Thursday, February 26, 2015

SOMA HABARI KUBWA ZILIZOPEWA UZITO MAGAZETI YA LEO,TZ

Kutoka MAGAZETI ya leo Tanzania February 26, 2015 hapa nimekuwekea STORI 8 zilizopewa Headlines…

today
MWANANCHI
Kundi la Wanamgambo wa kiislamu la Al Shabaab lenye makao makuu yake Somalia limetishia kuzishambulia nchi za Magharibi ikiwemo Marekani.
Kundi hilo limesema kuwa litashambulia maeneo ya mbalimbali ya kibiashara  yaliyopo katika nchi hizo.
Kupitia mtandao wa Twitter kundi hilo limesema litashambulia maeneo ya Mall of America mjini Minnepolis nchini Marekani, Forum des Halles mjini Paris nchini Ufansa.
Al Shabaab walisema kuwa zitashuhudia mashambulizi yanayofanana na yaliyotokea Nairobi nchini Kenya mwaka 2013 ambapo watu 60 walifariki dunia na wengine kujeruhiwa.
Waziri wa Usalama wa Marekani Jeh Johnson aliwataka raia wa nchi hiyo kuwa makini katika kutoa taarifa kwa vyombo vya usalama ili kudhibiti mashambulizi ambayo yanweza kutokea.
MWANANCHI
Mbunge wa Bariadi Magharibi (CCM), Andrew Chenge ameibuliwa tuhuma nzito kwenye Baraza la Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma baada ya kudaiwa kuwa aliishawishi kampuni ya Independent Power Solution Limited (IPTL) kuingia mkataba na Tanesco na baadaye kuwa mshauri wa kampuni hiyo binafsi iliyomuingizia Sh1.6 bilioni zinazohusishwa na sakata la Akaunti ya Tegeta Escrow.
Hata hivyo, Chenge, ambaye ni mhitimu wa Shahada ya Umahiri wa Sheria kwenye Chuo Kikuu cha Harvard cha Marekani, aliwasilisha amri ya zuio ya Mahakama Kuu inayokataza chombo chochote cha Serikali kujadili sakata la escrow hadi hapo shauri lililopo mahakamani litakapotolewa uamuzi, jambo lililozua mjadala wa kisheria na kusababisha mwenyekiti wa Baraza la Sekretarieti ya Maadili, Jaji Hamisi Msumi, kuahirisha hadi leo.
Chenge ni mmoja wa watu kadhaa wanaotarajiwa kuhojiwa na kamati hiyo kutokana na kuhusishwa na kashfa ya uchotwaji wa zaidi ya Sh306 bilioni kutoka kwenye Akaunti ya Tegeta Escrow iliyofunguliwa Benki Kuu kwa makubaliano kati ya Tanesco  na IPTL baada ya pande hizo mbili kutofautiana kuhusu tozo za malipo ya umeme unaozalishwa na kampuni hiyo binafsi.
Mwingine ni mbunge wa Muleba Kusini (CCM), Anna Tibaijuka, aliyekuwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi na ambaye pia aliingiziwa kwenye akaunti yake Sh1.6 bilioni zinazohusishwa na akaunti hiyo ya escrow.
Wote wawili waliingiziwa fedha hizo na James Rugemarila, mkurugenzi wa VIP Engineering iliyokuwa ikimiliki asilimia 30 ya hisa za kampuni ya IPTL.
Lakini jana, akisoma hati ya malalamiko dhidi ya mbunge huyo wa Bariadi, mwanasheria wa Sekretarieti ya Maadili, Hassan Mayunga alisema mlalamikiwa, akiwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) mwaka 1995, aliishauri Serikali kuingia mkataba wa miaka 20 na IPTL wa kuongeza uzalishaji wa umme.
“Mlalamikiwa baada ya kustaafu wadhifa wa AG, Desemba 24 mwaka 2005, mwaka 2006 aliingia mkataba wa kuwa mshauri mwelekezi wa kampuni ya VIP Engineering and Marketing Limited iliyokuwa inamiliki asilimia 30 ya hisa za IPTL,” alisema Mayunga akikariri hati hiyo ya malalamiko.
MWANANCHI
Utafiti mpya umebaini kuwa asilimia kubwa ya Watanzania hawaridhishi na uwepo wa raia wa China nchini kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo kupokwa ajira.
Kadhalika utafiti huo uliofanywa na Afrobarometer kuhusu uwepo wa raia wa China nchini una faida au hasara kwa Watanzania’ ulibaini kuwa licha ya kuzinunua wa wingi bidhaa za nchi hizo lakini hawaridhishwi nazo.
Mtafiti kutoka Taasisi ya REPOA  Stephen Mwambole alisema wananchi 2,386 wa bara na visiwani walihojiwa kati ya Agosti 26 na September 29, 2014, kati yao 37% alisema bidhaa kutoka China zisizo na ubora zinachafua taswira ya nchi hiyo,20% walisema Wachina waishio nchini wamechukua ajira ambazo zingeweza kufanywa na Watanzania wenyewe.
Watanzania wanafurahishwa na bidhaa za kichina lakini hawafurahishwi na ubora wake:-Mwambole.
Ripoti hiyo inaonyesha kuwa 81% ya wasomi,72% wazee,wakazi wa mijini 77% na wanaume 75% ndiyo wanaofurahia uhusiano uliopo kati ya nchi hizo.
HABARILEO
Mtoto Pendo Emmanuel (4) mwenye ulemavu wa ngozi, aliyetekwa na kuchukuliwa na watu wasiojulikana nyumbani kwao wilayani Kwimba, imegundulika alihifadhiwa katika hoteli moja ya kifahari jijini Mwanza, kabla ya kukabidhiwa kwa watu wengine, walioondoka naye kusikojulikana.
Imeelezwa kwamba mtoto huyo alikuwa akilishwa chakula na watumishi wa hoteli hiyo, kabla ya kuchukuliwa na kukabidhiwa kwa watu hao wengine.
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Magesa Mulongo alisema mjini hapa jana kwamba Polisi inasaka watu hao waliokabidhiwa huku mzazi (baba yake), Emmanuel Shilinde, watumishi na mmiliki wa hoteli hiyo (haikutajwa jina) wakiendelea kuhojiwa.
Mulongo alitoa taarifa hiyo wakati wa hafla ya kuapisha wakuu wa wilaya wateule watatu, Pili Bayo wa Wilaya ya Kwimba, Zainabu Telaki wa Sengerema na Mwajuma Nyiruka wa Wilaya ya Misungwi.
Pendo alitekwa na watu wasiojulikana usiku wa Desemba 27 mwaka jana nyumbani kwao katika kijiji cha Ndami wilayani Kwimba mkoa wa Mwanza baada ya watu hao kumpora akiwa amelala na wazazi wake.
Baada ya kutoweka na polisi kutoa picha, kuwezesha atakayemwona, kutoa taarifa, pia ilitangaza kutoa dau la Sh milioni tatu kwa mtu atakayetoa taarifa, zitakazosaidia kupatikana kwa mtoto huyo.
, “Baadaye Pendo alichukuliwa na kukabidhiwa kwa watu wengine, ambao walitoweka naye, kwa sasa serikali inawasaka watu hao waliokabidhiwa pale hotelini.” Aliongeza, “Watu wote waliokuwa wanamhudumia Pendo, mzazi wake na mmiliki wa hoteli ile tunawashikilia ili watueleze alikopelekwa Pendo ingawa hatujui kama yuko hai au amekufa.
 NIPASHE
Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), umesema hauna imani na uandikishaji wananchi katika Daftari la Kudumu la Wapigakura kwa kutumia mfumo mpya wa Biometric Voters Registration (BVR), kutokana na kugubikwa na kasoro nyingi katika siku za mwanzo za uandikishaji huo unaoendelea mjini Makambako, mkoani Njombe.
Pia umesema serikali haina sababu ya kuwekeza fedha na muda kwenye kupiga kura ya maoni ya katiba inayopendekezwa, kwani uandikishaji wa wapigakura kwa ajili ya uchaguzi mkuu wa mwaka huu unasuasua.
Badala yake, umeishauri serikali kutumia fedha hizo kutoa elimu na kuhamasisha Watanzania kujiandikisha kwenye daftari hilo.
Mwenyekiti Mwenza wa Ukawa, Prof. Ibrahim Lipumba, alisema Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) inadanganya umma kuwa uandikishaji unaendelea vyema, wakati changamoto zilizojitokeza ni nyingi.
Alitaja kasoro zilizojitokeza kuwa ni alama za vidole sugu kutokusomeka kwenye mashine za BVR, mashine kubagua baadhi ya rangi za nguo na wafanyakazi kuchelewesha kazi hiyo kutokana na kukosa uelewa wa matumizi sahihi wa mashine hizo.
Serikali kupitia Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec), chini ya Mwenyekiti wake, Jaji mstaafu, Damian Lubuva, waache kutudang’anya Watanzania kwamba zoezi linaenda vizuri na kutuaminisha kuwa litakamilika ifikapo Aprili 16, wakati kuna changamoto lukuki, ikiwamo kubwa ya ukosefu wa fedha,”:- Prof. Lipumba.
Aliitaka Nec kuweka hadharani ripoti ya mshauri mwelekezi, Darall, kwa ajili ya Watanzania kuisoma na kujua mfumo mzima unavyoweza kufanya kazi.
Alisema hakuna haja ya Rais Jakaya Kikwete kutaka kukamilisha kazi ya upigaji kura ya maoni kwenye daftari hilo wakati Watanzania hawajaandikishwa na wala serikali haina uwezo wa kumaliza kazi hiyo kwa wakati na kwamba, haina fedha za kuendeshea.
NIPASHE
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Magesa Mulongo, amesema watu wote waliohusika ‘kuiba’ mtoto mwenye ulemavu wa ngozi (albino), Pendo Emmanuel (4), katika Kijiji cha Ndami, Wilaya ya Kwimba, mkoani humo wamekamatwa.
Akizungumza wakati akiwaapisha wakuu wapya wa wilaya wa mkoa huo jana, Manju Msambya (Misungwi), Zainab Rajab (Sengerema) na Pili Moshi (Kwimba), Mulongo alisema watu  wote waliohusika wamekamatwa na hivi sasa bado hawafahamu kama mtoto huyo yupo hai ama mfu.
Wezi wale baada ya kumuiba mtoto Pendo walimleta katika hoteli moja hapa jijini Mwanza, kisha kuwakabidhi watu walioonekana wanunuzi, lakini wote hao wamekamatwa akiwamo mmiliki wa hoteli hiyo,” Mulongo.
Alisema serikali ipo kazini wakati wote, ndiyo maana inafanya kazi usiku na mchana kuwasaka watu wote waovu mkoani Mwanza ambao hawawezi kusalimika kwa kile watakachokifanya.
Hata hivyo, alisema watu hao waliofanya uhalifu huo akiwamo baba wa mtoto huyo, Emmanuel Shilinde, wanashikiliwa na polisi huku mtu wa mwisho aliyetoweka na mtoto huyo toka hotelini hapo akiendelea kutafutwa.
NIPASHE
Mwanafunzi wa Shule ya Msingi Ilola, Kata ya Ilola Itwangi, Wilaya ya Shinyanga Vijijini, mkoani hapa, mwenye umri umri wa miaka 12 (jina lake linahifadhiwa kutokana na umri wake), anashikiliwa na polisi kwa tuhuma za kumuua mwenzake kwa kumpiga ngumi kichwani na kuangukia kisogo, wakati wakigombea daftari waliloazima.
Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga, Longinus Tibishubwamu, jana alisema tukio hilo lilitokea juzi saa 7:30 mchana na kwamba, wanamshikilia mwanafunzi huyo kwa mahojiano na kwamba wakikamilisha upelelezi atafikishwa mahakamani.
Alimtaja mwanafunzi aliyefariki dunia kuwa ni Veronica Venance (12), aliyekuwa anasoma darasa moja na mwezake aliyesababisha kifo hicho.
Mwalimu Mkuu wa Shule hiyo, Magere Jonas, alisema wakati wanafunzi hao wanagombea daftari hilo, alikuwa amepumzika chini ya mti akiwa na mwalimu mkuu msaidizi.
Jonas alisema baada ya kuingia darasani, walimkuta mwanafunzi huyo akiwa amelala chini akigalagala, hivyo kumkimbiza kwenye kituo cha afya Bugisi kilichoko jirani na shule hiyo, lakini kutokana na hali mbaya aliyokuwa nayo alifariki dunia.
Mtendaji wa Kata ya Ilola, Mahona Joseph, alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kuongeza marehemu alikuwa ameng’anga’nia daftari alilokuwa ameazimwa na Sophia Mathew kwa ajili ya kuandika ‘notes’ kitendo ambacho kilimkera mwenzake na kuzua ugomvi.
Tunahisi kifo cha mwanafunzi huyu kilitokana na kuanguka vibaya mara baada ya kusukumiwa ngumi na kukipiga kisogo, hivyo kukata mawasiliano na kusababisha kifo chake. Masuala mengi tumeviachia vyombo vya sheria”;-Joseph
MTANZANIA
Viongozi wa dini wameshauri majangali watakaokamatwa na kuthibitika kufanya ujangili , wang’olewe meno ili wasikie uchungu wa kufanya vitendo hivyo kwa wanyama.
Aidha alionya ni wakati kwa waovu hao kufika mwisho na kuacha ujangili wa kuua wanyama na kuchezea rasilimali nyingine za nchi bila kuchukua hatua.
Baddhi ya viongozi hao wadini walionya kulegalega kwa viongozi wa Serikali na kushindwa kukabiliana na ujangili na kwamba hali hiyo ni kuwadanganya wananchi katika jambo kubwa linalohusu uchumi wao.
Sheikh Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam Alhad Musa Salum alisema umefika wakati wa viongozi wa dini kujitokeza waziwazi na kuisaidia Serikali katika vita dhidi ya ujangili.
Askofu Joseph Mwingira alisema  Serikali ina dhamana ya kulinda rasilimali  kama itasimamiwa vizuri ujangili utaisha na umaskini nao utaisha.
Nitaendelea kukupatia kila stori inayonifikia , niko tayari kukutumia wakati wowote kupitia www.tangakumekucha.blogspot.com

No comments:

Post a Comment