Thursday, February 26, 2015

SHULE ILIYOSHIKA MKIA KIDATO CHA NNE, MANOLO SEKONDARI MLALO WILAYANI LUSHOTO

Tangakumekuchablog

Lushoto,Msingi mbovu wa  usimamizi wa wanafunzi  katika shule ya Sekondari  iliyoshika mkia katika matokeo ya mtihani wa Taifa wa kidato cha nne ya Manolo iliyopo Wilayani Lushoto mkoa wa Tanga pamoja na utoro ni miongoni mwa sababu zilizochangia kufanya vibaya.

Usimamizi mbovu wa uongozi wa shule ambao ulichangia migogoro ya mara kwa mara baina ya uongozi na walimu,walimu na wazazi uliweza kutoa mwanya kwa wanafunzi kutohudhuria masomo na badala yake kubobea kwenye kilimo cha mboga na biashara ndogo.

Haya yamebainika baada ya Makala hii kufika shule hapo na kufahamishwa kwamba kati ya wanafunzi  56 waliokuwa wamejisajili kufanya mtihani wa kidato cha nne mwaka jana ni  watano hadi 12 tu ndiyo waliokuwa wakihudhuria masomo darasani.

Shule hiyo iliyoanzishwa mwaka 2005 huku mtihani wa kitaifa wa kidato cha nne wakianza kufanya mwaka 2009 haijawahi kupata matokeo mabaya kama ya mwaka huu.

“Hakuna haja ya kumtafuta mchawi,haya matokeo tuliyatarajia,uongozi wa shule hapo awali haukuwa na usimamizi mzuri,mkuu wa shule alikuwa Mungu mtu alijenga mahusiano mabaya kwa walimu na hata sisi wazazi”anasema Seifa Ayoub mmoja wa wazazi wa wanafunzi wa shule hiyo

Wakazi wa Kijiji cha Manolo Tarafa ya Mlalo Wilayani Lushoto wanasema hii ni aibu kubwa kwao shule yao kushika mkia ni fedheha kubwa na hawakuitegemea.

Matokeo haya yalitarajiwa kwa sababu wanafunzi waliofanya mtihani wa kidato cha nne mwaka jana hawakupewa msingi mzuri kuanzi walipojiunga kidato cha kwanza mwaka 2011 hawakuwa wakihudhuria masomo licha ya kwamba walimu walikuwepo.

Makala hii imefahamishwa kwamba chimbuko la matokeo  hayo mabovu lilianza mwaka 2012 ambapo menejimenti ya shule ilikuwa katika mgogoro mkubwa baina yake na walimu kwa upande mmoja na kamati ya shule kwa upande mwingine na hivyo kusababisha migomo ya chini kwa chini ya walimu huku wanafunzi wakikosa kuhudhuria darasani.

Hayo yanadhihirishwa na matokeo ya miaka miwili iliyopita ambapo mwaka 2012 waliofaulu shuleni hapo kwa kupata divisheni ya kwanza hadi ya tatu walikuwa sita kati ya 23 wakati 2013 idadi ya waliopata ufaulu mzuri ilikuwa 15.

Mwaka jana waliofanya mtihani ambao matokeo yake yametoka hivi karibuni na kusababisha kushika mkia walikuwa 56 wasichana wakiwa 34 na waliopata alama za pass ikiwa kama divisheni 4 ni watatu tu huku wengine wote wakiambulia ziro

Mkuu wa Shule hiyo,Cheka Machaku ambaye aliyehamishiwa hapo msimu uliopita kuokoa jahazi baada ya migogoro kuvuka mipaka anasema hakuna  tatizo la uhaba mkubwa wa walimu kwani wapo nane ingawa.

“Tuna uhaba wa walimu wa kufundisha masomo ya kiingereza,hisabati na bailojia,lakini huwezi kulinganisha na shule za wenzetu ambazo nyingine hazina kabisa walimu na zimefanya vizuri”nasema Machaku.

Mwandishi wa makala hii ameshuhudia mazingira ya shule hiyo kuwa mazuri kwani majengo ya madarasa ni ya kuvutia,vyoo vipo katika hali nzuri kwa sababu vya wasichana vina matundu 12 na wavulana 10 wakati madarasa yote yana madawati.

Hata mazingira ya shule si ya kumfanya mwanafunzi akose kusoma kwa sababu majengo yake yamejitenga na makazi ya wanakijiji kwa hivyo hakuna bughudha.

Mwanafunzi wa kidato cha tatu,Asha Miraji ameyaelezea matokeo ya kidato cha nne mwaka huu kuwa yamewavunja nguvu ambapo baadhi yao wamewaomba wazazi wao wawahamishe.

Lakini yeye binafsi amesema matokeo hayo anayachukulia kama changamoto kwake na atahikisha anafanya vizuri ili aweze kufaulu kwa alama za juu.

Afisa elimu ya Sekondari wa Wilaya ya Lushoto Kassim Sengasu anasema pamoja na kwamba amehamishiwa Wilayani hapo hivi karibuni akitokea Mkoani Rukwa lakini matokeo hayo yamemfedhehesha na tayari imewekwa mikakati ya kuhakikisha Shule ya Manolo na ile ya Mnazi zinafanya vizuri mwakani.

“Tatizo la shule ya Manolo ni msingi mbovu waliokuwa wamewekewa wanafunzi,wenzangu waliliona hilo wakamhamisha aliyekuwa mkuu wa shule na kumpeleka mwingine,tumeanzia hapo na macho yetu yote yapo kwa hawa walioingia form four mwaka huu tutahakikisha wanafaulu vizuri”anasema Sengasu

         MWISHO
 Wanafunzi wa Shule ya Sekondari ya Manolo Serkondari Wilayani Lushoto Mkoani Tanga wakiwa katika moja ya jengo la shule hiyo kama walivyokutwa na camera ya tangakumekuchablog


 Mkuu wa Shule ya Manolo Sekondari Wilayani Lushoto Mkoani Tanga , Cheka Machaku akiwaongoza wanafunzi wake kukagua jengo la maabara.
 Mkuu wa Shule ya Manolo Sekondari, Cheka Machaku akiwa ofisini kwake akiwajibika kama alivyokutwa na Camera ya Tangakumekuchablog
 Mkuu wa Shule ya Manolo Sekondari,Wiklayani Lushoto Mkoani Tanga, Cheka Machaku akizungumza na Mkurugenzi Mkuu wa Tangakumekuchablog, Salim Mohammed ofisini kwake kuzungumza mambo mbalimbali ya maendeleo ikiwemo pia sababu za kufanya vibaya katika matokeo ya kitaifa na kuwa ya mwisho .
 Mwalimu wa Darasa Shule a Manolo Sekondari akiwajibika darasani kama alivyokutwa na Camera ya Tangakumekuchablog
 Wanafunzi wa shule ya Manolo Sekondari Mlalo Wilayani Lushoto Mkoani Tanga wakiwa makini wakifuatilia masomo darasani

 Wanafunzi wa shule ya Manolo Sekindari Tarafa ya Mlalo Wilayani Lushoto Mkoani Tanga wakitoka katika jengo la shule hiyo na kwenda katika ofisi za Mwalimu Mkuu wa Shule  kupokea taarifa za ujio wa timu mzima ya Tangakumekuchablog

Wanafunzi wa Shule ya Manolo Sekondari Tarafa ya Mlalo Wilayani Lushoto Mkoani Tanga wakiwa katika mshangao mara baada ya kuiona timu mzima ya Tangakumekuchablog ikiwa na vifaa vya kufanyia mahojiano pamoja na Camera.

No comments:

Post a Comment