Friday, February 20, 2015

SOMA HABARI KUBWA ZILIZOPEWA UZITO MAGAZETI YA LEO,TZ

Stori kubwa zilizopewa Headlines kwenye Magazeti ya leo Tanzania February 20, 2015

tops
NIPASHE
Wasomi, wanasiasa na wanaharakati nchini, wamepokea kwa hisia tofauti uteuzi alioufanya na Rais Jakaya Kikwete, wa wakuu wa wilaya wapya, huku baadhi wakikosoa uteuzi wa mkuu mpya wa wilaya ya Kinondoni, Paul Makonda na wengine wakiunga mkono.
Juzi Rais Kikwete aliteua wakuu wa wilaya wapya 27, akiwamo Katibu wa Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM) Uhamasishaji na Chipukizi, Makonda, kuwang’oa 19 na kuwahamisha 64.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti jana, baadhi walisema Rais Kikwete amefanya jambo la busara kuboresha utendaji kazi serikalini, lakini wakasema kumpa Makonda wadhifa huo  kunaweza kudhoofisha utendaji wa kazi katika wilaya ya Kinondoni.
Aliyekuwa mjumbe wa iliyokuwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Prof. Mwesiga Baregu,alisema Makonda alituhumiwa kumfanyia fujo aliyekuwa Mwenyekiti wa tume hiyo, Jaji Joseph Warioba, lakini hakuna hatua zozote zilizochukuliwa dhidi yake.
Hakuna uchunguzi wa polisi au kiusalama juu ya Makonda. Kutochukuliwa hatua kunadhihirisha mambo aliyoyafanya aliagizwa,”:- Prof. Baregu.
Alisema uteuzi huo wa wakuu wa wilaya wapya unaweza ukawa kinga kwa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kujiimarisha katika uchaguzi mkuu na kura ya maoni za katiba inayopendekezwa.
Rais wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT), Gratia Mukoba, alisema Rais Kikwete amefanya kitendo kizuri kuteua wakuu wa wilaya, lakini akasema kitendo cha kumpa Makonda ukuu wa wilaya ya Kinondoni siyo chema.
Alisema Makonda amepewa wilaya kubwa na hana uzoefu wowote wa kuongoza wilaya, kwani hajawahi hata kuongoza kata.
Sijawahi kumsikia akiongoza hata kata. Sana sana amewahi kuongoza Tahliso (Umoja wa Wanafunzi wa Vyuo vya Elimu ya Juu). Mtoto mdogo kama yule kumfanyia fujo mzee kama yule aliyeliletea sifa taifa na leo anakuwa mkuu wa wilaya ni jambo la kushangaza sana,Mukoba.
NIPASHE
Wananchi wa vitongoji vya Kazunzu, kijiji cha Nyambemba, kata ya Kazunzu, wakishirikiana na wa kitongoji cha Lueseselo, kata ya Bulyaheke,  wamempiga kwa marungu, mawe na mapanga na kisha kumchoma moto mtu ambaye bado hajafahamika, wakimtuhumu kuwa wakala wa kuteka watoto wakiwamo walemavu wa ngozi (albino), akishirikiana na waganga wa kienyeji wapiga ramli kwa imani za kishirikina za kupata utajiri.
Mbali ya kumuua, wananchi hao pia wamevunja na kuchoma moto nyumba 13 zilizoezekwa kwa bati mali ya mganga wa kienyeji mwanamke mpiga ramli mwenye umri wa miaka 40 (jina linahifadhiwa), Hata hivyo, mganga huyo na familia yake walifanikiwa kuwatoroka wananchi hao.
Tukio hilo lilitokea jana saa saba mchana katika kijiji cha Bulyaheke, kata Bulyaheke,baada ya wananchi kumkamata mtuhumiwa huyo katika kijiji cha Kazunzu na kuwaongoza hadi kijiji cha Bulyaheke kwa mganga huyo.
Richard Mangalamu baba wa mwanafunzi aliyetekwa, Winfrida (11) anayesoma darasa la nne Shule ya Msingi Kazunzu, alisema mtuhumiwa alimwachia mwanafunzi huyo kutokana na kumkuta ana chale mgongoni na kifuani akidai amepoteza ubora.
Mkuu wa Polisi wa Kituo cha Wilaya ya Sengerema, Babu Sanare na Ofisa Mtendaji wa kata hiyo, Enock Mabula, kwa nyakati tofauti walithibitisha kutokea kwa tukio hilo.
Naye Diwani wa Bulyaheke, Bagadi Nyuki, akiwa eneo la tukio, alisema chanzo cha mauaji hayo ni marehemu kudaiwa kuwa juzi alimteka mwanafunzi wa kike anayesoma darasa la nne katika Shule ya Msingi Kazunzu na kumvutia vichakani na kisha kumvua nguo na kumpapasa.
 NIPASHE
Mkoa wa Pwani umekumbwa na maafa kufuatia mvua kubwa zilizoyesha mapema wiki hii zikiambatana na kimbunga na radi katika wilaya za Kibaha na Bagamoyo, kujeruhi watu 12, kubomoa nyumba 128 na nyingine kuezuliwa paa.
Hayo yalisemwa katikati ya wiki hii na Mkuu wa Mkoa wa Pwani,  Evarist Ndikilo wakati akitoa salamu za mkoa wake kwa Makamu wa Rais, Dk. Gharib Bilal wakati wa hafla ya uzinduzi wa barabara ya Msoga- Msolwa yenye urefu wa kilomita 10 na ukaguzi wa mzani wa Vigwaza.
Ndikilo alisema mvua hizo zilizonyesha kwa saa mbili mfululizo katika wilaya hizo, zimesababisha  zaidi ya watu 200 kukosa mahali pa kuishi, wengi wao wakiwa ni wa Jimbo la Chalinze lililopo wilayani Bagamoyo.
Alisema tathimini ya awali inaonyesha katika kijiji cha Msoga,  nyumba 47, Shule ya Msingi Msoga na Ofisi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya kata zimeathiriwa na mvua hizo na watu  11 kujeruhiwa.
Alisema vilevile katika kijiji cha Tonga nyumba nne zimeathirika, kijiji cha Ngeta Kibaha Vijijini nyumba 77 na mtu mmoja kujeruhiwa.
Alisema majeruhi  wawili baba na mtoto wake wamelazwa Hospitali ya Tumbi  Kibaha kwa uangalizi  zaidi wa madaktari.
Alisema  Serikali ya Wilaya ya Bagamoyo na Kibaha kwa ushirikiano na Serikali ya Mkoa zinaendelea kufanya tathimini ya maafa hayo ili kuwasaidia waathirika ambao kwa sasa wanahifadhiwa kwa ndugu, jamaa na jirani zao.
MWANANCHI
Ilikuwa ni kama marudio ya ajali ya mwaka 2002, lakini ukubwa wa athari za tukio la jana unatofautiana baada ya watu watatu kufariki dunia na wengine 18 kujeruhiwa wakati wakijaribu kuchota mafuta kutoka kwenye lori lililopinduka katika Kijiji cha Idweli.
Lori hilo lililokuwa likitoka Mbeya kwenda Malawi, lilipinduka kwenye milima ya Mporoto, eneo ambalo ajali kama hiyo ilitokea mwaka 2002 na kuua watu 40 na wengine 100 kujeruhiwa na moto uliolipuka wakati wanakijiji wakijaribu kuiba mafuta kutoka kwenye lori hilo.
Usiku wa kuamkia jana, hali ilikuwa kama hiyo katika Kijiji cha Idweli, Rungwe wakati lori jingine lilipolipuka kwenye Barabara ya Mbeya-Malawi.
Katika tukio hilo, watu watatu walifariki dunia na wengine 18 kujeruhiwa kwa moto uliowafuata hadi kwenye nyumba zao walikoficha mafuta waliyoiba kutoka kwenye lori hilo.
Ofisa Tabibu wa Hospitali ya Igogwe, Alexanda Masaru alisema alipokea miili miwili ya watu na mmoja alifariki wakati akipatiwa matibabu na wengine 16 walilazwa baada ya kuungua sehemu mbalimbali.
MWANANCHI
Wakati Watanzania wakizidi ‘kutoboa’ mifuko yao kununua vifurushi vya kupiga simu na kutuma ujumbe wa mfupi, baada ya mabadiliko ya viwango vya huduma hizo, Kampuni ya Simu za Mkononi ya Tigo imesema mabadiliko hayo hayazuiliki kutokana na changamoto za uwekezaji.
Mkurugenzi Mkuu mpya wa Tigo, Cecile Tiano alisema jana kuwa Tanzania ni nchi yenye bei za chini za huduma za simu Afrika Mashariki, huku kodi zake zikiwa juu, jambo linalowapa ugumu kibiashara.
Tuna mipango yetu ya kuwekeza Sh221 bilioni mwaka huu, lakini hatuwezi kuendeleza uwekezaji huo kwa mazingira magumu yaliyopo,” :- Tiano.
Tigo ambao waliongeza wateja wao kwa asilimia 20 hadi kufikia wateja milioni tisa mwaka jana, wanatarajia kuongeza minara 787 ya intaneti ya 3G na 4G.
Mabadiliko ya huduma za vifurushi vya simu katika mitandao ya Tigo na Vodacom yamezua mjadala mzito nchini hasa kwa watumiaji wa mtandao wa intaneti.
MWANANCHI
Mtoto mwenye ulemavu wa ngozi, Yohana Bahati (1), aliyetekwa juzi katika Kijiji cha Ilelema, wilayani Chato mkoani Geita na kuokotwa katika Hifadhi ya Biharamulo akiwa amekufa bila mikono wala miguu, atazikwa leo saa 5 asubuhi katika Kijiji cha Ibondo, mkoani Geita chini ya ulinzi mkali wa polisi.
Yohana alitekwa nyumbani kwao saa mbili usiku, akiwa amebebwa na mama yake. Tukio la kutekwa mtoto huyo lilifanywa na watu wawili, ambao pia walimjeruhi mama huyo kwa kumkata mapanga kichwani.
Kamanda wa Polisi mkoani Geita, Joseph Konyo alisema juzi kuwa mwili wa mtoto huyo ulikutwa kwenye shamba la mahindi katika Kijiji cha Kimasa.
Alisema mwili huo uliokotwa juzi Februari 17, saa 12 jioni kwenye makazi yasiyo rasmi.
Ndugu wa marehemu, walisema Kamanda Konyo ameahidi kutoa ulinzi mkali wakati wa mazishi hayo kutokana na mazingira ya tukio lenyewe.
MTANZANIA
Mwakilishi wa Magomeni visiwani Zanzibar, Salmin Awadhi Salmin (CCM), amefariki dunia ghafla baada ya kuanguka katika kikao cha Chama Cha Mapinduzi (CCM), kilichokuwa kinafanyika katika ofisi kuu ya chama hicho, Kisiwandui mjini Unguja.
Taarifa hiyo ilianza kuenea mjini Unguja jana saa 6 mchana, na hata kuzua maswali kutoka kwa wananchi kuhusu utata wa kifo chake.
Salmin (57) ambaye pia alikuwa ni mnadhimu wa wawakilishi wa CCM na mjumbe wa Kamati Kuu ya chama hicho (CC), alikuwa mmoja wa wawakilishi wanaopinga mfumo wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK) kwa kutaka wananchi waulizwe kama bado wanahitaji muundo huo wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar.
Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Vua Ali Vuai, alisema kabla ya kufikwa na mauti, alianguka ghafla wakati akitoka katika kikao hicho cha kawaida.
Baada ya Salmin kuanguka, baadhi ya viongozi na wafanyakazi kwa haraka walimbeba na kumpeleka katika Hospitali ya Mnazi Mmoja kwa ajili ya matibabu na baada ya kufikishwa alipelekwa katika chumba cha wagonjwa mahututi (ICU), ambako baada ya muda mfupi madaktari walithibitisha kuwa amefariki dunia kwa maradhi ya shinikizo la damu.
HABARILEO
Wanasiasa wamenyooshewa vidole, wakihusishwa na mauaji ya watu wenye ulemavu wa ngozi baada ya matukio hayo kuhusishwa na harakati za kuelekea katika uchaguzi mkuu.
Vyama vya watu wenye ulemavu pamoja na baadhi ya wadau kutoka vyama vya siasa, vimetaka Serikali kutopuuzia dhana hiyo ya kuhusisha harakati za kisiasa na mauaji hayo.
Aidha, Chama cha Walemavu wa Ngozi Tanzania, kimesema kiko katika maandalizi ya kufanya maandamano ya amani hadi Ikulu kwa ajili ya kumwona Rais Jakaya Kikwetewapange mikakati ya kutokomeza mauaji hayo ya ukatili .
Akizungumza katika mkutano ulioandaliwa na Shirikisho la Vyama vya Walemavu na Vyama vya Siasa nchini, mwanachama kutoka Chama cha Wananchi (CUF), Abdallahalisema katika kipindi hiki kuelekea uchaguzi, alisema albino wanaishi kwa wasiwasi kutokana na uwezekano wa mauaji hayo kuanza kuibuka tena kwa kasi.
Mimi mwenyewe nina tatizo la ngozi (albino), hivi sasa tuko kwenye kipindi cha uchaguzi, na tetesi ni kwamba wengi wanauawa kwa imani potofu za baadhi ya watu kutaka madaraka, tusaidieni jamani ukweli ni kwamba tunaishi kwa hofu,” alisema.
Alisema ni vyema Serikali ikaacha kupuuzia tetesi hizo za kuwahusisha baadhi ya watu wanaotaka madaraka na kuagiza watu wenye ulemavu wauawe kwa imani za kishirikina.
Alitaka hatua madhubuti zichukuliwe kuokoa maisha ya Watanzania hao. “Jamani tujue kuwa hii ni damu inayomwagika ni ya ndugu zetu, kama hatua zisipochukuliwa inaweza kuwa laana kwa vizazi vyetu. Tukijipanga Tanzania tunaweza kuwa salama, alisisitiza.
Nitaendelea kukupatia kila stori inayonifikia mtu wangu, niko tayari kukutumia wakati wowote kupitia www.tangakumekucha.blogspot.com

No comments:

Post a Comment