Thursday, February 19, 2015

WAKULIMA LUSHOTO WALALAMIKA MAOFISA UGANI KUJIFUNGIA MAOFISINI

Tangakumekuchablog

Lushoto,WAKULIMA wa nafaka na mbogamboga  kata ya Maore na Kidundai Wilayani Lushoto Mkoani Tanga, wameitaka Serikali kuwaajibisha maofisa kilimo baada ya kushindwa  kutekeleza wajibu wao na badala yake  wamekuwa waking’ang’ania kukaa mjini.

Wakizungumza katika mkutano wa wananchi leo, wakulima hao walisema kuna baadhi ya maofisa kilimo ambao hawatekelezi wajibu wao na badala yake wanajifungia maofisini huku wakulima wakishindwa kupata huduma za kitaalamu.

Walisema wakulima wengi wamekuwa wakiendesha kilimo chao kwa hasara baada ya mazao yao kushindwa kupata rutba na kuharibiwa na wadudu aina ya kiduha na magugu.

“Jitihada za Serikali kuwapeleka wataalamu wa kilimo kila tarafa limekuwa msaada sana kwa wakulima----ila kuna jambo ambalo bado haijalijua ambalo ni kuwa hawafiki mashambani na badala yake wamekuwa wakijifungia maofisni” alisema Sued Bushir

“Nadhani ni wakati sasa wa Serikali kutambua kuwa Lushoto ni eneo la wakulima wakubwa na wenye bidii ya maendeleo----kila utupapo macho ni aina ya kilimo na hakuna pori kwani ardhi yote  iko na rutba” alisema
Kwa upande wake mkulima wa njegere na mabamia, Ashraf Sadik, 
ameiomba Serikali kuwapatia soko la uhakika la kuuzia mazao yao na kuepuka ulanguzi kwa matajiri wenye pesa.

Alisema vipindi vya mavuno wamekuwa wakishuhudia kumiminika matajiri wakiwa na lengo la kuwalangua wakulima baada ya kutokuwa na soko la uhakika la  kuuzia mazao yao kama ilivyo kwa baadhi ya Wilaya na Mikoa.

“Lushoto hakuna kiwanda cha kusindika matunda na mbogamboga bali wapo wanaozuka vipindi vya mavuno na kuwalalalia wakulima hasa wale wachanga” alisema Sadik

Akitoa ushauri kwa wakulima wenzake , Sadik  aliwataka kuacha tamaa ya kuuza mazao yao kwa bei ya chini na kuwataka kuwa na misimamo  jambo ambalo litasaidia  katika kukuza kilimo  na kuwa mkulima wa kisasa.

Alisema wako wakulima kwa mtazamo wamekuwa wakiuza mazao yao kwa bei ya chini jambo ambalo limekuwa likiwakandamiza wakulima wenzao kila siku na kusababisha kuwa  kuwa wanaweza kupoteza nguvu zao bila tija.

                                             Mwisho

No comments:

Post a Comment