Sunday, May 3, 2015

SOMA MAKUBWA YALIYOANDIKWA MAGAZETINI LEO, MAY 3 TZ

Uchambuzi huu wa magazeti unaletwa kwenu kwa hisani kubwa ya kituo cha Elimu Cha Candle Education Centre Tanga. Kituo kinaongoza kufaulisha wanafunzi kidato cha pili hadi cha sita. Wapo Tanga mkabala na Bank ya CRDB simu 0715 772746

BRIIF
MWANANCHI
Hatimaye makada wa CCM wanaotajwa kuwania urais wa Jamhuri ya Muungano, juzi walipata nafasi ya kutunishiana misuli baada ya kualikwa kuchangia mfuko wa maendeleo wa mkoa mpya wa CCM wa Magharibi visiwani hapa.
Edward Lowassa, Mizengo Pinda, Bernard Membe, Makongoro Nyerere, Mark Mwandosya na Steven Wasira walishiriki kwenye hafla hiyo na kuchangia zaidi ya nusu ya fedha zilizokusanywa juzi kwa ahadi, hundi na taslimu kwenye harambee hiyo iliyofanyika Hoteli ya Zanzibar Beach Resort mjini hapa.
Hata hivyo, pamoja na cheche za makada hao kuonekana visiwani hapa, Ni Waziri Mkuu Pinda aliyehudhuria harambee hiyo iliyokusanya jumla ya Sh. milioni 644.54 na ambayo Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk Ali Mohamed Shein alikuwa mgeni rasmi.
Waziri Pinda ndiye aliyetia fora kwenye hafla hiyo baada ya yeye na marafiki zake kuchangia jumla ya Sh203 milioni, wakati Lowassa, Membe, Wasira, Dk Shein, Mwandosya, Makongoro, Shamsi Vuai Nahodha na Amina Salum Ali walichangia jumla ya Sh101.5 milioni.
Makada hao hawakukutana kwa bahati mbaya kwenye hafla hiyo.
“Tuliwapelekea mwaliko maalumu wote waliotangaza nia ya kugombea urais,” alisema mratibu wa shughuli hiyo, Naibu Waziri wa Afya Mahmoud Thabit Kombo kabla ya harambee kuanza.
Kombo alisema si vyema kwa wanachama wa CCM kubaguana wakati viongozi wakuu wa nchi hawajambagua mtu kwa sababu ya makundi ya wagombea uongozi.
Kati ya fedha zilizokusanywa, Sh120.7 milioni zilikuwa fedha taslimu, wakati ahadi zilikuwa Sh490.8 milioni na hundi Sh33 milioni.
Katika hafla hiyo vitu mbalimbali vya asili pamoja na picha za kumbukumbu za kitaifa, ikiwamo picha ya kuchora ya Rais Dk Shein ambayo ilinunuliwa kwa Sh23 milioni.
MWANANCHI
Tishio la ugaidi limezidi kuwa tete baada ya watu wanaoshukiwa kufanya vitendo hivyo kulipua bomu na kusababisha watu watano kujeruhiwa wakati wakitoka kwenye maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi katika Kijiji cha Msolwa Ujamaa, kilichoko Kata ya Sanje wilayani Kilombero.
Hili ni tukio la pili kutokea kwenye Wilaya ya Kilombero mkoani Morogoro baada ya watu tisa kukamatwa kwenye Msikiti wa Suni wakiwa na silaha na vifaa vingine vinavyohusishwa na harakati za kigaidi.
Mbali na matukio hayo ya Morogoro, hivi karibuni vikosi vya ulinzi na usalama vilipambana vikali na watu wanaoshukiwa kuwa ni magaidi kwenye mapango ya kihistoria ya Amboni mkoani Tanga.
Hadi sasa polisi haijatoa taarifa ya kina kuhusu tukio hilo lililopoteza maisha ya mwanajeshi mmoja.
Kamanda wa polisi mkoani Morogoro hakuweza kupatikana kuzungumzia suala hilo, wakati msemaji wa Jeshi la Polisi alisema tukio hilo liko ndani ya mipaka ya mkoa hivyo linatakiwa lizungumzwe na mamlaka hiyo badala ya makao makuu ya chombo hicho cha dola.
Mashuhuda wa tukio hilo lililotokea walieleza kuwa bomu hilo lilirushwa kuelekea kwenye gari la mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilombero saa 2:00 usiku.
Bomu hilo lilirushwa na watu wawili ambao awali walidhibitiwa na wananchi baada ya kuwashuku kuwa siyo raia wema.
Baada ya kuwatilia shaka, wananchi waliwaweka watu hao chini ya ulinzi na wakati wakiwapekua, walitoa bomu na kulirusha kwenye gari hilo lililokuwa limeegeshwa na kujeruhi  watu watano, akiwamo dereva.
Mwenyekiti wa halmashauri hiyo, David Ligazio aliwataja waliojeruhiwa katika tuko hilo kuwa ni Novatus Ngapi, ambaye ni dereva na Thomas Manjole, ambaye ni mgambo na hali yake inadaiwa kuwa siyo nzuri.
Wengine waliojeruhiwa ni Amos Msopole, Azama Naniyunya, ambao wamelazwa katika Hospitali ya Mtakatifu Kizito iliyopo Mikumi wilayani Kilosa na Anna Pius ambaye amepata majeraha kidogo na kuruhusiwa.
MWANANCHI
Mwenyekiti wa Chama cha Tanzania Labour Party (TLP), Augustino Mrema amesema hakuna ubaya Rais Jakaya Kikwete akiachwa kuongeza nchi kwa muda ili akamilishe mchakato wa Katiba Inayopendekezwa pamoja na Daftari la Kudumu la Wapigakura.
Hivi karibuni viongozi wanaounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA), walidai kuwa Serikali na Tume ya Uchaguzi (NEC) inachelewesha uboreshaji wa Daftari la Wapigakura kwa lengo la kutaka kumwongezea Rais Kikwete muda wa kukaa Ikulu.
Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe alisema ni miezi mitatu imebaki kabla ya kampeni za uchaguzi, lakini mpaka sasa ratiba, majimbo yaliyogawanywa, watumishi wala vituo vya uchaguzi bado haviwekwa bayana na wala haifahamiki kazi ya uandikishaji katika Daftari la Wapigakura halijakamilika katika mikoa miwili.
Hiyo ni hatari sana kwa Taifa. Tunaionya NEC isijaribu kufanya mbinu zitakazosababisha kuahirishwa kwa Uchaguzi Mkuu wa Oktoba mwaka huu,” Mbowe.
Mrema alisema yeye ndiye aliyekuwa mtu wa kwanza kutoa wazo la kutaka Rais Kikwete aongezewe muda zaidi wa kukaa Ikulu kwa kuwa kuna mambo mengi ambayo ni ya muhimu kwa Taifa yanayotakiwa kukamilika kabla ya Uchaguzi Mkuu.
Mrema alisema alitoa maoni hayo mwaka jana wakati viongozi wa Kituo cha Demokrasia Tanzania (TCD) walipokutana na Rais Kikwete mjini Dodoma, lakini alishangaa kuona viongozi wengine wakipinga wazo hilo.
“Nilitoa ushauri Rais Kikwete akiwepo. Nilisema tusogeze Uchaguzi Mkuu mbele kwa miaka miwili ili atuachie nchi ikiwa salama, lakini wapinzani wamejiandaa kuingia Ikulu waliniona mimi kama bundi,” Mrema.
JAMBOLEO
Waziri wa Nishati na madini George Simbachawene ameiagiza menejmenti ya Shirika la Umeme TANESCO kuwachukulia hatua za kinidhamu wahandisi wa shirika hilo.
Kauli hiyo ilitolewa jana wakati wa mkutano na watendaji wa Tanesco wa kanda ya Dar na Pwani, ambapo alisema Muhandisi wa Wilaya ya Temeke, Tabata na Tazara wameshindwa kusimamia majukumu waliyopewa na Shirika hilo,hivyo amewataka wakurugenzi wahakikishe wanawahadhibu.
Alisema huo ni mwanzo kwani ataendelea kuwachukulia hatua watumishi ambao watashindwa kufanyia kazi majukumu waliyopewa na Shirika katika kuhakikisha wanawapa huduma nzuri Watanzania.
“Wengine wakae mguu sawa, huu ni mwanzo tu, sitaki kuwa na watendaji ambao hawajui wanachokifanya katika vitengo walivyopewa, yeyote atakayeshindwa kufanya kazi yake ni vyema aachie ngazi” Simbachawene.
Alisema wahandisi watatu aliowatolea maagizo wachukuliwe hatua za kinidhamu wanamtosha kwani anaamini litakuwa fundisho kwa wengine.
MTANZANIA
Meli ya Tanzania iliyokamatwa kwenye bahari ya Kaskazini nchini Marekani ikiwa na tani tatu za dawa za kulevya aina ya Cocaine ilisajiliwa Zanzibar.
Taarifa iliyopatikana kutoka vyombo ya habari vya kimataifa ilisema meli hiyo ilikutwa na tani tatu za dawa za kulevya zenye thamani ya shilingi trilioni 1.5.
Meli hiyo inayojulikana kwa jina la Mv Hamal ilikamatwa na meli ya kivita ya Uingereza na kikosi chamipaka ikiwa umbali wa kilometa 160 kuelekea katika Pwani ya Aberdeen nchini Scotland na ilikuwa ikiendeshwa na waturuki.
Msemaji wa SUMATRA, David Mziray aamesema wanaendelea kufuatilia kama meli hiyo ilisajiliwa bara ama visiwani na baadaye alisema wao hawahusiki n usajili wa meli hiyo.
Mkurugenzi mkuu wa Mamlaka ya Usafiri Zanzibar Abdi Maalim alikiri kuwa meli hiyo ilisajiliwa Zanzibar kupitia kwa wakala wao aliyepo Dubai.
HABARILEO
Wafanyabiashara wadogo na waendesha bodaboda wanaofanya biashara zao kwenye njia kubwa za kusafirishia umeme wapo hatarini kupungukiwa nguvu za kiume.
Kutokana na kuwepo wengi kwenye njia hizo kubwa za kusafirishia umeme, wametahadharishwa kutoendelea kufanya biashara kwenye maeneo hayo.
Hayo yalibainishwa jana na Ofisa Mahusiano Msaidizi huduma kwa wateja wa Tanesco Mwanza, Haji Bwegege  baada ya uzinduzi wa maonyesho ya siku ya wafanyakazi uliofanywa na Mkuu wa mkoa wa Mwanza, Magesa Mulongo kwenye viwanja vya Furahisha, jijini hapa.
Tumekuwa tukiielimisha jamii mara kwa mara kutofanya biashara kwenye njia ya umeme mkubwa unaopita kutokana na madhara wanayoweza kuyapata na hii ya kupungukiwa nguvu za kiume ni moja ya madhara ambayo yanaweza kuwapata hivyo wachukue tahadhari mapema,”
Aliyataja madhara mengine kuwa pamoja na mwili kupoteza nguvu kutokana na mionzi hivyo wananchi kutakiwa kuishi umbali wa mita 30 kila upande pamoja na mjamzito kuharibu mimba.
HABARILEO
Wakimbizi 800 kutoka nchini Burundi wameingia nchini kupitia mkoani Kigoma huku wengine 87 wakirejeshwa nchini mwao baada ya kuingia nchini kwa kupitia wilayani Ngara mkoani Kagera.
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya ndani ya Nchi, Isack Nantanga alisema wakimbizi hao wameingia nchini kwa makundi madogo madogo na watahifadhiwa kwa muda karika kambi ya wakimbizi ya Nyarugusu.
Nantanga alisema wakimbizi wanaofikia 800 wameshaingia nchini huku walioingia kupitia mkoani Kagera ilibidi warejeshwe walipotoka kutokana na kukiuka sheria za kimataifa kwa wakimbizi kuingia nchi nyingine wakivuka nchi moja.
Alisema hawapokei wakimbizi wanaotokea Rwanda kutokana na kuwa sheria za kimataifa haziruhusu wakimbizi kuvuka nchi moja ndiyo maana waliwarejesha wakimbizi hao.
Alisema kati ya wakimbizi hao waliopokelewa mkoani Kigoma wameingia kupitia vijijini ambapo serikali za vijiji wanawapokea na kuwahoji kisha kuwapleka kigoma mjini kwenye kituo maalum.
Alisema serikali za vijiji na wilaya kwa kushirikiana na halmshauri wamekuwa wakaifanya kazi ya kuwahoji kujua sababu hasa ya kuwafanya wakimbilie nchini humu kwani isije kutumika vurugu za Burundi watu kuingia nchini.
“Serikali kwa kushirikiana na Shirika la umoja wa mataifa la kuhudumia wakimbizi (UNHCR) baada ya kuwahoji na kuwapa misaada muhimu wanaobainika kupata hifadhi wana mpango wa kuwapeleka kwenye kambi ya Nyarugusu kwa muda,”alisema.
Msemaji huyo alisema baada ya kuhifadhiwa katika kambi hiyo mipango inaendelea kufahamu njia nyingine za kuwahifadhi.
Wengi wa wakimbizi hao wametokea mji wa Bujumbura na wameingia Kigoma kwa usafiri wa boti kupitia bandari ndogo ya Kibirizi mjini Kigoma.
Inaelezwa kuwa kundi kubwa la wakimbizi liliingia nchini juzi katika mpaka wa Tanzania na Burundi kwenye kijiji cha Kagunga mwambao wa kaskazini wa ziwa Tanganyika ambapo kundi la wakimbizi 200 waliingia kupitia kijiji hicho.
Tayari wakimbizi 68 ambao waliingia na kufikia kambi ya muda ya NMC kibirizi mjini Kigoma wamepelekwa kwenye kambi ya Nyarugusu wilayani Kasulu ambayo kwa sasa ndiyo kambi pekee mkoani Kigoma inayohifadhi wakimbizi.
Akizungumzia kuingia kwa wakimbizi mkoani humo Mkuu wa mkoa Kigoma, Issa Machibya alisema kuwa wameanza kupokea wakimbizi kutoka vijiji mbalimbali vya wilaya za Buhigwe,Kasulu na Kibondo ambao wanakimbia hali ya machafuko nchini Burundi.
Machibya alitaja maeneo ambayo hadi sasa yamekuwa yakipokea wakimbizi hao kuwa ni pamoja na Kijiji cha Kagunga wilaya ya Kigoma, Muyama,Kibande na Kilelema ambavyo vyote vipo katika wilaya ya Buhigwe mkoani Kigoma.
Kuingia kwa wakimbizi wa Burundi nchini Tanzania kunatokana kuanza kwa machafuko nchini humo kati ya wananchi wanaopinga kitendo cha Rais wa nchi hiyo, Pierre Nkurunzinza kuongoza muhula wa tatu wa uongozi dhidi ya polisi na wanajeshi wanaomtii raisi huyo.
Kwa siku mbili mfululizo kumekuwepo na taarifa za kuchomwa mwa mabasi mawili ya abiria na moja kulipuliwa kwa bomu la kurushwa kwa mkono huku kukiwa na vifo vya watu kadhaa kutokana na makabiliano ya waandamanaji na polisi.
Wageni wamekuwa wakizuiliwa kuingia mji mkuu wa Burundi, Bujumbura ambako kwa kiasi kikubwa maandamano ya kupinga hatua ya Rais Nkurunzinza kuongoza muhula wa tatu yanaendelea ambapo kwa sasa maandamano hayo yameanza kusambaa mikoa ya jirani na mji Mkuu wa Bujumbura.
NIPASHE
Agizo la serikali la kupiga marufuku uingizaji wa mabehewa ‘feki’ ili kuliokoa taifa dhidi ya ufisadi na ajali zinazogharimu mali na maisha ya watu, limepuuzwa baada ya Kampuni ya Reli (TRL) kupokea mabehewa 47, mwanzoni mwa wiki iliyopita.
Mabehewa hayo ni sehemu ya yaliyoanza kuingizwa nchini, Julai 24, mwaka jana na kupokelewa na aliyekuwa Waziri wa Uchukuzi wa wakati huo, Dk. Harrison Mwakyembe.
Hata hivyo, serikali kupitia kwa Waziri wa Uchukuzi, Samwel Sitta, ilizuia uingizwaji wake, Aprili 16, mwaka huu, kwa madai kuwa hayana ubora.
Akitangaza uamuzi wa kuzuia mabehewa hayo, Sitta alisema baada ya bodi kupitia taarifa hiyo, ilibaini  mabehewa mengi kati yaliyoagizwa yalikuwa na kasoro, kuwepo kwa uzembe katika uagizaji na ufuatiliaji kuanzia kiwandani  na kuwapo kwa uzembe katika mchakato wa kuyapokea.
Sitta alisema kilichowashtua ni kubaini ukiukwaji mkubwa wa masharti ya mkataba wa ununuzi ambao ulipangwa kufanyika kwa awamu.
Alisema katika makubaliano ya ununuzi wa mabehewa hayo, malipo yalitakiwa yafanywe kwa awamu kwa kuanza na asimilia 50 awamu ya kwanza,  asilimia 40 awamu ya pili  na awamu ya mwisho ya malipo ilikuwa ni asilimia 10.
Hata hivyo, wiki mbili tangu Sitta atoe agizo hilo, gazeti hili limebaini kuwa mabehewa 47 yaliingizwa nchini na kuhifadhiwa kwenye karakana ya Malindi jijini Dar es Salaam.
Chanzo hicho kimesema inavyoonyesha mkataba wa kuyaleta mabehewa hayo haujavunjwa ndio maana yamewasili tena licha ya Waziri Sitta kusema yaliyobaki yasiingie nchini.
Mabehewa hayo ni kati ya 274, ambapo 150 yalishaingizwa nchini na mengine 124 yalizuiliwa.
Sakata la ununuzi wa mabehewa hayo limesababisha serikali hasara ya Sh. bilioni 230. Kufuatia sakata hilo Sitta aliwasimamisha kazi vigogo watano kutokana na kubainika kuihujumu serikali.
Waliosimamishwa ni Mkurugenzi Mtendaji, Kipallo Kisamfu, Mhandisi Mkuu wa Mitambo, Ngosomwile Ngosomiles, Mhasibu Mkuu,  Mbaraka Mchopa, Mkaguzi Mkuu wa Ndani, Jasper Kisiranga na Meneja Mkuu wa Manunuzi Fedinarnd Soka.
NIPASHE
Wakati serikali ikijitetea kuwa kushuka kwa shilingi ya Tanzania kunatokana na kuimarika kwa dola ya Marekani, Mbunge wa Kigoma Kusini (NCCR-Mageuzi), David Kafulila ametaja sakata la Escrow kuchangia pia anguko hilo.
Kafulila alisema hayo jana alipozungumza na waandishi wa habari jana Jijini Dar es Salaam, wakati wa kikao cha Kamati ya Bunge ya Uchumi, Viwanda na Biashara, iliyokutana na Wizara ya Fedhana mamlaka zake.
Alisema, kwa mujibu wa maelezo ya Gavana wa Benki Kuu (BoT), Profesa Benno Ndulu, sababu za kushuka kwa shilingi ni kuimarika kwa dola ya Marekani na kusababisha sarafu zote duniani kuathirika katika mbadilishano na dola.
Aidha, sababu nyingine ni uhaba wa dola uliosababishwa na kukosekana kwa fedha za wafadhili.
Kafulila alisema misaada iliyokuwa inatarajiwa kutoka kwa wahisani imekwama kutokana na sakata la Escrow.
Alisema mikopo ya  kibiashara ambayo Tanzania ilikuwa ikitarajia kupata dola milioni 800, imekatwa na  kutolewa dola milioni 300, tafsiri inayoonyesha kuwa Tanzania haiaminiki.
Alisema fedha za wafadhili zaidi ya Sh. tirioni 1.0, sawa na dola milioni 740, hazijaidhinishwa kupewa Tanzania na mwaka jana Wizara ya Fedha ilisema zitaidhinishwa Desemba, mwaka jana.
Mwaka huu wanazungumzia labda zitasainiwa Septemba tafsiri yake ni kwamba hiyo hela ambayo ni sawa na tirioni 1.5 haitaletwa hadi hatua zichukuliwe kwenye jambo la Escrow,” Kafulila
Hata hivyo, alisema mikopo ya biashara ya dola milioni 500-800 iliyoahidiwa kuletwa imekwama kwa sababu ya sakata la Escrow.
Alisema tatizo la serikali ni kusema hatua zimechukuliwa wakati,  IPTL inalipwa zaidi ya Sh bilioni 5 kila mwezi, kama tozo ya uzalishaji  (Capacity Charge).
Kama kawaida tangakumekuchablog inakuta yote yaliyoandikwa katika magazeti, ni hapa hapa

No comments:

Post a Comment