nayo,” alisema.
Alisema baadaye polisi huo walimruhusu Mgoba kuondoka na kumpatia Sh 2,000, ingawa wakati huo alikuwa akijisikia vibaya.
Inaelezwa kuwa baada ya kuruhusiwa hakufika mbali, alidondoka na alizinduka akiwa amelazwa katika Hospitali ya Mnazi Mmoja, jijini Dar es Salaam.
Mwandishi wa habari hizi alishuhudia magari ya polisi (defender) matatu na basi moja la Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) yakiwa yameegeshwa katika viunga vya hospitali hiyo.
Alipotafutwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, Ulrich Matei, kuzungumzia tukio hilo, alikiri askari wake kumpokea Mgoba na kisha kumpeleka katika Hospitali ya Tumbi baada ya kumuona kuwa yupo katika hali mbaya.
Kamanda Matei alisema alipofikishwa katika hospitali ya Tumbi madaktari walithibitisha kuwa hana matatizo yoyote, na hivyo kuruhusiwa.
“Polisi wangu walimsaidia kutafuta ndugu zake na miongoni mwa waliofika ni mmoja aliyejitambulisha kama askari polisi na mwingine Usalama wa Taifa, aliyejitambulisha polisi alidai kuwa ni shemeji wa Mgoba, lakini yule aliyedai usalama wa Taifa alisema ni ndugu yake kwa hiyo sisi tuliishia hapo, hayo mengine siyafahamu, waulizwe polisi wa Dar es Salaam,” alisema Kamanda Matei.
Kamada wa Polisi, Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Suleiman Kova, alisema ofisi yake ipo katika hatua za awali za upelelezi na taarifa itatolewa leo ingawa kuna taarifa za kukanganya kuhusu kijana huyo.
Daktari mmoja wa hospitali ya Amana aliyezungumza na gazeti hili kwa sharti la kutotajwa jina alisema mgonjwa huyo anaweza kuhamishiwa katika Hospitali ya Muhimbili kwa kuwa hospitali hiyo haina baadhi ya vipimo ambavyo vinaweza kubaini kitu kilichotokea kwenye damu yake baada ya kulalamika maumivu sehemu za siri na kudaiwa kuchomwa sindano.
RAIA TANZANIA
Mwenyekiti wa Kamati ya LAAC, Rajab Mbarouk Mohamed amesema pamoja na mambo mengine, mbio za Urais ndani ya Chama cha CCM zimeifilisi nchi.
“Chanzo cha tatizo hili ni Serikali kuingia kwenye miradi mikubwa inayohitaji fedha nyngi kwa wakati mmoja.. Kikubwa zaidi ni Uchaguzi Mkuu na dili za Urais ndani ya CCM. Hawa jamaa wanakomba fedha nyingi kwa wakati mmoja..”– Mbarouk.
Mbarouk alitaja miradi iliyokwama kuwa ni Bunge Maalum la Katiba, uandikishwaji wa daftari la Wapigakura, Kura za Maoni uuandikishwaji wa Vitambulisho vya Taifa NIDA na Uchaguzi Mkuu unaosimamiwa na NEC akisema hata huko fedha hazijaenda za uhakika.
Uchunguzi wa gazeti la RAIA TANZANIA umebaini kuwa hali ya kifedha ndani ya Halmashauri ni mbaya na nyingine zikitamani kufungwa, lakini alipotafutwa Waziri wa Fedha, Saada Mkuya Salum alisema kucheleweshwa kwa fedha kunatokana na kitendo cha baadhi ya Halmashauri kutorejesha maelezo ya matumizi ya fedha kutoka Halmashauri husika.
NIPASHE
Hali ya afya za Watazania zipo hatarini kutokana na kasi ya kuingizwa dawa zisizofaa kwa tiba asilia kutoka nchi kadhaa za Asia hasa Korea Kaskazini.
Uchunguzi wa Gazeti la NIPASHE umeonesha dawa hizo zinaingizwa na kuuzwa nchini bila kuwa na maelezo yoyote ya uthibitisho wa usalama wa dawa hizo pamoja na kuwa na ujazo wa madini yanayozidi kiwango kinachotambullika kwa afya za watu.
Chanzo kimojawapo cha gazeti la NIPASHE kilibaini kuwa dawa hizo zinauzwa na waganga wa jadi kutoka Korea Kaskazini zilipaswa kuwa na viambata vya maelezo vilivyomo kwenye dawa lakini hali haipo hivyo na wala hazina majina.
“Mimi ninasafirisha dawa zangu nje ya nchi na huko lazima dawa iwe na jina, aina ya mti na uthibitisho kwamba hazina sumu”– Maneno Tamba.
Akizungumza kwa niaba ya mtaalamu wa masuala hayo Mwamaja amesema dawa zote zinaangaliwa na TFDA na sio rahisi zikasajiliwa pasipo kukubalika na Mamlaka hiyo.
JAMBO LEO
Wanafunzi zaidi ya 503 wameshindwa kuhudhuria masomo katika Shule ya Msingi Lengatei kutokana na mgogoro wa mpaka uliopo kati ya Kijiji cha Lengatei na Zambia ambapo wazazi wa wanafunzi hao waliwazuia watoto wao wasiende shule.
Ofisa ya Mtendaji wa Kijiji hicho Ezekiel Pingwa amesema baadhi ya wazazi walivamia shuleni hapo na kuwacharaza viboko na makofi wanafunzi akiwadia amri yao ya kutokuhudhuria shule.
Mtendaji huyo amesema sakata hilo la mpaka linazidi kuchukua sura mpya baada ya Tume Maalum kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu kuweka mpaka katikati ya Shule hiyo jambo ambalo limepingwa na wananchi hao.
MWANANCHI
Rais Kikwete amekuwa Mwenyekiti wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), akichukua jukumu hilo kutoka kwa Rais Uhuru Kenyatta aliyemaliza muda wake ambapo makabidhiano hayo yalifanyika jana katika mkutano wa 16 wa wakuu hao wa nchi hizo uliofanyika kwenye Ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano wa Jomo Kenyatta.
Nchi hizo zilizindua mfumo wa mawasiliano ya pamoja ambapo Rais Kikwete aliwasiliana na Balozi Sefue na kuzungumza naye, kwa mfumo huo utaziwezesha nchi wanachama kupunguza gharama za uendeshaji wa mikutano baina ya wajumbe ambapo awali wajumbe walilazimika kusafiri na kukutana sehemu moja.
“Mfumo huu (video conferencing) utaondoa haja ya wajumbe kukutana. Marais, mawaziri, makatibu wakuu pamoja na wafanyakazi wa Serikali wataendesha mikutano yao bila ya kukutana. Hii itapunguza matumizi ya fedha kwa ajili ya kujikimu na bajeti nyingine za mikutano,”– Mkurugenzi Msaidizi wa Huduma za Jamii Wizara ya Ushirikiano Afrika Mashariki, Eliabi Chodota
Kuhusiana na katazo ambalo limetangazwa na Kenya kwa gari za kitalii kuingia baadhi ya maeneo nchini humo, Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue alisema hafahamu sababu ya Kenya kuzuia magari hayo.
Nitaendelea kukupatia kila stori inayonifikia mtu wangu, niko tayari kukutumia wakati wowote kupitia www.tangakumekucha.blogspot.com

No comments:

Post a Comment